Mambo Ambayo Watunzaji Waweza Kufanya
“SIKUZOTE nimeshangazwa na jinsi [watu] tofauti-tofauti wanavyoweza kukabiliana na hali,” asema Margaret, mtaalamu wa kitiba kutoka Australia ambaye kwa miaka mingi amewashughulikia wagonjwa wa Alzheimer na wale wanaowatunza. “Familia fulani zinakabiliana vizuri chini ya hali ngumu sana,” aendelea kusema, “huku familia nyinginezo ni kama haziwezi kabisa kukabiliana na hali mara tu mgonjwa adhihirishapo badiliko kidogo tu la utu.”—Nukuu kutoka katika kitabu When I Grow Too Old to Dream.
Ni nini hutokeza tofauti hiyo? Jambo moja laweza kuwa ubora wa uhusiano uliokuwapo kabla ya maradhi hayo kuanza. Familia zenye uhusiano wa karibu na wenye upendo hupata ikiwa rahisi kukabili hali hiyo. Na mtu ambaye ana maradhi ya Alzheimer (AD) akitunzwa vizuri, inaweza kuwa rahisi zaidi kushughulikia maradhi hayo.
Japo kudhoofika kwa uwezo wa kiakili, wagonjwa wengi mara nyingi hufanya vizuri mpaka hatua za mwisho kabisa za maradhi hayo iwapo wanatendewa kwa upendo na kwa wororo. “Maneno,” chasema kile kijarida cha mashauri Communication, kilichochapishwa na Shirika la Maradhi ya Alzheimer la London, “si njia pekee ya mawasiliano.” Mawasiliano yasiyohusisha maneno yatia ndani wonyesho mchangamfu na wenye urafiki usoni na sauti ya upole. Jambo muhimu pia ni kumtazama macho na vilevile kusema polepole na kwa wazi—na kutumia jina la mgonjwa mara nyingi.
“Kudumisha mawasiliano na mpendwa wako kunawezekana,” asema Kathy, aliyetajwa katika makala iliyopita, “na ni muhimu pia. Miguso michangamfu na yenye upendo, sauti ya upole na, kuwapo kwako tu kwenyewe kutampa usalama mpendwa wako na kumfariji.” Shirika la Maradhi ya Alzheimer la London lasema hivi kwa ujumla: “Shauku yaweza kuwafanya mwe karibu, hasa wakati mazungumzo yawapo magumu. Kumshika mgonjwa mikono, kuketi nao kama umewawekea mikono, kuzungumza kwa sauti ya uanana au kuwakumbatia ni njia za kuwaonyesha kwamba bado unajali.”
Ikiwa kuna uhusiano mchangamfu, mtunzaji na mgonjwa wanaweza kuangua kicheko pamoja hata wakati makosa yanapofanywa. Kwa mfano, mume mmoja akumbuka jinsi ambavyo mke wake aliyevurugika kiakili alitandika kitanda lakini akatandika blanketi kati ya shiti kimakosa. Waligundua kosa hilo walipoenda kulala usiku huo. “Mpenzi!” mke huyo akasema, “nimekuwa mjinga.” Na wote wakaangua kicheko.
Fanya Maisha Yawe Sahili
Wagonjwa wa AD hufanya vizuri zaidi katika mazingira wanayoyafahamu. Pia wanahitaji mambo ya kawaida kila siku. Kwa sababu hiyo, kalenda kubwa yenye mambo ya kufanywa kila siku yaweza kuwa yenye msaada sana. “Kumhamisha mtu kutoka mahali ambapo amepazoea,” aeleza Dakt. Gerry Bennett, “kwaweza kudhuru sana. Hali zilezile na mwendelezo ni muhimu sana kwa mtu ambaye amevurugika.”
Maradhi hayo yasitawipo, wagonjwa wa AD hupata ikiwa vigumu zaidi kuitikia maagizo. Maagizo yatolewe kwa njia rahisi na ya wazi. Kwa mfano, kumwambia mgonjwa avae nguo laweza kuwa jambo gumu sana. Huenda ikahitajika nguo atakazovaa zipangwe kwa utaratibu na mgonjwa kusaidiwa hatua kwa hatua kuvaa kila nguo.
