Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 2/8 kur. 8-9
  • Watoto Waliotupwa na Walio Watoro

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Watoto Waliotupwa na Walio Watoro
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Watoto Waliotupwa
  • Watoto Watoro
  • Watoto Waliotumiwa Vibaya Kuumizwa Kihisia-Moyo
  • Kutafuta “Uhuru”
  • Kwa Sababu Gani Kuna Watoto Wengi Sana Wanaotoroka?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Msiba Utakwisha Lini?
    Amkeni!—1995
  • Jinsi ya Kuimarisha Vifungo vya Kijamaa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • “Sasa Ninaipenda Huduma!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2021
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 2/8 kur. 8-9

Watoto Waliotupwa na Walio Watoro

“MIMI nilikata nywele zangu, nilivaa kama mwanamume, niliweka minyororo na mikufu shingoni mwangu, na nilibandika pini ya kujikinga shavuni mwangu, na kwa njia hii nilianza maisha yangu nikiwa mhuni.”—Tamara.

Ikiwa ulimwona Tamara mitaani, je, ungeshuku kwamba alikuwa tineja mpweke, mtendwa vibaya ambaye maisha ya nyumbani yalimwacha bila uangalifu na shauku aliyokuwa akililia? Je, ungemfikiri kuwa ni mwasi aliyeelekea matatani na sheria na labda afuate maisha ya uhalifu? Tamara afunulia Amkeni! matukio yenye kuogofya yaliyoongoza kwenye aina ya maisha aliyoishi tangu umri wa miaka 14, mtindo wa maisha ambao hakuupenda kamwe.

Watoto Waliotupwa

Tamara asimulia hivi: “Nilikulia katika mji mdogo wa mlimani katika Italia, katika familia ambayo shauku haikujulikana. Kwa kusikitisha, nilishuhudia mabishano makali yaliyofoka kati ya wazazi wangu na matusi yasiyosemeka waliyotupiana kwenye pindi hizo. Mara nyingi nilijikuta katika ugomvi huo na kucharazwa vilivyo na baba aliyekosa rehema. Nilikuwa na alama za mipigo hiyo kwa majuma.

“Nilipokuwa na miaka 14, baba yangu alinipatia dola kadhaa na tiketi ya kunifikisha tu kwenye jiji lililo karibu, ambapo palikuwa na hatari nyingi. Nilifanya urafiki na vijana wengine ambao, kama mimi, hawakuwa na yeyote aliyependezwa nao. Wengi wetu tukawa waraibu wa alkoholi. Nikawa mjeuri, mshenzi wa maneno, na mkali. Mara nyingi nilikosa chakula. Jioni moja wakati wa baridi marafiki zangu pamoja nami tulizichoma fanicha ili kujiendeleza tukiwa na ujoto. Jinsi nilivyopenda kuwa na familia yenye kunijali, iliyopendezwa na maoni yangu, mahangaiko yangu, hofu zangu. Lakini nilikuwa peke yangu, mpweke hoi.”

Kuna mamia ya maelfu ya “akina Tamara” katika ulimwengu wa leo. Katika kila kontinenti, kuna watoto walioachwa na wazazi waliopuuza madaraka yao.

Watoto Watoro

Vijana wengine huamua kuondoka nyumbani kwa sababu “ni mahali penye kutisha mno wasiweze kubaki hapo; ni penye kuumiza mno, ni penye hatari mno, nao hukimbilia mitaani.”—New York State Journal of Medicine.

Domingos, aliachwa akiwa na miaka tisa kwenye makao ya uyatima wakati mama yake alipoolewa tena. Kwa sababu ya kucharazwa alikopata kwa mapadri, alipanga kutoroka. Mama yake alimchukua tena, lakini alitiishwa kwa kuchapwa daima na baba yake wa kambo. Kutoroka kulikuwa ndio njia pekee aliyopata utulizo kutoka kwa ukatili nyumbani.

Kwa kusikitisha, “mamilioni ya watoto hawawezi kutumaini watu wazima walio nyumbani kwao wenyewe kwa ajili ya kiwango kidogo sana cha utunzi wenye usalama,” aandika Anuradha Vittachi katika kitabu chake Stolen Childhood—In Search of the Rights of the Child. Mwanamke huyo pia aandika hivi: “Watoto watatu wanakadiriwa kuwa hufa kila siku kwa sababu ya kutendwa vibaya na wazazi wao katika Marekani.” Katika visa vingi sana, ujinsia wa mtoto huchafuliwa badala ya kulindwa na washiriki wa familia.

Watoto Waliotumiwa Vibaya Kuumizwa Kihisia-Moyo

Domingos alilazimika kuishi pamoja na watoto wengine wa mitaani waliohusika na unyang’anyi na wizi, pamoja na kutumia vibaya dawa za kulevya na kuzichuuza. Kwa kusikitisha, wengi wakimbiao hali mbaya nyumbani hutumiwa vibaya na watafuta-walawitiwa, wagoni-watoto, na vigenge vya ponografia. Wakiwa wenye njaa na wapweke, vijana hawa hupewa mahali pa kukaa na ahadi za kuwa wanakuwa mali ya mtu mzima “anayejali,” kuja tu kupata kwamba wanalipa kwa miili yao katika maisha ya umalaya. Bila ustadi wa kazi, wengi hujifunza kumudu maisha mitaani kwa njia yoyote wawezayo, kutia ndani kutongozwa na kutongoza. Baadhi yao hawamudu maisha. Madawa ya kulevya, uuaji kikusudi, na kujiua huzoa vijana wengi kwa kuwaua.

Akieleza kuhusu maisha ya watoto wa mitaani, mmoja aliyekuwa kahaba-mtoto alisema hivi: “Watishika ukiwa huku nje. Unajua, kinikasirishacho ni kwamba [watu] wengi hufikiri kwamba waonapo mtoto amelala kwenye gari-moshi, au wakimwona mtoto mitaani kila mara, wao hufikiri kwamba anataka kuwa huko. Sasa kwa sababu nina umri mkubwa zaidi, hivyo sivyo ninavyoona. Watoto hawa kila mmoja aonyesha kwa njia ya kipekee kwamba ataka msaada. Hawataki kuwa hivyo, lakini wazazi wao hawawataki.”

Kutafuta “Uhuru”

Kuna mamia ya maelfu mengine ya vijana wameripotiwa kuwa wamepotea kutoka nyumbani walioshawishwa kuingia mitaani na uhuru waudhaniao kuwa unapatikana huko. Wengine hutaka uhuru wa kutokuwa na umaskini. Wengine hutamani uhuru kutoka kwa mamlaka ya kimzazi na sheria ambazo huenda wakahisi ni zenye kuzuia sana.

Kijana mmoja aliyeonja eti ule uitwao uhuru kutoka kwa udhibiti wa kimzazi na kanuni za nyumba ya Kikristo aliitwa Emma. Akiwa ameondoka nyumbani ili kuonja maisha pamoja na marafiki zake, alikuja kuwa mtumwa wa madawa ya kulevya. Lakini baada ya kuona ukatili wa mitaani, Emma alionyesha tamaa ya kurudi na kumaliza zoea lake la madawa ya kulevya. Ingawa hivyo, kwa kusikitisha, hakuacha kushirikiana na ushirika mbaya, na katika jioni fulani wakati wa kiangazi pamoja na marafiki zake, walijidunga heroini. Kwa Emma ilikuwa mara yake ya mwisho. Alikosa fahamu akafa siku iliyofuata, akiwa peke yake na ameachwa na “marafiki” zake.

Je, wakati ujao wa watoto waliodhulumiwa na wazazi au watu wengine waweza kuwa bora? Je, kutapata kuwako ulimwengu ambao hautawatumia vibaya vijana? Ni tumaini gani lililopo kwamba maisha ya familia yaweza kuboreshwa na kuthaminiwa ili kwamba walio wachanga hawatataka kutoroka? Majibu yaweza kupatikana katika makala inayofuata.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki