Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g92 7/8 kur. 20-22
  • “Usiseme Kamwe Haiwezekani Kamwe!”

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Usiseme Kamwe Haiwezekani Kamwe!”
  • Amkeni!—1992
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Damu Yawa Suala
  • Hata Ikiwa Angekufa, Hakutaka Damu
  • Maponyo Kamili Bila Damu
  • Wala Wafanya-Mizungu Wala Miungu
    Amkeni!—1994
  • Kulinda Salama Watoto Wenu na Matumizi Mabaya ya Damu
    Huduma Yetu ya Ufalme—1992
  • Je! Wewe Uko Tayari Kukabili Hali Ngumu ya Kitiba Yenye Kujaribu Imani?
    Huduma Yetu ya Ufalme—1990
  • Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
    Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1992
g92 7/8 kur. 20-22

“Usiseme Kamwe Haiwezekani Kamwe!”

MHUBIRI 9:11 [NW] hutuambia kwamba ‘wakati na tukio lisilotazamiwa huwapata wote.’ Lilitukia kwa familia yetu kuelekea mwishoni mwa Novemba 1986. Tiarah, mmoja wa watoto wetu watatu, alikuwa na umri wa miaka mitatu na nusu alipopatwa na tulilodhani kuwa ni mafua, yakiambatana na kukohoa kwenye kuendelea. Tulimpeleka kwenye tabibu wa magonjwa ya watoto aliyetutuma kwa daktari wa watu wote. Yeye pia alifikiri kwamba Tiarah alikuwa na mafua, pamoja na msongamano fulani kifuani, lakini halikuwa jambo la kutia wasiwasi. Alituagiza dawa nyingine ya kukohoa pamoja na viuajisumu.

Hali ya Tiarah ikawa mbaya sana. Alikuwa na homa ya sentigredi 41°, pamoja na kutapika, mchafuko wa tumbo na maumivu ya kifua. Alifanyiwa eksirei za kifua, na dawa viuajisumu vikaongezwa. Muuguzi wa kike alitupigia simu wakati eksirei za Tiarah ziliporudi. Madaktari walifikiri kwamba alikuwa na mchochota wa pafu mbaya sana. Kufikia wakati huo alikuwa na homa ya sentigredi 42° hadi sentigredi 43°. Ilikuwa inasababisha idadi ya chembe za damu yake iwe ya chini sana, yaani 2.0. Katika Desemba 16, Tiarah alilazwa hospitalini.

Sisi ni Mashahidi wa Yehova na tunatii shauri lililopewa Wakristo kwenye Matendo 15:29, la ‘kujiepusha na damu.’ Hata hivyo, sisi, hatukuhangaikia sana suala la damu. Tabibu wa Tiarah ni mstadi wa damu, na alikuwa anajua vizuri kwamba hatungekubali damu itiwe mishipani. Tiarah alipokuwa alazwe hospitalini, mara moja tulimkumbusha tabibu huyo juu ya msimamo wetu kuhusu damu. Jibu lake lilikuwa: “Naam, naam, naelewa itikadi zenu, lakini sifikiri mnahitaji kuhangaikia suala la damu.”

Baada ya hospitali kuchukua eksirei zao wenyewe, EKG (ELEKTROKADIOGRAMU ya kuchunguzia ugonjwa wa moyo), na majaribio ya damu, Tiarah alichukuliwa kwenye chumba fulani. Tulikaa hadi alipolala. Asubuhi iliyofuata niliambiwa kwamba Tiarah alikuwa na mchochota wa pafu, kwamba ilikuwa hali mbaya sana, na hakuna shaka kwamba angekaa hospitalini kwa siku karibu 10 hadi 15. Hali joto ya mwili wake ilikaa karibu sentigredi 43°, ambalo liliwafanya madaktari wahangaike sana. Walizichunguza tena eksirei, ile EKG, na majaribio ya damu, na wakaamua kufanya majaribio zaidi. Majaribio haya yalionyesha kwamba hakuwa na mchochota wa pafu bali labda aina fulani ya uvimbe kwenye pafu lake.

Damu Yawa Suala

Bila shaka, hilo liliweka mwangaza tofauti kwenye hali ya Tiarah. Walifanya majaribio yasiyoisha, kutia ndani ya kifua kikuu, ambayo hayakuonyesha lolote. Walifanya sonogramu, skani za CAT (uchunguzi wa sehemu za mwili kwa kompyuta), eksirei nyingi zaidi. Eksirei za mwisho zilionyesha kuambukizwa kwingi kwa pafu lake la kulia. Pafu la kushoto lilionekana kuwa halina nguvu—na pafu hilo lilikuwa la maana sana, kwani ndilo lililokuwa likifanya kazi yote ya kupumua. Suala la damu lilitokezwa tena. Tulikuwa tumetia sahihi juu ya kutohusisha hospitali daraka lolote kuhusu kukataa kwetu damu wakati Tiarah alipolazwa hospitalini. Walihisi kwamba sasa kwa sababu uhai wa mtoto wetu ulikuwa hatarini, tungebadilisha mawazo yetu.

