Maisha Yawapo Magumu
NILIKUWA mchanga sana nilipolazimika kukabili magumu makali ya maisha. Waweza kukubaliana nami kwamba maisha ulimwenguni leo hayafai kabisa. Ndivyo ilivyo kwetu sisi sote—hatimaye. Sisi sote huwa wagonjwa. Ni kweli kwamba huenda wengine wakazeeka bila kushikwa na ugonjwa wowote mbaya, lakini sisi sote hukabili kifo.
Labda ninafikiria juu ya kifo isivyofaa. Lakini, acheni nieleze sababu, na pia kwa nini nimenufaika na yale yaliyonipata.
Nilipokuwa na Miaka Tisa
Nilizaliwa mnamo Septemba 1968 mjini Brooklyn, New York, nikiwa mtoto mchanga zaidi kati ya watoto watano. Baba alikuwa hajiwezi, na mama alikuwa akifanya kazi akiwa karani wa kutunza fedha ili aturuzuku. Karibu na wakati nilipofikia umri wa miaka tisa, mama aligundua kwamba tumbo langu liliinuka upande mmoja. Alinipeleka katika kituo cha afya cha kwetu. Daktari alihisi uvimbe mkubwa, na siku chache baadaye, nililazwa katika Hospitali ya Kings County.
Baada ya mama kuondoka nililia sana kwa sababu nilishikwa na woga. Siku iliyofuata watu wawili waliovalia mavazi yenye rangi ya buluu waliniingiza katika chumba cha upasuaji. Nakumbuka kwamba jambo la mwisho nililoona kabla ya kuamka katika chumba cha kupata nafuu lilikuwa taa nyangavu sana iliyokuwa juu yangu na kitu fulani kikiwekwa mdomoni mwangu. Madaktari walifanikiwa kuondoa kitu kilichoitwa uvimbe wa Wilms (aina fulani ya kansa), mojapo mafigo yangu, na sehemu ya ini langu.
Nilikaa katika chumba cha utunzi wa dharura kwa majuma matano. Kila siku madaktari walibadili bandeji. Nilikuwa nikipiga kelele walipokuwa wakivuta utepe wa gamu unaoshikilia bandeji. Ili kupunguza maumivu yangu, madaktari walikuwa wakileta mtu wa kuja kujaribu kunikengeusha fikira. Nakumbuka mtu huyo alikuwa akiongea sana juu ya vyura.
Baada ya kutoka katika chumba cha utunzi wa dharura, nilikaa hospitalini kwa majuma mengine manne zaidi. Matibabu ya mnururisho yakaanza wakati uo huo. Hayo yalikuwa yenye maumivu mengi—si kwa sababu ya mnururisho—lakini kwa sababu ilikuwa ni lazima nilale kifudifudi, na tumbo lilikuwa lingali linauma kwa sababu ya ule upasuaji. Nilitibiwa kwa njia ya mnururisho kila siku tokea Jumatatu hadi Ijumaa.
Nilipotoka hospitalini mwishoni mwa Novemba 1977, niliendelea kwenda hospitalini nikitoka nyumbani kwa ajili ya matibabu ya mnururisho. Matibabu hayo yalipoisha, nilianza kutibiwa kwa njia ya kemotherapi (matibabu ya kutumia dawa za kemikali). Nililazimika kuamka asubuhi kila siku tokea Jumatatu hadi Ijumaa ili kwenda hospitalini nikadungwe dawa zenye nguvu. Daktari alikuwa akiingiza sindano kwenye mshipa na kuingiza dawa moja kwa moja ndani yao. Niliogopa sana sindano na nilikuwa nikilia, lakini mama aliniambia kwamba ilikuwa ni lazima nipitie mambo hayo yote ili nipone.
Matibabu ya kemotherapi yalikuwa na madhara mabaya sana. Yalinichafua roho, na mara nyingi nilikuwa nikitapika. Damu yangu ikapungua, nami nikapoteza nywele zangu zote.
Nazuiwa na Ugonjwa
Katika kipindi cha masika kilichofuata, katika Jumapili ya Ista, tulikuwa tikijitayarisha kwenda kanisani wakati pua yangu ilipoanza kuvuja damu kwa sababu ya hali yangu ya kuwa na damu kidogo. Wazazi wangu walijaribu kila kitu, lakini damu iliendelea kuvuja. Madaktari walikomesha damu kwa kujaza pua yangu nguo laini sana, lakini damu ikaanza kuvuja kupitia mdomo wangu. Nikadhoofika sana kwa sababu ya kupoteza damu nami nikalazwa hospitalini. Ili nisiambukizwe, wale waliokuwa wakinitembelea walilazimika kuvaa glovu za mkono, visetiri uso, na joho juu ya mavazi yao. Kwa muda wa juma moja damu yangu iliongezeka kwa kiasi cha kwamba ningeweza kutoka hospitalini.
Mara hiyo matibabu ya kemotherapi yalianza tena. Nisingeweza kuhudhuria shule, na nilihisi upweke sana kwa kutoenda shuleni. Nilihisi nimekosa marafiki wangu sana na kucheza nao nje. Nilikuwa nikifundishwa nyumbani, kwa kuwa madaktari walihisi kwamba sikupaswa kuhudhuria shule nilipokuwa ningali nikitibiwa kwa kemotherapi au hata kuenda upesi baada ya matibabu kukoma.
Nilitaka kutembelea babu na nyanya katika Georgia msimu huo wa kiangazi kama nilivyokuwa nikifanya, lakini sikuruhusiwa kwenda. Lakini, hospitali hiyo ilipangia wagonjwa wa kansa wazuru bustani ya tafrija katika New Jersey. Ingawa baadaye nilichoka sana, nilifurahia sana.
Nilimaliza matibabu ya kemotherapi mwishoni mwa 1978 lakini niliendelea kufundishwa nyumbani—kwa muda uzidio miaka mitatu kwa ujumla. Niliporudi shuleni mnamo Januari 1981, ilikuwa vigumu kujipatanisha na mambo baada ya kufundishwa nyumbani kwa muda mrefu sana. Nyakati nyingine nilikuwa nikipotea nikitafuta darasa langu. Lakini, nilipenda shule sana. Hasa nilipenda masomo ya muziki, kupiga chapa ya maneno, na mazoezi ya viungo. Baadhi ya watoto walikuwa wenye urafiki, lakini wengine walikuwa wakinidhihaki.
Pigo
“Je! una mimba?” watoto wakaanza kuniuliza. Hiyo ni kwa sababu tumbo langu lilifura. Daktari aliniambia nisiwe na wasiwasi kwa sababu ini langu lilikuwa linakua tena. Hata hivyo, nilipochunguzwa mwezi wa Machi, daktari alinilaza hospitalini. Nikaanza kulia—nilikuwa nimehudhuria shule kwa miezi miwili na nusu tu.
Mnofu mdogo ulitolewa kutoka kwenye uvimbe mmoja uliokuwa katika ini ukachunguzwe. Nilipoamka kutoka kwenye hali hiyo, mtu wa kwanza niliyeona alikuwa mama yangu. Alikuwa akilia. Aliniambia kwamba nilikuwa na kansa tena na kwamba uvimbe ulikuwa mkubwa mno usiweze kutolewa na ilikuwa lazima nitibiwe na kemotherapi ili uvimbe huo upunguke. Nilikuwa na miaka 12 tu.
Matibabu ya kemotherapi yalifanywa hospitalini, jambo lililomaanisha kwamba niende kwa siku mbili au tatu wakati mmoja kila baada ya majuma machache. Kama kawaida, nilikuwa nikichafuka roho na kutapika. Chakula kilikosa ladha, nami nikapoteza nywele zangu zote. Matibabu ya kemotherapi yaliendelea mwaka wote wa 1981. Wakati uo huo, katika Aprili, nilianza kusomea nyumbani tena.
