Mtoto Alaleje?
WATOTO wengi sana ulimwenguni wamekufa kutokana na Ugonjwa wa Kifo cha Ghafula cha Watoto (SIDS). Katika Marekani, ndicho kisababishi cha kawaida cha kifo miongoni mwa watoto wenye umri wa kati ya mwezi 1 hadi 12. Je, kuna njia yoyote ya kupunguza hatari hiyo? Kulingana na jarida The Journal of the American Medical Association (JAMA), uchunguzi wa miaka ya karibuni waonyesha kwamba hatari ya SIDS yaonekana ikipungua zaidi watoto wanapolala chali badala ya kulala kifudifudi. Nchi kadhaa zimeanzisha programu za kutahadharisha wazazi juu ya uhusiano uliopo kati ya namna mtoto alalavyo na SIDS. Katika Australia, Uingereza, Denmark, New Zealand, na Norway, ugonjwa wa SIDS ulipungua kwa angalau asilimia 50 baada ya mwaka mmoja hadi miwili ya kampeni za hadharani za kuchochea kuwalaza watoto chali.
Jinsi mtoto anavyolala kifudifudi kunavyohusiana na SIDS hakujulikani, lakini wachunguzi fulani hudokeza kwamba upande huo wa kumlaza mtoto waweza kumfanya apumue tena pumzi yake aliyoitoa, hivyo kukiongeza kiwango cha kabonidioksidi katika damu yake. Huenda pia mwili wa mtoto ukawa na joto kupita kiasi kwa sababu ya kukosa kuondoa joto anapolala kifudifudi. Kwa vyovyote vile, watoto wachanga waliolazwa chali au kifudifudi huelekea kubaki katika hali hiyo. Uchunguzi pia wadokeza kwamba ni afadhali kumlaza chali mtoto mchanga wa kawaida, mwenye afya kuliko kumlaza kwa upande.
Kwa nini akina mama hupendelea upande mmoja wa kulaza kuliko mwingine? Jarida JAMA hutaarifu kwamba akina mama mara nyingi hufuata tu desturi—huwalaza watoto wao kitandani namna ambavyo mama zao au wengine katika jumuiya yao wangefanya. Au huenda wakapendelea zoea waliloona hospitalini. Pia akina mama fulani huhisi kwamba mtoto wao hupendelea au hulala vema anapolazwa kwa upande hususa. Mama wengi hulaza mtoto chali nyakati zote mwezi wa kwanza kisha hubadili kumlaza kifudifudi baadaye. “Zoea hilo ni lenye kutia wasiwasi,” lasema jarida JAMA, “kwa sababu hatari za kupatwa na SIDS ni kubwa miongoni mwa watoto wachanga wenye umri wa miezi 2 hadi 3.” Madaktari wanajitahidi kuwajulisha wazazi wa watoto wachanga kuhusu wanachosema kuwa ni hatua sahili na yenye matokeo ya kupunguza hatari ya SIDS—kuwalaza chali watoto wachanga wenye afya.a
[Maelezo ya Chini]
a Mtoto akiwa na maradhi ya kupumua au kumwaga mate kusiko kwa kawaida, lingekuwa jambo la hekima kumwona daktari ili akueleze upande mzuri wa kumlaza.