Kuhifadhi Hadhi ya Mgonjwa
SIKU mbili kabla ya Sally kumpeleka mume wake kumwona daktari wa ubongo, waziri mkuu mpya alichaguliwa nchini Afrika Kusini. Daktari huyo alipomwuliza Alfie kuhusu matokeo ya uchaguzi, Alfie alimtazama tu na kushindwa kujibu. Kisha, baada ya kumchunguza ubongo, daktari huyo akasema kwa njia isiyo ya fadhili: “Mtu huyu hata hawezi kujua jibu la mbili kuongezea mbili. Ubongo wake umekwisha!” Kisha akamshauri Sally: “Fanya mipango yako ya kifedha. Mtu huyu anaweza kukugeuka na kuwa mjeuri.”
“Hawezi kamwe!” Sally akajibu, “mume wangu hawezi kufanya hivyo!” Sally alisema kweli; Alfie hakupata kuwa mjeuri kwake, hata ingawa baadhi ya watu ambao wana maradhi ya Alzheimer (AD) huwa wakali. (Mara nyingi hiyo hutukia kwa sababu ya mfadhaiko, ambao nyakati nyingine waweza kupunguzwa kwa kumshughulikia vizuri mgonjwa wa AD.) Ingawa huyo daktari alifaulu kugundua ugonjwa wa Alfie, kwa wazi yeye hakujua kwamba kuna uhitaji wa kuhifadhi hadhi ya mgonjwa. La sivyo, yeye angemweleza Sally kwa fadhili hali ya Alfie faraghani.
“Uhitaji muhimu zaidi wa watu wenye kasoro za akili ni kuhifadhi hadhi yao, heshima na kujistahi,” chasema kitabu When I Grow Too Old to Dream. Njia muhimu ya kuhifadhi hadhi ya mgonjwa inaelezwa katika kijarida cha mashauri kiitwacho Communication, ambacho kimechapishwa na Shirika la Maradhi ya Alzheimer la London: “Usizungumze kamwe juu ya [wagonjwa wa AD] mbele ya watu wengine kana kwamba hawapo. Hata kama hawaelewi unayosema, wao waweza kuhisi kwamba wanapuuzwa kwa njia fulani na wahisi wameshushiwa hadhi.”
Kuna uhakika kwamba baadhi ya wagonjwa wa AD huelewa mambo ambayo wengine husema juu yao. Kwa mfano, mgonjwa mmoja kutoka Australia alienda na mke wake kwenye mkutano mmoja wa shirika la kuwasaidia wagonjwa wa Alzheimer. Baadaye alisema hivi: “Walikuwa wakiwafundisha watunzaji mambo ya kufanya na jinsi wapaswavyo kuyafanya. Nilishtuka kwa sababu mimi nilikuwapo na hakuna mtu aliyezungumza juu ya mgonjwa. . . . Nilifadhaika sana. Eti kwa sababu nina Alzheimer, yale niyasemayo hayafai: hakuna mtu atakayesikiliza.”
Uwe na Maoni Mazuri
Kuna njia nyingi nzuri za kuwasaidia wagonjwa wahifadhi hadhi yao. Wao waweza kuhitaji msaada wa kuendelea na kazi zao za kila siku ambazo zamani zilikuwa rahisi. Kwa mfano, ikiwa zamani walikuwa wanapenda kuandika barua, basi labda unaweza kuketi nao na kuwasaidia kujibu barua kutoka kwa marafiki wenye kuwahangaikia. Katika kitabu Alzheimer’s—Caring for Your Loved One, Caring for Yourself, Sharon Fish ataja njia nyinginezo za kuwasaidia wagonjwa wa AD: “Tafuta mambo rahisi mnayoweza kufanya pamoja na ambayo ni yenye maana na yenye matokeo: kuosha na kukausha vyombo, kufagia, kukunja nguo na kupika.” Kisha aelezea hivi: “Mgonjwa wa Alzheimer huenda asiweze kusafisha nyumba nzima au kupika mlo wote, lakini polepole yeye hupoteza uwezo wa kufanya hayo. Unaweza kutumia uwezo ambao bado wanao na kuwasaidia kuutumia kwa muda mrefu iwezekanavyo. Ukifanya hivyo, pia unasaidia kuhifadhi kujistahi kwa mpendwa wako.”
