Kuutazama Ulimwengu
Msononeko wa Watoto Wachanga Waliositawi kwa Haraka
Maneno “watoto wachanga waliositawi kwa haraka” yalitungwa kuwafafanua watu waliozaliwa kati ya mwisho wa vita ya ulimwengu ya pili na mwanzo wa miaka ya 1960. Wakati wa pindi hiyo nchi nyingi zilizokuwa katika upande ulioshinda wa vita hiyo ziliripoti ongezeko dhahiri la idadi ya watu. Ukaguzi uliohusisha nchi 16 ulionyesha kwamba watoto wachanga waliositawi kwa haraka, ambao wakati mmoja walikuwa wachangamfu na wenye kutumainia mema kuhusu wakati ujao, sasa “huhisi wakikosa usalama pamoja na watoto wao, na kuona uzee wao kuwa kama kitu chenye kutia wasiwasi sana,” lasema gazeti la habari la European. Kwa nini msononeko huo? “Sasa wanakabiliwa na ulimwengu ambao wanahisi umepita kiasi kwa habari ya ubinafsi, ufuatiaji wa vitu vya kimwili na ukosefu wa kujidhibiti na tabia nzuri,” yataarifu ripoti hiyo.
Maambukizo Yaliyofichika ya Mchochota wa Ini-C
“Mchochota wa ini-C waonekana kuwa hangaiko kubwa la afya ya umma katika Ufaransa,” yasema ripoti moja kutoka kwa kikundi cha madaktari wa Ufaransa. Madaktari wanaonyesha kwamba mengi ya maambukizo ya mchochota wa ini-C hugunduliwa baada tu ya mgonjwa kudodoswa kuwa amekuwa na maradhi ya ini ya kudumu kwa kipindi cha miaka 10 hadi 30. Ambukizo la virusi vya mchochota wa ini-C laweza kufisha na mara nyingi hupitishwa kwa kutiwa damu mishipani na matumizi ya dawa za kulevya zipitishwazo mishipani. Ripoti hiyo yaonya kwamba njia zaidi za kuchuja zilizo kamili zahitajiwa kwa hima, kwa kuwa chini ya robo ya wale wapatikanao kuwa wameambukizwa walijua hapo awali kwamba walikuwa na virusi hivyo. Kulingana na jarida Hepatology, wakazi wa Ufaransa wanaokadiriwa kuwa 500,000 hadi 650,000 kwa sasa wameambukizwa na virusi hivyo.
Kunyonyesha Maziwa ya Mama Hupunguza Magonjwa
“Watoto wachanga wanyonyeshwao maziwa ya mama wana uwezekano mdogo wa kupatwa na maambukizo ya masikio na kuharisha, kulingana na uchunguzi uliofanyiwa zaidi ya watoto 1,700 wenye umri wa miezi 2 hadi 7,” lataarifu gazeti Parents. “Watafiti katika Vitovu vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi walipata kwamba mtoto mchanga ambaye hulishwa mchanganyiko wa maziwa pekee huwa na uwezekano wa mara mbili wa kusitawisha moja ya hali hizi kama mtoto mchanga ambaye ananyonyeshwa tu.” Ingawa kwa muda mrefu madaktari wamehisi kwamba maziwa ya matiti huzuia ambukizo kwa sababu hupitisha fingo za mama, uchunguzi huonyesha kwamba manufaa ni zenye maana. Asema Laurence Grummer-Strawn, mwandishi wa uchunguzi huo: “Ni sahihi kusema kwamba kadiri mtoto mchanga apewavyo maziwa ya matiti katika miezi sita ya kwanza, ndivyo huwa bora zaidi.”
Kutoboa Huleta Matatizo
Kutoboa mwili kwaweza kuwa ndio mtindo wa muda katika nchi fulani, lakini “midomo iliyotobolewa, mashavu, na ndimi huleta hatari zaidi ya ambukizo,” laripoti The Journal of the American Medical Association. Kulingana na madaktari wa meno katika Shule ya Utaalamu wa Meno, ya Chuo Kikuu cha West Virginia katika Morgantown, “maumivu, kuvimba, ambukizo, ongezeko la mtiririko wa mate, na jeraha la ufizi ni mambo yaliyo ya kawaida kwa wagonjwa waliotobolewa midomo. . . . Vito kwa ajili ya midomo iliyotobolewa husababisha hatari za ziada.” Vito vyaweza kubambua au kuvunja meno, vyaweza kutokeza vizuizi vya usemi, kusababisha uumbikaji wa tishu za kovu, na—ikiwa vitamezwa—vitaziba njia ya hewa.
Hakuna Mashindano Tafadhali
Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC), lenye washiriki wa makanisa 330, “limetoa mwito wa kukomeshwa kwa jitihada za ‘kushindana’ na makanisa fulani yanayowinda washiriki wapya kutoka kwa makanisa mengine,” laripoti ENI Bulletin. “Kihususa baraza hilo la WCC linachambua matumizi ya ‘misaada ya fadhila’ katika nchi zinazoendelea . . . ili kuwashawishi maskini, walio na upweke na wakimbizi wabadili uaminifu wao wa kidini.” Miongozo ilitolewa ya kutofautisha kati ya ‘ushuhuda unaokubalika wa Gospeli na kugeuza watu kidini kusikokubalika.’ Unaotiwa ndani ya kugeuza watu kidini kusikokubalika ni “uchambuzi usio na haki” wa kanisa jingine, kuonyesha itikadi za mtu kuwa ndizo za kweli, kuwatolea fursa ya elimu au misaada ya fadhila, kuwashawishi wengine wajiunge na kanisa lingine, matumizi ya nguvu au mkazo wa kisaikolojia ili kuwachochea watu wabadili ushirikishaji wao wa kidini, na kutumia kwa faida taabu za watu au “kufadhaika kwao na dini yao kusudi ‘kugeuza’ imani yao.”
Ukataji-Miti Katika Italia
Ingawa kwa kawaida si nchi ambayo hushirikishwa na majangwa, Italia imeanzisha Halmashauri ya Kitaifa ya Kupigana Dhidi ya Jangwa. Sababu? Ukosefu wa rutuba katika udongo wazidi kusonga kwa haraka kuelekea upande wa kaskazini katika Italia. “Ikiwa sera madhubuti za kimazingira hazianzishwi ili kupunguza gesi zinazochangia kuongezeka kwa joto na kubadili mazoea fulani yasiyofaa ya kilimo,” lasema gazeti la habari La Stampa, “katika muda wa miongo michache tu, asilimia 27 ya eneo la [Italia] laweza kuwa ardhi iliyounguzwa.” Onyo hilo lilitolewa kwenye mkutano wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo uliofanyiwa huko Roma kuhusu ukataji-miti. Ilielezwa kwamba kanda zilizo hatarini hazijawekewa mipaka tu kwa maeneo ya kusini mwa Italia ya Sicily, Sardinia, Calabria, Apulia, na Basilicata bali kwamba maeneo fulani ambayo kwa kawaida huzalisha ya kaskazini yameathiriwa pia na sasa yanaripoti upungufu wa rutuba katika udongo.
Kutibu Kuharisha kwa Utotoni
“Watafiti wa Venezuela wametokeza dawa ya chanjo ambayo karibu huondoa kabisa kuharisha kubaya miongoni mwa watoto,” lasema The Daily Journal la Caracas. “Dawa hiyo ya chanjo . . . imekusudiwa kulinda dhidi ya kuharisha kunakoletwa na rotavirus, ambayo huua karibu watoto 873,000 walio chini ya umri wa miaka mitano katika nchi zinazoendelea kila mwaka.” Hata katika Marekani, ugonjwa huu bado huwalaza hospitalini watoto wachanga na wale ambao bado kuanza shule zaidi ya 100,000 kila mwaka. Uchunguzi huo, uliochapishwa katika The New England Journal of Medicine, waripoti kwamba matumizi ya dawa hii ya chanjo yalikuwa na kiwango cha kuzuia cha asilimia 88 dhidi ya kirusi hicho na yalipunguza visa vya wenye kulazwa hospitali kwa asilimia 70. Hata hivyo, kuna kipingamizi. “Huenda matibabu haya yakawa ghali sana kwa nchi zinazoendelea ambapo dawa hii huhitajika zaidi,” lasema The Daily Journal—nchi “ambazo hutumia chini ya dola 20 kila mwaka kwa ajili ya utunzaji wa afya wa mtu mmoja.” Mpaka dawa hiyo ya chanjo itolewapo kwa bei ya chini, kuishiwa maji kunakotokana na kuharisha lazima kutibiwe kwa kurudisha umajimaji uliopotezwa, njia ambayo imetumiwa kwa matokeo kwa miaka 20.
