Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 9/22 kur. 3-4
  • Kukabili Maradhi ya Alzheimer

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kukabili Maradhi ya Alzheimer
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Alzheimer Ni Maradhi Gani?
  • Kuhifadhi Hadhi ya Mgonjwa
    Amkeni!—1998
  • Mambo Ambayo Watunzaji Waweza Kufanya
    Amkeni!—1998
  • “Gazeti Hili la Amkeni! Liliandikwa kwa Ajili Yetu Haswa”!
    Amkeni!—1999
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 9/22 kur. 3-4

Kukabili Maradhi ya Alzheimer

“MUME wangu, Alfie, alikuwa msimamizi katika mojawapo ya machimbo ya dhahabu ya Afrika Kusini,” aeleza Sally. “Nilishtuka aliponiambia kwamba alitaka kustaafu. Alikuwa na umri wa miaka 56 pekee na pia alikuwa mwerevu na mwenye bidii ya kazi. Baadaye, nilisikia kutoka kwa wafanyakazi wenzake kwamba Alfie alikuwa ameanza kufanya makosa yasiyo ya kawaida kazini. Mara nyingi walifunika makosa hayo.

“Alipostaafu, tulinunua hoteli. Kwa kuwa Alfie alijua mambo mengi ya kiufundi, tulifikiri kwamba angejishughulisha akirekebisha mahali hapo. Lakini, badala yake, sikuzote yeye alimwita fundi.

“Mwaka uo huo tulimpeleka mjukuu wetu mwenye umri wa miaka mitatu kutembelea ufuo katika Durban. Yeye alipenda mchezo wa kurukia turubali iliyokuwa ng’ambo tu ya barabara kutoka nyumba tuliyokaa. Alasiri moja, yapata saa 10:30, Alfie alimpeleka arukie turubali akisema kwamba wangerudi baada ya nusu-saa. Kufika saa 1:00 jioni hawakuwa wamerudi. Nikawapigia simu polisi, lakini wakasema kwamba wao hawatafuti watu waliopotea mpaka muda wa saa 24 uwe umepita tangu wakati walipotoweka. Usiku huo karibu nishikwe na kichaa, nikawaza na kuwazua kwamba wameuawa. Adhuhuri hivi siku iliyofuata, mtu alibisha mlango, kumbe ni Alfie akiwa amembeba mjukuu wetu.

“‘Mlikuwa wapi?’ nikauliza.

“‘Usinikasirikie,’ akajibu. ‘Sijui.’

“‘Bibi,’ akaeleza mjukuu wetu, ‘tulipotea.’

“Ebu wazia kwamba walipotea ng’ambo tu ya barabara! Bado sijui walilala wapi usiku huo. Lakini, rafiki yangu mmoja aliwapata na kuwaelekeza nyumbani.”

Baada ya kisa hicho, Sally alimpeleka Alfie kwa daktari wa ubongo, ambaye alithibitisha kwamba Alfie alikuwa na kasoro akilini. Kumbe Alfie alikuwa na maradhi ya Alzheimer (AD), ambayo bado hayana tiba wala ponyo lenye kufaa.a Jarida la Uingereza New Scientist lasema kwamba AD ni “muuaji mkuu namba nne yakifuatia maradhi ya moyo, kansa na mshtuko wa akili katika nchi zilizoendelea.” Maradhi hayo yameitwa “ugonjwa mkubwa wa wazee.” Lakini AD yaweza kutokea hata kwa watu ambao si wazee sana, kama ilivyomshika Alfie.

Huku idadi ya watu wanaoishi kwa muda mrefu ikizidi kuongezeka katika mataifa tajiri, inatabiriwa kwamba idadi ya watu ambao watakuwa na kasoro za akili inashtua. Kulingana na uchunguzi mmoja, baina ya mwaka wa 1980 na mwaka wa 2000, huenda kukawa na ongezeko la asilimia 14 nchini Uingereza, ongezeko la asilimia 33 Marekani, na ongezeko la asilimia 64 nchini Kanada. Katika 1990 kipindi kimoja cha televisheni nchini Australia kilisema: “Inakadiriwa kwamba kuna watu wapatao 100,000 wenye Alzheimer nchini Australia sasa. Lakini kufikia mwisho wa karne hii, watu 200,000 watakuwa na maradhi haya.” Watu wapatao milioni 100 ulimwenguni pote wataugua maradhi ya AD kufikia mwaka wa 2000.

Alzheimer Ni Maradhi Gani?

Ingawa utafiti unafanywa kuchunguza baadhi ya mambo ambayo huenda yanayasababisha, kisababishi kikuu bado hakijajulikana. Lakini, inajulikana kwamba AD huhusisha kuharibika polepole kwa chembe za ubongo, hivi kwamba sehemu fulani za ubongo zaweza kunyauka. Sehemu ambazo huathirika zaidi ni zile zinazohusu kumbukumbu na uwezo wa kufikiri. Chembe katika ubongo zinazohusika na hisia huathiriwa katika hatua za mapema za maradhi haya, zikimfanya mtu abadilike tabia. Sehemu nyinginezo za ubongo zaweza kubaki zikiwa sawa mpaka baadaye—hizo ni sehemu zinazohusu macho, kuhisi, na vilevile miendo ya mwili. Gazeti Scientific American lasema kwamba mabadiliko hayo “hufanya mtu aweze kutembea, kuzungumza na kula lakini asijue lolote linaloendelea.”

Kwa kawaida, maradhi hayo hudumu kwa miaka 5 hadi 10—lakini nyakati nyingine zaidi ya miaka 20. Maradhi hayo yaendeleapo, wagonjwa hudhoofika polepole. Hatimaye, hata wanaweza kushindwa kuwatambua wapendwa wao. Katika hatua zake za mwisho-mwisho, wagonjwa hawawezi kuamka kitandani na hawawezi kuzungumza wala kujilisha. Lakini, wengi wa wagonjwa hao hufa kutokana na visababishi vingine kabla ya kufikia hatua hizo za mwisho.

Ingawa AD haina uchungu inapoanza, hiyo husababisha maumivu mengi ya kihisia-moyo. Inaeleweka kwamba wengine hukosa kukabiliana nayo, wakifikiri kwamba tatizo hilo litapotea lenyewe.b Lakini, kuna manufaa mengi ya kukabili maradhi haya na kujifunza jinsi ya kupunguza maumivu ya kihisia-moyo ambayo husababishwa nayo. “Laiti ningalijua mapema jinsi ambavyo kudhoofika kwa kumbukumbu kungaliathiri mgonjwa,” asema Bert, ambaye mke wake mwenye umri wa miaka 63 ana AD. Ndiyo, inafaa familia ijifunze juu ya hali ya AD na vilevile mbinu za kukabiliana nayo. Tafadhali jiunge na Amkeni! linapochunguza mambo hayo na mengine katika makala mbili zifuatazo.

[Maelezo ya Chini]

a AD ilipata jina kutokana na Alois Alzheimer, ambaye alikuwa tabibu wa Ujerumani aliyeyafafanua maradhi hayo kwa mara ya kwanza katika 1906 baada ya kuchunguza maiti ya mtu aliyekuwa na kasoro kubwa ya akili. Inafikiriwa kwamba AD hufanyiza karibu asilimia 60 ya visa vyote vya kasoro za akili, ikiathiri kufikia sehemu moja kwa kumi ya watu wenye umri uzidio miaka 65. Kasoro nyingine ya akili, multi-infarct dementia, husababishwa na mishtuko kidogo-kidogo ya akili, ambayo hudhuru ubongo.

b Tahadhari: Ni lazima mtu achunguzwe kabisa kitiba kabla ya kuamuliwa kuwa ana AD. Asilimia 10 hadi 20 hivi ya visa vya kasoro za akili hutokana na magonjwa ambayo yanaweza kutibiwa. Kwa habari ya kutambua AD, kitabu How to Care for Aging Parents chaeleza: “Alzheimer yaweza kutambuliwa kwa uhakika kabisa kwa kuchunguza ubongo wakati wa kuchunguza maiti, lakini madaktari waweza kuondoa uwezekano wa magonjwa mengine kwa kuchunguza dalili zake.”

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Watu wapatao milioni 100 ulimwenguni pote wataugua maradhi ya Alzheimer kufikia mwaka wa 2000

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki