Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/8 kur. 12-16
  • Wakati Wao Ujao Una Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wakati Wao Ujao Una Nini?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Elimu ya Wenyeji wa Amerika
  • Ardhi Takatifu
  • Magumu ya Leo
  • Kukabiliana na Dawa za Kulevya na Alkoholi
  • Je, Suluhisho Ni Kasino na Kucheza Kamari?
  • Wakati Ujao Una Nini?
  • Maisha Katika Ulimwengu Mpya wa Upatano na Haki
  • Jina la Mungu Lilibadili Maisha Yangu!
    Amkeni!—2001
  • Jinsi Ulimwengu Wao Ulivyopotea
    Amkeni!—1996
  • Wazaliwa wa Amerika na Biblia
    Amkeni!—1999
  • Kukabiliana na Magumu ya Eneo la Pekee
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/8 kur. 12-16

Wakati Wao Ujao Una Nini?

KATIKA mahojiano na Amkeni!, chifu wa amani wa Wacheyenne Lawrence Hart alisema kwamba mojawapo matatizo yanayoathiri Wahindi ni kwamba “tumekabiliwa na kani za mchanganyo na mabadiliko ya utamaduni. Kwa kielelezo tunapoteza lugha yetu. Pindi fulani hii ilikuwa sera iliyofanywa kimakusudi na serikali. Jitihada nyingi zilifanywa za ‘kutustaarabisha’ kupitia elimu. Tulipelekwa shule za bweni na kukatazwa kusema lugha zetu za kienyeji.” Sandra Kinlacheeny akumbuka: “Nilipoongea kwa Kinavajo katika shule yetu ya bweni, mwalimu aliosha mdomo wangu kwa sabuni!”

Chifu Hart aendelea kusema: “Jambo lenye kutia moyo ni kwamba makabila mbalimbali yameamka. Hayo yanatambua kwamba lugha zayo zitatoweka jitihada zozote zisipofanywa za kuzihifadhi.”

Ni watu kumi tu wanaobaki ambao wanajua Kikaruk, lugha ya mojawapo makabila ya California. Mnamo Januari 1996, Wingu Radi-Nyekundu (Carlos Westez), Mhindi wa mwisho aliyejua lugha ya Kicatawba, alikufa akiwa na umri wa miaka 76. Hakuwa na mtu yeyote wa kuongea naye lugha hiyo kwa miaka mingi.

Kwenye Majumba ya Ufalme ya Mashahidi wa Yehova katika maeneo ya Wanavajo na Wahopi katika Arizona, karibu kila mtu huzungumza Kinavajo na Kihopi na Kiingereza. Hata Mashahidi wasio Wahindi wanajifunza lugha ya Kinavajo. Mashahidi wanahitaji kujua Kinavajo ili waweze kufanya kazi yao ya elimu ya Biblia, kwa kuwa Wanavajo wengi wanajua vizuri lugha yao pekee. Lugha za Kihopi na Kinavajo bado hujulikana sana, na vijana wanatiwa moyo kuzitumia shuleni.

Elimu ya Wenyeji wa Amerika

Kuna vyuo 29 vya Wahindi Marekani vyenye wanafunzi 16,000. Chuo cha kwanza kilifunguliwa Arizona katika 1968. “Hilo ni mojawapo mabadiliko mazuri zaidi katika Eneo la Wahindi, haki ya kuelimisha chini ya hali zetu wenyewe,” akasema Dakt. David Gipp wa Halmashauri ya Elimu ya Juu ya Wahindi. Katika Chuo Kikuu cha Sinte Gleska, somo la lugha ya Kilakota ni takwa.

Kulingana na Ron McNeil (Mhunkpapa wa Lakota), msimamizi wa Hazina ya Chuo ya Wahindi wa Amerika, idadi ya wasioajiriwa kazi miongoni mwa Wenyeji wa Amerika ni kati ya asilimia 50 hadi asilimia 85, nao Wahindi wana matarajio ya kuishi ya chini zaidi na viwango vya juu zaidi vya ugonjwa wa kisukari, kifua kikuu, na uraibu wa alkoholi kati ya kikundi kingine chochote katika Marekani. Elimu bora ni moja tu kati ya njia ziwezazo kusaidia.

Ardhi Takatifu

Kwa Wenyeji wengi wa Amerika, ardhi za mababu wao ni takatifu. Kama Radi Nyeupe alivyomwambia mbunge mmoja: “Ardhi yetu ndicho kitu tunachothamini zaidi duniani.” Walipokuwa wakifanya mikataba na mapatano, mara nyingi Wahindi walifikiria kwamba hayo yalikuwa ya kuruhusu wazungu watumie ardhi zao bali si kuzimiliki. Wahindi wa Sioux walipoteza ardhi yenye thamani sana katika Black Hills ya Dakota katika miaka ya 1870, wachimbaji walipomiminika huko wakitafuta dhahabu. Katika 1980, Mahakama Kuu Zaidi ya Marekani iliamuru serikali ya Marekani kulipa karibu dola milioni 105 za ridhaa kwa makabila manane ya Sioux. Kufikia leo hii makabila hayo yamekataa malipo hayo—wao wanataka ardhi yao takatifu, Black Hills ya South Dakota, irudishwe.

Wahindi wengi wa Sioux hawapendi kuona nyuso za marais wazungu zikiwa zimechongwa kwenye Mlima Rushmore, katika Black Hills. Katika mlima mmoja ulio karibu, wachongaji wanachonga mchongo mkubwa hata zaidi. Ni mchongo wa Farasi Mwehu, yule kiongozi wa vita wa Sioux wa Oglala. Mchongo huo utamalizika kufikia Juni 1998.

Magumu ya Leo

Ili kuokoka katika ulimwengu wa leo, Wenyeji wa Amerika wamelazimika kujirekebisha kupatana na hali katika njia mbalimbali. Wengi sasa wamesoma vizuri nao wamezoezwa katika vyuo, wakiwa na uwezo ambao wao waweza kutumia vizuri katika mazingira yao. Kielelezo kimoja ni Burton McKerchie aliye mwanana na ambaye ni Mchippewa kutoka Michigan. Yeye ametayarisha sinema za masimulizi za kutumiwa na Public Broadcasting Service na sasa anafanya kazi katika shule moja ya sekondari kwenye Eneo la Wahindi la Hopi katika Arizona, akiratibisha vipindi vya masomo kwa kutumia vidio katika jimbo hilo. Kielelezo kingine ni Ray Halbritter, kiongozi wa kabila la Oneida aliyesoma Harvard.

Arlene Young Hatfield, akiandika katika Navajo Times, alisema kwamba kijana Mnavajo hana uzoefu au hawezi kujidhabihu jinsi wazazi wake au wazazi wake wa kale walivyofanya walipokuwa wakikua. Yeye aliandika: “Kwa sababu ya mafaa [ya kisasa] wao hawajapata kamwe kukusanya au kutema kuni, kubeba maji, au kuchunga kondoo kama wazazi wao wa kale. Wao hawachangii maisha ya familia kama watoto wa siku nyingi zilizopita walivyofanya.” Yeye amalizia hivi: “Haiwezekani kuepuka matatizo mengi ya kijamii ambayo bila shaka yataathiri watoto wetu. Hatuwezi kuepusha familia zetu, au maeneo yetu na ulimwengu wote, wala hatuwezi kurudia maisha ambayo babu zetu wa kale waliyaishi.”

Hapo pana ugumu kwa Wenyeji wa Amerika—jinsi ya kushikilia mapokeo yao na maadili yao ya kipekee huku wakijipatanisha na ulimwengu wa nje unaobadilika haraka.

Kukabiliana na Dawa za Kulevya na Alkoholi

Hadi leo hii, uraibu wa alkoholi unaharibu kabisa jamii ya Wenyeji wa Amerika. Dakt. Lorraine Lorch, ambaye ametumikia miongoni mwa Wahopi na Wanavajo akiwa daktari wa watoto na wa kawaida kwa miaka 12, alisema hivi katika mahoji na Amkeni!: “Uraibu wa alkoholi ni tatizo kubwa sana kwa wanaume na wanawake. Miili yenye nguvu hushindwa na kunyauka kwa maini, vifo vya ghafula, ujiuaji kimakusudi, na mauaji. Inasikitisha kuona kwamba alkoholi inatangulizwa mbele ya watoto, mwenzi wa ndoa, na hata mbele ya Mungu. Kicheko hugeuka kuwa machozi, upole kuwa ujeuri.” Yeye aliongezea: “Hata baadhi ya sherehe, ambazo pindi moja zilionwa kuwa takatifu na Wanavajo na Wahopi, nyakati nyingine siku-hizi huchafuliwa na ulevi na uchafu. Alkoholi hunyang’anya watu hao wazuri afya yao, akili zao, uwezo wao wa kubuni, na utu wao wa kweli.”

Philmer Bluehouse, mpatanishi wa amani katika Idara ya Sheria ya kabila la Navajo, katika Window Rock, Arizona, alifafanua kwa njia isiyoudhi kuwa dawa za kulevya na alkoholi ni “dawa za kujitibu.” Matumizi hayo mabaya ya vitu hivyo hufunika huzuni nayo husaidia mtu kufunika magumu ya maisha bila kazi na mara nyingi bila kusudi.

Hata hivyo, Wenyeji wengi wa Amerika wamepigana kwa mafanikio dhidi ya hiki kinywaji cha “kishetani” ambacho kililetwa na mzungu nao wamejitahidi kushinda uraibu wa dawa za kulevya. Vielelezo viwili ni Clyde na Henrietta Abrahamson, kutoka Eneo la Wahindi la Waspokane katika Jimbo la Washington. Clyde ana mwili mnene, na nywele na macho meusi. Alieleza Amkeni! hivi:

“Tumeishi katika eneo letu sehemu kubwa ya maisha zetu, kisha tukahamia jiji la Spokane kuhudhuria chuo. Hatukupenda mtindo wetu wa maisha, ambao ulitia ndani alkoholi na dawa za kulevya. Tulijua aina hii tu ya maisha. Tulikua tukichukia mavutano hayo mawili kwa sababu ya matatizo ambayo tuliona yametokeza katika familia.

“Kisha tukakutana na Mashahidi wa Yehova. Hatukupata kusikia juu yao kabla ya kwenda jijini. Tulifanya maendeleo polepole. Labda kwa sababu hatukutumaini watu ambao hatukuwa tumewajua, hasa wazungu. Kwa kipindi cha miaka mitatu tulikuwa tukijifunza Biblia bila utaratibu. Tabia iliyokuwa ngumu zaidi kwangu kuacha ilikuwa kuvuta bangi. Nilikuwa mvutaji bangi tangu niwe na umri wa miaka 14, na nilikuwa na umri wa miaka 25 nilipoanza kujaribu kuacha. Nilikuwa nikilewa muda mwingi wa maisha yangu ya ujana. Katika 1986, nilisoma makala katika toleo la Januari 22 la Amkeni! (la Kiingereza), lenye kichwa “Kila Mtu Anavuta Bangi—Kwa Nini Nisivute?” Ilinifanya nifikirie jinsi ilivyokuwa upumbavu kuvuta bangi—hasa baada ya kusoma Mithali 1:22, ambalo lasema: ‘Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga? Na wenye dharau kupenda dharau yao, na wapumbavu kuchukia maarifa?’

“Nikaacha tabia hiyo, na katika masika ya 1986, tulifunga ndoa na Henrietta. Tulibatizwa mnamo Novemba 1986. Katika 1993 nikawa mzee kutanikoni. Binti zetu wote wawili walibatizwa kuwa Mashahidi 1994.”

Je, Suluhisho Ni Kasino na Kucheza Kamari?

Katika 1984 hakukuwa na kamari inayosimamiwa na Wahindi Marekani. Kulingana na The Washington Post, mwaka huu makabila 200 yanaendesha shughuli 220 za kamari katika majimbo 24. Tofauti kubwa sana ni Wanavajo na Wahopi, ambao kufikia sasa wamekataa vishawishi vya kamari. Lakini, je, majumba ya kasino na bingo ndiyo njia ya kupata ufanisi na kuleta kazi zaidi katika maeneo ya Wahindi? Philmer Bluehouse aliliambia Amkeni! hivi: “Kamari ni upanga wenye makali kuwili. Swali ni, Je, itafaidi watu wengi zaidi kuliko itakaowadhuru?” Ripoti moja yasema kwamba kasino za Wahindi zimewapa watu 140,000 kazi nchini kote lakini yasema kwamba ni asilimia 15 pekee kati ya kazi hizo zinazofanywa na Wahindi.

Chifu wa Wacheyenne, Hart, aliliambia Amkeni! maoni yake juu ya jinsi kucheza kamari kunavyoathiri maeneo ya Wahindi. Yeye alisema hivi: “Nina hisia tofauti-tofauti. Jambo zuri pekee ni kwamba kamari hutokeza kazi na mapato kwa makabila. Kwa upande mwingine, nimeona kwamba wateja wengi ni watu wetu wenyewe. Najua wengine ambao walinaswa na bingo, nao huondoka mapema nyumbani ili kwenda huko, hata kabla ya watoto kurudi kutoka shuleni. Kisha wao wawa watoto wa kubeba funguo na wa kukaa peke yao nyumbani mpaka wazazi wao warudi kutoka kucheza bingo.

“Tatizo kubwa ni kwamba familia zinaona kwamba zitashinda na kuongeza mapato yao. Kwa kawaida hawashindi; wao hupoteza. Nimewaona wakitumia pesa ambazo zimetengewa ununuzi wa bidhaa au mavazi ya watoto.”

Wakati Ujao Una Nini?

Tom Bahti aeleza kwamba kuna mambo mawili yapendwayo wakati wa kujadili wakati ujao wa makabila ya Kusini-Magharibi. “La kwanza latabiri kwa dhati kutoweka kunakokaribia kwa tamaduni za wenyeji katika maisha ya ujumla ya Waamerika. La pili halieleweki vizuri . . . Linasema kwa upole juu ya kuchanganyikana kwa tamaduni, likidokeza mchanganyiko wa uangalifu wa ‘utamaduni bora wa mapokeo ya zamani na mapya,’ aina fulani ya utamaduni bora kabisa ambao kwao Mhindi aweza kudumisha ustadi wake wa kale katika sanaa, na kuwa mwenye kuvutia katika dini yake na mwenye hekima katika falsafa yake—lakini mwenye kukubali sababu vya kutosha katika mahusiano yake nasi (utamaduni bora wa [mzungu]) na kuona mambo kwa njia yetu.”

Kisha Bahti auliza swali. “Ni lazima badiliko litukie, lakini ni nani atakayebadilika na kwa kusudi gani? . . . Sisi [wazungu] tuna tabia yenye kuchukiza ya kuwaona watu wengine wote kuwa tu Waamerika ambao hawajasitawi. Tunadhani kwamba ni lazima hawatosheki na njia yao ya maisha na wanatamani kuishi na kufikiri jinsi sisi tunavyofanya.”

Yeye aendelea kusema: “Jambo moja ni hakika—hadithi ya Mhindi wa Amerika haijaisha, lakini jinsi itakavyoisha au ikiwa itaisha ni jambo tunalongoja kuona. Labda, bado kuna wakati wa kuanza kufikiri juu ya jumuiya zetu za Wahindi kuwa vyanzo vyenye thamani vya utamaduni kuliko kuziona tu kuwa matatizo magumu ya kijamii.”

Maisha Katika Ulimwengu Mpya wa Upatano na Haki

Kutokana na maoni ya Biblia, Mashahidi wa Yehova wajua jinsi ulivyo wakati ujao wa Wenyeji wa Amerika na wa watu wa mataifa, makabila na lugha zote. Yehova Mungu ameahidi kuumba “mbingu mpya na nchi mpya.”—Isaya 65:17; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1, 3, 4.

Ahadi hii haimaanishi sayari mpya. Kama vile Wenyeji wa Amerika wanavyojua vema sana, dunia hii ni kito inapostahiwa na kutendewa ifaavyo. Badala ya hivyo, unabii wa Biblia waonyesha utawala mpya wa kimbingu ambao utachukua mahali pa serikali za wanadamu zenye kudhulumu. Dunia itafanyizwa kuwa paradiso yenye miti, nyanda, mito, na wanyama wa pori waliorudishwa. Watu wote watashiriki bila ubinafsi katika kutunza ardhi. Dhuluma na pupa hazitakuwapo tena. Kutakuwa na wingi wa chakula kizuri na utendaji wenye kujenga.

Pamoja na ufufuo wa wafu, ukosefu wote wa haki wa wakati uliopita utaondolewa. Ndiyo, hata wale Anasazi (neno la Kinavajo la “wakale”), wazazi wa kale wa wengi wa Wahindi wa Pueblo, wanaoishi Arizona na New Mexico, watarudi kupata fursa ya uhai udumuo milele hapa kwenye dunia iliyorekebishwa. Pia, wale viongozi maarufu katika historia ya Wahindi—Geronimo, Fahali Aketiye, Farasi Mwehu, Tecumseh, Manuelito, Chifu Joseph na Chifu Seattle—na wengine wengi waweza kurudi katika ufufuo huo ulioahidiwa. (Yohana 5:28, 29; Matendo 24:15) Ni tazamio zuri kama nini ambalo ahadi za Mungu zawatolea hao pamoja na wale wote wanaomtumikia sasa!

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nyumba ya asili ya Wanavajo, iliyojengwa kwa mbao na kukandikwa kwa udongo

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mfano wa Farasi Mwehu, unaotumiwa katika mchongo unaochongwa katika mlima unaonekana nyuma

[Hisani]

Picha ya Robb DeWall, kwa hisani ya Crazy Horse Memorial Foundation (shirika lisilo la kibiashara)

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mashahidi Wahopi na Wanavajo katika Keams Canyon, Arizona, hukutanikia Jumba la Ufalme lao, ambapo zamani palikuwa mahali pa biashara

[Picha katika ukurasa wa 16]

Makao ya “Anasazi” ya tangu zaidi ya miaka 1,000 iliyopita (Mesa Verde, Colorado)

[Picha katika ukurasa wa 16]

Geronimo (1829-1909), chifu mashuhuri wa Waapache

[Hisani]

Kwa hisani ya Mercaldo Archives/ Dictionary of American Portraits/Dover

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki