Uduvi—Chakula Kitamu Kutoka Kidimbwi cha Ufugaji?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA EKUADO
NDIYO, chakula hiki kitamu kifurahiwacho na mamilioni hutoka katika kidimbwi cha ufugaji. Hata hivyo, huenda mlaji asijue kwa sababu duvi wanaokuzwa katika kidimbwi hutofautiana kidogo sana, ikiwa kuna tofauti yoyote, na aina inayokuzwa baharini. Kwa kweli, vidimbwi vingi vya duvi katika Ekuado vimejaa duvi wachanga waliochukuliwa moja kwa moja kutoka baharini.
Duvi hawa wachanga, ambao hawazidi urefu wa sentimeta moja na nusu, huvuliwa na wavuvi waitwao larveros katika hori zenye mikoko kando-kando ya pwani au kwa kuvutwa kwa wavu mahali ambapo mawimbi hupiga ufuo. Kisha hupelekwa vidimbwini ili wakue. Hata hivyo, si duvi wa kutosha wawezao kuandaliwa kwa njia hii. Hivyo, vidimbwi vingi vya ufugaji wa duvi hutegemea viangulio vyenye njia za kisasa za ufugaji ili kupata uduvi. Acheni tuchunguze kwa ukaribu zaidi jinsi vidimbwi vya ufugaji wa uduvi vifanyavyo kazi.
Kuzuru Kiangulio
Kiangulio tulichozuru kilikuwa kwenye ufuo maridadi kwenye Pwani ya Pasifiki. Ni lazima kiangulio cha uduvi kiwe karibu na dimbwi kubwa la maji ya chumvi ili kutimiza mahitaji ya kiangulio ya mfumo tata wa usambazaji wa maji. Maji kutoka baharini hupigwa pampu kuingia ndani, huchujwa, kupashwa joto ifaavyo, na kupelekwa hadi matangi tofauti-tofauti ndani.
Tulikaribishwa na kikundi chenye urafiki cha wanabiolojia wa majini, mafundisanifu, na wafanyakazi wengine waliokuwa wamevalia hivi-hivi. Mahali pa kwanza tulipozuru palikuwa chumba cha upevushaji. Hapa, uduvi aliyekomaa kabisa aliyetolewa kwenye makao yao ya asili huwekwa katika matangi ya upevushaji ya lita 17,000. “Duvi hawa si wa kuliwa,” mwongozi wetu akaeleza. “Walikamatwa wakiwa wamekomaa na kuletwa hapa kwa ajili ya uzalishaji.”
Ratiba thabiti ya kunurisha hufuatwa katika chumba cha upevushaji. Kati ya saa 9:00 alasiri na usikukati—kipindi cha kujamiiana—taa zenye mwangaza mchache huzimwa, na wafanyakazi hutafuta kwa kutumia tochi majike walio tayari kutaga mayai. Ni rahisi kugundua majike wa spishi ya Penaeus vannemei, kwa kuwa dume hushikisha kifurushi cha manii nje kwenye eneo la fumbatio la majike hao. Mara tu wafanyakazi wamwonapo jike mjamzito, jike huyo hutolewa na kupelekwa hadi kwenye tangi la kutagia lililo dogo zaidi la lita 260.
Hapo jike huyo mjamzito huwekwa kwenye jukwaa karibu na sehemu ya juu ya tangi lililo na umbo la pia—jike mmoja kwa kila tangi—hadi anapotaga mayai yake 180,000 au zaidi. Kadiri mayai yanavyotolewa, ndivyo yanavyotungishwa mara tu yagusanapo na kifurushi cha manii chenye kunata-nata. Baadaye mayai hayo na maji, huondolewa kupitia sehemu ya chini ya tangi la kutagia lililo na umbo la mpare. Mafundisanifu hurekodi idadi ya mayai kutoka kila mtago.
Saa kadhaa baada ya kuanguliwa, mabuu huhamishwa kwa idadi inayowekewa mipaka hadi yale yaitwayo matangi ya ukuzaji wenye lishe. Haya hufanana na mabirika makubwa ya kuogea, nayo huwa na lita 11,000 hivi za maji. Kwa siku 20 hadi 25 zifuatazo, matangi haya hutumika yakiwa makao ya mabuu yanayokua, ambayo hula mwani na chakula cha baharini kilichokaushwa.
Mahali Duvi Wanapokomaa
Duvi hao, ambao sasa wamepita hatua ya mabuu, huhamishwa hadi kwenye vidimbwi vya ufugaji. Wanapokuwa huko, duvi wa kutokezwa kwenye viangulio na vilevile wale wa kuzalishwa baharini hupata utunzi sawa. Hao huwekwa katika vijidimbwi ili kudhibiti kujipatanisha kwao na halijoto na viwango vipya vya chumvi katika maji. Baada ya siku chache, hao huwa tayari kwa ajili ya vidimbwi vikubwa. Vidimbwi hivi vya kutengenezwa na wanadamu hupakana na njia ya maji. Maji hupigwa pampu kwa kawaida kutoka baharini au katika hori kuingia katika njia hii ya maji. Vidimbwi vinavyoshikana huwa na ukubwa wa kuanzia ekari 12 hivi hadi 25. Kwa miezi mitatu hadi mitano, duvi hao wachanga huachwa wakue katika vidimbwi hivi.
Wakati wa kipindi cha ukuzi, kiwango cha oksijeni katika maji ya vidimbwi hutazamwa kila siku. Pia, kiwango cha ukuzi wa uduvi huangaliwa kila juma ili kurekebisha programu ya ulishaji. Jitihada hufanywa ili kudumisha ongezeko la uzani la gramu 1 hadi 2 kwa juma.
Wakati wa Kuvuna
Wakati wa kuvuna, huku kidimbwi kikitolewa maji, duvi hushikwa kwa wavu au kutolewa wanapokaribia lango la kidimbwi. Kisha, uduvi waliovunwa karibuni hutakatishwa kwa maji na kufunikwa kwa barafu kwa ajili ya usafirishaji wa haraka hadi kwenye mahali pa upakizi. Huko, isipokuwa mnunuzi ataka vingine, vichwa vya duvi hutolewa, lakini mikia yao huachwa bila kutolewa magamba. Duvi hao huoshwa na kuainishwa kulingana na ukubwa, halafu hupakiwa na kugandishwa kwa barafu kwa ajili ya usafirishaji, kwa kawaida katika masanduku ya ratili tano.
Kwa hiyo, wakati ujao unapofurahia uduvi, waweza kukumbuka kwamba chakula hiki kitamu cha baharini huenda kilitoka katika kidimbwi katika mahali kama vile Amerika ya Latini au Asia.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Ukubwa wa uduvi wakati wa kuvunwa
[Picha katika ukurasa wa 24]
Wavuvi wakivua duvi wachanga kwa wavu
[Picha katika ukurasa wa 25]
Matangi ya ukuzaji wenye lishe ndani ya kiangulio
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kusafisha duvi mahali pa upakizi
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kupakia duvi kulingana na ukubwa