Mapema katika 1982, nilipolazwa hospitalini kwa ajili ya upasuaji, nilikuwa nimedhoofika hivi kwamba wauguzi walilazimika kunisaidia kutoka kwenye kipima-uzani. Kemotherapi ilikuwa imepunguza ule uvimbe, kwa hiyo madaktari-wapasuaji waliweza kuundoa pamoja na sehemu nyingine ya ini langu. Tena nikalazwa hospitalini kwa muda upatao miezi miwili. Kuelekea katikati ya 1982, nilianza tena matibabu ya kemotherapi, yaliyoendelea mpaka mapema katika 1983.
Nilikuwa na huzuni katika kipindi hicho kwa sababu nisingeweza kwenda shuleni. Lakini nywele zangu zikaanza kumea tena, nami nikaanza kuhisi vema tena. Nilifurahi kwamba nilikuwa hai.
Hatimaye, Kurudi Shuleni
Mwalimu wangu wa nyumbani alipanga nihitimu kutoka vidato vya chini vya shule ya sekondari pamoja na wanafunzi wa darasa nililokuwa kwa muda mfupi katika 1981. Nilisisimukia sana jambo hilo; nilifurahi kuwaona marafiki wangu na kupata marafiki wapya. Siku ya kuhitimu ilipofika mnamo Juni 1984, nilipiga picha za marafiki na walimu, na familia yangu ilinipiga picha ili kuweka rekodi ya tukio hilo la kipekee.
Katika kiangazi hicho nilienda kuzuru babu na nyanya katika Georgia nami nilikaa huko kwa karibu kipindi chote cha kiangazi. Niliporudi mwishoni mwa Agosti, ilikuwa ni wakati wa kujitayarisha kurudi shuleni. Naam, hatimaye nilikuwa nikirudi shuleni. Nilisisimuka kama nini!
Udadisi Juu ya Dini
Dawn na Craig walikuwa tofauti na wanafunzi wengine, nami nilivutiwa sana nao. Lakini nilipowapa zawadi za Krismasi, wao walisema kwamba hawasherehekei sikukuu hiyo. “Je! nyinyi ni Wayahudi?” nikauliza. Craig akaeleza kwamba walikuwa Mashahidi wa Yehova na kwamba Krismasi haikuwa sherehe ya Kikristo. Akanipa magazeti fulani ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! nisome juu ya habari hiyo.
Nikawa na udadisi na dini yao, iliyoonekana kuwa tofauti sana. Nilipoenda kanisani, tulikuwa tukisikia jambo lilelile tena na tena: ‘Amini Yesu Kristo, ubatizwe, nawe utaenda mbinguni.’ Lakini jambo hilo lilionekana kuwa rahisi sana. Nilikuwa nimeamini kwamba mambo yawapo rahisi mno, ama wewe ni mwerevu sana, ama kuna kasoro fulani. Nilijua kwamba sikuwa mwerevu sana, kwa hiyo niliamua kwamba kulikuwa na kasoro kwa yale ambayo kanisa lilikuwa likifundisha.
Hatimaye Craig alianza kujifunza nami Biblia wakati wa vipindi vya mapumziko ya mlo wa mchana. Siku moja alinialika kwenye kusanyiko la Mashahidi wa Yehova, nami nikaenda. Nilimpata Craig na kuketi pamoja na familia yao. Nilivutiwa sana na yale niliyoona—watu wa jamii tofauti-tofauti wakiabudu pamoja kwa muungamano—nami nilivutiwa sana na yale niliyoyasikia.
Craig nami tulipogawiwa madarasa mapya, hatungeendelea kusoma Biblia pamoja kwa sababu hatukuwa na kipindi kilekile cha mapumziko ya chakula cha mchana. Mama ya Craig alimwuliza mama yangu kama angesoma nami, lakini mama yangu alikataa. Baadaye, alinipa ruhusa ya kwenda mikutano ya Kikristo. Kwa hiyo nilipiga simu kwa Jumba la Ufalme lililoorodheshwa katika kitabu cha simu nami nikajua kwamba mkutano ulianza saa 3:00 asubuhi siku ya Jumapili. Siku moja kabla ya mkutano, nilitembea nikipita karibu barabara 30 kwenda kwenye Jumba la Ufalme ili kuhakikisha kwamba nilijua njia.
Nilipofika asubuhi iliyofuata, mtu mmoja aliniuliza kama ninazuru kutoka Jumba la Ufalme jingine. Nilimwambia kwamba hiyo ilikuwa ziara yangu ya kwanza lakini nilikuwa nimejifunza kwa muda mfupi. Kwa fadhili alinialika nikae naye pamoja na mke wake. Mikutano hiyo ilikuwa tofauti sana na kanisa. Nilishangaa jinsi watu wengi walivyotaka kujibu katika kipindi cha maswali na majibu. Hata watoto wadogo walitoa maelezo. Mimi pia nikainua mkono na kujibu swali. Tokea wakati huo na kuendelea, niliendelea kuhudhuria mikutano na kuanza kufanya maendeleo katika kuelewa kweli za Biblia.
Pigo Jingine
Mnamo Desemba 1986, wakati wa mwaka wangu wa mwisho katika shule ya sekondari, nilienda kwa uchunguzi wa kila mara. Kile ambacho daktari aliona katika pafu langu la kulia kilimfanya atie shaka, kwa hiyo niliambiwa nirudi nipigwe eksirei. Nilipojua kwamba eksirei iligundua kwamba hakika kulikuwa na kasoro fulani, nilianza kulia.
Uchunguzi wa mnofu ulifanywa; daktari alitumia sindano kuchukua kipande kidogo cha uvimbe huo kutoka kwenye pafu langu. Uvimbe huo ukawa una kansa. Kumbe vilikuwa vivimbe vitatu, kutia ndani mmoja uliokuwa mkubwa karibu na mishipa ya moyo. Baada ya mazungumzo pamoja na daktari, tuliamua kwamba ningepewa dawa mbili za kujaribia za kemotherapi ili zipunguze vivimbe kabla ya upasuaji. Madhara yangekuwa kama kawaida—kupoteza nywele kabisa, kuchafuka roho, kutapika, na kupunguka kwa damu.
Nilishuka moyo sana mara ya kwanza, lakini nikaanza kusali sana kwa Yehova, na kufanya hivyo kuliniimarisha sana. Uhitimu ulikuwa muda upunguao miezi sita ijayo. Walimu wangu walikuwa wenye kuelewa mambo na wenye fadhili; waliniambia nilete tu taarifa ya daktari na nijaribu kufanya kazi za shule.
Shule Haikuwa Rahisi
Mbali na ugumu niliopata wa kufanya kazi za shule nilipokuwa mgonjwa sana, nywele zangu zilianza kutoka. Niliponunua wigi, wanashule wenzangu walisema nywele zangu zilikuwa nzuri ajabu—hawakujua kwamba ilikuwa wigi tu. Kumbe, mvulana mmoja alijua. Kila wakati nilipoingia darasani, angeandika kwenye ubao neno “wigi,” naye na marafiki wake wangecheka na kufanya mzaha. Dhihaka zao zote zilinifanya nishuke moyo sana.
Kisha, siku moja katika ujia uliojaa watu, mtu kutoka nyuma aling’oa wigi kutoka kichwa changu. Niligeuka haraka na kuiokota. Lakini watoto wengi waliona upara wangu nami nilihisi uchungu sana wa moyo. Nilienda kwenye ngazi za orofa na kulia. Siku iliyofuata ningeweza kuona kutokana na nyuso za wanafunzi wengine kwamba walisikitika juu ya kisa kilichotokea. Wanadarasa wenzangu waliniambia kwamba msichana mmoja alikuwa amemlipa mvulana mmoja atoe hiyo wigi.