Tuliposhikamana na uamuzi wetu, kila kitu kilibadilika. Wasimamizi wa hospitali walituambia kuwa hatukuwa wazazi wazuri, kwamba wangepata amri ya korti ya kuwaruhusu wamtie Tiarah damu, na wangefanya tunyang’anywe wale watoto wetu wengine wawili. Wangengojea amri ya korti, na wakati ingekuja, wangetoa pafu lililoambukizwa. Kwa mara iliyoonekana kuwa kama ya 50, tuliwaelezea hatukatai matibabu ya kitiba, na tunapokataa damu, tunakubali kitu ambacho kingechukua mahali pa damu.

Yote hayo yalikuwa bure. Madaktari walikataa kusikiliza. Waliamua kutukaza tubadilishe mawazo yetu. Walianza kuambia kila mfanya kazi na waliofanya kazi katika orofa hiyo—kuanzia madaktari hadi wauguzi wa kike mpaka wasafishaji—tulilokuwa tunamfanyia mtoto wetu. Watu hawa kisha wangetujia na kutuuliza kwa nini tulikuwa tunamwacha mtoto wetu afe. Mume wangu na mimi tukawaambia madaktari kwamba tungetafuta daktari na hospitali ambayo ingemchukua Tiarah na kufanya mambo yoyote yaliyohitajiwa na kuyafanya bila damu. Walituambia hakuna hospitali ambayo ingemhamisha akiwa katika hali aliyokuwa nayo. Nikawaambia: “Msiseme kamwe haiwezekani kamwe!”

Hata Ikiwa Angekufa, Hakutaka Damu

Nilimwelezea Tiarah jinsi hali ilivyokuwa, nikamwambia walilosema madaktari, yaliyokuwa maoni ya Yehova juu ya jambo hilo, na lile tuliamua kufanya, ambalo lilikuwa ni kutafuta daktari na hospitali ambayo ingemsaidia bila kumtia damu. Tiarah alielewa vizuri sana katika umri wake mchanga. Alitaka kumtii Yehova. Hata ikiwa angekufa hakutaka damu. Kusikia binti yangu mwenyewe, alivyokuwa mgonjwa sana hivyo, akichukua msimamo wake mwenyewe jinsi hiyo kulinifanya nitoe machozi. Nilitambua wakati huo kabla ya wakati wowote mwingine umaana wa kuanza mafundisho ya Biblia tangu utoto, kwa kuwa hata kwenye umri wa miaka mitatu na nusu, Tiarah angetwambia katika njia yake rahisi kwamba alitaka kubaki mwaminifu kwa Yehova kujapotokea nini.—Waefeso 6:4; 2 Timotheo 3:15.

Katika jitihada zetu za kumtoa Tiarah kutoka hospitali hiyo kabla ya amri ya korti kuja ili apewe damu, mume wangu alikuwa ameongea na mmoja wa wazee wa kundi. Alizungumza na daktari ambaye alisema angeona lile ambalo angeweza kufanya. Hilo lilitupatia tumaini angalau.

Nilikuwa nimekaa hospitalini tangu ile jioni aliyolazwa Tiarah. Nilikuwa nimechoka kiakili, kimwili, na kihisia moyo. Mume wangu mpenzi, akitambua hilo, alisisitiza niende nyumbani, kwamba angekaa na Tiarah usiku huo. Nilienda nyumbani, lakini sikuweza kulala. Nilisafisha nyumba, nikapigia simu wazazi wangu, na nikazungumza na marafiki wengine ambao walikuwa Mashahidi. Hatimaye nikalala—sijui ilikuwa kwa muda gani—halafu simu ikalia. Niliogopa kuichukua, nikihofu kwamba alikuwa mume wangu akipiga kuniambia Tiarah alikuwa amekufa.

Mwishowe niliijibu. Alikuwa ni daktari yule ambaye mzee alikuwa amewasiliana naye akiniambia kwamba walikuwa wamepata daktari aliyekuwa na nia ya kuheshimu msimamo wetu juu ya damu na ambaye angemchukua Tiarah hata akiwa katika hali yake ya kuzorota. Alikuwa tayari amefanya mipango na hospitali yetu kwa ajili ya kumtoa Tiarah! Nilimshukuru sana nikitoa machozi. Niliiweka simu chini na nikapiga magoti nikamtolea shukrani Yehova.

Baada ya kuwa katika hospitali hiyo ya kwanza kwa siku kumi, Tiarah alilazwa katika sehemu nyingine ya Jiji la New York. Hospitali hiyo ilikuwa na ujuzi wa matatizo ya mapafu katika watoto. Tiarah alipofika, walikuwa wakimngojea. Walifanya mfululizo wa skani za CAT, eksirei, sonogramu, na EKG, na majaribio ya damu kwa rekodi zao, na wakachunguza rekodi tulizowapatia kutoka hospitali ile nyingine. Baada ya uchunguzi wote huu, daktari tuliyekuwa naye sasa, mwenye ujuzi wa mapafu, alihisi kwamba kumtia damu mishipani kungekuwa kosa na mwili wake ungeikataa.

Maponyo Kamili Bila Damu

Tiarah alipokuwa katika hospitali hii, alipewa utunzi mzuri sana na wale waliokuwa na ujuzi wa kuwashughulikia watoto wachanga wenye magonjwa ya mapafu. Walitujulisha matatizo ya kitiba na wakatushauri juu ya njia watakazofuata. Hawakumfanya alale kabisa bali walitumia dawa za kumfanya asione maumivu. Halafu wakatoa umajimaji katika shimo la pafu na wakaupeleka maabarani ili ufanyiwe majaribio kwa kutumia viuavijasumu mbalimbali. Walipata kiuavijasumu kimoja sahili kitumiwacho kwa mafua ambacho kingepigana na kijidudu hicho. Tiarah alipokea vipimo vingi vya kiuavijasumu hicho, na akawekwa kwenye hema ya oksijeni kwa siku kumi. Alifanya maendeleo kwa utaratibu.

Kwa kuchunguza skani zake za CAT na eksirei, madaktari waligundua kwamba alikuwa na jipu kwenye sehemu ya chini ya pafu lake la kulia. Hata ingawa kiuavijasumu kilikuwa kinapunguza kiasi cha umajimaji uliokuwa ukizunguka pafu, hakikuwa kinapigana na jipu hilo. Jipu hilo lilikuwa linatokeza umajimaji mwingi zaidi, na madaktari walihisi kwamba huenda likahitaji kutolewa kwa upasuaji. Lakini kwanza waliendeleza matibabu ya kiuavijasumu, aina nyingine ikaongezewa. Pia walimpa vipimo vikubwa vya chuma na wakamweka kwenye ulishaji wa mishipani kwa siku tatu, ukifuatiwa na ulaji wa chakula chepesi. Idadi ya chembe za damu yake iliongezeka hadi 5.0, halafu hadi 7.0. Mstadi wa damu na wa mapafu walishangazwa na maendeleo hayo ya upesi—sana hivi kwamba daktari wa mapafu alisema: “Ni lazima Mungu wenu awe anasaidia.”

Kwa vile jipu halikuathiriwa na vipimo vikubwa vya viuavijasumu, umajimaji uliotoka ndani ya jipu wenyewe ulifanyiwa majaribio. Ilipatikana kwamba aina nyingine ya kiuavijasumu kingeweza kupigana na kijidudu hicho hasa. Kwa vile kilikuwa kijidudu cha mafua kipatikanacho kwa kawaida kinywani, daktari alifikiria kwamba ni lazima Tiarah alikuwa amekimeza pamoja na chakula na kikaingia kwenye pafu lake kupitia koromeo. Viuavijasumu vilikuwa vikijaribu kuuwa kijidudu hicho, lililosababisha ukuta utokee kukizunguka, na likawa jipu. Kulingana na daktari, hilo lilikuwa jambo lisilo la kawaida, hivyo akaona ni lazima aandike mambo yote aliyovumbua na aliyoyafanya na kupeleka ripoti yake kwenye jarida la kitiba.

Baada ya kukaa katika hospitali hiyo kwa mwezi moja, Tiarah alitolewa awe mgonjwa wa nje. Bado ilihitajiwa kumwona mstadi huyo mara moja kila juma kwa miezi mitatu na kumeza vipimo vikubwa vya viuavijasumu na chuma. Hata hivyo, hakufanyiwa upasuaji kamwe. Amepona kabisa, bila doa katika mapafu yake.

Tiarah sasa ni mhubiri katika kundi la Kikristo la Mashahidi wa Yehova. Alitoa hotuba yake ya kwanza katika Shule ya Huduma ya Kitheokrasi Februari 14, 1991. Mume wangu na mimi twamshukuru Yehova kwa kubariki msimamo wetu imara wa kujiepusha na damu katika kutii amri Zake. Hebu sisi sote na tuendelee kumsifu Yehova kwa sababu anastahili kusifiwa. Na kumbuka, daktari akikuambia hautaweza kamwe kufaulu bila damu, mwambie, “Usiseme kamwe haiwezekani kamwe!”—Imechangwa na Nina Hooks, Brooklyn, New York.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki