Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Babu na Nyanya Asanteni kwa jinsi mlivyoshughulikia habari “Babu na Nyanya—Shangwe Yao, Magumu Yao,” kwa njia ya upendo. (Machi 22, 1999) Mimi ni nyanya asiye na mwenzi na ninalea wajukuu wa kiume wawili. Mama yao alikuwa na bado angali anatumia vibaya dawa za kulevya. Kama makala hiyo ilivyotaja, nilihitaji kukabiliana na hasira ya wavulana hao. Sikuelewa kabisa namna mtu anavyohisi anapoachwa na wazazi wote wawili. Lakini ni mwaka jana tu mjukuu wangu wa kiume aliye mchanga zaidi aliponiambia, “Asante kwa kututunza.” Maneno hayo yalifaa kwa sababu ya jitihada yote niliyofanya na machozi niliyotoa.
D. B., Marekani
Asante kwa upendo na uaminifu wa nyanya yetu mpendwa, mimi na ndugu zangu tulihimili miaka ya kupuuzwa na kutendwa vibaya na wazazi. Kweli za Biblia alizokazia kikiki mioyoni mwetu zilitupa nguvu za kusonga mbele. Leo, wajukuu wake watatu na vitukuu wake saba wote ni Wakristo waliojiweka wakfu.
B. L. B., Brazili
Nina mtoto mwenye umri wa miezi 17, na tumekuwa tukivutana na mama mkwe wangu kuhusu kumtunza. Nilikuwa na wivu sana kiasi cha kwamba singeweza hata kufurahia mikutano ya Kikristo. Hata hivyo, makala hiyo ilinisaidia kuona kwamba hana nia mbaya na kwamba hajaribu kumchukua. Namshukuru Yehova kwamba nilipokea habari hiyo wakati nilipoihitaji sana.
M. Z. C., Mexico
Wana Watano Niliona makala “Namshukuru Yehova kwa Ajili ya Wana Wangu Watano” (Machi 22, 1999) kuwa yenye kupendeza, kwa kuwa kulikuwa na mambo yanayofanana kati ya Helen Saulsbery na mama yangu. Wote wawili walibatizwa mwaka uleule. Sawa na Helen, mama yangu alikaa nyumbani na kututunza wakati familia yetu ilipokuwa na shida nyingi za kiuchumi—kampuni iliyomwajiri baba ilifilisika. Hali kadhalika alitumikia akiwa painia, mweneza-evanjeli wa wakati wote, na sikuzote alitusimulia mambo yaliyoonwa yenye kupendeza kutoka shambani. Jambo hilo lilifanya nivutiwe sana na utumishi wa painia. Sasa kwa kuwa nina binti wawili, naweza kuelewa jitihada ambayo mama alifanya kwa ajili yetu.
M. S., Japani
Natoa shukrani za pekee kwa ajili ya makala hiyo. Kwa vile mimi ni baba, mimi hujaribu kufuata shauri la Biblia, lakini mara nyingi nahisi kuwa nimepungukiwa. Simulizi la familia ya Saulsbery liliniimarisha kusonga mbele.
R. M. R., Brazili
Kutaka Vitu Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 12. Nataka kuwashukuru kwa ajili ya makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Sipati Vitu Ninavyotaka?” (Machi 22, 1999) Kuna vitu ninavyotaka—kama vile baiskeli na gitaa. Lakini baba hawezi kuninunulia vitu hivyo. Jambo hilo hunitamausha. Hata hivyo, makala yenu ilinitia moyo sana. Asanteni kwa kuchapisha shauri hilo linalofanana na la baba.
C. U., Nigeria
Misuli Baada ya kufanya mazoezi asubuhi ya leo, niliketi chini ili nisome makala “Misuli—Kazi Bora ya Ubuni.” (Aprili 8, 1999) Nilipokuwa nikisoma kila ukurasa nilikuwa nikifikiri juu ya misuli ya jicho langu ikisonga, misuli ya mkono wangu ikijibana na kujilegeza nikinywa kahawa kutoka kwenye kikombe, misuli ya miguu yangu ikifanya kazi nilipokuwa nikizunguka kwenye kiti changu. Lo! Ni ajabu ya ubuni iliyoje!
N. T., Belize
Misuli yetu hufunua sehemu ndogo tu ya hekima na akili nyingi ya Muumba wetu Mtukufu, Yehova Mungu. Sikuzote nimevutiwa sana kusoma juu ya mwili wa binadamu. Lakini hii ndiyo mara ya kwanza kusoma makala ya namna hiyo iliyoandikwa vizuri sana na iliyo rahisi kueleweka.
P. J. O. S., Brazili