Msimamo Juu ya Damu Si Rahisi
Kwa sababu ya kemotherapi, damu yangu ilipunguka sana. Na jambo baya hata zaidi, pua yangu ilikuwa ikivuja damu, nyakati nyingine hata mara mbili au tatu kwa siku. Sikuwa nimebatizwa, lakini nilichukua msimamo thabiti na kusema kwamba nikiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, nisingekubali damu. (Matendo 15:28, 29) Dada yangu mkubwa zaidi alitia moyo mmojawapo wapwa wangu wachanga aniambie kwamba hakutaka nife. Baba alikasirika, akiamuru kwamba nikubali damu, naye mama akawa ananieleza mara kwa mara kwamba Mungu atanisamehe nikitiwa damu mishipani.
Wakati uo huo, madaktari walionya kwamba nikiwa na damu kidogo sana hivyo, ningepata maradhi ya moyo au maradhi ya ghafula. Kwa kuwa nilikuwa nimeazimia kusimama thabiti, walinifanya nitie sahihi fomu ya kuwaondolea hatia iliyosema kwamba iwapo ningekufa, hawangelaumiwa. Upesi nilipata nafuu kiasi cha kuweza kurudi nyumbani na kurudi shuleni. Lakini kwa sababu ya damu yangu ya kiasi kidogo, madaktari waliamua kwamba sasa nilipaswa kutibiwa kwa njia ya mnururisho badala ya kemotherapi. Nilipata matibabu hayo kila siku baada ya shule tangu Aprili hadi mapema katika Juni 1987.
Uhitimu, Kisha Ubatizo
Uhitimu ulikuwa pindi ya pekee. Dada yangu alikuwa amenisaidia kununua nguo, na nilikuwa nimenunua wigi mpya. Mama yangu na dada zangu wawili walihudhuria sherehe ya uhitimu, na baadaye tulienda pamoja kula mlo ninaoukumbuka sana.
Wakati huo, sikuwa nikitibiwa kwa kemotherapi wala kwa mnururisho. Lakini majuma machache baadaye, daktari aliniambia niende hospitalini kwa duru nyingine tena ya matibabu ya kemotherapi. Sikutaka kwenda kwa sababu kwa muda wa juma moja nilikuwa nihudhurie mkusanyiko wa wilaya wa Mashahidi wa Yehova katika Stediamu ya Yankee katika New York City. Lakini, mama alisema niende tu ili nimalize matibabu. Basi nikafanya hivyo.
Nilisisimuka sana wakati wa mkusanyiko kwa sababu ningebatizwa siku ya Jumamosi, Julai 25, 1987. Tulisindikizwa na polisi kwenda Orchard Beach, ambapo palikuwa mahali pa ubatizo. Baada ya kubatizwa nilirudi stediamu kwa ajili ya programu yote ya siku hiyo. Nilihisi nimechoka sana jioni hiyo, lakini Jumapili asubuhi nilijitayarisha na kuhudhuria siku ya mwisho ya mkusanyiko.
Nakabili Suala la Damu Tena
Alasiri iliyofuata, nililazwa hospitalini nikiwa na joto ya digrii 39 sentigredi, ambukizo katika figo, na kupunguka damu sana. Daktari huyo alinitisha kwamba kama nisingetia sahihi fomu ya kukubali kutiwa damu mishipani, angepata amri ya mahakama ya kunitia damu kwa lazima. Niliogopa sana. Familia yangu ilikuwa imenikaza nikubali damu; dada yangu hata alijitolea anipe kiasi fulani cha damu yake, lakini nilikataa.
Nilisali sana kwa Yehova anisaidie kusimama imara. Kwa uzuri, damu yangu ikaanza kuongezeka, na mkazo wa kukubali damu ukakoma. Ingawa nilihitaji kuendelea na matibabu ya kemotherapi, sikuwa na mahali pengine katika mishipa ambapo ningedungwa. Kwa hiyo daktari-mpasuaji alitoboa kitundu kidogo chini tu ya mfupa wa mtulinga ili aingize chombo ambacho kingetumiwa kwa matibabu.
Akizungumza juu ya kuondolewa kwa vivimbe katika pafu langu, daktari-mpasuaji huyo alisema kwamba hangenitia damu ila tu kwa hali ya dharura. Mama alikuwa akiniambia nikubali, kwa hiyo nikakubali. Lakini baadaye nikahisi vibaya, kwani hiyo ilimaanisha kwamba nilikuwa ninakubali damu. Mara hiyo nilianza kutafuta daktari-mpasuaji ambaye angenihakikishia kwamba hangetumia damu. Ikaonekana kwamba sitapata, lakini hatimaye nilipata mmoja, na mpango ukafanywa wa upasuaji kufanywa Januari 1988.
Daktari huyo hakutoa uhakikisho wowote kwamba ningepona. Kwa kweli, ule usiku wa kabla ya upasuaji, alikuja chumbani mwangu na kusema: “Nitajaribu kufuata utaratibu huo.” Niliogopa; nilikuwa na miaka 19 tu na sikutaka kufa. Hata hivyo, vivimbe hivyo vitatu viliondolewa kwa mafanikio, pamoja na theluthi mbili za pafu langu. Kwa kustaajabisha, nilikaa hospitalini kwa muda wa juma moja tu. Baada ya kupata nafuu nikiwa nyumbani kwa muda upatao miezi miwili na nusu, nilianza tena matibabu ya kemotherapi, nikipata madhara yaleyale ya kawaida.
Karibu na wakati uo huo baba yangu vilevile akapatwa na kansa, na usiku mmoja miezi michache baadaye, mama alimpata akiwa amekufa katika chumba cha kulala. Baada ya kifo chake, nilianza kwenda shule ya kiufundi nilikoanza kujifunza kazi ya karani. Nilikuwa ninaendelea vizuri kimwili, kimasomo, na kiroho, hata kufanya upainia msaidizi (mhudumu wa muda wa kazi ya wakati wote).
Pigo Jingine Tena
Mnamo Aprili 1990, nilihudhuria karamu ya arusi ya ndugu yangu mkubwa katika Augusta, Georgia. Nilipokuwa huko ndugu yangu alisema: “Mguu wako ni mkubwa sana.”
“Unadhani ni nini?” nikauliza.
“Sijui,” akajibu.
“Labda ni uvimbe,” nikasema.
Baada ya kurudi New York City, nilienda kwa daktari. Uchunguzi wa mnofu uliofanywa nikiwa chini ya dawa ya nusu-kaputi ya hapo uligundua uvimbe mwingine wa Wilms katika shavu la mguu wa kushoto. Uchunguzi ulionyesha kwamba mfupa haukuathiriwa, lakini uvimbe ulikuwa mkubwa mno usiweze kutolewa. Kwa hiyo matibabu ya kawaida ya kemotherapi yakafuata.
Baada ya muda fulani nilishindwa kujizuia kutapika; utumbo wangu ulikuwa umefungwa. Upasuaji wa dharura ukaondoa tatizo hilo. Lakini, matumbo yangu yakajipinda, na upasuaji mwingine ukahitajika. Hesabu ya hemoglobini ilishuka hadi nne, na daktari akaendelea kusema-sema: “Ni lazima ukubali damu. Unakaribia kufa. Labda utakufa usiku.” Nikawa na ndoto mbaya kuhusu makaburi na kufa.
