Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 4/8 kur. 6-10
  • Njia za Kuokoka Kansa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Njia za Kuokoka Kansa
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uzuiaji na Ulaji
  • Ugunduzi wa Mapema
  • Matibabu
  • Mkazo wa Akili na Kansa ya Matiti
  • Mambo Ambayo Wanawake Wapaswa Kujua Juu ya Kansa ya Matiti
    Amkeni!—1994
  • Kansa ya Matiti Utazamie Nini? Ukabiliane Jinsi Gani?
    Amkeni!—2011
  • Utegemezo Ufaao
    Amkeni!—1994
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 4/8 kur. 6-10

Njia za Kuokoka Kansa

IKIWA ungepata habari kwamba kulikuwa na muuaji katika ujirani wako, je, ungechukua hatua za kujilinda mwenyewe na familia yako? Yaelekea ungefunga milango yako kwa vifuli na makomeo ili mtu asiweze kuingia kwa urahisi. Pia ungekuwa macho kuona watu wasiojulikana wanaotilika shaka na kuwaripoti mara moja.[1]

Je! wanawake wasifanye vivyo hivyo kwa habari ya kansa ya matiti yenye kuua? Wao wanaweza kuchukua hatua gani ya kujilinda wenyewe na hivyo kuongeza uwezekano wao wa kuokoka?

Uzuiaji na Ulaji

Inakadiriwa kwamba kansa 1 kati ya 3 katika United States husababishwa na ulaji.[2] Ulaji ufaao utakaodumisha mfumo wa kinga wa mwili wako huenda ukawa kinga yako ya kwanza. Ingawa hakuna chakula kijulikanacho kiwezacho kutibu kansa, kula vyakula fulani na kupunguza vyakula vingine kwaweza kuwa hatua za kuizuia. “Kula ifaavyo kwaweza kupunguza hatari yako ya kupatwa na kansa ya matiti kufikia asilimia hamsini,” akasema Dakt. Leonard Cohen wa Shirika la Afya la Amerika mjini Valhalla, New York.

Vyakula vyenye makapi mengi, kama vile mikate na nafaka, vyaweza kupunguza kiwango cha hormoni za prolaktini na estrojeni, labda kwa njia ya hayo makapi kushikana na hormoni hizo na kuziondoa nje ya mwili.[7] Kulingana na jarida Nutrition and Cancer, “matokeo hayo yangeweza kukandamiza maendeleo yoyote ya visababishi vya kansa.”[8]

Kupunguza ulaji wa mafuta yaliyo magumu kuyeyuka kwaweza kupunguza hatari za kupatwa na kansa. Gazeti Prevention lilipendekeza kwamba kuacha kutumia maziwa yenye mtindi na kuanza kutumia maziwa yasiyoenguliwa, kupunguza ulaji wa siagi, kula nyama isiyo na mafuta, na kuondoa ngozi ya kuku kwaweza kupunguza mafuta magumu hadi kiwango salama.[9]

Mboga zenye vitamini-A nyingi, kama vile karoti, maji ya matunda, viazi vitamu, na mboga za majani-majani, kama vile spinachi na sukuma-wiki na mboga za haradali, zaweza kusaidia.[10] Yafikiriwa kwamba vitamini-A huzuia mfanyizo wa mageuko ambayo husababisha kansa. Na mboga kama brokoli, kabichi vifundo, kauliflawa, kabichi, na vitunguu vichanga zina kemikali zenye kutokeza vimeng’enya vya ulinzi.

Katika kitabu Breast Cancer—What Every Woman Should Know, Dakt. Paul Rodriguez asema kwamba mfumo wa kinga, ambao hutambua na kuharibu chembe zenye kasoro, waweza kuimarishwa kwa ulaji ufaao. Yeye apendekeza kula vyakula vyenye chuma kingi, kama vile nyama isiyo na mafuta, mboga za majani-majani, kamba wa baharini, na matunda na mboga zenye vitamini C nyingi.[15] Matunda na mboga zenye vitamini C nyingi hupunguza hatari ya kupatwa na kansa ya matiti, laripoti Journal of the National Cancer Institute.[16] Maharagwe ya soya na vitu vingine visivyochachushwa vinavyotokana na soya vina jenisteni, ijulikanayo kukandamiza ukuzi wa mavimbe katika majaribio ya maabara, lakini bado haijulikani ina matokeo gani kwa wanadamu.

Ugunduzi wa Mapema

“Ugunduzi wa mapema wa kansa ya matiti wabaki kuwa hatua muhimu zaidi ya kupunguza mwendo wa kansa ya matiti,” chasema kichapo Radiologic Clinics of North America.[21] Kwa habari hii hatua tatu kuu za kuizuia ni kujichunguza matiti kwa ukawaida, kuchunguzwa na daktari kila mwaka, na kuchunguzwa matiti kupitia eksirei ya matiti.

Kujichunguza matiti kwapaswa kufanywa kwa ukawaida kila mwezi, kwa vile mwanamke apaswa kuwa macho kuona kitu chochote au hisi yoyote yenye kutilika shaka katika matiti yake, kama vile matiti kuwa magumu au uvimbe. Hata ugunduzi wake uonekane kuwa kidogo kadiri gani, anapaswa kumwona daktari mara hiyo.[24] Kadiri uvimbe ugunduliwavyo mapema, ndivyo awezavyo kudhibiti wakati ujao wake zaidi. Ripoti moja kutoka Swedeni yaonyesha kwamba kama kansa ya matiti ilikuwa na ukubwa wa milimeta 15 au iwe ndogo zaidi na iondolewe kupitia upasuaji, kulikuwa na uwezekano wa asilimia 94 wa kuishi miaka 12.[25]

Dakt. Patricia Kelly aeleza hivi: “Kansa ya matiti isipokurudia baada ya miaka 12 1/2, yaelekea sana haitarudi tena. . . . Na wanawake wanaweza kufundishwa kugundua kansa za matiti zilizo ndogo zaidi ya sentimeta moja wakitumia vidole vyao tu.”

Inapendekezwa kwamba uchunguzi ufanywe na daktari wa mambo hayo au daktari wa kawaida kila mwaka bila kuchelewa, hasa mwanamke afikapo umri wa miaka 40. Uvimbe ukigunduliwa, itakuwa vizuri kupata maoni mengine kutoka kwa daktari wa matiti au daktari-mpasuaji.[31]

Taasisi ya Kitaifa ya Kansa katika United States yasema kwamba silaha nzuri dhidi ya kansa ya matiti ni kuchunguzwa kwa kawaida kwa eksirei ya matiti.[32] Aina hiyo ya eksirei yaweza kugundua uvimbe labda miaka miwili kabla haijaweza kuhisiwa.[33] Eksirei hiyo inapendekezwa kwa wanawake wenye miaka zaidi ya 40. Hata hivyo, Dakt. Daniel Kopans atujulisha hivi: “Lakini haifanyi kazi kikamilifu.”[37] Haiwezi kugundua aina zote za kansa za matiti.

Dakt. Wende Logan-Young wa hospitali ya matiti katika Jimbo la New York aeleza Amkeni! kwamba mwanamke au daktari wake akigundua kasoro lakini eksirei haionyeshi ishara ya kasoro hiyo, huenda elekeo likawa ni kupuuza magunduzi hayo na kuamini eksirei. Yeye asema kwamba “hilo ndilo kosa kubwa zaidi tuonalo siku hizi.”[40] Yeye ashauri wanawake wasitegemee sana uwezo wa eksirei wa kugundua kansa lakini wategemee sana uchunguzi wa matiti.[41]

Ingawa eksirei ya matiti inaweza kugundua vivimbe, haiwezi hasa kutambua kama vivimbe hivyo ni vile visivyodhuru (visivyo na kansa) au kama ni vyenye kudhuru (vya kansa).[42] Hilo laweza kufanywa tu kwa kupitia uchunguzi wa kipande kidogo cha mnofu. Ebu fikiria kisa cha Irene, aliyeenda kupigwa eksirei ya matiti. Kwa kutegemea picha ya eksirei, daktari wake aliona uvimbe kwenye matiti yake kuwa maradhi ya matiti yasiyodhuru naye akasema: “Nina hakika kabisa huna kansa.” Muuguzi aliyepiga picha ya eksirei ya matiti alikuwa na wasiwasi, lakini Irene alisema: “Nilihisi kwamba ikiwa daktari alikuwa na hakika, labda nilikuwa na hofu isiyo na sababu.” Upesi huo uvimbe ukawa mkubwa zaidi, kwa hiyo Irene akamwendea daktari mwingine. Uchunguzi ulifanywa kwa kipande cha mnofu nao ukaonyesha kwamba alikuwa na karsinoma ya kuchochota, aina ya kansa yenye kukua kwa kasi. Ili ijulikane kama uvimbe ni ule usiodhuru (kama ulivyo kwa visa 8 kati ya 10) au ni wenye kudhuru, ni lazima uchunguzi wa mnofu ufanywe. Uvimbe huo ukionekana kuwa wenye kutilika shaka au ukiwa unaendelea kukua, uchunguzi wa mnofu wapaswa ufanywe.[50A]

Matibabu

Kwa wakati huu, upasuaji, mnururisho, na tiba ya dawa ndizo njia za kawaida za kutibu kansa ya matiti. Habari kuhusu aina ya uvimbe, ukubwa wao, na mwelekeo wao wa kuenea, kama umeenea kwa mafundo ya limfu, na hali ya hedhi yako yaweza kukusaidia wewe na daktari wako kujua aina ya matibabu yafaayo.[51]

Upasuaji. Kwa miongo mingi ya miaka upasuaji wa kuondoa matiti pamoja na mafundo yote ya limfu umetumiwa sana. Lakini kwa miaka ya karibuni matibabu ya kuhifadhi matiti yanayotia ndani kuondolewa kwa uvimbe na mafundo ya limfu tu, pamoja na mnururisho, yametumiwa huku uwezekano wa kuokoka ukitoshana na ule wa upasuaji wa kuondoa matiti. Jambo hilo limewapa baadhi ya wanawake amani zaidi ya akilini wanapoamua kuondolewa uvimbe, kwa vile kutolewa kwa uvimbe hakuharibu mwili sana. Lakini jarida British Journal of Surgery lasema kwamba wanawake wachanga, wale wenye kansa katika sehemu kadhaa za lile titi au wenye vivimbe vikubwa kuliko sentimeta 3, wana uwezekano mkubwa zaidi wa kurudiwa na kansa wakitibiwa bila kuondolewa matiti.[54]

Jambo kuu la kuokoka kansa na isikurudie latajwa na Cleveland Clinic Journal of Medicine: “Utiaji-damu mishipani huathiri vibaya sana uwezekano wa kuokoka [kansa] na uwezekano wayo wa kurudi tena. . . baada ya upasuaji wa matiti unaobakiza misuli ya kifua.” Ripoti hiyo ilisema kwamba kikundi kimoja kilichotiwa damu mishipani kilikuwa na uwezekano wa asilimia 53 wa kuokoka kansa kwa miaka mitano, tofauti na uwezekano wa kuokoka kansa wa asilimia 93 kwa kikundi kisichotumia damu.

Msaada mwingine wa kuokoka kansa waripotiwa kwenye The Lancet, ambamo Dakt. R. A. Badwe alisema hivi: “Kupima wakati wa upasuaji kwa kuhusiana na kawaida za hedhi kuna athari kubwa sana juu ya matokeo ya baadaye kwa wagonjwa wa kansa ya matiti ambao hawajakoma hedhi.” Ripoti hiyo yaonyesha kwamba wanawake walioondolewa uvimbe walipokuwa wakichochewa na estrojeni hawakuendelea vizuri kuliko wale waliopasuliwa katika vipindi vingine vya hedhi—asilimia 54 waliokoka miaka kumi kwa kulinganisha na asilimia 84 ya kikundi hicho cha pili. Wakati bora zaidi wa upasuaji kwa wanawake wenye kansa ya matiti ulisemwa kuwa angalau siku 12 baada ya hedhi ya mwisho.

