Masaibu ya Maggy na Baraka Yangu
Jumanne, Mei 2, 1995, ndiyo siku ambayo binti yangu alizaliwa na mke wangu akafa. Kwa kusikitisha Maggy hakupata kuona uso wa mtoto wake. Sasa tumaini langu ni kumjulisha Tamara kwa mamake atakapofufuliwa.
BAADA ndoa ya miaka 16, mke wangu, Maggy, aliambiwa na daktari wake kwamba alikuwa ameshikwa na kansa ya matiti na kwamba angeishi kwa miezi kadhaa tu. Hiyo ilikuwa miaka mitano iliyopita. Kwa uzuri, Maggy aliweza kuishi kwa njia ya kawaida katika miaka hiyo ya mwisho ya uhai wake. Ni karibu mwisho tu ndipo maumivu yalipomlemea zaidi.
Kwa sababu ya mweneo wa kansa yake, madaktari walisema kwamba ilikuwa vigumu ashike mimba. Basi waweza kuwazia jinsi tulivyoshtuka wakati wa uchunguzi wa kawaida wa njia ya ultrasound wa kupima mweneo wa vivimbe vyenye kansa, wakamwona mtoto katika tumbo la uzazi! Alikuwa msichana. Maggy alikuwa mja-mzito kwa miezi minne na nusu. Alifurahi sana kutazamia kuwa mama kwa mara ya kwanza.
Maggy alifanya kila kitu alichoweza ili kuhakikisha kwamba mtoto huyo angezaliwa akiwa mwenye afya. Alikuwa mwangalifu sana na ulaji wake, na hata katika majuma mawili ya mwisho ya uhai wake wakati ambapo maumivu yalikuwa makali sana, alimeza dawa za kutuliza maumivu wakati tu asingeweza kuvumilia maumivu hayo.
Nabarikiwa na Mtoto Mwenye Afya
Jumamosi, Aprili 29, Maggy alipatwa na mipigo ya moyo akasema: “Nafikiri nitakufa.” Nikabaki naye mwisho-juma wote. Baada ya kumwita daktari siku ya Jumatatu, mara moja nilimpeleka hospitali katika Montreal, Kanada, ambayo si mbali na nyumbani kwetu katika St. Jérôme.
Karibu saa 11:30 alfajiri iliyofuata, muuguzi alipitia mlango wa chumba cha Maggy akatambua kwamba alikuwa na matatizo. Inaonekana alikuwa akipatwa na mshiko wa moyo. Mara moja daktari aliitwa kutoka chumba kilichokuwa kando. Ingawa Maggy alikufa, kikundi cha wanatiba kiliweza kuokoa mtoto wetu. Tamara alizaliwa miezi miwili na nusu kabla ya wakati wake naye alikuwa na uzito wa kilo 1.1 pekee.
Kwa kuwa Tamara alikuwa na damu kidogo, madaktari walitaka kumtia damu mshipani. Hata hivyo walitiwa moyo kutumia homoni sanisia ya erithropoietini. Walifanya hivyo, na ilipofanikiwa kuongeza damu yake, muuguzi mmoja alisema: “Kwa nini wasitumie hiyo kwa watoto wote?”
Tamara alikuwa na matatizo mengine yahusikayo na kuzaliwa mapema, lakini hayo yote yalitatuliwa. Hata wakati Dakt. Watters, mtaalamu wa mishipa ya neva, alipomchunguza baadaye, alimwambia muuguzi: “Nafikiri hukunipa yule mtoto aliyepaswa kuchunguzwa; huyu ni mwenye afya nzuri.”
Kukabili Kifo na Kukabili Hali Baadaye
Ilikuwa vigumu kwangu kumtazama Maggy akifa. Nilihisi hoi kabisa. Ilikuwa vigumu sana kuzungumza juu ya kifo cha Maggy. Lakini, nilifanya hivyo wakati ndugu na dada zangu Wakristo walipokuja hospitalini. Uchungu uliisha polepole kadiri nilivyozungumza juu ya jambo hilo. Wakati wowote ninaposoma makala ya Mnara wa Mlinzi au Amkeni! ambayo hasa inanihusu, ninaiweka kando katika sehemu fulani ya faragha ya maktaba yangu na kuichukua na kuisoma ninapohisi uhitaji.
Ugumu mwingine umekuwa kurudi katika nyumba isiyo na mtu. Ni vigumu sana kukabili upweke. Hisia hiyo hutokea bado, hata ingawa mimi hunufaika na uandamani wenye kujenga wa Kikristo. Maggy nami tulikuwa tumezoea kufanya mambo pamoja, na sisi tulizungumza juu ya tatizo ambalo nitapata la upweke. Yeye alitaka nioe tena. Lakini mambo si rahisi hivyo.
Utegemezo wa Wakristo Wenzangu
Sijui ningalifanya nini bila utegemezo wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali (HLC) ya Mashahidi wa Yehova. Asubuhi ambayo Maggy alikufa, Shahidi mmoja mwenye ujuzi wa HLC alikuwa hapo hospitalini naye aliniandalia msaada niliohitaji.
Wafanyakazi wa hospitali walivutiwa na msaada niliopokea kutoka kutaniko letu la Kikristo katika St. Jérôme na vilevile kutoka makutaniko mengine katika eneo hilo. Usiku ambao kifo cha Maggy kilitangazwa katika mikutano yetu ya Kikristo, zaidi ya marafiki wapendwa 20 walijitolea kusaidia. Utegemezo wao ulisaidia sana.
Marafiki walinitayarishia chakula; friza ilikuwa imejaa kwa miezi kadhaa. Familia yetu na ndugu na dada Wakristo hata walishughulikia kutafuta nguo za binti yangu. Waliniletea vitu vingi sana hivi kwamba sikuwa na nafasi ya kuviweka vyote.
Furaha Sasa na Matazamio ya Wakati Ujao
Tamara hunisaidia kuondosha upotezo wangu akilini. Nimempenda sana. Kila siku ninapomsalimia “habari ya asubuhi” kwa uchangamfu, yeye hujibu kwa tabasamu kubwa, akianza “kuongea,” na kutikisa mikono yake na miguu, akisisimuka.
Nikiwa mwastronomia asiye stadi, mimi hutazamia kumbeba Tamara kwenye paja na kumfanya aone kupitia darubini-upeo yangu maajabu ya kimbingu ya Muumba wetu Mtukufu, Yehova. Kufikiria maisha yasiyo na kikomo katika Paradiso duniani ni chanzo kikubwa cha faraja. Na kujua kwamba hilo ndilo tazamio la Tamara hunifanya nifurahi hata zaidi.—Zaburi 37:9-11, 29.
Kwa kufikiria matukio ya miaka mitano iliyopita, naweza kuyafafanua kwa njia bora zaidi kuwa yenye kufadhaisha na vilevile yenye shangwe. Nimejifunza mengi kujihusu na vilevile kuhusu maisha yenyewe. Nangoja kwa hamu wakati ujao ambao, kama Biblia inavyofafanua, “mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena.”—Ufunuo 21:3, 4.
Kisha, katika ufufuo, Maggy ataweza kupumua kwa ndani sana bila kuhisi maumivu. Zaidi ya yote, tumaini langu thabiti na tamaa yangu ni kumjulisha Tamara kwa Maggy, ili Maggy aweze kumwona msichana mdogo ambaye yeye alijidhabihu kwa ajili yake.—Kama ilivyosimuliwa na Lorne Wilkins.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Nikiwa na mke wangu
[Picha katika ukurasa wa 26]
Binti yetu, Tamara