Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Watoto Mashakani Ningependa kutoa shukrani kwa ajili ya mfululizo katika toleo la Aprili 8, 1999, “Watoto Mashakani—Ni Nani Atakayewalinda?” Nafikiri kwamba habari yenye kushtua ya kuwatenda watoto vibaya yapasa ichochee umma daima. Ni wajibu wetu kulinda ulimwengu wa watoto wetu. Endeleeni na kazi yenu nzuri.
P. P., Ofisi ya Mjumbe wa Watoto, Jiji la Roma, Italia
Ni jambo linaloshtua kufikiri kwamba mwanzoni mwa karne ya 21, watoto wengi wangali wanatumikishwa kama watumwa na wanatumiwa kuwaua wengine. Na jambo lililo gumu zaidi kukubali ni uhakika wa kwamba wengi wao hawatazamii kuwa na maisha bora. Kwa mara nyingine tena, Amkeni! limeeleza kwa usahihi hali mbaya ya watoto ulimwenguni.
S. R. B., Brazili
Baada ya miaka 36 ya ndoa, sasa mimi nimemtaliki mume wangu. Niligundua kwamba mume wangu aliwatenda vibaya kingono binti zangu wapendwa kwa miaka mingi. (Hakuwa Mkristo.) Nilipogundua jambo hilo nilifadhaika sana. Hakuna mtu awaye yote aliyeonekana kuwa anaelewa athari za kutendwa vibaya kingono au maumivu yasiyoelezeka yanayowatesa wale wasio na hatia. Kwa hiyo namshukuru Yehova kwa kuwa mmeandika juu ya tatizo hilo linaloenea.
N. M., Marekani
Kuwajali Wazee-Wazee Nilithamini kikweli ile makala “Onyesha Kwamba Unajali.” (Aprili 8, 1999) Watu wengi wazee kwa umri walio katika hospitali za kibinafsi husahauliwa na familia zao. Lakini miezi michache iliyopita, wachache kati yetu tuliamua kuwa na mazungumzo ya Biblia na watu kadhaa katika hospitali moja ya kibinafsi ya mahali hapa. Baadaye, tuliwapigia muziki wa piano na tukaongea nao. Sasa tunapanga kuwazuru kwa ukawaida.
C. V., Marekani
Dhoruba ya Afrika Nina umri wa miaka 12, na ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala “Baada ya Dhoruba, Ukristo Ulidhihirishwa.” (Machi 8, 1999) Nilivutiwa sana na ndugu waliowasaidia wale waliokumbwa na taabu! Jambo hilo lilinikumbusha jinsi ambavyo ndugu zetu waliwasaidia wengine baada ya tetemeko kubwa la dunia la Hanshin huko Japani. Makala hiyo ilinitia moyo kuwa mwenye moyo mkuu na kuwatendea wengine mema.
R. K., Japani
Watoto Wanaolala Asanteni kwa ajili ya makala “Mtoto Alaleje?” (Machi 22, 1999) Mtoto wangu wa kwanza mwenye umri wa miezi miwili na nusu alikufa kutokana na kifo cha ghafula cha watoto (SIDS). Laiti ningekuwa na habari hiyo! Licha ya kwamba nina watoto wengine wawili wa kupendeza, mimi bado huhisi maumivu makali yasiyoelezeka.
A. D., Italia
Kuna hatari kadhaa kubwa zinazosababisha SIDS. (Ona “Kuutazama Ulimwengu” katika toleo la “Amkeni!” la Januari 22, 1997.) Hata hivyo, tatizo la SIDS lingali fumbo la kitiba. Kwa hiyo wazazi ambao mtoto wao alikufa kutokana na SIDS hawapaswi kujilaumu kwa sababu ya msiba huo. Mazungumzo yenye kina juu ya SIDS yaliyo katika toleo letu la Januari 22, 1988, yamethibitika kuwa yenye kufariji kwa wazazi wengi wenye huzuni.—Mhariri.
Maradhi ya Utumbo Mwembamba Tulipokea makala “Kukabiliana na Maradhi ya Utumbo Mwembamba” (Machi 22, 1999) miezi mitatu baada ya kugundua kwamba mtoto wetu wa umri wa miaka sita alikuwa nayo. Katika Urusi maradhi hayo hayajulikani hata kidogo hata na madaktari. Ni jambo lenye kufariji kama nini kwamba ndugu na dada zetu Wakristo wataelewa kwa nini binti yetu anakula mlo maalum! Makala hii imetuimarisha na kutuhakikishia kwamba Yehova huwaandalia mahitaji watu wake daima.
V. P. na L. P., Urusi
Kutaka Vitu Usivyoweza Kupata Ndipo tu nimemaliza kusoma makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Sipati Vitu Ninavyotaka?” (Machi 22, 1999) Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala hiyo kwa sababu ilinisaidia kung’amua kwamba siwezi kupata kila kitu ninachotaka. Lakini kama makala hiyo ilivyosema, Yehova anajua mahitaji yetu, na ninafurahi kwamba ninaishi maisha sahili.
C. K., Kanada