Uhitaji wa Kuendelea Kuwa Mtendaji
Baadhi ya wagonjwa wa AD hutembea-tembea ndani ya nyumba au kutembea mbali na nyumbani kwao na kupotea. Kutembea-tembea ndani ya nyumba ni mazoezi mazuri kwa mgonjwa na kwaweza kumsaidia kupunguza mkazo na kuboresha usingizi. Hata hivyo, kuondoka nyumbani kwaweza kuhatarisha. Kitabu Alzheimer’s—Caring for Your Loved One, Caring for Yourself chaeleza: “Mpendwa wako akipotea, unakabili hali ya dharura ambayo ni rahisi iwe msiba. Jambo la kukumbuka ni tulia. . . . Watu wanaomtafuta wanahitaji ufafanuzi mzuri wa mtu ambaye wanamtafuta. Uweke nyumbani picha zake za rangi za karibuni.”a
Kwa upande mwingine, wagonjwa fulani huwa wachovu sana na huenda wakataka tu kuketi kitako siku nzima. Jaribu kuwafanya wafanye jambo fulani ambalo nyote wawili mtaweza kufurahia. Mwafanye waimbe, wapige mbinja, au kucheza ala fulani ya muziki. Wengine hufurahia kupiga makofi, kutembea, au kucheza dansi za muziki waupendao. Dakt. Carmel Sheridan aeleza: “Utendaji wenye kufanikiwa sana kwa watu wenye A.D. mara nyingi ni ule unaohusisha muziki. Mara nyingi familia hueleza kwamba muda mrefu baada ya maana ya [mambo] mengine kusahauliwa, mtu wao wa ukoo bado hufurahia nyimbo za kale ambazo alizifahamu.”
“Nilitaka Kufanya Hivyo”
Mke mmoja aishiye Afrika Kusini ambaye mume wake alikuwa katika hatua za mwisho-mwisho za AD alifurahia kukaa naye kila siku katika makao ya kutunzia wagonjwa. Lakini, washiriki wa familia ambao hawakuwa na nia mbaya walimchambua kwa kufanya hivyo. Ilionekana kwao kwamba labda alikuwa akipoteza wakati wake, kwa kuwa mume wake hakuonekana kama anamtambua na hakuwa akisema kamwe. “Lakini,” mke huyo akaeleza baada ya kifo chake, “nilitaka kuwa naye. Wauguzi walikuwa na shughuli nyingi sana, basi alipojichafua, ningeweza kumwosha na kumbadilishia mavazi. Nilifurahia kufanya hivyo—Nilitaka kufanya hivyo. Pindi moja aliumiza mguu wake nilipokuwa nikimsukuma katika kiti chenye magurudumu. Nikauliza, ‘Umeumia?’ akajibu, ‘Ndiyo!’ Nikatambua kwamba bado angeweza kuhisi na kuzungumza.”
Hata katika hali ambazo uhusiano mzuri wa familia haukuwapo kabla ya AD kuanza, watunzaji bado wanaweza kukabiliana na hali.b Kujua tu kwamba wanafanya kilicho sawa na kinachompendeza Mungu kwaweza kuwapa uradhi sana. Biblia yasema, “Heshimuni uso wa mtu mzee” na, “Usimdharau mama yako akiwa mzee.” (Mambo ya Walawi 19:32; Mithali 23:22) Isitoshe, Wakristo wanaamriwa: “Ikiwa mjane yeyote ana watoto au wajukuu, acha hawa wajifunze kwanza kuzoea ujitoaji-kimungu kwa watu wa nyumbani mwao wenyewe na kufuliza kulipa wazazi na babu na nyanya zao fidia ipasayo, kwa maana hili ni lenye kukubalika machoni pa Mungu. Hakika ikiwa yeyote hawaandalii kitu wale walio wake mwenyewe, na hasa kwa ajili ya wale walio washiriki wa nyumbani mwake, ameikana imani naye ni mbaya zaidi kuliko mtu asiye na imani.”—1 Timotheo 5:4, 8.
