Kichocho—Je, Kitaondolewa Karibuni?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA
JAPO maendeleo makubwa katika nyanja za tiba na sayansi, wanadamu wameshindwa kusuluhisha mengi ya matatizo yao ya kale. Na ndivyo ilivyo na jitihada zao za kumaliza ugonjwa wa kichocho.
Yaonekana kwamba kuna njia zote za kutibu maradhi hayo. Madaktari wanafahamu maisha ya kimelea kinachohusika. Maradhi hayo hugunduliwa kwa urahisi. Kuna dawa nzuri za kuyaponya. Viongozi wa serikali wanatamani kuendeleza jitihada za kuyazuia. Lakini, mwisho hauonekani kwa maradhi haya ambayo yameambukiza mamilioni ya watu katika Afrika, Amerika Kusini, Asia, Karibea, na Mashariki ya Kati.
Kichocho kimekumba mwanadamu kwa maelfu ya miaka. Mayai yaliyohifadhiwa kwa chumvi yaliyopatikana katika miili iliyohifadhiwa ya Wamisri yanathibitisha kwamba maradhi hayo yalikumba Wamisri katika siku za mafarao. Karne 30 baadaye, maradhi hayohayo yaendelea kukumba Misri, yakidhoofisha afya za mamilioni ya wakazi wa nchi hiyo. Katika vijiji fulani vya Delta ya Naili, watu 9 kati ya kila watu 10 wameambukizwa.
Misri ni mojawapo tu ya nchi 74 au zaidi ambamo kichocho kimeenea sana. Kulingana na tarakimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), watu milioni 200 wameambukizwa maradhi hayo. Kati ya wenye kuugua daima milioni 20, karibu 200,000 hufa kila mwaka. Miongoni mwa maradhi ya vimelea vya kitropiki, kichocho ni cha pili kwa malaria tu kwa habari ya idadi ya watu wanaoambukizwa na madhara ya kijamii na kiuchumi ambayo kinasababisha.
Maisha ya Kimelea Hicho
Kuelewa kichocho, na hivyo kujua jinsi ya kukiepuka na kukitibu, kunamaanisha kuelewa kimelea kinachokisababisha. Jambo kuu ni hili: Ili kuishi na kufanikiwa kizazi kwa kizazi, kimelea hicho huhitaji makao mawili, viumbe viwili ambavyo kimelea hicho chaweza kukua ndani yavyo na kusitawi. Kimoja ni mamalia, kama mwanadamu; kingine ni konokono wa maji yasiyo ya chumvi.
Hivi ndivyo mambo hutukia. Mtu aliyeambukizwa kimelea hicho anapokojoa au kunya katika maji ya kidimbwi, ziwa, kijito, au mto, yeye humwaga mayai ya kimelea hicho—yawezekana kufikia mayai milioni moja kila siku. Mayai haya ni madogo sana hivi kwamba hayawezi kuonekana bila msaada wa hadubini. Mayai hayo yagusapo maji, hayo huanguliwa, yakiachilia vimelea. Vimelea hivyo hutumia manyoya madogo sana kwenye miili yao ili kuogelea kutafuta konokono wa maji yasiyo ya chumvi, ambaye hivyo huingia mwilini mwake. Ndani ya huyo konokono, vimelea hivyo huzaana kwa muda wa majuma manne hadi saba.
Vinapoondoka kwenye mwili wa konokono, vimelea hivyo vina muda wa saa 48 pekee wa kupata na kuingia ndani ya mwanadamu au mamalia mwingine. La sivyo, vitakufa. Kinapofikia mtu au mnyama ambaye amekuja majini, kimelea hicho hupenya ngozi na kuingia katika mkondo wa damu. Hilo laweza kufanya mtu huyo ahisi mwasho fulani, ingawa mara nyingi hana habari kwamba ameambukizwa. Ndani ya mkondo wa damu, kimelea hicho huingia katika mishipa ya damu ya kibofu au ya matumbo, ikitegemea aina ya kimelea. Kwa majuma kadhaa kimelea hicho hukua hadi kufikia minyoo waliokomaa wa kiume na wa kike wenye urefu wa milimeta 25. Baada ya kujamiiana, wa kike huanza kutaga mayai katika mkondo wa damu na hivyo kukamilisha maisha ya kimelea hicho.
Karibu nusu ya mayai hayo huondoka mwilini katika kinyesi (kichocho cha utumbo) au katika mkojo (kichocho cha njia ya mkojo). Mayai yaliyosalia hubaki mwilini na kudhuru viungo muhimu. Maradhi hayo yazidipo, mtu huyo aweza kushikwa na homa, kufura kwa tumbo, na kuvuja damu kindani. Hatimaye maradhi hayo yaweza kutokeza kansa ya kibofu cha mkojo au kushindwa kwa ini au mafigo kufanya kazi. Wahasiriwa wengine hupoteza uwezo wa kuzaa au hupooza. Wengine hufa.
Masuluhisho na Matatizo
Ili kuzuia mweneo wa maradhi haya, angalau mambo manne yaweza kufanywa. Ikiwa mojawapo ya hatua hizo nne yaweza kutumiwa duniani pote, maradhi hayo yanaweza kufutiliwa mbali.
Hatua ya kwanza ni kuondosha konokono katika maji. Konokono ni muhimu sana katika ukuzi wa kimelea hicho. Ukosefu wa konokono ni ukosefu wa kichocho.
