Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 9/22 kur. 26-27
  • “Gazeti Hili la Amkeni! Liliandikwa kwa Ajili Yetu Haswa”!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Gazeti Hili la Amkeni! Liliandikwa kwa Ajili Yetu Haswa”!
  • Amkeni!—1999
  • Habari Zinazolingana
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
  • Kuhifadhi Hadhi ya Mgonjwa
    Amkeni!—1998
  • Mambo Ambayo Watunzaji Waweza Kufanya
    Amkeni!—1998
  • Kukabili Maradhi ya Alzheimer
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 9/22 kur. 26-27

“Gazeti Hili la Amkeni! Liliandikwa kwa Ajili Yetu Haswa”!

TOLEO la Amkeni! la Septemba 22, 1998 lilikazia mfululizo wa makala “Maradhi ya Alzheimer—Kupunguza Maumivu.” Wasomaji kadhaa walionyesha uthamini mkubwa kwa madokezo yenye kusaidia yaliyokuwa katika mfululizo huo. Yafuatayo ni baadhi ya maelezo yao.

“Tangu mume wangu alipochunguzwa na kupatikana ana maradhi ya Alzheimer zaidi ya miaka miwili iliyopita, nimesoma mambo mengi kuhusu habari hiyo. Amkeni! lilikuwa na habari bora. Lilitoa muhtasari wa habari zote nilizokuwa nimesoma. Tulitoa nakala hizo kwa madaktari pamoja na watu wengineo kwenye hospitali ambapo mume wangu amelazwa.”—M. L., Marekani.

“Mama alikufa miaka miwili iliyopita, akiwa na umri wa miaka 83. Alikuwa Shahidi mwaminifu tangu mwaka wa 1937. Ilihuzunisha sana kuona kumbukumbu na mwili wake ukizorota. Asanteni kwa habari hiyo yenye mafaa na inayofariji. Makala hizi zitakuwa zenye thamani sana katika kuwasaidia wanaougua na wale wanaowatunza kukabiliana na hali ya msiba na inayotisha.”—D. C., Marekani.

“Daktari wao na wataalamu wengineo wanaona kwamba mama yangu pamoja na dada yake wana maradhi ya Alzheimer, kwa hiyo nikampelekea mjomba wangu gazeti hilo. Aliitikia: ‘Kwa kutumia kompyuta yangu, nilipata habari nyingi sana juu ya AD [maradhi ya Alzheimer]—nyingi sana hivi kwamba sina wakati wa kuzichunguza zote. Nilisoma makala za Amkeni! juu ya AD mlizoniletea, na ninaweza kusema kwa unyofu kwamba zina kiasi kinachofaa cha habari, iliyoandikwa kwa njia yenye kueleweka pia! Je, naweza kuwapa washiriki wengine wa familia baada ya kulisoma tena?’”—B. E., Kanada.

“Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo cha uuguzi, na ningependa kuwapongeza kuhusu mfululizo wenu juu ya AD. Ulitoa madokezo mengi ya kisasa yaliyosadifiana na mihadhara yetu ya Sayansi Inayohusu Uzee na Alzheimer. Ninapanga kutumia makala hizi ninapowatunza wagonjwa wangu na ninapowasaidia wale wanaowatunza.”—G. L., Marekani.

“Mama yangu alikufa Agosti 18, 1998. Nilipokea gazeti hilo juma hilohilo. AD ni maradhi yanayoumiza hisia-moyo sana, hasa mwishoni—si kwa wale wanaougua tu bali pia kwa wapendwa wao. Bila shaka, makala hizo zathibitisha kwamba Yehova anaona yale tunayokabili. Tunathamini sana msaada wake wenye upendo!”—M. S., Marekani.

“Nataka kuwashukuru kwa moyo mkunjufu kwa ajili ya makala hizi. Ninasoma ili niwasaidie watu walio na maradhi haya. Kwa kweli habari hiyo inanifaa sana.”—T. N., Italia.

“Nyanya yangu, aliye na kichaa, ameishi nami kwa mwaka mmoja uliopita. Hali yake imekuwa mbaya zaidi na amekuwa mkali na mwenye uhasama mwingi kunielekea. Nilihisi kana kwamba nilikosea familia yetu na Yehova. Baada ya kusoma makala zenu, niliweza kutambua makosa yangu na kuona jinsi ambavyo ningeweza kubadili mtazamo wangu kuhusu hali yake. Sasa naona jinsi lilivyo jambo la maana kumwonyesha ufikirio kwa ajili ya kupungukiwa kwake.”—S. S., Marekani.

“Kwa miaka mingi, mimi na mume wangu tulikuwa mapainia, waeneza-evanjeli wa wakati wote. Tulihuzunika tulipolazimika kuacha, lakini tulihitaji kusaidia kumtunza mama yangu. Nimesoma vitabu na makala nyinginezo zinazohusu maradhi ya Alzheimer, lakini moyo wangu uliguswa sana nilipopokea habari yenye mafaa kutoka kwa tengenezo la Yehova. Nitaweka makala hizi karibu ili niweze kuzisoma mara nyingi.”—P. M., Marekani.

“Nina umri wa miaka 12. Ninapendezwa na makala kuhusu maradhi ya Alzheimer kwa sababu baba ya babu yangu alikuwa na maradhi haya na ndivyo na dada mpendwa Mkristo mwenye umri mkubwa ninayemjua. Makala hizo zilinisaidia kuona jambo ninaloweza kufanya, na zilinipa uelewevu bora wa maradhi haya. Nitafurahi kama nini siku ifikapo wakati ‘hakuna mwenyeji atakayesema: Mimi mgonjwa’!” (Isaya 33:24)—P. W., Marekani.

“Mimi na binti yangu mwenye umri wa miaka 15 tulizungumzia mara moja mambo makuu ya toleo hilo. Mapendekezo ya kuwa na uso mkunjufu, kuzungumza kwa sauti yenye kuliwaza, kuhifadhi hadhi ya mgonjwa kwa kutomsahihisha, na kadhalika, yalikuwa yenye manufaa hasa. Ninatumaini kugawanya gazeti hili kwa wafanyakazi wanaowatunza watoto mchana.”—Y. K., Japani.

“Hatuwezi kueleza jinsi familia yetu inavyothamini makala zenu za ajabu. Mama-mkwe wangu aliposhindwa kujitunza, tulimleta Marekani aishi pamoja nasi. Alikuwa na umri wa miaka 80, na badiliko hilo lilimvuruga kabisa. Hatukuelewa kwa nini hali yake ilizorota mpaka tuliposoma makala zilizo katika Amkeni! Ufafanuzi kamili wa ugonjwa huo na jinsi ya kushughulika na mgonjwa ulijibu maswali mengi ambayo hata madaktari wake hawakuweza kujibu. Tafadhali pokeeni shukrani zetu, na Yehova aendelee kubariki jitihada zenu za kutusaidia sote.”—O. S., Marekani.

“Ningependa kuwapongeza kwa makala hizi zinazoeleza mambo kikamili. Zilikuja wakati tulipohitaji kumtunza nyanya yetu. Familia yetu iliona kwamba gazeti hili la Amkeni! liliandikwa kwa ajili yetu haswa kwa sababu lilitufariji na kutupa msaada tulipouhitaji. Asanteni kwa makala kama hizi. Huja kwa wakati wake daima.”—R. N., Zambia.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki