Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/8 kur. 7-12
  • Jinsi Ulimwengu Wao Ulivyopotea

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jinsi Ulimwengu Wao Ulivyopotea
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Upatano Uliosababisha Mapambano
  • “Mgawanyiko Katika Uelewano”
  • Muuaji Hatari Zaidi
  • Ni Nini Kilichopata Mikataba?
  • “Safari Ndefu” na Njia ya Machozi
  • Wakati Wao Ujao Una Nini?
    Amkeni!—1996
  • Wazaliwa wa Amerika na Biblia
    Amkeni!—1999
  • Wenyeji wa Amerika—Mwisho wa Muhula
    Amkeni!—1996
  • Jina la Mungu Lilibadili Maisha Yangu!
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/8 kur. 7-12

Jinsi Ulimwengu Wao Ulivyopotea

KWA miaka mingi hadithi ya Marekani ilielezwa kwa ufupi katika maneno haya, “Jinsi tulivyoshinda Magharibi.” Sinema za Hollywood zilionyesha masetla Wazungu wakivuka nyanda na milima ya Amerika, zikiwa na wanajeshi wanaofanana na John Wayne, cowboys, na masetla wakipigana na Wahindi wakali, wakatili, wenye mashoka ya vita. Mzungu alipokuwa akitafuta ardhi na dhahabu, makasisi wengine wa Jumuiya ya Wakristo na wahubiri eti walikuwa wakiokoa nafsi.

Historia hiyo ikoje kulingana na maoni ya wakazi wa awali, wenyeji wa Amerika? Kwa kufika kwa watu wa Ulaya, Wahindi “walilazimika kukabiliana na kuingiliwa kwa mazingira yao na mshambulizi mbaya zaidi waliopata kukabili wakati wowote ule: washambulizi kutoka Ulaya,” chasema kitabu The Native Americans—An Illustrated History.

Upatano Uliosababisha Mapambano

Mwanzoni, wengi wa watu wa Ulaya waliofika kwanza Kaskazini-Mashariki mwa Amerika walitendewa kwa fadhili na ushirikiano na wenyeji. Simulizi moja lasema: “Bila msaada wa Wapowhatan, makao ya Waingereza katika Jamestown, Virginia, ambayo yalikuwa koloni ya kwanza ya kudumu ya Uingereza katika yale Mabara Mapya, hayangeokoka majira ya kwanza ya kipupwe ya 1607-1608. Vivyo hivyo, koloni ya Wahamiaji katika Plymouth, Massachusetts, ingeanguka kama haingesaidiwa na Wawampanoaga.” Wenyeji fulani waliwaonyesha wageni hao jinsi ya kurutubisha udongo na kukuza mimea. Na safari ya uvumbuzi ya Lewis na Clark ya 1804-1806—ingefanikiwaje kupata njia nzuri ya uchukuzi kati ya Eneo la Louisiana na kile kilichoitwa Eneo la Oregon bila msaada na kuingilia mambo kwa mwanamke Mshoshone aliyeitwa Sacagawea? Yeye alikuwa “ishara [yao] ya amani” walipokutana ana kwa ana na Wahindi.

Hata hivyo, kwa sababu ya jinsi watu wa Ulaya walivyokuwa wakitumia ardhi na ugavi mdogo wa chakula, kuhamia Amerika Kaskazini kwa wingi kulisababisha uhasama kati ya washambulizi na wenyeji. Mwanahistoria Mkanada Ian K. Steele aeleza kwamba katika karne ya 17, kulikuwa na Wanarragansett wapatao 30,000 katika Massachusetts. Chifu wao Miantonomo, “akiona hatari, . . . alijaribu kujenga muungano wake pamoja na Wamohawk ili kufanyiza upinzani wa ujumla wa Wahindi wa Amerika.” Inaripotiwa kuwa aliwaambia Wamontauk hivi katika 1642: “Ni [lazima] tuungane kama vile wao [Waingereza] wameungana, la sivyo tutatokomea karibuni, kwa kuwa mwajua baba zetu walikuwa na dia wengi na ngozi nyingi, nyanda zetu zilijaa dia, na pia misitu yetu, na kujaa [bata mzinga], na ghuba zetu kujaa samaki na ndege. Lakini Waingereza hawa baada ya kunyakua ardhi yetu, walifyeka nyasi wakitumia vifyekeo, na kwa shoka wakakata miti; ng’ombe na farasi zao hula nyasi, na nguruwe zao huharibu fuo zetu za vivaaute, nasi tutakufa njaa.”—Warpaths—Invasions of North America.

Jitihada za Miantonomo za kufanyiza muungano wa Wenyeji wa Amerika hazikufua dafu. Katika 1643, alishikwa katika vita ya kikabila na Chifu Uncas wa kabila la Mohegan, aliyempeleka kwa Waingereza kuwa yeye ni mwasi. Waingereza hawakuweza kumhukumu Miantonomo kisheria na kumuua. Wao wakafikiria suluhisho bora. Steele aendelea kusema: “Wakishindwa kumfisha [Miantonomo], ambaye hangehukumiwa na yoyote ya koloni zilizokuwapo, makamishna walimlazimisha Uncas amuue, kukiwa na mashahidi wa Uingereza kuthibitisha kwamba kweli ameuawa.”

Jambo hili halionyeshi tu mapambano ya daima kati ya wakoloni wenye kushambulia na wenyeji bali pia uadui wa kuchinjana-chinjana na hila miongoni mwa makabila, ambao ulikuwapo hata kabla ya mzungu kupata kufika Amerika Kaskazini. Katika vita vyao na Ufaransa juu ya udhibiti wa koloni ya Amerika Kaskazini, Waingereza walifanya makabila fulani yaiunge mkono, huku mengine yakiunga mkono Wafaransa. Haidhuru ni upande gani ulioshindwa, makabila yote yalipata hasara.

“Mgawanyiko Katika Uelewano”

Lifuatalo ni oni moja juu ya ushambulizi wa watu wa Ulaya: “Kile ambacho viongozi wa makabila ya Wahindi hawakuelewa, mara nyingi mpaka kuchelewa mno, ni jinsi watu wa Ulaya walivyowaona Wahindi. Wao hawakuwa Wazungu wala Wakristo. Wao walikuwa wakatili—hayawani wakorofi—akilini mwa wengi, watu hatari wasio na ubinadamu ambao walifaa tu kuuzwa utumwani.” Mtazamo huu wa kuwa bora uliathiri sana hayo makabila.

Wenyeji wa Amerika hawakuelewa maoni ya watu wa Ulaya. Kulikuwako, kama alivyouita mshauri fulani Mnavajo Philmer Bluehouse katika mahoji ya majuzi na Amkeni!, “mgawanyiko katika uelewano.” Wenyeji hawakuona ustaarabu wao ukiwa duni lakini badala ya hivyo, kuwa tofauti, ukiwa na maadili tofauti kabisa. Kwa kielelezo, kuuza ardhi kulikuwa jambo la kigeni sana kwa Wahindi. Je, unaweza kumiliki na kuuza hewa, upepo, na maji? Basi kwa nini uuze ardhi? Ardhi ni ya kutumiwa na kila mtu. Hivyo, Wahindi hawakuweka kingo kwenye ardhi zao.

Kufika kwa Waingereza, Wahispania, na Wafaransa kukatokeza kile ambacho kimeitwa “kukutana kwenye msiba kwa tamaduni mbili za kigeni.” Wenyeji walikuwa watu ambao kwa mamia ya miaka wameishi kwa kupatana na ardhi na asili na ambao walijua jinsi ya kuishi bila kuharibu usawaziko wa mazingira. Lakini, upesi mzungu akaja kuona wakazi wenyeji kuwa viumbe vya hali ya chini na wakali—mzungu akisahau ukatili wake mwenyewe katika kuwatiisha! Katika 1831, Mwanahistoria Mfaransa Alexis de Tocqueville, alitaja kifupi maoni ya mzungu yaliyoenea juu ya Wahindi: “Mungu hajawafanya wastaarabike; ni lazima wafe.”

Muuaji Hatari Zaidi

Masetla wapya walipoendelea kwenda magharibi kuvuka Amerika Kaskazini, jeuri ikatokeza jeuri. Hivyo, iwe ni Wahindi au watu wa Ulaya walioshambulia kwanza, pande zote mbili zilifanya mambo ya ukatili. Hao Wahindi waliogopwa kwa sababu ya sifa yao ya kung’oa ngozi ya kichwa ikiwa na nywele, zoea ambalo watu wengine wanaamini kwamba walijifunza kutoka kwa watu wa Ulaya ambao walikuwa wakiwapa vitu kwa kubadilishana na ngozi za vichwa vya watu. Hata hivyo, hao Wahindi walikuwa wakishindwa vitani dhidi ya Wazungu waliokuwa wengi na wenye silaha bora. Katika visa vingi makabila hayo yalilazimika kuacha ardhi zao za uzaliwa au kufa. Mara nyingi hali hizo zote ziliwapata—waliacha ardhi zao kisha wakauawa au kufa kwa maradhi na njaa kali.

Lakini, si vita vilivyowaua makabila ya wenyeji zaidi. Ian K. Steele aandika: “Silaha kali zaidi katika ushambulizi wa Amerika Kaskazini haikuwa bunduki, farasi, Biblia, au ‘ustaarabu’ wa Ulaya. Ilikuwa maradhi.” Kuhusu athari za maradhi ya Mabara ya Zamani katika Amerika, Patrica Nelson Limerick, ambaye ni profesa wa historia, aliandika: “Yalipopelekwa Mabara Mapya, maradhi yaleyale [ambayo watu wa Ulaya walikuwa wamesitawisha kinga kwayo baada ya karne nyingi]—tetekuwanga, surua, kamata, malaria, homa ya kimanjano, homa ya chawa, kifua kikuu, na zaidi ya yote, ndui—yaliwashika wenyeji. Kiwango cha vifo vijijini kikawa juu kufikia asilimia 80 na 90.”

Russell Freedman asimulia mweneo wa ndui iliyotokea 1837. “Kwanza ni Wamandan walioshikwa, wakifuatwa kwa mfululizo na Wahidatsa, Waassiniboin, na Waarikara, Wasioux, na kabila la Blackfeet.” Wamandan karibu watokomee kabisa. Kutoka watu wapatao 1,600 katika 1834, wao walipunguka hadi 130 katika 1837.

Ni Nini Kilichopata Mikataba?

Hadi leo hii wazee wa makabila waweza kutaja tarehe za mikataba ambayo serikali ya Marekani ilifanya na babu zao wa kale katika karne ya 19. Lakini mikataba hiyo hasa iliandaa nini? Mara nyingi ilikuwa ni ubadilishano usiofaa wa ardhi nzuri kwa maeneo makavu na msaada kidogo kutoka kwa serikali.

Kielelezo cha jinsi makabila ya wenyeji yalivyotendwa vibaya ni kisa cha makabila ya Wairoquois (toka mashariki hadi magharibi, Wamohawk, Waoneida, Waonondaga, Wacayuga, na Waseneca) baada ya Waingereza kushindwa na wakoloni wa Amerika katika vita ya uhuru, ambayo iliisha 1783. Wairoquois waliunga mkono Waingereza, nao walilipwa tu, kulingana na Alvin Josephy, Jr., kuachwa na matusi. Waingereza, “wakipuuza [Wairoquois], walikuwa wameipa Marekani enzi juu ya ardhi za Wairoquois.” Yeye aongeza kwamba hata Wairoquois ambao walikuwa wamependelea wakoloni dhidi ya Waingereza “walishawishiwa na makampuni ya kununua ardhi na wahatarishaji wa fedha ili kupata faida na serikali yenyewe ya Amerika.”

Wakati mkutano wa mkataba ulipofanywa katika 1784, James Duane, aliyekuwa zamani mwakilishi wa Halmashauri ya Masuala ya Wahindi ya Bunge la Bara, alihimiza wawakilishi wa serikali “kudhoofisha kujistahi kokote kulikobaki miongoni mwa Wairoquois kwa kuwatendea kama watu wa hali ya chini kimakusudi.”

Madokezo yake ya kiburi yalitekelezwa. Baadhi ya Wairoquois walishikwa mateka, na “majadiliano” yakafanywa wakielekezewa bunduki. Ingawa wanajiona kuwa hawakushindwa vitani, Wairoquois walilazimika kuacha ardhi yao yote magharibi ya New York na Pennsylvania na kukubali eneo dogo katika Jimbo la New York.

Mbinu kama hizo zilitumiwa pia dhidi ya makabila mengine mengi ya wenyeji. Josephy asema pia kwamba wawakilishi wa Amerika walitumia “hongo, matisho, vileo, na hila za wawakilishi wasio rasmi kuwanyang’anya ardhi Wadelaware, Wawyandot, Waottawa, Wachippewa [au Waojibwa], Washawnee, na makabila mengine ya Waohio.” Si ajabu kwamba upesi Wahindi wakaja kukosa kumtumaini mzungu na ahadi zake zisizotimizwa!

“Safari Ndefu” na Njia ya Machozi

Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe ya Marekani (1861-1865) ilipotokea, hiyo iliondoa majeshi kutoka nchi ya Wanavajo katika Kusini-Magharibi. Wanavajo wakatwaa pindi hiyo kushambulia makao ya Waamerika na Wamexico katika Bonde la Rio Grande katika eneo la New Mexico. Serikali ikampeleka Kanali Kit Carson na kikosi chake cha Wajitoleaji wa New Mexico kukomesha Wanavajo na kuwapeleka katika eneo fulani katika ukanda wa ardhi kavu iliyoitwa Bosque Redondo. Carson akafuatia sera ya kuharibu kabisa riziki ili kufanya Wanavajo wapate njaa na kuwaondosha kwenye ile Canyon de Chelly yenye kutisha, katika kaskazini-mashariki mwa Arizona. Hata aliharibu zaidi ya miti 5,000 ya pichi.

Carson alikusanya watu wapatao 8,000 na kuwalazimisha kutembea “Safari Ndefu” ya maili zipatazo 300 hadi kambi ya kizuizi ya Bosque Redondo katika Fort Sumner, New Mexico. Ripoti moja yasema hivi: “Kulikuwa na baridi kali sana, na wengi wa wahamishwa hao wasiovalia vizuri na kupungukiwa chakula walikufa njiani.” Hali zilizokuwa katika kambi zilikuwa mbaya sana. Wanavajo walilazimika kuchimba mashimo ardhini ili kujaribu kupata himaya. Katika 1868, baada ya kugundua makosa makubwa iliyokuwa imefanya, serikali iliwapa Wanavajo ekari milioni 3.5 ya ardhi yao ya uzaliwa katika Arizona na New Mexico. Walirudi, lakini walikuwa wamelazimika kulipa gharama kubwa kama nini!

Kati ya 1820 na 1845, makumi ya maelfu ya Wachoctaw, Wacherokee, Wachickasaw, Wacreek, na Waseminole waliondoshwa kutoka ardhi zao katika Kusini-Mashariki na kulazimishwa kutembea kuelekea magharibi, ng’ambo ya Mto Mississippi, hadi pale paitwapo sasa Oklahoma, wengine walitembea kufikia mamia ya maili. Wengi walikufa katika hali ngumu za kipupwe. Hiyo safari ya kulazimishwa kuelekea magharibi ikapata sifa mbaya ya Njia ya Machozi.

Ukosefu wa haki waliotendewa Wenyeji wa Amerika wathibitishwa zaidi na maneno ya jenerali mmoja wa Amerika George Crook, ambaye alikuwa amewawinda Wasioux na Wacheyenne katika kaskazini. Yeye alisema: “Upande wa Wahindi katika kesi mara nyingi hausikilizwi. . . . Kisha wakati [Wahindi] wanapoasi ndipo uangalifu wa umma unaelekezewa Wahindi, uhalifu wao na ukatili wao pekee unashutumiwa, huku watu ambao ukosefu wao wa haki umewafanya watende hivyo huachwa bila kuadhibiwa . . . Hakuna mtu ajuaye jambo hili kwa njia bora kuliko Wahindi wenyewe, na kwa hiyo yeye hana hatia akiona ukosefu wa haki wa serikali ambayo inamwadhibu tu, huku ikimruhusu mzungu kumpora kama atakavyo.”—Bury My Heart at Wounded Knee.

Wenyeji wa Amerika wanaendeleaje leo baada ya kudhibitiwa na watu wa Ulaya kwa zaidi ya miaka mia moja? Je, wako katika hatari ya kutoweka kwa sababu ya kuchanganyikana na wengine? Wao wana tumaini gani kwa wakati ujao? Makala ifuatayo itafikiria maswali haya na mengine.

[Sanduku katika ukurasa wa9]

Maisha Magumu kwa Wanawake

Huku wanaume wakiwa wawindaji na wapiganaji katika makabila mengi, wanawake walikuwa na kazi nyingi sana, kutia ndani kulea watoto, kupanda na kuvuna nafaka, na kuzisaga kuwa unga. Colin Taylor aeleza hivi: “Daraka kubwa la wanawake Wahindi . . . lilikuwa kudumisha nyumba iliyoanzishwa, kuzaa watoto na kutayarisha chakula. Katika jamii za ukulima wao pia walilima mashamba, . . . huku, katika makabila ya kuhama-hama ya kuwinda nyati-singa katika magharibi, wao walisaidia kuchinja huyo mnyama, wakileta nyama kambini na kutayarisha nyama na ngozi kwa ajili ya matumizi ya wakati ujao.”—The Plains Indians.

Kitabu kingine chasema hivi kuhusu Waapache: “Kazi za shamba zilikuwa kazi za wanawake na haikuwa kamwe kazi ya kushusha hadhi au ya kutweza. Wanaume walisaidia, lakini wanawake walichukua ukulima kwa uzito kuliko wanaume. . . . Sikuzote wanawake walijua jinsi ya kudumisha desturi za ibada za kilimo. . . . Wanawake wengi walisali wakinyunyizia ardhi maji.”—The Native Americans—An Illustrated History.

Wanawake pia walijenga makao ya muda yaitwayo tepees, ambayo mara nyingi yalidumu kwa miaka miwili. Wao waliyajenga na kuyaharibu kabila lilipolazimika kuhama. Bila shaka, wanawake waliishi maisha magumu. Na ndivyo ilivyokuwa na wanaume ambao walikuwa walinzi wa hilo kabila. Wanawake walistahiwa nao walikuwa na haki nyingi. Katika baadhi ya makabila, kama vile Hopi, hata leo hii ni wanawake ndio wenye mali.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Mnyama Aliyebadili Ulimwengu Wao

Watu wa Ulaya walileta mnyama mmoja Amerika Kaskazini ambaye alibadili mtindo-maisha wa makabila mengi—farasi. Katika karne ya 17, Wahispania walikuwa wa kwanza kuleta farasi katika kontinenti ya Amerika. Wenyeji wa Amerika wakawa waendeshaji farasi stadi bila tandiko, kama vile watu wa Ulaya wenye kushambulia walivyotambua upesi. Wakiwa na farasi, wenyeji waliweza kuwinda nyati-singa kwa urahisi zaidi. Na makabila ya kuhama-hama yaliweza kwa njia rahisi zaidi kushambulia makabila jirani yaliyoishi katika vijiji vya kudumu na hivyo kupora mali, wanawake na watumwa.

[Ramani katika ukurasa wa 7]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Mahali pa baadhi ya makabila katika Amerika Kaskazini katika karne ya 17

Kutenai

Spokan

Nez Perce

Shoshone

Klamath

Northern Paiute

Miwok

Yokuts

Serrano

Mohave

Papago

Blackfoot

Flathead

Crow

Ute

Hopi

Navajo

Jicarilla

Apache

Mescalero

Lipan

Plains Cree

Assiniboin

Hidatsa

Mandan

Arikara

Teton

Cheyenne

Sioux

Yankton

Pawnee

Arapaho

Oto

Kansa

Kiowa

Comanche

Wichita

Tonkawa

Atakapa

Yanktonai

Santee

Iowa

Missouri

Osage

Quapaw

Caddo

Choctaw

Ojibwa

Sauk

Fox

Kickapoo

Miami

Illinois

Chickasaw

Alabama

Ottawa

Potawatomi

Erie

Shawnee

Cherokee

Catawba

Creek

Timucua

Algonquian

Huron

Iroquois

Susquehanna

Delaware

Powhatan

Tuscarora

Micmac

Malecite

Abnaki

Sokoki

Massachuset

Wampanoag

Narragansett

Mohegan

Montauk

[Habari kuhusu chanzo cha ramani]

Mhindi: Mchoro unategemea picha ya Edward S. Curtis; North America: Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 8]

Ufumaji na vito vya kisanii vya Wanavajo

[Picha katika ukurasa wa 11]

Canyon de Chelly, ambako “Safari Ndefu” ilianza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki