Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 2/8 kur. 14-17
  • Bara Ligeukapo Kuwa Jangwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Bara Ligeukapo Kuwa Jangwa
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Majangwa Hubadilika-Badilika, na Fasili Kubadilika
  • Ugeukaji wa Bara Kuwa Jangwa
  • Visababishi vya Msingi na Matokeo
  • Hakuna Suluhisho la Mara Moja
  • ‘Nyika Itafurahi’
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1998
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1994
  • Mali za Asili za Dunia Zinapungua
    Amkeni!—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 2/8 kur. 14-17

Bara Ligeukapo Kuwa Jangwa

YASEMEKANA kwamba bara katika karibu nchi 100 lageuka polepole kuwa jangwa, ikiathiri maisha ya zaidi ya watu milioni 900 na kusababisha hasara ya kila mwaka inayokadiriwa kuwa dola bilioni 42 katika mapato ya ulimwenguni pote. Ingawa maeneo yenye umaskini ndiyo yenye kuathiriwa vibaya sana (81 kati ya nchi hizo ni nchi zinazoendelea), ugeukaji wa bara kuwa jangwa hutisha nchi katika kontinenti zote.

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) huita ugeukaji wa bara kuwa jangwa “moja ya matatizo mabaya sana ya mazingira ya tufeni pote.” Wakati huohuo, watafiti wasema pia kwamba “jangwa halienei.” Hilo lawezekanaje?

Majangwa Hubadilika-Badilika, na Fasili Kubadilika

Baada ya ukame wa muda mrefu katika eneo la Afrika la Sahel (1968-1973), picha ya majangwa yakifunika mashamba ilikazwa katika akili za watu. Hata hivyo, “mandhari za huzuni na msiba” ambazo wanasayansi walizifafanua wakati huo, asema Donald A. Wilhite, mkurugenzi wa Kitovu cha Kimataifa cha Habari za Ukame kwenye Chuo Kikuu cha Nebraska (Marekani), “zilitegemea habari chache sana kwa kipindi kifupi sana cha wakati kwa kulinganishwa ambazo zilitoa wazo lisilo sahihi.”

Picha za hali ya juu za satelaiti ambazo hutambua kiwango cha vitu vilivyo hai sasa huonyesha kwamba kiwango cha mimea hubadilika-badilika wakati wa misimu mikavu na ya mvua. Mabadiliko-badiliko haya, wasema wataalamu, “hutoa wazo kwamba jangwa linapanuka au kupunguka.” Kwa hiyo majangwa “hubadilika-badilika” lakini si sikuzote “yanapoenea.” Hata hivyo, asisitiza Dakt. Wilhite, “ugeukaji wa bara kuwa jangwa unatokea.” Lakini hilo lamaanisha nini hasa?

Ugeukaji wa Bara Kuwa Jangwa

“Ugeukaji wa bara kuwa jangwa” mara nyingi hukosa kutofautishwa na kupanuka na kupunguka kwa majangwa. Hata hivyo, ugeukaji wa bara kuwa jangwa, chaeleza kikundi kimoja cha watafiti, hurejezea jambo tofauti. Ingawa kupanuka na kupunguka hutokea kwenye viunga vya majangwa yaliyopo, ugeukaji wa bara kuwa jangwa hutokea sana katika maeneo yaliyokauka, mengine yayo yakiwa mbali sana na jangwa lolote. Maeneo makubwa ya mabara hayo makavu ya kilimo, ambayo hufanyiza asilimia 35 ya uso wa bara la dunia, polepole yanageuka kuwa majangwa. Jambo hilo ndilo sasa huonwa kuwa ugeukaji wa bara kuwa jangwa.

Hata hivyo, japo maoni haya mapana kuhusu ni wapi ugeukaji wa bara kuwa jangwa hutukia, kukanganyikiwa kuhusu mambo hayo mawili huendelea. Kwa nini? Panos, shirika la habari linaloshughulikia hasa masuala ya maendeleo lililo na makao yalo makuu katika London, hutaja sababu moja. Nyakati nyingine, wafanyiza sera huendelea kuzungumza juu ya kupanuka kwa jangwa kwa sababu ni “rahisi kuamsha utegemezo wa kisiasa kwa dhana hii kuliko utaratibu tata zaidi wa ‘ugeukaji wa bara kuwa jangwa.’”

“Ujuzi wenye kubadilika,” lataja Panos, “umechochea mjadala mkubwa juu ya maana hasa ya ‘ugeukaji wa bara kuwa jangwa.’” Suala ni nini? Wanadamu dhidi ya tabia ya nchi. Kwanza, UM lilidokeza kufasili ugeukaji wa bara kuwa jangwa kuwa “kuharibiwa kwa bara katika maeneo yaliyo na ukame, na yasiyo makame sana na maeneo yasiyo na unyevu mwingi kukitokezwa hasa na athari mbaya kubwa ya mwanadamu.” (Italiki ni zetu.) Fasili hii haikufurahisha nchi nyingi, asema Camilla Toulmin, mkurugenzi wa Mradi wa Mabara-Kavu kwenye Taasisi ya Kimataifa ya Mazingira na Maendeleo, kwa sababu humwelekezea mwanadamu lawama la ugeukaji wa bara kuwa jangwa. Hivyo, hivi majuzi, sehemu ya mwisho ya fasili hiyo ilibadilishwa kuwa “kukitokezwa na mabadiliko-badiliko ya tabia ya nchi na utendaji wa mwanadamu.” (Italiki ni zetu.) Fasili hii mpya huweka lawama la ugeukaji wa bara kuwa jangwa juu ya mwanadamu na vilevile tabia ya nchi, lakini haikumaliza huo mjadala. Kwa nini?

“Wataalamu fulani huamini,” lasema Panos, “kwamba kuongezeka huko kwa fasili na mabishano yatokeayo kwa kweli ni jaribio la kupata fedha zaidi kwa ajili ya nchi nyingi zaidi zionwazo kuwa hatarini.” Tokeo la bishano lenye kuendelea ni kwamba “neno hilo ni kama limekosa maana.” Kuna wale ambao hata huhisi kwamba neno “ugeukaji wa bara kuwa jangwa” lapaswa kuachwa kabisa. Hata hivyo, kulibadili kwa neno jingine, bila shaka hakutatatua tatizo hilo au kuondoa visababishi vyalo. Ni nini vilivyo visababishi vya ugeukaji wa bara kuwa jangwa?

Visababishi vya Msingi na Matokeo

Kitabu Desertification, kilichoandikwa na Alan Grainger, husema kwamba visababishi vya msingi ni kulima shamba kupita kiasi, kulisha wanyama mahali kupita kiasi, kukata miti, na mazoea ya hali ya chini ya unyunyizaji wa maji. Viwili au zaidi ya visababishi hivi vinapotukia pamoja, tokeo kwa kawaida ni ugeukaji wa bara kuwa jangwa. Isitoshe, mambo yenye kuchangia—kama vile kubadilika kwa idadi ya watu, tabia ya nchi, na hali za kijamii na kiuchumi—hufanya tatizo hilo liwe baya zaidi.

Moja ya matokeo ya wazi ya ugeukaji wa bara kuwa jangwa ni kuharibika kwa uwezo wa bara kavu kutokeza chakula. Hilo latukia ulimwenguni pote lakini hasa katika Afrika, ambapo asilimia 66 ya kontinenti hiyo ni jangwa au bara kavu. Hata hivyo, ugeukaji wa bara kuwa jangwa, una matokeo mengine mabaya zaidi. Huongoza kwenye vita. “Katika utata wa visababishi vinavyoongoza kwenye ukosefu wa uthabiti kijamii na kisiasa, umwagikaji wa damu na vita,” chaonelea kitabu Greenwar—Environment and Conflict, “kuharibiwa kwa mazingira kunazidi kuchangia.”

Hata jitihada za kuzuia vita hudhuru mazingira, ikitokeza umaskini. Jinsi gani? “Zikikabiliwa na ukosefu wa uthabiti unaotokezwa na kupigania rasilimali zenye kutoweka kunakotokezwa na kuharibiwa kwa bara,” laeleza Panos, “serikali mara nyingi huitikia kwa mbinu za kijeshi ili kukandamiza jeuri. Kwa njia hii, serikali huelekeza fedha zilizopo katika bajeti za kijeshi badala ya kuondosha umaskini.” Hata hivyo, badala ya kupambana na matokeo ya ugeukaji wa bara kuwa jangwa, ni nini kiwezacho kufanywa ili kupambana na visababishi hivi?

Hakuna Suluhisho la Mara Moja

Baada ya kutafakari swali hilo kwa miezi 13, wawakilishi wa zaidi ya nchi 100 walianzisha “Kongamano la UM la Kupambana na Ugeukaji wa Bara Kuwa Jangwa,” mpango ambao kulingana na UM ni “hatua ya muhimu kusonga mbele” katika kupambana na ugeukaji wa bara kuwa jangwa. Kongamano hilo lilihitaji, miongoni mwa mambo mengine, kuhamishwa kwa tekinolojia za kupambana na ugeukaji wa bara kuwa jangwa kutoka nchi zilizoendelea hadi kwenye nchi zinazoendelea, kuanzisha programu za utafiti na mazoezi na, hasa, utumizi bora zaidi wa ujuzi wa wenyeji. (UN Chronicle) Je, mwafaka huu mpya utakomesha kuharibiwa kwa bara kavu?

Ili kufaulu katika pambano hilo, lasema Panos, maneno na vile vile utegemezo uonekanao wahitajiwa. Hama Arba Diallo, mmoja wa wapangaji wa kongamano hilo, aliripoti kwamba kati ya 1977 na 1988, dola zipatazo bilioni moja kwa mwaka zilitumiwa kwa hatua za kuzuia ugeukaji wa bara kuwa jangwa. Hata hivyo, ili kufanya maendeleo ya kweli, kulingana na UNEP, mataifa hayo 81 yanayoendelea yahitaji kutumia kiasi kipatacho mara nne hadi nane cha kiwango hicho.

Lakini ni nani atakayelipia gharama hizo? “Kutakuwa na fedha mpya chache kutoka nchi zilizoendelea kwa ajili ya kazi ya kuzuia ugeukaji wa bara kuwa jangwa,” laonya Panos, likiongeza kwamba ni “jambo lisilo halisi kwa nchi zinazoendelea ambazo zapatwa na ugeukaji wa bara kuwa jangwa kutarajia suluhisho la haraka kutoka kwa kongamano hilo.” Hata hivyo, lamalizia Panos kwa hali chanya, uhakika wa kwamba ugeukaji wa bara kuwa jangwa unazungumziwa ulimwenguni pote hufanya tatizo hilo lijulikane hadharani, “jambo ambalo ni mafanikio.”

‘Nyika Itafurahi’

Kwa kweli, katika kipindi cha miongo iliyopita, wanaume na wanawake wengi wamefaulu katika kuwafahamisha wanadamu juu ya msiba mkubwa utakaoletwa na ugeukaji wenye kuendelea wa bara kuwa jangwa. Maneno ya shime kama vile “Mwanadamu hutanguliwa na misitu, na kufuatwa na jangwa” hutolea watu mwito wa ushindani wa kubadili hali hiyo.

Hata hivyo, watu wenye ufahamu hutambua pia kwamba tatizo la ugeukaji wa bara kuwa jangwa ni tata. Wanatambua vyema kadiri ya kujua kwamba mwanadamu, hata awe na nia nzuri kadiri gani, ana mapungukio kwa habari ya kushughulika na visababishi vya matatizo ya leo ya tufeni pote.

Hata hivyo, kwa wakati uleule, inachangamsha moyo wa watu wanaohangaikia wakati ujao wa sayari yetu kujua kwamba Muumba wa dunia ameahidi kushughulikia kwa matokeo tatizo hili na matatizo mengineyo ya mazingira. Na kwa kuwa ahadi za Mungu zilizorekodiwa katika Biblia sikuzote zimethibitika kuwa kweli, ni jambo la akili kutazamia utimizo wa kile Yehova alimpulizia nabii wake Isaya kuandika kuhusu wakati ujao wa majangwa na mabara yaliyoharibiwa: “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. . . . Maana katika nyika maji yatabubujika, na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji.” (Isaya 35:1-7; 42:8, 9; 46:8-10) Itakuwa shangwe iliyoje kushuhudia, katika wakati ujao karibuni, utaratibu wa ugeukaji wa bara kuwa jangwa kukomeshwa na kubadilishwa!

[Sanduku katika ukurasa wa 16]

Asilimia ya Bara Ambalo Ni Jangwa au Bara Kavu

Afrika․ Asilimia 66

Asia․ Asilimia 46

Australia․ Asilimia 75

Ulaya․ Asilimia 32

Amerika Kaskazini․ Asilimia 34

Amerika Kusini․ Asilimia 31

Ulimwengu․ Asilimia 41

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

Je, Unyunyizaji wa Maji Hugeuza Bara Kuwa Jangwa?

Je, unyunyizaji wa maji—kumwagilia bara maji—waweza kugeuza bara kuwa jangwa? Ndiyo, unyunyizaji wenye kasoro hufanya hivyo. Hilo hutukia wakati bara lililonyunyiziwa maji haliondolewi maji ifaavyo. Kwanza, udongo hujaa maji; kisha, hugeuka kuwa na chumvi; na baadaye, ganda la chumvi hujifanyiza kwenye uso wa bara. “Unyunyizaji wenye kasoro,” laonelea Panos, “unageuza bara kuwa jangwa haraka sana kadiri mifumo mipya ya unyunyizaji ianzishwavyo.”

[Ramani katika ukurasa wa 16, 17]

JANGWA LILILO

HATARINI

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1995 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Bara la kilimo likigeuka polepole kuwa jangwa

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki