Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 6/22 kur. 26-27
  • Kukabili Hali ya Dharura ya Kitiba

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kukabili Hali ya Dharura ya Kitiba
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Suala la Dhamiri
  • Kutibiwa kwa Mafanikio Bila Damu
  • Kujipatanisha na Mapungukio ya Kimwili
  • Maisha Yawapo Magumu
    Amkeni!—1994
  • Wala Wafanya-Mizungu Wala Miungu
    Amkeni!—1994
  • Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
    Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
  • Je! Wewe Uko Tayari Kukabili Hali Ngumu ya Kitiba Yenye Kujaribu Imani?
    Huduma Yetu ya Ufalme—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 6/22 kur. 26-27

Kukabili Hali ya Dharura ya Kitiba

“NITASEMA wazi; wewe una uvimbe wa kufisha. Tusipouondoa haraka, utadhuru viungo vingine muhimu. Hiyo ndiyo sababu napendekeza mguu wako ukatwe.”

Hayo maneno ya daktari yalinishtua, kama tusemavyo hapa Peru, kana kwamba nimemwagiwa maji baridi ya ndoo. Nilikuwa na umri wa miaka 21 pekee. Mwezi mmoja mapema nilikuwa nimeanza kuhisi uchungu kwenye goti langu la kushoto nikatibiwa ugonjwa wa baridi-yabisi. Hata hivyo, baada ya siku chache nilishindwa hata kusimama.

Wakati huo, nilikuwa nikitumikia nikiwa mhudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova huko Andes katika Peru ya kati. Baada ya kurudi mji wa kwetu Huancayo, niliandamana na mama yangu kwenda jiji la Lima kwenye pwani. Huko, mnamo Julai 22, 1994, nilienda hospitali bora zaidi ya kansa nchini, ambako nilipata habari kwamba maradhi yangu yalikuwa kansa ya mifupa.

Suala la Dhamiri

Upesi niliambiwa kwamba hiyo hospitali haikuwa inafanya upasuaji bila kutumia damu. Daktari mmoja hata alisema: “Afadhali ufe nyumbani kuliko kufa mikononi mwangu.” Lakini Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali (HLC) ya kwetu, ambayo ni kikundi cha Mashahidi wa Yehova wanaoendeleza uhusiano mwema kati ya hospitali na mgonjwa, iliingilia mambo kwa niaba yangu. Tokeo likawa kwamba mkuu wa upasuaji wa hospitali alitoa idhini kwa daktari yeyote miongoni mwa madaktari wake afanye upasuaji huo ikiwa angekubali jaribu hilo. Daktari mmoja alikubali, nami mara hiyo nikatayarishwa kwa ajili ya upasuaji.

Nilitembelewa na wageni wengi kabla ya kupasuliwa. Kasisi mmoja, akiwa amebeba Biblia, alikuja kuniona naye akasema kwamba ugonjwa wangu ulikuwa adhabu kutoka kwa Mungu. Alinisihi sana nikubali matibabu yoyote yale ambayo yangeokoa uhai wangu. Nilimwambia kwamba nimeazimia kutii amri ya Biblia ya ‘kujiepusha na damu.’—Matendo 15:19, 20, 28, 29.

Wauguzi pia walikuwa wakija na kunung’unika: “Upumbavu ulioje, upumbavu!” Vikundi vya madaktari pia vilikuja. Walitaka kumwona kijana aliyekataa kutiwa damu mishipani kwa aina ya upasuaji ambayo waliona kuwa damu ni ya lazima. Hata hivyo, ziara zilizo kuwa muhimu zaidi kwangu zilikuwa zile za Wakristo wenzangu na watu wa ukoo. Wauguzi walivutiwa sana na ziara hizi nyingi zenye kutia moyo.

Kutibiwa kwa Mafanikio Bila Damu

Dakika chache tu kabla ya kutiwa usingizi kwa dawa ya nusukaputi, nilimsikia mmoja wa madaktari wa nusukaputi akisema: “Sitalaumika kwa kitakachotokea!” Lakini yule daktari mwingine wa nusukaputi, pamoja na mpasuaji na vilevile waelekezi wa hospitali, walikubali ombi langu la kutotiwa damu. Jambo nililofuata kusikia lilikuwa daktari mmoja wa nusukaputi akisema: “Samuel, amka. Upasuaji wako umemalizika.”

Ingawa mguu wangu wote ulikuwa umeondolewa, nilianza kusikia maumivu makali mahali ambapo ulikuwa. Nilitaka kuondoa maumivu hayo kwa kusugua paja langu, ambalo, bila shaka halikuwapo. Nilikuwa nikipatwa na hali ya ajabu ambayo huitwa uchungu-bandia. Nilisikia maumivu sana, nayo yalikuwa makali sana, hata ingawa mguu ambao ulionekana kuwa unaumia ulikuwa umeondolewa.

Kisha, nilipangiwa kupokea tiba ya kemikali. Athari moja ya tiba hii ni kupoteza chembe nyekundu na nyeupe za damu na pia vigandisha-damu, ambavyo ni muhimu sana kwa kuganda kwa damu. Hilo lilimaanisha kwamba kikundi kipya cha madaktari kilipaswa kujulishwa kwamba nakataa kutiwa damu mishipani. Tena ile HLC iliwasiliana na wenye kuhusika, na hao madaktari wakakubali kunitibu bila damu.

Athari za kawaida zikafuata baada ya tiba ya kemikali—nilianza kupoteza nywele na kuchafuka moyo, kutapika, na kushuka moyo. Nilikuwa nimeambiwa kwamba kungekuwa na hatari ya asilimia 35 ya ubongo kuvuja damu. Nikalazimika kuuliza mmoja wa madaktari ni nini ambacho kitaniua—hiyo kansa au ile tiba ya kemikali.

Baadaye, madaktari walisema kwamba hawawezi kunitibu kwa duru nyingine ya tiba ya kemikali bila kwanza kuongeza damu yangu kwa kunitia damu mishipani. Daktari mmoja aliniambia kwa hasira kwamba kama angekuwa na uwezo, angefanya nilale na kunitia damu mshipani. Nilimwambia kwamba kabla ya kuruhusu hilo, ningeacha kabisa tiba ya kemikali. Daktari huyo alivutiwa na msimamo wangu thabiti.

Nilikubali kutumia hormoni ya erythropoietin ili kuongeza damu yangu. Ilipotumiwa, damu yangu ikaongezeka. Baadaye, nilitibiwa kwa njia ya kemikali kupitia mishipa kwa muda wa siku kadhaa. Nililala nikifikiria, ‘Je, ni duru hii itakayofanya nivuje damu katika ubongo?’ Kwa shukrani nilimaliza tiba bila matokeo mabaya.

Kabla ya upasuaji wangu hiyo hospitali ilikuwa na sera ya kukataa kutibu watu ikiwa wangekataa kutiwa damu mshipani. Lakini sera hiyo ilibadilika. Kwa hakika, siku ileile niliyofanyiwa upasuaji, mpasuaji wangu alifanya upasuaji mwingine bila kutumia damu, na wakati huu mgonjwa hakuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova! Sasa madaktari kadhaa katika hospitali hiyo wanashirikiana na ile HLC, nao wamekubali kupokea wagonjwa wanaotaka kupasuliwa bila kutumia damu.

Kujipatanisha na Mapungukio ya Kimwili

Tangu niwe mtoto, nilikuwa nimefundishwa njia za Mungu. Nina hakika jambo hilo lilinisaidia kudumisha itikadi zangu zenye kutegemea Biblia katika hali hii ya dharura ya kitiba. Hata hivyo, karibuni nimefadhaika kwamba sijaweza kufanya kadiri ambavyo ningependa kufanya katika utumishi wa Mungu. Nilimweleza mjomba wangu ambaye ni mzee Mkristo ninavyohisi. Alinikumbusha kwamba hata mtume Paulo alikuwa na kile alichokiita “mwiba katika mwili” na kwamba hilo lilimzuia asimtumikie Mungu kwa ukamili kama ambavyo angetaka. Lakini Paulo alifanya yale aliyoweza kufanya. (2 Wakorintho 12:7-10) Maneno ya mjomba wangu yalinisaidia sana.

Hivi majuzi nilipata mguu bandia. Natumaini huo utaniwezesha kutoa utumishi zaidi kwa Mungu wetu, Yehova. Nashukuru kwamba nilidumisha dhamiri nzuri wakati wa hali ya dharura ya kitiba. Nina uhakika kwamba nikiendelea nikiwa mwaminifu, Yehova atanithawabisha kwa mwili wenye afya nzuri na uhai udumuo milele katika dunia iliyo paradiso, ambamo maumivu na mateseko hayatakuwapo tena.—Ufunuo 21:3, 4.—Kama ilivyosimuliwa na Samuel Vila Ugarte.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki