Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 12/22 kur. 25-27
  • Madaktari Walijifunza Kutokana na Hali Yangu ya Kukaribia Kifo

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Madaktari Walijifunza Kutokana na Hali Yangu ya Kukaribia Kifo
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Wakati wa Kuzaa
  • Kukataa Katakata Kukubali Damu
  • Uhai Hatarini
  • Madaktari Wajifunza
  • “Sasa Ni Mia Tu na Yehova”
    Amkeni!—1995
  • Wala Wafanya-Mizungu Wala Miungu
    Amkeni!—1994
  • Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
    Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
  • Kutia Damu Mishipani— Je! Ndio Ufunguo wa Kuokoa Uhai?
    Amkeni!—1991
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 12/22 kur. 25-27

Madaktari Walijifunza Kutokana na Hali Yangu ya Kukaribia Kifo

KATIKATI mwa Mei 1991, tulipata kujua kwamba tulikuwa tukitazamia mtoto wetu wa nne. Mtoto wetu mchanga zaidi, Mikael, alikuwa na umri wa miaka tisa, na mabinti wetu pacha, Maria na Sara, walikuwa na miaka 13. Ingawa mtoto mwingine hakuwa amepangiwa, baada ya muda mfupi tulikuja kuzoea wazo la kuwa na mtoto mwingine.

Jioni moja katika mwezi wa tatu wa mimba, nilihisi maumivu ya ghafula katika pafu langu. Siku iliyofuata singeweza kutembea hata kidogo. Daktari alisema kwamba nilikuwa na mchochota wa pafu, kisha akanipa Peninsilini. Nilianza kuhisi vema baada ya siku kadhaa, lakini nilikuwa mnyonge sana. Kisha ghafula nikapata maumivu katika pafu langu jingine, na taratibu ileile ikarudiwa.

Siku zilizofuata, singeweza kulala kwa sababu ya ugumu wa kupumua. Zaidi ya juma moja hivi baada ya shambulio la kwanza la maumivu, mmoja wa miguu yangu ukawa rangi ya buluu na ukafura. Wakati huu nililazwa hospitalini. Daktari alinijulisha kwamba maumivu katika mapafu yangu hayakusababishwa na mchochota wa pafu bali migando ya damu. Yeye pia alisema kwamba nilikuwa na mgando wa damu katika kinena changu. Nilipata kujua kwamba migando ya damu ni moja ya visababishi vya kifo vya kawaida miongoni mwa wanawake wajawazito katika Sweden. Siku chache baadaye, nilihamishwa hadi Hospitali ya Karolinska Sjukhuset katika Stockholm, ambayo ina kliniki ya kipekee ya ujauzito kwa ajili ya mimba zinazotatanisha.

Madaktari waliamua kunipa matibabu ya kuifanya damu kuwa nyepesi na kutoganda upesi. Walinihakikishia kwamba hatari ya kutokwa damu kwa sababu ya dawa ya kufanya damu kutoganda upesi ilikuwa ndogo ikilinganishwa na hatari ya kupatwa na mgando mwingine mapafuni. Baada ya majuma kadhaa, nilihisi nafuu vya kutosha kurudi nyumbani. Nilihisi furaha yenye uchangamfu kwa kuwa hai pamoja na mtoto mdogo sana aliyekuwa akikua ndani yangu.

Wakati wa Kuzaa

Iliamuliwa kwamba kuzaa kuchochewe, lakini kabla ya hatua kuchukuliwa kuanza hiyo taratibu, nilihisi maumivu makali mno katika sehemu ya chini ya fumbatio langu. Kwa hiyo nikakimbizwa hospitali. Hata hivyo, madaktari hawakuweza kupata kasoro yoyote.

Jioni iliyofuata fumbatio langu lilivimba sana, na maumivu hayakuwa yamepungua. Katikati mwa usiku, daktari alinichunguza na kupata kwamba nilikuwa katika maumivu ya kuzaa. Asubuhi iliyofuata fumbatio langu lilivimba hata zaidi, na maumivu yalikuwa yasiyovumilika. Daktari alionekana akiwa na wasiwasi kisha akauliza ni lini mara ya mwisho nilipotambua kusogea-sogea kwa mtoto. Nilitambua ghafula kwamba ni muda mrefu sana ulikuwa umepita.

Nilikimbizwa mara hiyo hadi kwenye chumba cha kuzalia. Kwa mbali ningeweza kusikia wafanyakazi wakizungumza. “Anakataa kutiwa damu mishipani,” mtu fulani akasema. Kisha muuguzi mmoja akainama juu yangu na kusema kwa sauti kubwa: “Unajua mtoto wako amekufa, sivyo?” Nilihisi kana kwamba mtu alikuwa amechoma moyo wangu kwa upanga.—Mithali 12:18.

Kukataa Katakata Kukubali Damu

Mara daktari wangu akatokezea na kuniambia kwamba hali yangu ilikuwa mbaya mno. Yeye aliuliza ikiwa bado nilitaka kushikamana na uamuzi wangu wa kutokubali utiaji-damu mishipani. Nilitaarifu kwa uthabiti kwamba nilishikamana na uamuzi wangu, lakini sikumbuki mengi baada ya hapo. Hata hivyo, nilikuwa nimeweka wazi kabisa kwa daktari wangu kwamba Wakristo wanaamriwa wajiepushe na damu na kwamba nilitaka kuwa mtiifu kwa sheria ya Mungu.—Matendo 15:28, 29; 21:25.

Wakati huohuo walimwita daktari mwingine, Barbro Larson, daktari-mpasuaji stadi. Yeye alifika haraka na kufanya upasuaji mara hiyo. Walipofungua fumbatio langu, waligundua kwamba nilikuwa nimepoteza lita tatu za damu kupitia kuvuja damu kwa ndani. Lakini Dakt. Larson alistahi uamuzi wangu kuhusu utiaji-damu mishipani.

Baadaye, daktari mwingine alisema kwamba lilikuwa jambo la madakika tu kabla ya mimi kufa. “Sijui kama angali hai saa hizi,” yeye akadai. Baadaye ilijulikana kwamba hao madaktari hawakuweza kupata chanzo cha mvujo wa damu, kwa hiyo wakaweka kipande cha kitambaa ili kufinya ndani ya fumbatio langu. Madaktari na wauguzi hawakutoa tumaini lolote lile la kuokoka kwangu.

Watoto wangu walipofika hospitalini na kujua kuhusu hali yangu, mmoja wao alisema kwamba Har–Magedoni itakuja karibuni na kwamba baada ya hapo wataniona tena katika ufufuo. Jinsi ufufuo ulivyo mpango mzuri ajabu na wa haki!—Yohana 5:28, 29; 11:17-44; Matendo 24:15; Ufunuo 21:3, 4.

Uhai Hatarini

Hemoglobini yangu ilikuwa imeshuka hadi gramu nne kwa desilita, lakini kuvuja damu kulionekana kulikuwa kumekoma. Mapema nilikuwa nimeweka nakala ya gazeti la Amkeni! (Kiingereza) la Novemba 22, 1991, katika mahali pa kuwekea rekodi za mgonjwa. Dakt. Larson alilipata na kuona kichwa, “Kuzuia na Kudhibiti Kuvuja kwa Damu Bila Utiaji-Damu Mishipani.” Yeye alilipitiapitia kwa hamu ili kuona ikiwa kulikuwa na jambo ambalo angetumia ili kunisaidia kuokoka. Macho yake yaliangukia neno “erythropoietin,” ambayo ni aina ya utibabu unaochochea mwili kutokeza chembe nyekundu za damu. Sasa yeye aliutumia. Lakini utibabu huo huchukua wakati kuwa na matokeo. Kwa hiyo swali lilikuwa, Je, utibabu wa erythropoietin ungefanya kazi kwa wakati?

Siku iliyofuata kiwango changu cha hemoglobini kilikuwa kimeshuka hadi 2.9. Nilipoamka na kupata familia yangu yote kando ya kitanda changu, nilijiuliza ni nini kilikuwa kimetokea. Singeweza kuzungumza kwa sababu ya mashine ya kusaidia kupumua. Nilihisi hisia nyingi mno kwa huzuni, lakini singeweza hata kulia. Kila mtu aliniambia kwamba ilikuwa lazima nihifadhi nguvu zangu ili niweze kuokoka.

Siku iliyofuata nilipata homa kwa sababu ya kuvimba kulikosababishwa na kile kitambaa cha kufinya kilichoachwa katika fumbatio langu. Hemoglobini yangu ilikuwa imeshuka hadi 2.7. Ingawa ni hatari mno kumtia mtu unusukaputi katika hali hiyo, Dakt. Larson alielezea kwamba licha ya hiyo hatari, walilazimika kufanya upasuaji tena ili kuondoa kitambaa cha kufinya.

Kabla ya upasuaji watoto waliruhusiwa kuja ndani kuniona. Kila mtu alifikiri ilikuwa kwaheri ya kuonana. Washiriki kadhaa wa wafanyakazi wa kitiba walikuwa wakilia. Hawakuamini ningeokoka. Watoto wetu walikuwa jasiri sana, na hili lilinifanya niwe mtulivu na mwenye uhakika.

Kwa kuwa nusukaputi niliyopewa ilikuwa chache, nyakati fulani ningeweza kusikia kile wafanyakazi walichokuwa wakisemezana. Wengine waliongea kunihusu kana kwamba nilikuwa mfu tayari. Baadaye, niliposimulia kile nilichokuwa nimesikia wakati wa upasuaji, muuguzi mmoja aliomba msamaha. Lakini alisema alikuwa na uhakika kwamba nilikuwa nife na bado hakuelewa jinsi nilivyookoka.

Siku iliyofuata nilihisi nafuu kidogo. Hemoglobini yangu ilikuwa 2.9, na hematokriti ilikuwa 9. Ndugu na dada zangu wa Kikristo walinitembelea, wakiletea familia yangu chakula na kahawa. Tulishukuru kwa upendo na shauku yao. Kufikia jioni hali yangu ilikuwa mbaya bado lakini thabiti, na nilihamishwa kwa wadi nyingine.

Madaktari Wajifunza

Washiriki wengi wa wafanyakazi wa kitiba walikuwa wadadisi kunihusu, na wengi wao walikuwa wenye fadhili. Muuguzi mmoja alisema hivi: “Ni lazima Mungu wako alikuokoa.” Daktari kutoka wadi nyingine alikuja na kusema hivi: “Nataka tu kuona jinsi mtu mwenye hemoglobini ya chini hivyo anavyofanana. Siwezi kufahamu jinsi unavyoweza kuwa macho namna hiyo.”

Siku iliyofuata, ingawa ilikuwa siku yake ya likizo, daktari wangu alikuja kuniona. Yeye aliniambia kwamba alihisi unyenyekevu kwa sababu ya kilichotukia. Ikiwa ningepata nafuu kabisa, yeye akasema, wangeanzisha utafiti mpya katika vibadala ya tiba ya utiaji-damu mishipani katika kutibu wagonjwa.

Kupona kwangu kulikuwa kwenye kutazamisha. Majuma mawili na nusu baada ya kuzaa kwangu kwa kimsiba, kiwango changu cha hemoglobini kilikuwa kimeongezeka hadi kidogo zaidi ya 8. Kwa hiyo niliruhusiwa kutoka hospitalini. Siku tatu baadaye tulikuwa na kusanyiko letu la mzunguko la kila mwaka la Mashahidi wa Yehova, nami nilikuwako pale. Jinsi ilivyotia moyo kuona tena ndugu na dada zetu wa Kikristo ambao walikuwa wenye kutegemeza wakati wa shida yetu!—Mithali 17:17.

Kama Dakt. Larson alivyoahidi, ripoti kuhusu kisa changu iliyokuwa na kichwa, “Erythropoietin Yachukua Mahali pa Utiaji-Damu Mishipani,” ilichapishwa baadaye katika jarida la kitiba la Kisweden Läkartidningen. Ilisema hivi: “Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 35, mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alipatwa na kuvuja damu nyingi kubaya sana kunakohusiana na kuzaa. Yeye alikataa utiaji-damu mishipani lakini akakubali tiba ya erythropoietin. Baada ya siku tisa za utibabu wa baada ya upasuaji uliokuwa na viwango vya juu ya erythropoietin, hemoglobini iliongezeka kutoka gramu 2.9 hadi 8.2 kwa desilita bila athari zozote za baadaye.”

Makala hiyo ilimalizia hivi: “Mwanzoni mgonjwa huyo alikuwa mnyonge sana, lakini akapata nafuu kwa haraka yenye kushangaza. Isitoshe, hatua ya baada ya upasuaji ilikuwa bila utatanishi wowote kabisa. Mgonjwa aliweza kutolewa hospitalini baada ya majuma mawili.”

Hata ingawa ono hili lilikuwa gumu na lisilofurahisha kwetu, tunafurahi kwamba kama tokeo, madaktari fulani huenda walijifunza zaidi kuhusu vibadala vya utiaji-damu mishipani. Tunatumaini kwamba watakuwa tayari kujaribu njia nyinginezo za utibabu ambazo zimethibitika kuwa zenye kufaulu.—Kama ilivyosimuliwa na Ann Yipsiotis.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Nikiwa na daktari wangu mwenye kusaidia sana

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki