“Sasa Ni Mia Tu na Yehova”
KUFIKIA Mei 1991, mwili wangu tayari ulikuwa umeonyesha kwamba kulikuwa na kasoro fulani. Baada ya kutembea mbali au kutumia baiskeli kwa mwendo mrefu, ningehisi maumivu makali katika mikono na miguu yangu, na maungo yangu yangefura. Nilipohudhuria harusi ya mmoja wa ndugu zangu katika Julai 1991, nikawa mgonjwa. Baada ya hili, mwingi wa wakati wangu nililala kitandani, na nilipatwa na mapaku mekundu usoni na mwilini.
Mama yangu alinipeleka kwa daktari fulani, aliyenipeleka haraka kwenye hospitali iliyo karibu na nyumbani kwetu Askim katika Norway. Uchunguzi ulionyesha utendaji uliopungua wa figo na msongo wa damu. Kiwango cha hemoglobini kilikuwa gramu 7.3 kwa kila desilita tu, kikilinganishwa na kile cha kawaida cha 11.5 hadi 16. Baada ya siku mbili nilihamishwa kwa hospitali kubwa yenye chumba maalumu cha matibabu ya maradhi ya figo. Baada ya kuona matokeo ya machunguo kadhaa ya damu, daktari huyo aliamua kwamba nilikuwa na ugonjwa wa ngozi ya mapaku-mekundu mwilini, na kwamba mfumo wangu wa kinga ulikuwa ukitokeza mazindiko yaliyokuwa yakishambulia damu yangu na tishu za figo. Nilipatiwa steroidi-koteksi na tibakemili.
Kwa sababu maradhi yenyewe pamoja na baadhi ya utibabu huvunja-vunja damu, jambo la kutiwa damu mishipani likawa suala. Nilijikakamua kwa nguvu zangu zote na kusema hivi: “Mimi ni Shahidi aliyejitoa wakfu na kubatizwa, na sitaki damu.” (Mwanzo 9:4; Matendo 15:28, 29) Kisha daktari aliongea na mama faraghani, naye mama alieleza kwamba tungependa kutumia vibadala vya kutia damu mishipani. Alisema kwamba alikuwa radhi kustahi msimamo wangu na kwamba angefanya vyovyote awezavyo ili kunisaidia.
Rekodi ya kitiba, ambayo baadaye tuliipokea, yasema hivi: “Mgonjwa ni mtu mzima na ni timamu kiakili na anaelewa. Hivyo basi, mmoja hupata kuwa lazima kustahi maoni ya mgonjwa.” Pia yataarifu hivi: “Idara ya kitiba imeamua kustahi maamuzi ya mgonjwa ya kutokubali damu, hata tokeo likiwa ni kifo.”
Matibabu ya Kitiba
Siku zilizofuata, tiba za namna-namna zilijaribiwa ili kupunguza msongo wa damu yangu na basi kukomesha ule mkazo kwenye mafigo. Mwili wangu haungemudu utibabu huo, na nikumbukacho kuhusu wakati huo ni kutapika tena na tena. Kwa vipindi nilijihisi kushuka moyo mno, na wazazi wangu nami kwa ukawaida tulisali kwa Yehova kwa ajili ya msaada na nguvu. Baada ya mwezi hospitalini, niliruhusiwa kwenda nyumbani kwa ajili ya mwisho-juma. Baadaye, wakati wa pili niliporuhusiwa kutoka hospitalini, nilipatwa na kifafa kikuu kikifuatiwa na vingine vinne vidogo. Maradhi yaliathiri mfumo mkuu wa neva. Nilirudishwa haraka hospitalini tena.
Madaktari waliamua kuandaa matibabu ya badala. Plazima ilitolewa kutoka kwa damu, na basi mazindiko yaliyoshambulia chembe za damu yangu na tishu za figo yaliondolewa. Kisha nilidungwa sindano za myeyusho-maziwa-chumvi wa Ringer pamoja na albumini. Nilikuwa nimezungumzia matibabu haya pamoja na madaktari na nikawapa idhini iliyoandikwa ili kuitumia.a Yajapo matibabu haya hali yangu iliendelea kuwa mbaya sana. Niliwapa pia idhini ya kunitibu na imunoglobulini, lakini kwa wakati huo hawakutumia hizi.b
Utendaji wa figo zangu ulipungua mno. Umaji-maji ufanyizao damu ulikuwa 682, ukilinganishwa na ule wa kawaida wa 55 hadi 110. Msongo wa damu wangu ulibaki juu, na kiwango cha hemoglobini kilibaki kati ya gramu 5 na 6 kwa kila desilita. Siku moja idadi ya vigandishadamu ilikuwa 17,000 kwa kila milimeta mche-mraba ya damu (idadi ya kawaida huwa kuanzia 150,000 hadi 450,000), ikiongeza zaidi hatari ya kuvuja damu. Kwa kupendeza, idadi ya vigandishadamu mara ilianza kuongezeka. Siku iliyofuata idadi yavyo ilikuwa 31,000, na ongezeko likaendelea.
Utegemezo Wenye Upendo
Wafanyakazi wa hospitali walivutiwa na maua, barua, kadi, na simu zote nilizozipokea kutoka kwa ndugu na dada Wakristo kote Norway. Walishangaa jinsi mwenye umri wa miaka 18 angaliweza kuwa na marafiki wengi mno hivyo. Hiyo ilitupa fursa ya kuwaambia kuhusu tumaini letu la Kikristo na tengenezo la Yehova lenye upendo.—Yohana 5:28, 29; Ufunuo 21:3, 4.
Wakati huohuo, Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali ya Mashahidi wa Yehova ilikuwa ikijitahidi sana kupata habari zaidi juu ya matibabu ya ugonjwa wa ngozi ya mapaku-mekundu. Kutoka kwa ofisi ya tawi ya Norway tulipokea nakala ambayo ilichapishwa katika jarida la kitiba. Ilifafanua visa viwili tata vya ugonjwa wa ngozi ya mapaku mekundu mwilini ambavyo imunoglobulini ilitumiwa kwa wanawake wawili wachanga—ikiwa na matokeo mazuri. Wakati wa mkutano pamoja na madaktari, wazazi wangu waliwaomba wasome makala hiyo ili kuona kama habari hiyo ingelisaidia katika kisa changu. Madaktari walikuwa na maoni tofauti juu ya la kufanya. Kwa kielelezo, kulikuwa na hangaiko kwa kukosa habari ya kutosha kuhusu athari za kando za matibabu ya imunoglobulini.
Mkazo wa Kukubali Damu
Kufikia hapo nilikuwa nimelazwa hospitalini kwa karibu majuma manane. Usiku mmoja nilihisi umivu kali tumboni, na kulikuwa na damu katika choo kutokana na kuvuja damu kwa ndani. Daktari wa upasuaji alifikiwa. Alisema nilihitaji upasuaji wa haraka na kutiwa damu, la sivyo ningekufa kwa muda wa saa chache. Daktari huyu wa upasuaji alimwambia dada yangu, aliyekuwa akikaa nami, kwamba ni afadhali anirai ili nikubali damu ama sivyo angelaumika kwa ajili ya kifo changu. Hili lilinikasirisha, kwani uamuzi wa kukataa kutiwa damu mishipani ulikuwa wangu mwenyewe.
Madaktari walitaka kuongea nami peke yangu ili kuhakikisha kama kweli uamuzi ulikuwa wangu mwenyewe na kwamba nilifahamu kikamili walichoamini kingetokea kwa kukataa damu. Baada ya dakika 15 walisadiki kwamba singebadili maoni yangu. Badala ya kufanya upasuaji, madaktari walitumia dawa za viuavijasumu ili kupigana na ambukizo.
Siku ya Septemba 30, iliyofuatia mazungumzo na madaktari, kiwango changu cha hemoglobini kilipungua kutoka 6.5 hadi 3.5. Nilipelekwa kwenye chumba cha utunzi wa dharura. Nilikuwa dhaifu sana hivi kwamba nilihitaji kusaidiwa kupumua na kichochea-oksijeni. Hata ingawa nilikuwa nusu-fahamu wakati huu wote wa duru gumu, siwezi kukumbuka chochote. Kwa hiyo kilichotukia wakati wa siku chache zilizofuata nilisimuliwa baadaye na familia yangu na wazee wawili wa Kikristo.
Kuchungulia Kaburi
Wakati huu madaktari walikubaliana kujaribu kunidunga sindano za imunoglobulini kwa kudunga kupitia ndani. Kuanzia Oktoba 9 hadi 11, nilipewa vima vya imunoglobulini vya gramu sita kila siku. Nilishindwa kudhibiti ukojoaji na uondoaji wangu wa choo, na daima wauguzi walibadili nguo za matandiko. Kiwango changu cha damu kiliendelea kupungua. Rekodi za kitiba husema hivi: “Kiasi cha chini kabisa cha kiwango cha hemoglobini kilikuwa 1.4, ambapo baadaye alikuwa na melena ya ziada [choo chenye damu], na iliamuliwa kuepuka kuchunguza kiasi cha damu yangu. Kufikia wakati huu alikuwa mahututi [yuafa].”
Madaktari walikuwa kwa wakati huo wamekata tamaa ya kupata kwangu ahueni, wakitaarifu kwamba nikiokoka, ningekuwa na madhara ya ubongo na labda pia kupooza upande mmoja. Walikuwa na uhakika sana hivi kwamba hakuna jambo lolote lingine lingeliweza kufanywa hivi kwamba Oktoba 12 iliamuliwa kusimamisha utibabu wowote na kutumia vioevu tu. Baba yangu, aliyenitia moyo kwa kuendelea ili kuendelea kupigana, alikuwa amekaa kando ya kitanda changu, akisema: “Sasa Ni Mia Tu na Yehova.”
Sikuzote katika kipindi hiki kigumu kulikuwako mtu kutoka kwa kutaniko kando ya kitanda pamoja na familia yangu. Mmoja wao alisimulia hivi: “Jumamosi jioni, Oktoba 12, hakuna yeyote aliyeamini Mia angeokoka usiku huo. Lakini asubuhi ya Jumapili alikuwa bado yu hai. Katika alasiri kupumua kwake kulikuwa kuzito, na kila mmoja alitazamia huku kuwa mwisho. Familia nzima ilikusanyika kukizunguka kitanda chake. Alivuta pumzi kwa nguvu na, baada ya kile kilichoonekana kama umilele, akashusha pumzi. Wazazi wake walipata umivu lililo kubwa zaidi wazazi wawezalo kupata—kumwona mtoto wampendao akipeperuka pole kwa pole. Baba ya msichana huyo alisema iliwapasa wote kumgeukia Yehova kwa sala. Baadaye tuliongea kichini-chini, tukitumaini kwamba Mia hangeliweza kuumia kwa muda zaidi.
“Lakini Mia hakufa. Madaktari na wauguzi hawajapata kamwe kuona jambo kama hilo—mtu kuishi akiwa na damu kidogo sana hivyo. Mvujo wa damu ulikoma, hivyo hali haikuharibika zaidi. Usiku wa Jumapili ulipita, na Mia alikuwa bado yu hai.”
Badiliko Kuu
Asubuhi ya Jumatatu, Oktoba 14, mmoja wa madaktari alikuja kuniona. Nilikuwa nasinzia na sikumbuki hilo tukio. Daktari alisimama kando ya kitanda changu, na mama alisema hivi: “Daktari yuko hapa ili kukuamkia.” Itikio langu lilikuwa “halo” yenye kusikika vizuri. Hakutazamia hilo, na alishangaa na kuguswa kihisia-moyo.
Ubongo wangu ulikuwa sawa, na sikupooza. Tiba ilirudiwa tena. Nilipewa erithropoietini na madini ya deksitrani kwa kupitishia ndani, pamoja na vima vya imunoglobulini viwili kila siku. Polepole hali yangu iliboreka. Oktoba 16 kiwango changu cha hemoglobini kiliongezeka hadi 2.6 na tarehe 17 kilifikia 3.0. Niliendelea kupata nafuu. Novemba 12 niliruhusiwa kuondoka hospitalini nikiwa na kiwango cha hemoglobini cha 8.0.
Hatujui kwa kweli ni kwa nini kuharibiwa kwa chembe nyekundu za damu kulikoma au kwa nini kiwango cha damu yangu kiliongezeka haraka hivyo. Zile sindano za imunoglobulini, erithropoietini, na madini ya deksitrani kwa wazi zilichangia sana. Kufikia mwanzo-mwanzo wa Mei 1992, kiwango changu cha hemoglobini kilikuwa kile cha kawaida 12.3, na kimebaki katika kiwango cha kawaida.
Sasa niko chini ya matibabu ya udumishaji ili kuidhibiti hali yangu, na mwili wangu unatenda vizuri. Novemba 28, 1992, niliolewa na Mkristo mwenzangu, na sasa tunamtumikia Yehova pamoja. Maradhi yangu, pamoja na kutii sheria ya Yehova juu ya damu, kumenivuta karibu zaidi na Yehova. Sasa natazamia kumtumikia kwa nguvu zangu zote kwa umilele wote.—Kama ilivyosimuliwa na Mia Bjørndal.
[Maelezo ya Chini]
a Utaratibu huu wajulikana kuwa plazimafesisi na hutia ndani mzunguko wa mfumo wa damu nje ya mwili. Uamuzi wa kutumia utaratibu huu umeachiwa dhamiri ya kila mmoja, kama ilivyozungumziwa katika Mnara wa Mlinzi wa Machi 1, 1989, kurasa 30 na 31.
b Uamuzi wa kutumia imunoglobulini, iliyo na kiasi kidogo cha damu, umeachiwa dhamiri ya kila mmoja, kama ilivyozungumziwa katika Mnara wa Mlinzi wa Juni 1, 1990, kurasa 30 na 31.