Maisha Yangu Yalikuwa Muziki, Dawa za Kulevya, na Unywaji wa Kupindukia
WAZAZI wangu ni Wahindi Waamerika. Baba, ambaye alikufa miaka minne iliyopita, alikuwa Mchippewa, kutoka Sugar Island, Michigan, Marekani. Mama yangu kutoka Ontario, Kanada, ni wa mataifa ya Wahindi ya Ottawa na Ojibwa. Kupitia baba yangu mimi ni wa kabila la Sault Sainte Marie la Wahindi wa Chippewa. Kwa sababu ya uvutano wa shule za misheni ya Kikatoliki na za bweni, tulilelewa tukiwa Wakatoliki, jambo ambalo lilimaanisha kuhudhuria Misa kila Jumapili.
Utoto wangu kwenye eneo lililotengwa la Wahindi ulikuwa sahili na wenye furaha. Kulingana na maoni ya mtoto, viangazi vilikuwa virefu, vyenye kusonga polepole, na vyenye amani. Tuliishi katika eneo la mbali—hatukuwa na maji ya mfereji wala vyoo vya ndani, na tulioga katika ziwa au katika birika kubwa la kufulia nguo. Mahali petu pa kucheza palikuwa nje. Farasi, ng’ombe, na wanyama wengineo wa shamba ndio waliokuwa vichezeo vyetu. Kwa wakati huo, nilitamani ulimwengu wote ungekuwa hivyo milele.
Magumu ya Kukua
Nilipokuwa na umri mkubwa zaidi na kwenda kwenye shule ya umma, ziara zangu nyumbani zikawa chache. Shule, michezo, na muziki zikaanza kuchukua wakati wangu mwingi. Nikiwa tineja katika miaka ya 1960, niliathiriwa na mtazamo wa wakati huo. Kufikia wakati nilipokuwa na umri wa miaka 13, dawa za kulevya na alkoholi zikawa sehemu ya kawaida ya maisha yangu. Uasi dhidi ya jamii ulipendwa na wengi, nikachukia kila kitu ambacho utaratibu wa kijamii ulikitegemeza. Sikuweza kuelewa kwa nini watu walifanyiana mambo yasiyo ya ubinadamu.
Karibu na wakati huu, nilipata gitaa yangu ya kwanza. Familia yetu ilipenda muziki. Baba yangu alikuwa mcheza-piano na mcheza dansi wa kugogota, na ndugu zake walipenda muziki pia. Kwa hiyo baba yangu na wajomba zangu walipokutana pamoja, tulicheza dansi aina ya jig na hoedown hadi alfajiri. Nilipenda hilo. Muda si muda, nikajifunza kucheza gitaa na kujiunga na kikundi cha rock-and-roll. Tulifanya maonyesho katika dansi za shule na matukio mengineyo. Hilo liliongoza kwenye mabaa na vilabu vya usiku, jambo lililomaanisha alkoholi na dawa za kulevya nyingi zaidi. Bangi na methamphetamine zilikuwa sehemu ya mtindo-maisha wangu.
Utumishi wa Kijeshi Katika Vietnam
Kufikia wakati nilipokuwa na umri wa miaka 19, nilikuwa nimeoa na mke wangu alikuwa mjamzito. Kwenye umri uo huo, nilisajiliwa kwa Wanajeshi wa Majini wa Marekani. Huo ulikuwa msongo mwingi sana kwangu. Ili kushughulikia kazi hiyo, nikabaki katika hali ya kulewa sana dawa za kulevya na alkoholi kwa saa 24 kwa siku.
Nilipewa mgawo katika kambi ya mazoezi ya msingi ya wanajeshi wa majini kwenye Marine Corps Recruit Depot katika San Diego, California, na kisha hadi mazoezi ya kijeshi ya juu kwenye Camp Pendleton, California. Nikapata mazoezi katika mawasiliano ya kijeshi ya uwanja wa pigano. Hiyo ilikuwa mwishoni mwa 1969. Sasa, mtihani halisi ulikuwa waja—utumishi katika Vietnam. Hivyo, nikiwa na umri wa miaka 19, miezi michache tangu nitoke shule ya sekondari, nilijipata nimesimama kwenye mchanga mwekundu wa Vietnam. Sawa na Wahindi Waamerika wengine wengi, uzalendo ulikuwa umenichochea kutumika jeshini japo ukosefu wa haki ambao jamii zilikuwa zimetufanyia sisi washiriki wa kikundi cha wachache.
Mgawo wangu wa kwanza ulikuwa katika Kikosi cha Kwanza cha Hewa cha Wanajeshi wa Majini, nje tu ya Da Nang. Wanaume 50 hivi—kwa kweli wavulana—walihusika katika kudumisha mfumo wa mawasiliano katika kambi ya jeshi. Tulikuwa na daraka la kushughulikia eneo lililoondolewa majeshi kati ya Vietnam Kaskazini na Vietnam Kusini hadi kilometa 80 kusini mwa Da Nang.
Wakimbizi walikuwa wakija kwa wingi Da Nang, na vibanda vilikuwa vikijengwa haraka kotekote. Kulikuwa pia na vituo vingi vya kutunzia mayatima. Kuona watoto hao wachanga, wengi wao wakiwa wamelemazwa, kulifanya niguswe moyo sana. Lilionekana kuwa jambo geni kwangu ajabu kwamba karibu wote walikuwa wasichana na wavulana wadogo. Punde nikajua sababu. Wavulana hao kuanzia umri wa miaka 11 kuendelea walikuwa wakipigana vitani. Baadaye, nilikutana na askari-jeshi mchanga wa Vietnam, nikamwuliza alikuwa na umri gani. Jibu lilikuwa “miaka 14.” Tayari alikuwa amekuwa vitani kwa muda wa miaka mitatu! Hilo lilinishangaza. Alifanya nimkumbuke ndugu yangu mwenye umri wa miaka 14, isipokuwa kwamba upendezi wa ndugu yangu haukuwa kuua bali Ligi Ndogo ya besiboli.
Wakati wa utumishi wangu katika jeshi la wanamaji, nilianza kuwa na maswali ambayo yalihitaji majibu. Usiku mmoja, nilienda kanisani katika kambi yetu. Kasisi wa jeshi Mkatoliki alitoa mahubiri juu ya Yesu, amani, na upendo! Nilitaka kupiga kelele. Mahubiri yake yalikuwa kinyume cha kila kitu kilichokuwa kikitendeka hapo. Baada ya kawaida hiyo ya ibada nilimwuliza jinsi angetetea kuwa Mkristo na kwa wakati uleule kupigana katika vita hiyo. Jibu lake? “Askari, hivi ndivyo tunavyopigana vita vyetu kwa ajili ya Bwana.” Nilienda zangu na kujiambia kwamba sikutaka kamwe kujihusisha na dini tena.
Mgawo wangu ulipokwisha, nilijua kwamba nilikuwa heri kuwa hai; lakini kiakili na kiadili nilikuwa nimeteseka sana. Kusikia, kuona, na kunusa vita na kifo kila siku kuliacha kovu kubwa kwenye akili na moyo wangu mchanga. Hata ingawa ilitukia miaka zaidi ya 25 iliyopita, kumbukumbu hizo zaonekana ni kama za jana.
Mng’ang’ano wa Kuishi Maisha ya Kiraia
Niliporudi nyumbani, nilianza kukazia fikira zangu kwenye kazi-maisha yangu ya muziki. Maisha yangu ya kibinafsi yalikuwa yamevurugika—nilikuwa nimeoa na nilikuwa na mtoto, na bado nilikuwa nikitumia sana dawa za kulevya na alkoholi. Uhusiano wangu na mke wangu ukawa na mkazo, na tokeo likawa talaka. Yaelekea hiyo ndiyo iliyokuwa hatua yenye mshuko-moyo kuliko zote maishani mwangu. Nilianza kujitenga na kutafuta kitulizo nje ya nyumba, kuvua samaki aina ya tirauti katika maeneo ya mbali sana ya Minnesota na Upper Michigan.