Jitihada ambazo zimefanywa zimekuwa kutokeza sumu iliyo na nguvu kiasi cha kuua konokono lakini isiyoweza kuchafua mazingira. Katika miaka ya 1960 na 1970, majaribio yaliyofanywa ya kuondosha konokono yaliua uhai wote uliokuwa katika sehemu kubwa-kubwa za maji. Jitihada zimefanywa katika Taasisi ya Utafiti ya Theodor Bilharz ya Misri za kutafuta dawa ya kuua konokono ambayo haidhuru namna nyingine za uhai. Dakt. Aly Zein El Abdeen, msimamizi wa taasisi hiyo, asema hivi kuhusu dawa kama hiyo: “Hiyo itawekwa katika maji, ambayo hutumiwa kwa mimea, ambayo hunywewa na watu na wanyama, na ambamo mna samaki, kwa hiyo ni lazima tuwe na hakika kabisa kwamba hali hizo zote hazipati madhara.”
Hatua ya pili ni kuua vimelea vilivyo katika wanadamu. Kufikia katikati ya miaka ya 1970, tiba ilihusu dawa ambazo zilisababisha athari nyingi na hitilafu nyinginezo. Mara nyingi, tiba ilihusisha kudungwa mfululizo wa sindano zenye uchungu. Wengine walilalamika kwamba hiyo tiba ilikuwa mbaya zaidi ya maradhi yenyewe! Tangu wakati huo, dawa mpya, kama vile praziquantel, ambazo zinafanya vizuri dhidi ya kichocho zimetengenezwa, nazo zaweza kumezwa.
Ingawa dawa hizi zimefanikiwa katika miradi ya majaribio katika Afrika na Amerika Kusini, tatizo kubwa kwa nchi nyingi limekuwa gharama. Shirika la WHO liliomboleza hivi katika 1991: “Nchi zenye pigo zaidi zimeshindwa kuendeleza programu za kudhibiti [kichocho] kwa sababu tiba ni ghali sana; gharama ya kifedha ya dawa yenyewe mara nyingi ni maradufu ya bajeti ya mapato yote ya wizara nyingi za afya za nchi za Afrika.”
Hata mahali ambapo mgonjwa anapata dawa bila malipo, watu wengi hawaendi kutibiwa. Kwa nini? Sababu moja ni kwamba vifo vinavyotokana na maradhi hayo ni vichache kwa kulinganisha, kwa hiyo watu fulani hawayaoni kuwa tatizo kubwa. Sababu nyingine ni kwamba sikuzote watu hawatambui dalili za maradhi hayo. Katika sehemu fulani za Afrika, damu katika mkojo (dalili kubwa ya maradhi hayo) ni kawaida sana hivi kwamba hiyo huonwa kuwa jambo la kawaida la kufikia utu-uzima.
Hatua ya tatu ni kutoacha mayai hayo yafikie mifumo ya maji. Vyoo vikichimbwa ili kuepusha vijito na vidimbwi vya sehemu fulani visichafuliwe na kila mtu akivitumia, hatari ya kushikwa na kichocho inaweza kupunguka.
Uchunguzi wa duniani pote waonyesha upungufu mkubwa wa maradhi hayo baada ya kuletwa kwa maji ya mfereji na kujengwa kwa vyoo vya kuchimbwa, lakini maandalizi hayo hayahakikishi kwamba maradhi haya yatazuiwa. “Mtu mmoja tu akinya katika maji, maisha ya kimelea hicho yaendelezwa,” asema mwanasayansi Alan Fenwick, ambaye amefanya utafiti wa kichocho kwa zaidi ya miaka 20. Pia kuna hatari ya mabomba ya maji machafu yaliyotoboka yakiingiza mavi yenye vimelea ndani ya maji safi.
Hatua ya nne ni kuzuia watu wasitumie maji yaliyoambukizwa na kimelea hicho. Hiyo pia si rahisi hivyo. Katika nchi nyingi maziwa, vijito, na mito ambayo hutokeza maji ya kunywa hutumiwa pia kwa kuoga, kunyunyizia mimea maji, na kufua. Wavuvi huwa majini kila siku. Na katika joto kali la kitropiki, kwa watoto maji yaweza kuwa kidimbwi cha kuogelea kisichoweza kuepukika.
Kuna Tumaini Gani kwa Wakati Ujao?
Hakuna shaka kwamba watu wenye mioyo myeupe na mashirika wanafanya kazi kwa bidii ili kupigana na kichocho na kwamba maendeleo makubwa yamefanywa. Watafiti hata wanajaribu kutokeza chanjo dhidi ya maradhi haya.
Hata hivyo, matazamio ya kuondosha kabisa maradhi haya ni machache sana. Dakt. M. Larivière asema hivi katika jarida la kitiba la Ufaransa La Revue du Praticien: “Japo mafanikio hayo . . . , maradhi hayo hayapotei kamwe.” Ingawa watu mmoja-mmoja wanaweza kukizuia na kukitibu, suluhisho la ulimwenguni pote la kichocho huenda lisipatikane mpaka ulimwengu mpya wa Mungu uje. Biblia yaahidi kwamba “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.”—Isaya 33:24.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Wanapoingia katika maji yaliyochafuliwa, wanadamu wanaweza kuambukizwa vimelea ambavyo husababisha kichocho