Kwa msaada wa Mungu, watunzaji wengi wamefaulu kuwatunza vizuri watu wao wa ukoo ambao ni wagonjwa, kutia ndani wale ambao wana maradhi ya Alzheimer.
[Maelezo ya Chini]
a Watunzaji fulani wamepata likiwa jambo lenye kunufaisha kumpa mgonjwa aina fulani ya kitambulisho, labda bangili au mkufu.
b Kwa habari zaidi juu ya utunzaji na jinsi wengine wawezavyo kusaidia, tafadhali ona mfululizo wa makala “Utunzaji—Kukabili Huo Ugumu,” kwenye ukurasa wa 3-13 wa Amkeni! la Februari 8, 1997.
[Sanduku katika ukurasa wa11]
Maradhi ya Alzheimer na Tiba
INGAWA kuna tiba zipatazo 200 ambazo huenda zikatibu Alzheimer (AD) ambazo bado zinachunguzwa kwa wakati huu, bado AD haina tiba. Inaripotiwa kwamba dawa fulani hurekebisha hali ya kupoteza kumbukumbu kwa muda fulani katika hatua za mapema za AD au hupunguza kuendelea kwa maradhi hayo katika wagonjwa fulani. Lakini inahitaji kutahadhari kwa sababu dawa hizo hazifaulu kwa wagonjwa wote, na baadhi ya dawa hizo zaweza kusababisha madhara. Lakini, tiba nyinginezo nyakati nyingine hutumiwa kutibu hali ambazo huandamana na AD, kama vile kushuka moyo, hangaiko, na ukosefu wa usingizi. Kwa kushauriana na daktari wa mgonjwa, kila familia yaweza kupima manufaa na hatari za tiba kabla ya kufanya uamuzi.
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
Jinsi Wageni Wawezavyo Kusaidia
KWA sababu ya kudhoofika kwa uwezo wa akili, watu wenye maradhi ya Alzheimer (AD) hawawezi kuzungumzia matukio ya karibuni kindani. Lakini, kuzungumza juu ya mambo yaliyopita ni tofauti. Kumbukumbu za mambo ya zamani zaweza kudumu, hasa katika hatua za mapema za ugonjwa huo. Wagonjwa wengi wa AD hufurahia kukumbuka wakati wao uliopita. Basi uwaombe wasimulie hadithi wazipendazo, hata kama umezisikia mara nyingi awali. Kwa njia hiyo unachangia furaha ya mgonjwa. Wakati uo huo, unaweza kuwa unampa mtunzaji wake wa kawaida pumziko analohitaji sana. Kwa hakika, kujitolea kumtunza mgonjwa kwa kipindi fulani cha wakati, labda kwa siku nzima, kwaweza kumburudisha sana yule ambaye humtunza kwa ukawaida.
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Kukabiliana na Hali ya Mgonjwa Kutodhibiti Haja
INGAWA kutodhibiti haja huenda “kukaonekana kuwa pigo kali la mwisho,” chasema kijarida cha mashauri Incontinence, “kuna mambo ambayo yaweza kufanywa ili kupunguza tatizo hilo au kufanya lisitokeze mkazo mwingi sana.” Kumbuka kwamba huenda tatizo hilo la kutodhibiti haja lisiendelee daima; huenda tu alivurugika akili au huenda ikawa alifanya polepole kwenda msalani. Isitoshe, huenda mgonjwa anaugua ugonjwa mwingine uwezao kutibiwa unaosababisha hali yake ya kutodhibiti haja, na basi huenda akahitaji kumwona daktari.
Hali ya kutodhibiti haja hata iwe imesababishwa na nini, inaweza kushughulikiwa kwa urahisi ikiwa mgonjwa avalia mavazi ya nje yaliyo rahisi kuvaa na kuvua na suruali zilizoshonwa kufaana na hali yake. Pia litakuwa jambo lenye kunufaisha ikiwa utaweka matandiko yenye kuzuia haja kwenye kitanda na viti. Epuka kuwasha ngozi na kutokeza vidonda kwa kuhakikisha kwamba vitu vya plastiki havigusani na ngozi ya mgonjwa. Pia, osha mgonjwa kwa maji yenye joto na sabuni na kumpangusa kabisa kabla ya kumvalisha nguo. Ondoa vitu ambavyo huenda vikamzuia mgonjwa asiende upesi na kwa usalama msalani. Huenda ikafaa kuacha taa ya usiku ikiwaka ili asipotee. Kwa sababu huenda mgonjwa akawa hana usawaziko mzuri wakati huu, weka kitu cha kushikilia mahali pafaapo ambacho kitamsaidia kwenda msalani bila matatizo mengi.
“Ikiwa unaweza kuwa mcheshi pia,” ladokeza Shirika la Maradhi ya Alzheimer la London, “huenda hiyo ikaondoa mkazo.” Mtunzaji aweza kukabilije magumu hayo? Mtunzaji mmoja mwenye uzoefu ajibu: “Saburi, uungwana, fadhili, na upole wa hisani zitamsaidia mgonjwa adumishe hadhi yake nyakati zote, bila hofu ya kuaibika au kuona haya.”
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Je, Mgonjwa Ahamishwe?
KWA kusikitisha, kuendelea kudhoofika kwa hali ya watu wenye Alzheimer (AD) kunaweza kuhitaji wahamishwe kutoka nyumbani kwao hadi kwenye nyumba ya mtu wa ukoo au makao ya kutunzia wagonjwa. Lakini, kabla ya kufanya uamuzi wa kumhamisha mgonjwa kutoka kwenye mazingira anayofahamu, ni vizuri kufikiria mambo fulani muhimu.
Anaweza kuvurugika sana akili kwa sababu ya kuhama. Dakt. Gerry Bennett atoa mfano wa mgonjwa ambaye alikuwa amependa kutembea-tembea nje na nyakati nyingine kupotea. Lakini, bado alifaulu kuishi peke yake. Lakini, familia yake ikaamua kwamba anapaswa kuhamishwa aishi karibu nao ili wamtunze kwa njia bora zaidi.
“Kwa ubaya,” aeleza Dakt. Bennett, “hakukubali kamwe makao yake mapya. . . . Kwa kusikitisha hakupazoea hapo mahali papya, na kwa kweli walimfanya awategemee zaidi kwa sababu sasa hangeweza kufanya lolote katika mazingira hayo mapya. Hakufahamu jikoni na hakuweza kukumbuka njia mpya ya kuelekea msalani, akawa anajiendea haja. Kutokana na nia nzuri matokeo yakawa msiba na hatimaye ikalazimika atunzwe katika makao fulani.”—Alzheimer’s Disease and Other Confusional States.
Lakini, namna gani ikionekana kwamba hakuna namna ila tu kumhamisha kwenye makao ya kuwatunza? Huo si uamuzi rahisi kamwe. Kwa hakika, umefafanuliwa kuwa “mojawapo ya [maamuzi] yenye kutokeza hisia ya hatia zaidi” ambazo watunzaji hupata, mara nyingi wakihisi kwamba wamemtamausha na wamemtupa mpendwa wao.
“Ni jambo la kawaida kuhisi hivyo,” asema muuguzi mmoja mwenye uzoefu sana wa kutibu wagonjwa wa AD, “lakini ni hatia isiyofaa.” Kwa nini? “Kwa sababu” yeye ajibu, “utunzaji na usalama wa [mgonjwa] ungekuwa jambo kuu la kufikiriwa.” Madaktari Oliver na Bock wakubali: “Uamuzi wa kwamba mtu ameshindwa kabisa kihisia-moyo na kwamba maradhi hayo yameenea kufikia hatua ambayo inafanya iwe vigumu sana kumtunza mgonjwa nyumbani ni mojawapo ya uamuzi ulio mgumu zaidi kufanya.” Lakini, baada ya kupima mambo yote yanayohusika katika hali hususa, watunzaji fulani huenda bado wakakata kauli ya kwamba “kumpeleka mgonjwa katika makao ya kuwatunzia wagonjwa ni . . . bora zaidi kwa mgonjwa.”—Coping With Alzheimer’s: A Caregiver’s Emotional Survival Guide.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Msaidie mgonjwa aelewe mambo yanayoendelea kila siku