Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/8 kur. 3-5
  • Mambo Ambayo Wanawake Wapaswa Kujua Juu ya Kansa ya Matiti

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mambo Ambayo Wanawake Wapaswa Kujua Juu ya Kansa ya Matiti
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Historia ya Familia
  • Visababishi vya Kimazingira
  • Historia ya Mtu Binafsi na Hormoni
  • Mbona Matiti Yaambukizwe kwa Urahisi Zaidi
  • Mweneo
  • Njia za Kuokoka Kansa
    Amkeni!—1994
  • Kansa ya Matiti Utazamie Nini? Ukabiliane Jinsi Gani?
    Amkeni!—2011
  • Utegemezo Ufaao
    Amkeni!—1994
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/8 kur. 3-5

Mambo Ambayo Wanawake Wapaswa Kujua Juu ya Kansa ya Matiti

IDADI ya visa vya kansa ya matiti inaongezeka katika kila bara.[1] Kulingana na makadirio fulani, kufikia mwaka wa 2000, visa vipya vipatavyo milioni moja vya kansa ya matiti vitakuwa vikigunduliwa kila mwaka ulimwenguni pote.[2]

Je! kuna mwanamke yeyote asiyeweza kupata maradhi hayo? Je! kuna jambo lolote liwezalo kufanywa ili kuizuia? Na wale wanaopigana na adui huyu wanahitaji faraja na utegemezo gani?

Kansa nyingi za ngozi husababishwa na miale ya kiuka-urujuani (miale isiyoonekana) kutoka kwenye jua. Kansa nyingi za mapafu husababishwa na uvutaji wa sigareti. Lakini hakuna kitu maalumu kinachojulikana kusababisha kansa ya matiti.[3]

Hata hivyo, kulingana na utafiti wa hivi karibuni, chembe za urithi, mazingira, na hormoni zaweza kushiriki kuleta kansa ya matiti.[4] Wanawake walio katika hali hizo wanaweza kuwa hatarini zaidi.

Historia ya Familia

Mwanamke aliye na mtu wa ukoo mwenye kansa ya matiti, kama vile mama, dada, au hata shangazi au nyanya kutoka upande wa mama, ana uwezekano mkubwa wa kuipata. Ikiwa watu kadha wa kadha kati yao walikuwa na maradhi hayo, basi anaweza kupatwa kwa urahisi zaidi na kansa ya matiti.

Dakt. Patricia Kelly, mstadi wa chembe za urithi nchini United States, aambia Amkeni! kwamba ingawa kuna visababishi vya kansa vinavyotokana na urithi, hivyo vyaweza kuwa asilimia 5 hadi 10 tu ya kansa zote za matiti. Yeye asema hivi: “Twafikiria, kwamba kansa nyingine nyingi huletwa na visababishi visivyohusika sana na urithi lakini vinavyoungana na mazingira.”[7] Washiriki wa familia wenye chembe za urithi zinazofanana huelekea kuwa katika mazingira yaleyale.

Visababishi vya Kimazingira

“Kwa wazi kuna visababishi vingi vya kimazingira vinavyodhaniwa kuwa vyahusika” katika kusababisha maradhi hayo, akasema Devra Davis, ambaye ni mwanachuo akitoa maelezo katika jarida Science. Kwa kuwa titi la mwanamke ni mojapo sehemu za mwili zenye kuathiriwa kwa urahisi na mnururisho, wanawake wanaofanyiwa mnururisho wa uionishaji (kuongezwa ioni) huwa hatarini zaidi kupatwa na kansa ya matiti. Ndivyo ilivyo na wanawake wanaopatwa na kemikali zenye sumu.[10][11]

Jambo jingine la kimazingira ni ulaji. Watu fulani wadokeza kwamba kansa ya matiti yaweza kuwa maradhi yasababishwayo na upungufu wa vitamini nao wanataja ukosefu wa vitamini D. Vitamini hiyo husaidia mwili kufyonza kalsiamu, ambayo nayo yaweza kusaidia kuzuia ukuzi wa kupita kiasi wa chembe.[12]

Uchunguzi mwingine wataja mafuta katika chakula, si yakiwa kisababishi, bali kuwa ni kichochezi cha kansa ya matiti.[13] Gazeti FDA Consumer lilisema kwamba kiwango cha kifo kutokana na kansa ya matiti kilikuwa juu zaidi katika nchi kama United States, ambako mafuta na protini ya wanyama huliwa sana. Lilisema hivi: “Tangu zamani wanawake Wajapani hawahatarishwi sana na kansa ya matiti, lakini hatari hiyo imekuwa ikiongezeka sana, ikiambatana na tabia za ulaji wa ‘Kimagharibi’; yaani, kuacha ulaji usio na mafuta mengi na kula vyakula vyenye mafuta mengi.”[14]

Uchunguzi mmoja wa hivi karibuni ulidokeza kwamba kula kalori nyingi sana katika chakula chenye mafuta mengi mno kwaweza kutokeza hatari kubwa sana. Science News lilisema: “Kila kalori ya ziada huongeza hatari ya kupata kansa ya matiti, huku kila kalori ya ziada itokanayo na mafuta ikitokeza hatari ya asilimia 67 zaidi ya kalori zitokanazo na vyanzo vingine.”[15] Kalori za ziada zaweza kuongeza uzito zaidi, na inafikiriwa kwamba wanawake wenye uzito kupita kiasi wana uwezekano wa mara tatu kupata kansa ya matiti, hasa wale ambao wamekoma hedhi. Mafuta ya mwili hutoa estrojeni, hormoni ya wanawake inayoweza kuathiri vibaya mnofu wa matiti, jambo lenye kutokeza kansa.

Historia ya Mtu Binafsi na Hormoni

Kuna hormoni nyingi katika matiti ya mwanamke zinazotokeza mabadiliko matitini muda wote wa maisha yake. Dakt. Paul Crea, mpasuaji wa vivimbe, aandika hivi katika Australian Dr Weekly: “Lakini, katika wanawake fulani, hormoni zichocheapo mnofu wa matiti kwa muda mrefu . . . hizo huanzisha mfululizo wa mabadiliko katika chembe ambazo hatimaye hubadilika kuwa zenye [kansa].”[21] Kwa sababu hiyo inafikiriwa kwamba wanawake ambao walianza hedhi katika umri wa mapema, wakiwa na miaka 12, au ambao wamekawia kukoma hedhi, wakiwa katikati ya umri wa miaka ya 50, wana hatari kubwa zaidi.

Kumekuwa na mjadala sana kama estrojeni za ziada zipokewazo kutokana na tiba ya ERT (tiba ya kuongeza estrojeni) zahusika na kansa ya matiti. Ingawa baadhi ya uchunguzi waonyesha kwamba tiba ya ERT haiongezi hatari, uchunguzi mwingine mwingi waonyesha hatari ya waziwazi kwa wale wanaopata tiba hiyo kwa muda mrefu. Kwa kufikiria uchunguzi wote uliofanywa, British Medical Bulletin la 1992 lilisema kwamba kuna uwezekano kwamba “estrojeni isiyo ya kuzuia mimba huongeza hatari ya kupatwa na kansa ya matiti kwa asilimia 30 hadi 50” baada ya kutumiwa kwa muda mrefu.

Ripoti za uhusiano kati ya tembe za kuzuia uzazi na kansa za matiti hazionyeshi hatari kubwa ya kuzitumia. Lakini, kuna kikundi cha wanawake ambao wamo hatarini zaidi. Wanawake wachanga, wanawake ambao hawajazaa watoto kamwe, na wanawake ambao wametumia tembe za kuzuia uzazi kwa muda mrefu wanaweza kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata kansa ya matiti kwa asilimia 20.

Lakini, wanawake 3 kati ya kila 4 wenye kansa ya matiti hawajui hasa kilichochangia kuleta maradhi yao. Na basi swali lazuka, je, kuna mwanamke yeyote anayeweza kujiona kuwa hawezi kupatwa na kansa ya matiti? FDA Consumer laripoti hivi: “Kwa maoni ya kitiba, wanawake wote wapaswa waonwe kuwa wamo hatarini ya kupatwa na kansa ya matiti.”[33]

Hivyo, ni rahisi kwa wanawake, hasa wale wenye umri mkubwa zaidi, kupatwa na maradhi hayo. Dakt. Kelly aeleza kwamba ingawa kuna visababishi kadhaa vya kansa ya matiti, ‘nafikiria, baadhi yavyo ni kwa sababu ya umri wa uzee, na migawanyiko mibaya katika chembe.’[34]

Mbona Matiti Yaambukizwe kwa Urahisi Zaidi

Uchunguzi wa maumbile ya matiti ya kike waonyesha sababu inayofanya yapatwe na kansa kwa urahisi. Ndani ya matiti mna michirizi, ambayo ni vijia vyembamba, ibebayo maziwa kutoka mifuko ya kuyatengeneza hadi kwenye chuchu. Kwenye kuta za ndani za michirizi mna chembe zenye kujigawa na kubadilika-badilika nyakati zote kufuatana na hedhi ya kila mwezi ya mwanamke, zikimtayarisha kwa ajili ya mimba, unyonyeshaji, na utunzi wa mtoto. Basi, kansa nyingi hutokea katika michirizi hiyo.[37]

Katika kitabu Alternatives: New Developments in the War on Breast Cancer, mtafiti Rose Kushner aeleza hivi: “Njia yoyote ya kawaida ambayo hubadilishwa nyakati zote na jambo moja au jingine—hata kama ni ya kawaida kabisa . . . —inaweza kupatwa na makosa makubwa zaidi.” Yeye aendelea kusema hivi: “Ile chembe ya matiti ambayo imechoka nyakati zote na hormoni fulani iamuruyo, ‘Acha hiyo. Fanya hii.’ Si ajabu kwamba chembe zitokezwazo na migawanyiko hiyo hukosa udhibiti.”[38]

Kansa ya matiti huanza wakati chembe yenye kasoro inapojigawanya, inapopoteza njia yayo ya ukuzi, na kuanza kuongezeka kwa kasi. Chembe kama hizo haziachi kuzaana, na baada ya muda chembe hizo hushinda mnofu wenye afya unaozizunguka, zikigeuza kiungo chenye afya kuwa chenye maradhi.[39]

Mweneo

Kansa ikiwepo katika matiti, ambukizo laweza kuondolewa. Wakati kansa ya matiti imekwisha kuenea katika sehemu za mbali za mwilini, inaitwa kansa-enezi ya matiti. Yaelekea sana kwamba hicho ndicho kisababishi kikuu cha vifo vya wagonjwa wa kansa ya matiti. Chembe za kansa ziongezekapo katika matiti na uvimbe kuendelea kuwa mkubwa, chembe za kansa zaweza kuondoka mahali pa uvimbe polepole na kisiri na kupenya kuta za mishipa ya damu na mafundo ya limfu.

Kufikia hatua hii chembe za uvimbe zaweza kusafiri hadi sehemu za mbali za mwili. Chembe hizo zikiepa kinga za mwili, zinazotia ndani chembe za asili za kuua adui zenye kuzunguka-zunguka katika damu na umajimaji wa limfu, chembe hizo zenye kudhuru zaweza kuteka viungo muhimu mwilini, kama vile ini, mapafu, na ubongo. Chembe hizo zaweza kuongezeka sana katika viungo hivyo na kuenea tena, baada ya kuambukiza viungo hivyo kansa. Mweneo huo ukianza tu, basi uhai wa mwanamke umo hatarini.

Kwa hiyo, njia tu ya kuokoka kansa ya matiti ni kuigundua mapema inapokua, kabla haijapata nafasi ya kuenea. Kila mwanamke anaweza kufanya nini ili aweze kuigundua mapema?[42] Je! kuna chochote kiwezacho kufanywa ili kuzuia kansa ya matiti?

[Blabu katika ukurasa wa 4]

Wanawake 3 kati ya kila 4 wenye kansa ya matiti hawajui hasa kilichochangia kuleta maradhi yao

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki