Wala Wafanya-Mizungu Wala Miungu
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA MERCY UWASI, NAIJERIA
MAUMIVU yaliyo ndani yangu yalianza katika Afrika Magharibi alasiri moja yenye kuangaza jua katika Machi 1992.[1] Nilikuwa nimeenda pamoja na familia yetu kwenye kishamba chetu ili kuvuna muhogo. Tukiwa huko, maumivu hayo yalianza kuniwasha tumboni. Kufikia wakati tuliporudi nyumbani, maumivu yalikuwa yamewaka kama moto mkali. Nilikuwa nikitapika; nilitatizika kupumua. Ingawa maumivu hayo yalifanya iwe vigumu kwangu kusimama au kutembea, mama yangu aliweza kuniingiza katika teksi, nayo ikaenda kasi kwenye hospitali kuu ya hapo karibu.[2]
Huko hospitali, kumbe daktari aliyekuwa akishika zamu ni mwanamume mmoja niliyekuwa nimemtolea ushahidi juu ya tumaini la Biblia wakati mmoja. Daktari huyo alinigusa tumbo; lilikuwa limefura. Akauliza kama nilikuwa nimekuwa nikikojoa damu, na mama yangu akasema ndiyo nilikuwa nikipata hedhi.
“Binti yako ana mimba ya miezi mitano,” daktari akasema. “Sababu ya yeye kutoa damu ni kwamba amejaribu kutoa mimba.”
Mama kakinza hivi: “Sivyo, Daktari! Yeye si msichana wa aina hiyo.”
“Usiseme hivyo. Wasichana siku hizi hudanganya wazazi wao. Yeye ana mimba.”
Ndipo nikajisemea. Nikasema kwamba mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova na nilikuwa nimelelewa katika nyumba ya Kikristo na kwamba dhamiri yangu iliyozoezwa na Biblia haingeniruhusu nishiriki katika kitendo cha kukosa adili.
Daktari akajibu kwa kumwambia mama yangu: “Mama, tuache dini kando tuseme kweli. Mimi nakuambia kwamba msichana huyu ana mimba ya miezi mitano.”
“Simama,” Mama akaniambia. “Tutaenda hospitali nyingine.” Tulipokuwa tukiondoka kwenye jengo hilo, nilikalia nyasi nikilia kwa sababu maumivu yalikuwa mabaya sana. Mama alinipeleka nyumbani upesi akamwambia baba yangu yaliyokuwa yamesemwa na daktari.
Wakaamua kunipeleka kwenye hospitali iliyo kubwa zaidi na ya ki-siku-hizi zaidi,[3] hospitali ya mafundisho. Tukiwa njiani kwenda huko, nilisali kwa Yehova aniokoe ili watu wasiwe wakishutumu jina lake takatifu kwa kusema nilikufa kutokana na mimba isiyotakwa. Nikasema kwamba kama ningekufa, wakati ambapo daktari huyo angewaona Mashahidi wa Yehova wakija kumhubiria, angekuwa akisema: ‘Kwani si mmoja wenu alikuja hapa akiwa na mimba kitambo fulani kilichopita?’ Nikasali pia kwamba niweze kurudi kwa daktari huyo na kumtolea ushahidi tena.
“Yeye Bado Ni Bikira!”
Kwenye hiyo hospitali kubwa zaidi, ubishi uleule uliotokea katika hospitali ya kwanza ulitokea tena; madaktari walifikiri nilikuwa na mimba. Maumivu yalikuwa makali mno. Nilikuwa nikilia. Daktari mmoja alinena kwa ukali, akisema: “Hivyo ndivyo nyinyi wasichana hufanya sikuzote. Mwapata mimba, kisha mwaanza kupiga mayowe.”
Wakafanya uchunguzi fulani-fulani. Katika muda huo wakaanza kunirushia maswali. “Umeolewa?”
“La,” nikasema.
“Una miaka mingapi?”
“Kumi na minane.”
“Una wapenzi wangapi?”
“Sina wapenzi wowote.”
Kisha daktari aliye mkubwa akaanza kupiga kelele, “Wacha maneno. Wataka kuniambia katika umri wa miaka 18 huna wapenzi wowote?” Hapo tena, kama ilivyokuwa kwenye hospitali ya kwanza, nikaeleza msimamo wangu wa Kikristo. Halafu yeye akaniuliza kama mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Nikasema ndiyo. Baada ya hapo, hakuuliza swali jingine.
