Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kuwafundisha Watoto Wapende Uumbaji Sehemu inayohusika katika kuwazoeza watoto wetu ni kujaribu kusitawisha uthamini wao kuelekea uzuri wa mambo ya asili ambao Yehova huandaa kwa upendo. Tunapenda kutumia makala ambazo hutokea kwa ukawaida katika Amkeni!, kama vile “Jenny Wren—Ndege Mdogo, Mwenye Sauti Kubwa.” (Septemba 8, 1998) Watoto wetu huitikia kwa shauku! Inafurahisha kuwafundisha habari hizi.
K. A., Marekani
Ndoto za Kutisha Kwa kweli nilithamini madokezo katika “Kuutazama Ulimwengu,” kuhusu “Ndoto za Kutisha Ni Kawaida kwa Watoto.” (Septemba 8, 1998) Watoto wangu huwa na ndoto za kutisha, lakini sikuzote nimewaambia wasizungumze kuzihusu bali warudi wakalale. Sasa, kukiwa na madokezo hayo, ninaweza kukabiliana na tatizo hili kwa njia bora. Tafadhali msiache kuchapisha habari kama hiyo yenye kusaidia.
R. N., Zimbabwe
Simba Wauaji Kwa kweli nilifurahia makala “‘Reli ya Kichaa’ ya Afrika Mashariki.” (Septemba 22, 1998) Lakini mlikosea kwa kuorodhesha simba wala-watu kuwa wa kiume na wa kike. Wote walikuwa wa kiume.
K. B., Marekani
Gazeti la “Amkeni!” lilikosea kuhusu habari hii, na tunathamini ufafanuzi huo.—Mhariri.
Maradhi ya Alzheimer Ninaongoza kikundi cha watafiti wa maradhi ya Alzheimer wa kampuni moja kubwa ya dawa. Hivyo nilisoma kwa upendezi mwingi makala yenu mfululizo yenye kutokeza yenye kichwa “Maradhi ya Alzheimer—Kupunguza Maumivu.” (Septemba 22, 1998) Nilivutiwa sana na jinsi mlivyoshughulikia kikamilifu tatizo hili la afya ya umma ambalo limeenea kote. Na nikiwa mzee wa kutaniko, nimeona shauri lenye kutumika katika makala hizi kuwa lenye thamani kubwa sana.
S. S., Marekani
Makala hizo ziligusa moyo wangu kwa sababu mama yangu amekuwa akiugua maradhi ya Alzheimer kwa muda unaozidi miaka kumi. Nawashukuru kutoka moyoni kwa kushughulikia habari hii kwa njia ya busara na yenye kustahi wale wanaougua maradhi haya.
E. M., Italia
Mfanyakazi mwenzangu ambaye ameandikisha Amkeni! alinipa toleo hili kwa sababu baba yangu ana maradhi ya Alzheimer. Niliguswa hasa na ile makala “Kuhifadhi Hadhi ya Mgonjwa.” Hiyo ni hoja kubwa sana. Asanteni kwa madokezo ya wakati unaofaa. Nina hakika kwamba makala hizi zimesaidia watu wengi.
M. P., Kanada
Nataka kuwashukuru kutoka moyoni kwa ajili ya makala hizo. Tangu mama yangu alipopimwa na kupatikana kuwa na maradhi ya Alzheimer mnamo mwaka wa 1986, tumesoma vichapo vingi juu yake. Hata hivyo, makala zenu zilishinda kwa mbali habari yoyote ambayo tumesoma kuhusu uchangamshi, kuwa na hisia, na hisia-mwenzi. Mnasema ukweli kabisa kwamba wale wanaougua maradhi ya Alzheimer wanahitaji upendo na utunzaji mwororo, hadi wanapofikia hatua ya mwisho. Mama yangu hawezi kula wala kuongea. Lakini makala hizo hutupatia nguvu za kumwonyesha upendo na shauku hata zaidi.
H. E., Austria
Nikiwa msimamizi wa Shirika la Brazili la Maradhi ya Alzheimer, nataka kuwapongeza kwa makala hizo. Mlifafanua kwa njia iliyo wazi maradhi ya Alzheimer na jinsi yanavyoathiri familia. Mlikuwa waangalifu kustahi hadhi ya mgonjwa, na mlitoa masimulizi ya watu wanaohusika mkionyesha kwamba bado upendo ndio tiba bora.
V. C., Brazili