Risiti ya Hekalu Yapatikana
Ile “inayoonekana kuwa risiti ya mchango ya shekeli tatu za fedha kwa Hekalu la Yahweh,” “hivi karibuni imetokea kwenye masoko ya vitu vya kale,” lataarifu Biblical Archaeology Review. “Huu ndio mtajo wa kale zaidi usiokuwa wa Kibiblia kuhusu Hekalu la Mfalme Solomoni uliopata kugunduliwa. [Yale maneno] BYT YHWH, ‘nyumba ya Bwana [Yahweh],’ . . . yalipatikana yakiwa kamili katika moja tu ya mwandiko wa ziada usiokuwa wa Kibiblia,” na kwa sababu ya muktadha usio dhahiri, maana yake imebishaniwa. Kigae kipya kilichoandikwa, kilicho na ukubwa wa sentimeta 10.9 kwa sentimeta 8.6 na chenye mistari mitano na maneno 13, ni dhahiri na husomeka kwa urahisi. Kikiwa na tarehe ya mapema inayofikia karne ya tisa K.W.K., angalau ni kizee kwa karne moja kuliko mwandiko ule mwingine na kimetangazwa kuwa halisi na wataalamu.
Bishano Juu ya Malkia wa Sheba
Katika Ethiopia yeye huitwa Makeda. Katika Yemen jina lake ni Bilqis. Anajulikana vizuri zaidi kuwa malkia wa Sheba, anayetajwa katika Biblia na Kurani pia. Kila nchi hudai alikuwa shujaa wao wa kike na kutumaini kwamba karibuni ziara lake litapatikana hapo, wakitia moyo waakiolojia wazidi kuchimba ili kupata ithibati. Ikiwa uthibitisho wa malkia wa Sheba waweza kupatikana, eneo hilo litakuwa sehemu kubwa ya kuwavutia watalii na itahalalisha madai ya nchi hiyo ya kuwa na uhusiano na ustaarabu wa kale. “Waakiolojia wamepata michoro mingi kutoka kwa ufalme wa kale wa Sheba kwenye mawe ya kale katika Ethiopia na Yemen,” laonelea The Wall Street Journal. “Jambo la ajabu ni kwamba, hakuna moja itajayo Makeda au Bilqis.” Laongezea: “Biblia haisaidii sana. Inaeleza kwa undani dhahabu na viungo ambavyo Sheba alipeleka kwa Solomoni, lakini haisemi alikotoka.”
Hatikunjo Zilizotekwa Nyara
Wasamaria, ambao sasa wamepunguka kufikia 600 tu, lazima watokeze dola milioni moja kama fidia ili kuvipata tena vitabu vyao vitakatifu. Hizo hatikunjo mbili, zinazosemekana kuwa zenye miaka 700 na 400, kila moja ziliibiwa kutoka kwenye sinagogi la Wasamaria katika jiji la West Bank la Nablus miaka mitatu iliyopita. Wezi waliiba kisiri hatikunjo hizo na kuzitoa nje ya nchi, na ni juzi tu zilipoonekana katika Amman, Yordani, ambapo zilitazamwa na wazee Wasamaria. Inaaminiwa kwamba ziliibiwa na mtu aliyefahamiana na mahali zilipowekwa. Wasamaria wengi huishi kwenye kilele cha mlima juu ya Nablus, ambalo ndilo eneo lao lililo takatifu zaidi. Wanaamini kwamba, ni hapo, ambapo Mungu alimwamuru Abrahamu amtoe mwana wake Isaka kuwa dhabihu.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 29]
Kwa hisani ya: Shlomo Moussaieff