Uthibitisho wa Mafaa ya Maziwa ya Mama
Na mleta habari za Amkeni! katika Nigeria
EBU wazia chakula cha watoto wachanga ambacho ni kitamu, ni rahisi kuyeyuka, na chenye mahitaji yote ya vitoto vinavyokua. Ebu wazia chakula ambacho ni “tiba ya kiajabu” yenye kukinga mwili na vilevile kutibu maradhi. Chakula ambacho hakigharimu chochote na hupatikana kwa urahisi kwa kila familia duniani pote.
Wasema haiwezekani? Ndiyo, kuna chakula kama hicho, ingawa hakijasitawishwa na wanasayansi wa kibiashara. Ni maziwa ya mama.
Katika historia yote ya ainabinadamu chakula hiki kizuri kimeonwa kuwa muhimu sana kwa utunzi wa mtoto. Kwa kielelezo, Biblia yatuambia kwamba binti ya Farao alipokipata kitoto Musa, aliagiza dada yacho amtafute ‘mwanamke mlezi’ amtunzie huyo. (Kutoka 2:5-9) Baadaye, katika jamii za Kigiriki na Kiroma, wanawake watunzi wenye nguvu kwa kawaida waliajiriwa kunyonyesha vitoto vya wazazi matajiri. Hata hivyo, katika miongo ya miaka ya karibuni, zoea la kunyonyesha limepunguka sana, sababu moja ikiwa ni matangazo ya kibiashara ambayo yamefanya watu wafikiri kwamba maziwa ya matiti si bora kuliko vyakula vyenye kutengenezwa kwa tekinolojia ya kisasa. Leo, mwendo huo unabadilika kadiri mama wengi zaidi na zaidi wanavyokuja kutambua kwamba “matiti ni bora zaidi.”
Lishe Bora Zaidi
Je! wanasayansi wamefanya iwe bora ile njia ya kindani ya ulaji wa watoto? La hasha. Shirika la Hazina ya Watoto Ulimwenguni (UNICEF) lasema: “Maziwa ya matiti pekee ndicho chakula bora na kinywaji bora zaidi kwa watoto walio katika umri wao wa miezi minne hadi sita ya kwanza.” Maziwa ya matiti huwa na protini zote, vichochezi vya ukuzi, mafuta, wanga, vimeng’enya, vitamini, na vitu vidogo-vidogo ambavyo ni muhimu kwa ukuzi wenye afya wa kitoto katika miezi ya kwanza ya maisha.
Si kwamba maziwa ya matiti ni chakula bora tu kwa ajili ya watoto waliotoka kuzaliwa bali hayo pia ndiyo chakula cha pekee wanachohitaji. Mkutano wa Afya Ulimwenguni ulithibitisha katika Mei 1992 kwamba “katika miezi minne hadi sita ya kwanza ya uhai hakuna chakula au kinywaji chochote mbali na mazi-wa ya matiti, wala hata maji kinachohitajika kuandaa mahitaji ya lishe ya kitoto.” Maziwa ya matiti huwa na maji ya kutosha kuridhisha kiu cha mtoto hata katika hali-hewa zenye joto jingi na ukavu. Kumlisha mtoto maji ya ziada au vinywaji vyenye sukari kwa chupa hakufai tu bali pia kwaweza kumfanya mtoto aache kabisa kunyonya matiti, kwa sababu kwa kawaida watoto hupendelea ule urahisi wa kunyonya chupa. Bila shaka, baada ya miezi michache ya kwanza ya uhai, vyakula na vinywaji vingine vyapasa viongezwe polepole kwa ulaji wa mtoto.
Hakuna chakula kingine cha badala kiwezacho kuandaa mchanganyiko wenye kusawazika wa kuendeleza ukuzi wenye afya na maendeleo ya vitoto. Kitabu Reproductive Health—Global Issues chasema: “Majaribio ya kubadili maziwa ya matiti hayajafanikiwa. Fasihi ya historia ya habari ya ulishaji wa kitoto imejaa na uthibitisho kwamba vitoto visivyonyonyeshwa matiti vimo katika hatari kubwa zaidi ya uambukizo na utapiamlo kuliko vyenye kunyonyeshwa matiti.”
Kunyonyesha Matiti Huokoa Uhai
Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), vifo vya vitoto milioni moja ulimwenguni pote vingeepukwa kila mwaka ikiwa mama wote wangelisha watoto wao maziwa ya matiti pekee katika miezi minne hadi sita ya kwanza ya uhai. Ripoti ya UNICEF State of the World’s Children 1992 yasema: “mtoto mwenye kunyonyeshwa chupa katika jumuiya ya hali ya chini ana uwezekano wa karibu mara 15 kufa kutokana na maradhi ya kuhara na uwezekano wa mara 4 kufa kutokana na ugonjwa wa kichomi kuliko mtoto anyonyeshwaye matiti pekee.”
Kwa nini? Sababu moja ni kwamba maziwa ya unga haina lishe bora kwa kulinganisha na maziwa ya matiti na mara nyingi hutiwa kupita kiasi maji yasiyo safi na kutumiwa katika chupa za kunyonyesha zisizo safi. Kwa hiyo maziwa ya chupa yanaweza kwa urahisi kuwa na bakteria na virusi vinavyosababisha maradhi ya kuhara na maambukizo ya kupumua, magonjwa yenye kuua watoto zaidi katika nchi zinazoendelea. Kwa kutofautisha, maziwa yatokayo moja kwa moja kutoka kwenye matiti hayaambukizwi kwa urahisi, hayahitaji kuchanganywa, hayaharibiki, na hayawezi kuwa na maji kupita kiasi.
Sababu ya pili ifanyayo kunyonyesha matiti kuokoe maisha ni kwamba maziwa ya mama huwa na viua-vijasumu vinavyolinda kitoto hicho dhidi ya maradhi. Na hata maradhi ya kuhara au maambukizo mengine yakitokea, mara nyingi hayawi makali sana na ni rahisi kutibu miongoni mwa vitoto vyenye kunyonyeshwa matiti. Watafiti wadokeza pia kwamba watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya matiti huonekana hawapatwi sana na maradhi ya meno, kansa, kisukari, na mizio. Na kwa sababu kunyonyesha hutaka tendo la kunyonya kwa bidii, kunyonyeshwa matiti kwaweza kuendeleza ukuzi unaofaa wa mifupa na misuli ya uso wa vitoto.
Manufaa kwa Akina Mama
Kunyonyesha matiti hakunufaishi mtoto mchanga tu; hunufaisha mama vilevile. Sababu moja ni kwamba kunyonya kwa mtoto huchochea kutokezwa kwa hormoni inayoitwa oksitosini, ambayo haisaidii tu kutokezwa na kutiririka kwa maziwa bali pia hufanya mji wa mimba upungue ukubwa. Mji wa mimba unapopungua bila kukawia baada ya kujifungua mtoto, uwezekano wa kutokwa damu kwa muda mrefu huwa mdogo. Kunyonyesha matiti hukawiza kurudi kwa vipindi vya kutoa mayai na hedhi. Tendo hilo huelekea kukawiza kushika mimba kunakofuata. Vipindi virefu kati ya mimba humaanisha afya bora zaidi kwa akina mama na watoto.
Manufaa mengine makubwa kwa wanawake ni kwamba kunyonyesha matiti hupunguza uwezekano wa kupatwa na kansa ya kifuko cha mayai na ya matiti. Wastadi wengine husema kwamba hatari ya kansa ya matiti kwa mwanamke ambaye hunyonyesha kitoto chake ni nusu ya kama hangefanya hivyo.
Jambo lisilopasa kupuuzwa katika orodha ya manufaa ya kunyonyesha matiti ni ule ushikamano wa mama na mtoto. Kwa sababu kunyonyesha matiti hakutii ndani tu kutoa chakula bali pia kugusana moja kwa moja, mgusano wa ngozi kwa ngozi, na ujoto wa kimwili, huko kwaweza kufanyiza ushikamano muhimu kabisa kati ya mama na mtoto na kwaweza kuchangia ukuzi wa mtoto wa kihisia-moyo na kijamii.
Kuamua Kunyonyesha Matiti
Karibu mama wote huwa na uwezo wa kimwili wa kuandaa maziwa ya kutosha kwa vitoto vyao ikiwa matakwa fulani yafuatwa. Kunyonyesha mtoto kwapaswa kuanze upesi iwezekanavyo baada ya kuzaa, katika muda wa saa ya kwanza baada ya kumzaa mtoto. (Maziwa ya matiti ya kwanza, umaji-maji mzito wenye rangi ya kimanjano unaoitwa kolostrumi, huwa mazuri kwa watoto na huwalinda dhidi ya maambukizo.) Baadaye, watoto wapaswa kunyonyeshwa wanapotaka, kutia ndani usiku, wala si kulingana na ratiba fulani rasmi. Ni muhimu pia kumweka mtoto ifaavyo kwenye matiti. Mshauri mwenye maarifa na mwenye huruma aweza kusaidia katika mambo haya.
Bila shaka, uamuzi wa mama wa kukinyonyesha kitoto au kutokinyonyesha wategemea mambo mengi kuliko tu uwezo wake wa kimwili wa kufanya hivyo. The State of the World’s Children 1992 huripoti: “Akina mama wahitaji utegemezo wa hospitali ikiwa watawapa watoto wao mwanzo bora kabisa uwezekanao; lakini ikiwa wataendelea kunyonyesha mtoto, watahitaji pia utegemezo wa waajiri, vyama vya wafanyakazi, jumuiya—na wa wanaume.”
[Sanduku katika ukurasa wa 13]
Kunyonyesha Matiti Katika Ulimwengu Unaoendelea
1. Maziwa ya matiti pekee ndiyo chakula na kinywaji bora zaidi kiwezekanacho kwa mtoto katika miezi minne hadi sita ya kwanza ya maisha.
2. Watoto wapaswa kuanza kunyonya matiti haraka iwezekanavyo baada ya kuzaliwa. Karibu kila mama aweza kumnyonyesha matiti mtoto wake.
3. Kunyonya mara nyingi kwahitajika ili kutoa maziwa ya matiti ya kutosha kwa mahitaji ya mtoto.
4. Kunyonyesha chupa kwaweza kutokeza ugonjwa mbaya na kifo.
5. Kunyonyesha matiti kwapasa kuendelee kupita mwaka wa pili wa maisha ya mtoto na hata zaidi ya hapo ikiwezekana.
Chanzo: Facts for Life, lililochapishwa pamoja na mashirika UNICEF, WHO, na UNESCO (Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Elimu, Sayansi na Utamaduni).
[Sanduku katika ukurasa wa 14]
Kunyonyesha Matiti na UKIMWI
Katika mwisho-mwisho wa Aprili 1992, mashirika WHO na UNICEF yalikutanisha pamoja kikundi cha wastadi kutoka mataifa mbalimbali ili kufikiria uhusiano wa UKIMWI na kunyonyesha matiti. Uhitaji wa mkutano huo ulielezwa na Dakt. Michael Merson, mkurugenzi wa Programu ya Ulimwenguni Pote ya UKIMWI. Alisema hivi: “Kunyonyesha mtoto ni muhimu sana katika wokovu wa maisha ya mtoto. Hatari ya mtoto kufa kwa UKIMWI kupitia kunyonyeshwa matiti ni lazima isawazishwe dhidi ya hatari ya kufa kwa mambo mengine ikiwa hanyonyeshwi matiti.”
Kulingana na WHO, karibu theluthi moja ya watoto wanaozaliwa na akina mama wenye ambukizo la virusi ya HIV (virusi ya UKIMWI) huambukizwa pia. Ingawa kupitishwa kwingi kwa maradhi hayo ya mama kwa mtoto hutukia wakati wa mimba na kuzaliwa, kuna uthibitisho kwamba kwaweza pia kutukia kupitia kunyonyesha matiti. Hata hivyo, shirika WHO lasema, “watoto wengi sana wanaonyonyeshwa matiti na akina mama wenye ambukizo la virusi ya HIV hawaambukizwi kupitia kunyonyesha matiti.”
Kikundi hicho cha wastadi chamalizia hivi: “Katika mahali ambapo maradhi ya kuambukiza na utapiamlo ndivyo visababishi vikuu vya vifo vya vitoto na kuna kiwango cha juu cha vifo vya vitoto, wanawake wenye mimba, kutia ndani wale wenye virusi ya HIV, wapasa kushauriwa kwa kawaida wanyonyeshe matiti. Hiyo ni kwa sababu uwezekano wa kitoto chao kuambukizwa virusi ya HIV kupitia maziwa ya matiti kwaelekea kuwa chini kuliko hatari yacho ya kufa kutokana na vyanzo vingine ikiwa hakinyonyeshwi matiti.
“Kwa upande mwingine, katika hali ambazo kisababishi kikuu cha kifo wakati wa utoto si maradhi ya kuambukiza na kiwango cha vifo vya vitoto ni kidogo, . . . wanawake wenye mimba wanaojulikana kuwa wameambukizwa virusi ya HIV wapaswa kushauriwa kwa kawaida watumie njia ya badala iliyo salama kwa mtoto wao badala ya kumnyonyesha matiti.”