Katika 1974, nilihamia Nashville, Tennessee, nikiwa na lengo la kufanyia maendeleo kazi-maisha yangu ya muziki nikiwa mpiga-gitaa na mwimbaji. Nilicheza katika vilabu vingi vya usiku, sikuzote nikitumaini kuingia katika utendaji mkuu wa muziki. Lakini mambo hayakuwa rahisi—kulikuwa na wacheza-gitaa wengi sana wenye vipawa, wote wakijaribu kuwa wanamuziki mashuhuri.
Hata hivyo, ilipofika tu hatua ambapo mambo yalikuwa yakianza kwenda nilivyotaka na kuhisi uwezekano wa mafanikio ya kitaaluma, jambo fulani lilitokea ambalo lilinishtua.
Mtindo-Maisha Hatari
Nilikwenda kumtembelea rafiki wa zamani ambaye hapo mbeleni nilikuwa nikifanya shughuli za dawa za kulevya pamoja naye. Alinisalimia mlangoni akiwa na bunduki. Nusu ya mwili wake ilikuwa na plasta, na kinywa chake kilikuwa kimefungwa kwa waya kwa sababu ya utaya uliovunjika. Akiongea kupitia meno yake yaliyobanwa, aliniambia kilichokuwa kimetukia. Bila mimi kujua, alikuwa amejihusisha na shirika kubwa la dawa za kulevya katika Nashville, na kiwango kikubwa cha kokeni kilipotea. Wakuu wa dawa za kulevya wakamwekea mashtaka. Wakatuma majambazi wampige. Walimwambia arudishe kokeni hiyo au alipe dola 20,000 ambazo zingeweza kupatikana kupitia kuuza hiyo kokeni. Hakutishwa tu bali mke wake na mtoto walikuwa hatarini. Aliniambia kwamba haikuwa salama kwangu kuonekana pamoja naye hivyo lingekuwa jambo la busara niondoke. Nilifahamu alichomaanisha nami nikaenda.
Kisa hiki kilifanya nihofie uhai wangu. Bila kutambua, nilikuwa nimekuwa sehemu ya ulimwengu wenye jeuri. Wengi wa watu niliojua katika biashara ya muziki na uwanja wa dawa za kulevya walibeba bastola. Karibu ninunue bastola kwa ajili ya kujilinda. Nilitambua kwamba kadiri nilivyokaribia utendaji mkuu wa biashara ya muziki, ndivyo gharama ilivyokuwa ya juu. Kwa hiyo basi, niliamua kuondoka Nashville na nilikuwa nikipangia kwenda Brazili kujifunza muziki wa Amerika ya Latini.
Maswali Mengi, Majibu Machache
Japo maono yangu hasi kuhusu dini, nilikuwa na tamaa yenye nguvu ya kumwabudu Mungu. Na bado nilikuwa na maswali yasiyojibiwa. Kwa hiyo, nikaanza kutafuta kweli. Nilihudhuria vikundi tofauti-tofauti vya kidini lakini nikabaki bila kuridhika. Nakumbuka kanisa moja nililohudhuria katika Minnesota. Pasta alifupisha mahubiri kwa sababu timu ya mpira ya Minnesota Vikings ilikuwa ikicheza siku hiyo. Yeye alitutia moyo sote twende nyumbani na kuombea ushindi wa Vikings! Nilisimama na kutoka nje. Kufikiri kwa kijuu-juu kwamba Mungu huhusiana na utendaji wa kijuu-juu wa michezo hunikasirisha hadi leo.