Nilipata nafuu kufikia Oktoba kiasi cha kutosha kuondolewa ule uvimbe. Walichukua karibu asilimia 70 ya shavu la mguu wangu pia. Kulikuwa na shaka kama kweli ningeweza kutembea tena. Lakini nilihitaji kutembea ili nisafiri katika New York City, kwa hiyo kwa kupitia tiba na azimio, nilianza kutembea—kwanza kwa kitu cha kusaidia kutembea, kisha mikongojo, halafu mkwaju, na hatimaye kishikilia-mguu, kilichonifanya nibaki na mikono miwili ya kutumia Biblia nikiwa katika huduma ya mlango kwa mlango. Wakati wa kemotherapi, nilipoteza kilo 27; mimi ni mwenye urefu wa futi tano na inchi moja (sentimeta 155) na uzito wangu kwa kawaida ni kilo 54. Nilipokuwa nikiongeza uzito na mguu wangu kukua, madaktari walikuwa wakipanua gango hilo mara kwa mara. Hatimaye, nilipokaribia uzito wangu wa kawaida, walinifanyizia jipya.
Maisha Yangali Si Rahisi
Kufikia kiangazi cha 1992, nilionekana kuwa mzima na nilikuwa nikitazamia labda hata kuchukua upainia msaidizi. Mnamo Novemba, nilipokea barua iliyonifurahisha sana. Ilisema kwamba maono yangu ya maisha yangeweza kuwa kitia-moyo kwa wengine, nami nilialikwa niyasimulie katika kichapo Amkeni! Furaha yangu ikageuka ikawa kutamauka juma lililofuata.
Uchunguzi wa eksirei unaofanywa kwa ukawaida uligundua vivimbe katika pafu langu pekee lililokuwa zuri. Nililia kupindukia. Nilikuwa nimekabili hali baada ya kupoteza figo moja, sehemu ya ini, sehemu kubwa ya pafu la kushoto, sehemu ya mguu, lakini hakuna mtu awezaye kuokoka potezo la mapafu yote mawili. Tena familia yangu na marafiki wangu walinitegemeza kihisia-moyo, nami nikaazimia kupigana na maradhi hayo mara nyingine tena.
Matibabu ya kemotherapi yalianzishwa ili kupunguza ukubwa wa vivimbe. Daktari mmoja alifikiri kwamba vingeweza kuondolewa na pafu hilo liokolewe. Mnamo Machi 1993, niliingia katika chumba cha upasuaji. Nilisikia baadaye kwamba waliangalia tu na kunishona bila kunifanyia upasuaji. Hawangeweza kuondoa vivimbe hivyo bila kuondoa pafu hilo. Tangu wakati huo nimekuwa nikitibiwa na kemotherapi zenye nguvu ili kujaribu kuua vivimbe hivyo.
Je! waona sababu inayofanya nikifikirie kifo nyakati zote? Je! ningejiuliza sana sababu inayofanya tufe na pia tumaini tulilo nalo la wakati ujao ikiwa maisha yangu yangekuwa rahisi? Sidhani. Hata hivyo, nina hakika kwamba jambo lililo la maana sana, si kama tuishi ama tufe sasa, bali ni kama tunapata baraka za Yehova Mungu, Yule awezaye kutupa uhai wa milele. Nikifikiria tumaini la maisha katika ulimwengu wake mpya, nikimtwika mizigo yangu, na kudumisha ukaribu na marafiki wenye tumaini kama langu kumesaidia kunitegemeza.—Zaburi 55:22; Ufunuo 21:3, 4.
Nina furaha kwamba vijana wengine wana afya yao. Natumaini kwamba yale ambayo nimesimulia yatagusa mioyo ya wengine watumie hali yao njema, si kwa kufuatia mambo ya ubatili, lakini kwa hekima katika utumishi wa Yehova. Litakuwa jambo tukufu kama nini kufurahia afya nzuri milele katika ulimwengu mpya wa Mungu! Katika ulimwengu huo hakutakuwa na madaktari, hospitali, sindano, mirija ya kupitisha chakula—hakuna chochote chenye kutukumbusha juu ya ulimwengu huu mgonjwa na unaokufa.—Kama ilivyosimuliwa na Kathy Roberson.
[Picha katika ukurasa wa 21]
Nilipohitimu kutoka vidato vya chini vya shule ya sekondari
[Picha katika ukurasa wa 23]
Nikisaidia katika utumishi wa chakula katika kusanyiko moja la mzunguko la New York