Uchunguzi ulithibitisha sikuwa na mimba. Mama alisikia mmoja wa madaktari hao akiambia wale wengine: “Yeye bado ni bikira!” Madaktari waliomba radhi, wakisema: “Huwezi kutulaumu kwa kufikiri vile. Sisi hujionea mambo ya jinsi hii kwa wasichana kila siku.” Hata hivyo, kivumbi hicho kilikuwa mwanzo tu wa majaribu yangu.
‘Wewe Utakubali Damu’
Uchunguzi wa kupima mwili kwa kutumia viwimbi vya sauti ulionyesha uvimbe mkubwa katika moja ya neli zangu za Falopi. Ulikuwa mkubwa kama balungi dogo. Upasuaji ulihitajiwa.
Bila kusita nikawaambia kwamba singekubali kutiwa damu mishipani ingawa ningekubali majimaji ya namna nyingine. Wao wakasisitiza kwamba damu ilikuwa ya lazima.
Mmoja wa hao madaktari wanafunzi akanigombeza, akisema: “Usemalo ndilo alilosema mmoja wenu kitambo. Lakini hali yake ilipokuwa mbaya zaidi, alikubali kutiwa damu mishipani.”
“Kisa changu ni tofauti,” nikajibu, “kwa maana ndiyo yangu ni ndiyo na la yangu ni la. Sitaridhiana kamwe kwa kuacha uaminifu wangu wa kiadili.”
Baadaye, madaktari watatu walitembelea kando ya kitanda changu kuuliza juu ya msimamo wangu dhidi ya damu. Nikaeleza kwamba Biblia husema Wakristo wapaswa “wajiepushe . . . na damu.”—Matendo 15:20.
“Lakini hutaitwaa kupitia kinywa chako,” wakasihi. “Utaitwaa kupitia mshipa fulani.”
Mimi nikasema kwamba si neno hata mtu aitwae kupitia kinywani au kupitia mshipa fulani, yote ni mamoja.
Jumamosi, Machi 14, juma moja baada ya yale maumivu kuanza, mpasuaji mkuu alinichunguza.[4] Aliratibiwa kufanya upasuaji wangu. Kufikia wakati huo uvimbe ulipanuka ukafika kifuani pangu.
Yeye akauliza, “Wamekuarifu kwamba utalazimika kukubali damu?”
“Waliniambia hivyo, Daktari, lakini mimi sitakubali damu,” nikajibu.
“Acha nikuambie kitu,” akaendelea. “Wewe utaikubali. Usipoikubali, utakufa. Jumatatu, nijapo, ikiwa damu haitakuwa imewekwa tayari kwa ajili yako, sitaufanya upasuaji. Kama hakuna cha damu, hakuna cha upasuaji.”
Kisha akaona kitabu fulani kando ya kitanda changu akauliza, “Hii ndiyo Biblia yako?” Nikasema sivyo; ilikuwa ni nakala yangu ya Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi.a Yeye akasema napaswa kutumia kitabu hicho kusali ili nisife. Nikaeleza kwamba sisi hatusomi sala zetu kutoka katika vitabu. Tuwapo na tatizo, sisi husali kwa Yehova kutoka moyoni mwetu.
Siku mbili zilizofuata, madaktari na wauguzi walifuliza kuja kunikaza nikubali kutiwa damu mishipani. Waliniambia nilikuwa mchanga mno kufa. “Kubali damu uishi!” wakasema.
‘Yehova Yuko Upande Wangu’
Katika nyakati hizo za msononeko, nilisoma Zaburi 118, isemayo hivi kwa sehemu: “Katika shida yangu nalimwita BWANA [Yehova, NW]; BWANA akanijibu akaniweka panapo nafasi. BWANA yuko upande wangu, sitaogopa; mwanadamu atanitenda nini?”—Zaburi 118:5, 6.
Baada ya mimi kuitafakari mistari hiyo, imani yangu katika Yehova ilitiwa nguvu. Asubuhi hiyo wazazi wangu walikuja hospitalini. Nikawaonyesha zaburi hiyo, nao pia wakahisi wametiwa imani nguvu.
Muda huo, si kwamba tu Mama na Baba walikuwa wakiunga mkono uamuzi wangu wa kutokubali damu bali pia walikuwa wakisali kwa ajili yangu. Washirika wa kutoka kutaniko letu walifuliza kusali na kunitia moyo kutokana na Maandiko.
“Sisi Si Wafanya-Mizungu”
Jumatatu, Machi 16, asubuhi ile ambayo upasuaji ulikuwa umeratibiwa kufanyika, mmoja wa madaktari aliingia katika chumba changu akaniona nimeshika kadi yangu ya Mwelekezo wa Kitiba, ambayo hueleza msimamo wangu juu ya kutiwa damu mishipani. Alisema, “Nini hii? Kweli wamaanisha vile umekuwa ukisema?”
“Ndiyo, nami sitakubali damu.”
“Haya basi,” akasema, “hiyo yamaanisha tutafuta upasuaji wako. Hakuna upasuaji.”
Ndipo daktari huyo akampigia mama yangu simu akiwa chumbani mwangu. Mama akasema: “Yeye ni mtu mzima kutosha kujiamulia mwenyewe. Mimi siwezi kumwamulia. Yeye asema dhamiri yake iliyozoezwa na Biblia haitamruhusu akubali damu.”
Hapo basi akatupa maandishi yangu mezani na kutoka humo chumbani kwa kishindo. Kwa muda wa saa tano hatukusikia lolote zaidi. Nilikuwa na maumivu na singeweza kula. Na hakukuwa na hospitali nyingine katika eneo hilo.
Halafu nikashangaa machela ilipoletwa ndani kunipeleka ndani ya chumba cha upasuaji. Nilikuwa nimeshika sana kadi yangu ya “Usinitie Damu.” Njiani kuelekea kwenye chumba cha upasuaji niliona vyombo vya upasuaji pamoja na pakiti za damu. Nikaanza kulia kwelikweli, nikisema kwamba singekubali kutiwa damu. Mmoja wa wauguzi alisema napaswa kuangusha kadi hiyo sakafuni. Akasema singeweza kuipeleka ndani ya chumba cha upasuaji. Mimi nikasema singeingia bila kadi hiyo na kwamba nilitaka kumwonyesha mpasuaji mkuu kadi hiyo. Kisha mwuguzi huyo akanipokonya ile kadi na kuipeleka ndani ya chumba cha upasuaji akamwonyesha mpasuaji huyo. Mara hiyo yule mpasuaji mkuu na madaktari wengine watano wakiwa wamevalia mavazi ya upasuaji wakaja nje nilipokuwa.
Mpasuaji mkuu aliwaka hasira. Aliomba mama yangu aitwe, akaelekeza kidole kwenye tumbo langu, na kumwambia: “Tazama, Mama. Hatujui tutapata nini ndani yake. Tukilazimika kumkata sana, damu itatoka nyingi sana. Je! wataka atoke damu mpaka afe?”
Mama akajibu akamwambia: “Daktari, mimi najua kwamba Yehova atakuwa pamoja na msichana huyu. Na atakuwa pamoja na wewe pia. Wewe fanya yote tu uwezayo na umwachie Yehova yale mengine.”
Halafu daktari huyo akasema: “Sisi si wafanya-mizungu wala waganga-wa-miti. Sisi huishi kwa yale ambayo tumejifunza. Siwezi kufanya upasuaji huu bila damu.”
Mama yangu akamsihi sana kwa mara nyingine afanye tu yote ambayo angeweza. Mwishowe, akakubali kupasua bila damu. Akaniuliza kama nilikuwa na woga. Nikajibu nikasema: “Mimi siogopi kifo. Najua Yehova yupo pamoja nami.”
‘Endelea Kumtumikia Mungu Wako’
Upasuaji huo ulifanywa katika muda wa saa moja. Walinifungua wakauondoa uvimbe kwa urahisi, ikashangaza wafanyakazi wa hospitali.
Baadaye mmoja wa wale madaktari alimwambia Mama kwamba madaktari wanafunzi huongea juu ya kisa changu wakati wa usiku katika makao yao. Sasa Mama au mimi tuendapo hospitali hiyo, wao hututendea kwa njia maalumu.
Siku mbili baada ya mimi kupasuliwa, yule mpasuaji alikuja ndani ya wodi yangu, akauliza nikoje, kisha akasema: “Yakupasa uendelee kumtumikia Mungu wako. Yeye alikusaidia kwelikweli.”
[Maelezo ya Chini]
a Kimetangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.