Nilipokuwa nikifanya kazi katika Duluth, Minnesota, rafiki mmoja aliacha Mnara wa Mlinzi nyumbani kwangu. Nilisoma mazungumzo yalo ya Mathayo sura ya 24, yakaonekana kuwa kweli. Yalinifanya nifikiri, ‘Hawa Mashahidi wa Yehova ni akina nani? Yehova ni nani?’ Sikupata majibu hadi mwaka 1975. Rafiki yuyo huyo aliniachia kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milelea na Biblia.
Usiku huo nilisoma kitabu hicho. Kufikia mwisho wa sura ya kwanza, nilijua kwamba nilikuwa nimepata kweli. Ilikuwa kana kwamba shela imeondolewa akilini mwangu. Nilimaliza kitabu hicho, na siku iliyofuata nilikwenda ng’ambo ya barabara kwa majirani fulani walio Mashahidi na kuwaomba wajifunze Biblia pamoja nami.
Niliacha mipango yangu ya kusafiri hadi Brazili na kuanza kuhudhuria mikutano kwenye Jumba la Ufalme. Kwa msaada wa Yehova, niliacha dawa za kulevya na alkoholi mara moja na kabisa, nikijiweka huru baada ya miaka 12 ya uraibu. Baada ya miezi michache, nilikuwa nikishiriki katika huduma ya nyumba hadi nyumba.
Hata hivyo, kulikuwa na tatizo nililolazimika kukabili. Sikuwa nimepata kamwe kuwa na kazi ya kawaida ya kuajiriwa, na lile wazo la kuzuiwa na ratiba liliniudhi. Sasa ilikuwa lazima niwe mtu mwenye kuchukua daraka, kwa kuwa Debi aliingia maishani mwangu tena. Mapema nilikuwa nikifanya miadi ya kijinsia pamoja naye; lakini alikwenda chuoni kujifunza kuwa mwalimu, nami nilikuwa niwe mwanamuziki. Sasa pia yeye alikubali kweli za Biblia, na tukavutiana tena. Tulifunga ndoa na kubatizwa tukiwa Mashahidi katika Sault Sainte Marie, Ontario, Kanada, katika 1976. Baada ya muda, tukawa na watoto wanne—wavulana watatu na msichana.
Ili kuandalia familia yangu, nilifungua duka la muziki na kufundisha utungaji wa jazz na kucheza gitaa. Pia niliendesha studio ndogo ya kurekodia na pindi kwa pindi nikacheza katika vilabu vya usiku. Kisha, kwa kushangaza, fursa zikajitokeza kwangu kurudi kwenye umashuhuri wa ulimwengu wa muziki. Nilijiwa mara tatu nicheze nikiwa mtu wa badala kwa wasanii mashuhuri wa kurekodi. Hii ilikuwa fursa yangu kubwa—kwa hakika, ya tatu kwa miaka miwili. Nilitolewa fursa ya kwenda Los Angeles, California, kucheza na kikundi cha jazz kijulikanacho sana. Lakini nilijua kwamba ingemaanisha kurudi kwenye safari za kila mara, maonyesho, na vipindi vya kurekodi. Nilifikiria toleo hilo kwa muda mfupi na kwa staha nikasema, “La, asante.” Kukumbuka tu maisha yangu yaliyopita ya dawa za kulevya, alkoholi, na hatari kutokana na majambazi kulinifanya nitambue kwamba toleo hilo halikustahili. Maisha yangu mapya ya Kikristo pamoja na mke na watoto wangu yalimaanisha mengi zaidi kwangu.
Kwa miaka kadhaa nilifanya kazi nikiwa mhandisi wa utangazaji kwa ajili ya programu za kielimu ambazo zilionyeshwa kwenye televisheni ya PBS (Mfumo wa Utangazaji wa Umma). Katika kazi yangu ya wakati huu, naratibu uwasiliano wa vidio kwa Eneo la Wahopi kwa ajili ya chuo kikuu fulani katika Arizona kaskazini.
Nimerudi kwa Watu Wangu Mwenyewe
Miaka ishirini imepita tangu nijiweke wakfu kwa Yehova Mungu. Pia nimekuwa na miaka ishirini ya ndoa yenye furaha. Debi, mwana wetu Dylan, ambaye ana umri wa miaka 19, na binti yetu, Leslie, mwenye umri wa miaka 16, wote wako katika utumishi wa wakati wote. Dylan hasa anatumikia kwenye majengo ya Watchtower Society ya upigaji chapa na shamba huko Wallkill, New York. Wavulana wetu wawili wachanga, Casey, mwenye umri wa miaka 12, na Marshall, mwenye umri wa miaka 14, waliweka maisha zao wakfu kwa Yehova na kubatizwa hivi majuzi.
Miaka mitatu iliyopita tulikubali mwaliko wa kuhamia mahali ambapo uhitaji wa kuhubiri kwa Kikristo ulikuwa mkubwa na tukaja Keams Canyon, Arizona, kutumikia miongoni mwa Wahindi wa Navajo na Hopi. Mimi ni mzee katika kutaniko. Ni furaha kuishi tena miongoni mwa Wahindi Waamerika. Kwa sababu ya tofauti kati ya utamaduni na hali ya kuishi hapa na ile ya mitaa ya kawaida ya Marekani, twapata hisi ya kuwa katika kazi ya umishonari. Tuliacha nyumba kubwa yenye starehe ili kuja kuishi—tukiwa sita—katika nyumba ndogo iwezayo kuchukulika. Maisha hapa ni magumu zaidi. Nyumba nyingi hazina mifereji ya ndani, vyoo vya nje tu. Familia fulani husafiri kilometa nyingi wakati wa kipupwe ili kupata tu kuni na makaa. Maji huchotwa kutoka visima vya jumuiya. Barabara nyingi ni za mchanga na hazimo katika ramani. Nikiwa mtoto katika eneo hilo lililotengwa, sikufikiri hiyo ilikuwa hali ngumu. Sasa, familia yangu nami twathamini ni kiasi gani cha kazi ngumu na nishati kihitajiwacho kufanya tu kazi ndogo-ndogo za lazima za maisha.
Hata ingawa Wahindi wana mamlaka zao kwenye hayo maeneo yao, bado wanakabiliwa na matatizo yaleyale yanayopata serikali zote—mapambano ya kindani, ubaguzi, ukosefu wa fedha, ufujaji wa fedha, na hata uhalifu miongoni mwa maofisa wao na viongozi. Wahindi wakabili matatizo ya uraibu wa alkoholi, utumizi mbaya wa dawa za kulevya, ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, kutendana vibaya katika familia, na matatizo ya ndoa na ya familia. Wengine bado wanalaumu mzungu kwa hali yao ya sasa, lakini mzungu anapatwa na mapigo yayo hayo. Hata hivyo, japo msongo kutoka familia, marafiki, na watu wa mbari, Wahindi Waamerika wengi wanaitikia kazi ya kielimu ya Biblia ya Mashahidi wa Yehova. Wanaona kwamba urafiki pamoja na Mungu unastahili gharama yoyote. Wengi husafiri zaidi ya kilometa 120 kila njia ili kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Tuna furaha kushiriki habari njema za Ufalme wa Mungu pamoja na Wanavajo na Wahopi.
Natazamia kwa hamu siku ambayo utawala wa Yehova ‘utaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia’ na wakati ambapo wanadamu wote wenye utiifu wataishi pamoja kwa amani na upatano wakiwa familia moja iliyoungana. Kisha maisha yatakuwa kama nilivyotamani yawe nilipokuwa mvulana Mchippewa katika Kanada. (Ufunuo 11:18; 21:1-4)—Kama ilivyosimuliwa na Burton McKerchie.
[Melezo ya chini]
a Kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.; sasa hakipigwi chapa tena.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Nilikuwa nikitafuta majibu kwa maswali yangu kumhusu Mungu
[Picha katika ukurasa wa 15]
Juu: Familia yangu na, kushoto, rafiki Mnavajo
Chini: Nyumba yetu yenye kuchukulika karibu na Jumba la Ufalme