Baadhi ya kazi zinazofanywa na wagonjwa wa AD hazitakuwa bora, basi huenda ukahitajika kufagia tena au kuosha vyombo tena. Lakini, kwa kumfanya mgonjwa aone kwamba anatumika, unamwezesha aridhike maishani. Mpongeze hata kama hajafanya kazi nzuri. Kumbuka kwamba yeye amefanya kadiri awezavyo kwa sababu ya ugonjwa wake. Wagonjwa wa AD huhitaji kukumbushwa nyakati zote kwamba wanathaminiwa na kupongezwa—na hata zaidi wazidipo kudhoofika na kushindwa kutimiza utendaji mbalimbali. “Wakati wowote ule—bila kutarajiwa kabisa wanaweza kulemewa na hisia ya kujiona kuwa wao ni bure tu. Mtunzaji ahitaji kumtuliza mara moja kwa kumliwaza kwamba ‘anaendelea vizuri.’” Asema Kathy, ambaye mume wake mwenye umri wa miaka 84 ana AD. Kitabu Failure-Free Activities for the Alzheimer’s Patient chakubali: “Sisi sote tunahitaji kusikia kwamba tunafanya vizuri, na kwa watu wenye kasoro za akili, uhitaji huo ni wenye nguvu hata zaidi.”
Jinsi ya Kushughulikia Tabia Zenye Kuaibisha
Watunzaji wanapaswa kujifunza jinsi ya kushughulikia tabia zenye kuaibisha za mpendwa wao. Mojawapo ya hofu kubwa zaidi ni kwamba mgonjwa hatadhibiti haja mbele ya watu. “Vitendo hivyo havitukii kwa ukawaida navyo vyaweza kuzuiwa ama kupunguzwa. Pia mtu apaswa kufikiria mambo kihalisi, kwa kuwa si tendo lenyewe wala watu wanaotazama wapaswao kuwa hangaiko bali ni kupoteza hadhi kwa mtu mwenye AD.” Aeleza Dakt. Gerry Bennett katika kitabu chake Alzheimer’s Disease and Other Confusional States.
Kisa kama hicho chenye kuaibisha kikitukia, usimzomee mgonjwa. Badala yake, jaribu kufuata shauri hili: “Tulia na uone mambo kihalisi na ukumbuke kwamba mtu huyo hafanyi hivyo kimakusudi. Isitoshe, wao huelekea zaidi kusikiliza ikiwa wewe ni mpole na mwenye udhibiti kuliko kama umekasirika na kukosa subira. Fanya yote uwezayo ili kufanya kisa hicho kisiharibu uhusiano wako na mgonjwa.”—kijarida cha mashauri cha Incontinence, cha Shirika la Maradhi ya Alzheimer ya London.
Je, Kweli Wao Wanahitaji Kusahihishwa?
Mara nyingi wagonjwa wa AD husema mambo yasiyo sahihi. Kwa mfano, wao waweza kusema kwamba wanatarajia ziara kutoka kwa mtu wa ukoo ambaye alikufa zamani. Au wao waweza kuota mambo, wakiona vitu ambavyo viko tu akilini mwao. Je, sikuzote inahitajika kumsahihisha mgonjwa wa AD kwa kukosea katika usemi?
“Kuna wazazi ambao hawakomi kuwasahihisha watoto wao kila wakati wanapotamka neno vibaya au wanapokosea kisarufi. . . . Mara nyingi mtoto hukasirika au kujitenga kwa sababu anaona jitihada zake za kujieleza zinakandamizwa na hazithawabishwi. Ndivyo inavyotokea kwa mgonjwa wa AD ambaye hukosolewa daima.” Aelezea Robert T. Woods katika kitabu chake Alzheimer’s Disease—Coping With a Living Death. Kwa kupendeza, Biblia inashauri hivi juu ya jinsi ya kuwatendea watoto: “Nyinyi akina baba, msiwe mkichochea watoto wenu wakasirike, ili wasishuke moyo.” (Wakolosai 3:21) Ikiwa watoto huchokozeka kwa sababu ya kukosolewa daima, sembuse mtu mzima! “Kumbuka kwamba mgonjwa ni mtu mzima ambaye ana uhuru wake na matimizo yake,” ndivyo inavyotahadharisha ARDA Newsletter ya Afrika Kusini. Kukosoa-kosoa mgonjwa wa AD kunaweza kumkasirisha na vilevile kumfanya ashuke moyo au hata awe mkali.
Tunaweza kupata somo kutokana na Yesu Kristo litakalosaidia wale wanaoshughulika na wagonjwa wa AD. Yeye hakuwa akisahihisha mara hiyo kila maoni yenye makosa ya mitume wake. Kwa hakika, nyakati nyingine yeye hakuwaambia mambo fulani kwa sababu bado hawangeweza kuyaelewa. (Yohana 16:12, 13) Ikiwa Yesu alifikiria mapungufu ya wanadamu wenye afya, sisi tunapaswa hata zaidi kupatana na maoni ya kiajabu-ajabu lakini ambayo hayadhuru ya mtu mzima ambaye ni mgonjwa sana! Kujaribu kumfanya mgonjwa aone ukweli wa jambo fulani hususa ni kutarajia—au kudai—zaidi ya mtu huyo awezavyo. Badala ya kubishana, mbona usinyamaze au ubadilishe mazungumzo kwa njia ya busara?—Wafilipi 4:5.
Nyakati nyingine, jambo lenye upendo zaidi laonekana ni kukubaliana na maono ya mgonjwa badala ya kujaribu kumsadikisha kwamba hayo si ya kweli. Kwa mfano, mgonjwa wa AD aweza kufadhaishwa kwa sababu “anaona” mnyama mkali au mtu fulani nyuma ya pazia. Huo si wakati wa kujaribu kusababu naye kiakili. Kumbuka kwamba ‘anachoona’ akilini mwake ni kitu halisi kwake, na basi haifai hofu zake za kweli zipuuzwe. Huenda ukahitaji kuchunguza nyuma ya pazia na kusema, “‘Ukimwona’ tena, niambie ili nikusaidie.” Kwa kutenda kwa kupatana na maoni ya mgonjwa, waeleza Madaktari Oliver na Bock katika kitabu chao Coping With Alzheimer’s: A Caregiver’s Emotional Survival Guide, “unampa hisia ya kushinda vitu vyenye kutisha na kuhofisha ambavyo akili yake inafanyiza. . . . Anajua kwamba anaweza kukutegemea.”
“Sisi Sote Hujikwaa Mara Nyingi”
Inaweza kuwa jambo gumu kutumia madokezo hayo yote ambayo yametajwa, hasa kwa wale ambao wana mzigo mzito wa kazi na madaraka mengine ya familia. Pindi kwa pindi, mtunzaji mwenye kufadhaika aweza kukasirika na kushindwa kumtendea mgonjwa wa AD kwa hadhi. Hilo litukiapo, usijiruhusu kamwe ulemewe na hisia ya hatia. Kumbuka kwamba kwa sababu ya hali ya maradhi hayo, labda mgonjwa atasahau kisa hicho haraka sana.
Pia mwandikaji wa Biblia Yakobo asema: “Sisi sote hujikwaa mara nyingi. Ikiwa yeyote hajikwai katika neno, huyu ni mtu mkamilifu.” (Yakobo 3:2) Kwa kuwa hakuna mtunzaji wa kibinadamu aliye mkamilifu, mtunzaji aweza kufanya kosa anapofanya kazi hiyo ngumu ya kumtunza mgonjwa wa AD. Katika makala ifuatayo, tutafikiria mambo mengine ambayo yamewasaidia watunzaji wakabiliane na hali ya kumtunza mgonjwa wa AD na hata kufurahia kumtunza.
[Blabu katika ukurasa wa 9]
Wagonjwa hufanya vizuri wakifarijiwa daima na kupongezwa
[Blabu katika ukurasa wa 9]
‘Mgonjwa aweza kuelewa mazungumzo. Basi usizungumze juu ya hali yake au kusema mambo yasiyofaa kando ya kitanda chake’
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Je, Umwambie Mgonjwa?
WATUNZAJI wengi hujiuliza kama wanapaswa kumwambia mpendwa wao kwamba ana maradhi ya Alzheimer (AD). Ukiamua kumwambia, basi utamwambiaje na wakati gani? Kijarida fulani cha habari cha Shirika la Alzheimer na Matatizo Yanayohusika Nayo cha Afrika Kusini kilikuwa na maelezo haya yenye kupendeza kutoka kwa msomaji mmoja:
“Mume wangu ameugua Alzheimer kwa miaka saba hivi. Sasa ana umri wa miaka 81, na kwa uzuri hadhoofiki haraka . . . Kwa muda mrefu niliona ni vibaya mno kumwambia kwamba ana Alzheimer na basi tukawa tunakubaliana tu na usemi wake wenye ‘udhuru’: ‘Hutarajii mzee mwenye umri wa miaka 80 afanye mambo sawasawa!’”
Kisha msomaji huyo akarejezea kitabu kilichopendekeza kwamba mgonjwa aambiwe kwa njia ya fadhili na sahili kuhusu maradhi aliyo nayo. Lakini mke huyo aliogopa kwa sababu alihofu jambo hilo lingemvunja moyo sana mume wake.
“Kisha siku moja,” akaendelea kusema, “mume wangu alitaja kwamba aliogopa kujiaibisha mbele ya marafiki wake. Nikatwaa fursa hiyo! Basi (huku nikitoka jasho jembamba) nilipiga magoti kando yake na kumwambia kwamba alikuwa na Alzheimer. Bila shaka hakujua Alzheimer ni kitu gani, lakini nikaeleza kwamba hayo ni maradhi ambayo yalikuwa yakifanya iwe vigumu kwake kufanya [mambo] ambayo sikuzote alikuwa akifanya kwa urahisi, na pia yalikuwa yakimfanya asahau mambo upesi. Nikamwonyesha sentensi mbili tu katika broshua yenu Alzheimer’s: We Can’t Ignore It Anymore: ‘Maradhi ya Alzheimer ni tatizo la ubongo linalosababisha kupoteza kumbukumbu na kudhoofika kubaya kwa akili . . . Hayo ni maradhi wala SI HALI YA KAWAIDA YA KUZEEKA.’ Pia nilimhakikishia kwamba marafiki wake walijua ana maradhi hayo na basi wanaelewa hali yake. Akafikiri kidogo, kisha akapaaza sauti: ‘Hayo ni mambo mapya ajabu! Kwa kweli hayo yanasaidia!’ Mnaweza kuwazia jinsi nilivyohisi nilipoona amefarijika sana baada ya kumjulisha hali yake!
“Na sasa, wakati wowote ambapo anaonekana kukasirikia jambo fulani, naweza kumkumbatia na kumwambia ‘Kumbuka, si kosa lako. Ni hiyo Alzheimer mbovu inayofanya mambo yawe magumu kwako,’ naye hupoa mara moja.”
Bila shaka, kila kisa cha AD ni tofauti. Pia, mahusiano kati ya watunzaji na wagonjwa hutofautiana. Basi kumwambia au kutomwambia mpendwa wako kwamba ana AD ni uamuzi wa kibinafsi.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Je, Kweli Haya Ni Maradhi ya Alzheimer?
MZEE akipatwa na hali mbaya ya kuvurugika akili, usikate kauli mara moja ya kwamba ana maradhi ya Alzheimer (AD). Mambo mengi, kama vile kufiwa, kuhamia kwa ghafula nyumba mpya, au maambukizo, yaweza kumfanya mzee avurugike akili. Mara nyingi kuvurugika akili kwa wazee kwaweza kuponyeshwa.
Hata kwa wagonjwa wa AD, kuzorota kwa ghafula kwa hali ya mgonjwa, kama vile kushindwa kudhibiti haja, huenda kusisababishwe na tatizo la AD. Maradhi ya AD hudhoofisha polepole. “Kuzorota kwa ghafula,” chaeleza kitabu Alzheimer’s Disease and Other Confusional States, “mara nyingi humaanisha kwamba kuna maambukizo mabaya (kama vile ya kifua au ya mkojo) ambayo yametokea. Kikundi cha wagonjwa wa [AD] huonekana kudhoofika haraka zaidi . . . Lakini, wengi wao hawadhoofiki haraka, hasa kama mtu huyo anatunzwa vizuri na matatizo mengine ya kitiba yanashughulikiwa mapema na kwa njia ifaayo.” Kutodhibiti haja kwa mgonjwa wa AD huenda kukasababishwa na matatizo mengine ya kiafya ambayo yanaweza kutibiwa. “Sikuzote hatua ya kwanza ni kumwona [daktari],” chaeleza kijarida cha kutoa shauri cha Incontinence, ambacho kimechapishwa na Shirika la Maradhi ya Alzheimer la London.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuwasaidia wagonjwa wa Alzheimer kwa kazi za kila siku huhifadhi hadhi zao