Tiba ya Mnururisho. Tiba ya mnururisho huua chembe za kansa. Katika kisa cha matibabu ya kuhifadhi matiti, mbegu ndogo-ndogo sana za kansa zaweza kuepa kisu cha daktari-mpasuaji anapojaribu kuhifadhi matiti. Tiba ya mnururisho yaweza kuondoa kabisa chembe zozote zinazobaki.[60] Lakini mnururisho una hatari kidogo ya kuweza kuambukiza titi jingine kansa. Dakt. Benedick Fraass apendekeza kutohatarisha sana titi jingine kwa mnururisho. Yeye asema hivi: “Kwa kufanya mambo machache sahili inawezekana kupunguza sana mnururisho unaopata titi jingine wakati wa kunururisha titi lenye ugonjwa.” Yeye apendekeza kwamba kipande cha risasi chenye unene wa sentimeta 2.5 kiwekwe juu ya titi jingine.

Tiba ya Dawa. Zijapokuwa jitihada za kuondoa kansa ya matiti kwa upasuaji, asilimia 25 hadi 30 ya wanawake wenye kansa ya matiti iliyotoka tu kugunduliwa watakuwa na mweneo uliofichika, ambao ni mdogo mno kuweza kutoa dalili mara ya kwanza.[69] Kemotherapi ni matibabu yanayotumia vitu vya kemikali kujaribu kuua zile chembe zinazojaribu kushambulia sehemu fulani za mwili.

Matibabu hayo ya kemotherapi hayana uwezo sana kwa sababu vivimbe vyenye kansa hufanyizwa kwa chembe za aina mbalimbali hivi kwamba kila aina ya chembe inaitikia tofauti kwa dawa. Zile chembe zinazookoka matibabu hayo zaweza kutokeza vivimbe vipya visivyoweza kutibiwa kwa dawa. Lakini toleo la The Lancet la Januari 1992 lilitoa uthibitisho kwamba kemotherapi iliongeza uwezekano wa mwanamke kuishi kwa miaka mingine kumi kwa asilimia 5 hadi 10, ikitegemea umri wake.

Matokeo ya ziada ya kemotherapi yaweza kutia ndani hali ya kutaka kutapika, kutapika, kupoteza nywele, kutokwa damu, madhara ya moyo, kudhoofisha kinga ya mwili, kuwa tasa, na leukemia. John Cairns, akiandika katika Scientific American, alieleza hivi: “Hizo zaweza kuonekana kuwa madhara madogo-madogo tu kwa mgonjwa ambaye ana kansa iliyokomaa na inayokua kwa kasi, lakini yangeonekana kuwa makubwa kwa mwanamke mwenye kansa ya matiti ya [sentimeta moja] katika sehemu fulani tu ya titi. Uwezekano wake wa kufa kwa kansa kwa miaka mitano ni asilimia ipatayo 10 tu hata asipopokea matibabu zaidi baada ya upasuaji.”

Tiba ya Hormoni. Tiba ya kuondoa estrojeni huharibu kile kichocheo cha ukuzi cha estrojeni. Jambo hilo hufanywa kwa kupunguza viwango vya estrojeni kwa wanawake ambao hawajakoma hedhi kwa upasuaji wa kuondoa vifuko vya mayai ama kwa kutumia dawa. The Lancet liliripoti uwezekano wa kuokoka kansa kwa miaka kumi kwa kila wanawake 8 hadi 12 kati ya wanawake 100 waliotibiwa kwa mojapo njia hizo mbili.

Kila mwanamke mwenye kansa ya matiti apaswa afanye jitihada za kufanyiwa uchunguzi wa baadaye katika maisha yake yote. Uchunguzi wa karibu-karibu wapaswa udumishwe, kwa sababu tiba moja ikishindwa na kansa irudi, matibabu mengineyo yaweza kutumiwa.

Aina nyingine ya tiba ya kansa inayotumia njia tofauti hushughulikia ugonjwa fulani unaoitwa kacheksia. Jarida Cancer Research laeleza kwamba theluthi mbili za vifo vyote vya kansa husababishwa na kacheksia, neno litumiwalo kufafanua kudhoofika kwa misuli na mnofu. Dakt. Joseph Gold, wa Taasisi ya Utafiti wa Kansa ya Syracuse katika United States, aeleza Amkeni! hivi: “Twahisi kwamba uvimbe hauwezi kupenya mwili mpaka vijia vya kibiolojia na kemia vya kacheksia viwe vimefunguliwa.”[89] Uchunguzi mmoja wa kitiba, ukitumia dawa isiyo na sumu iitwayo sulfati-hidrazini, ulionyesha kwamba baadhi ya vijia hivyo vyaweza kufungwa. Kati ya wagonjwa waliohusika wa kansa ya matiti iliyogunduliwa kwa kuchelewa, kulikuwa na mafanikio ya asilimia 50.

Tiba nyinginezo zaidi ziitwazo dawa za badala zimetumiwa na wanawake fulani ili watibiwe kansa ya matiti bila kupasuliwa na bila kutumia dawa zenye kudhuru. Tiba hutofautiana, nyingine ni za ulaji wa uangalifu na nyingine ni za miti-shamba, kama ilivyo na ile tiba ya Hoxsey. Lakini hakuna uchunguzi mwingi uliochapishwa unaoweza kusaidia mtu akadiri uwezo wa matibabu hayo.[96]

Ingawa makala hii imekusudiwa kuonyesha njia ziwezazo kusaidia kuokoka kansa, gazeti la Amkeni! halipendekezi matibabu yoyote kuwa yafaa au hayafai. Twatia moyo watu wote wachunguze kwa uangalifu njia mbalimbali za matibabu ya maradhi haya.—Mithali 14:15.

Mkazo wa Akili na Kansa ya Matiti

Katika jarida Acta neurologica, Dakt. H. Baltrusch aeleza kwamba mkazo wa akili ulio mkali sana au wenye kuendelea sana waweza kupunguza mfumo wa kinga ya mwili wa kukinza vivimbe.[97] Wanawake wachovu, wenye kushuka moyo, au wanaokosa utegemezo wa kihisia-moyo waweza kufanya mfumo wa kinga ya mwili wao udhoofike kwa kiwango kifikacho asilimia 50.

Hivyo, Dakt. Basil Stoll, akiandika katika Mind and Cancer Prognosis, alikazia hivi: “Kila jitihada yapaswa kufanywa ili kupunguza mtamauko usioepukika wa kimwili na kiakili unaopatwa na wagonjwa wa kansa wakati wa matibabu ya maradhi hayo na hata baadaye.”[101] Lakini ni utegemezo wa aina gani unaohitajika?[102]

[Blabu katika ukurasa wa 7]

Ingawa hakuna chakula kijulikanacho kiwezacho kutibu kansa, kula vyakula fulani na kupunguza vyakula vingine kwaweza kuwa hatua za kuizuia. ‘Kula ifaavyo kwaweza kupunguza hatari yako ya kupatwa na kansa kufikia asilimia hamsini,’ akasema Dakt. Leonard Cohen

[Blabu katika ukurasa wa 8]

“Ugunduzi wa mapema wa kansa ya matiti wabaki kuwa hatua muhimu zaidi ya kupunguza mwendo wa kansa ya matiti,” chasema kichapo “Radiologic Clinics of North America.”[21] Kwa habari hii hatua tatu kuu za kuizuia ni: kujichunguza matiti kwa ukawaida, kuchunguzwa na daktari kila mwaka, na kuchunguzwa matiti kupitia eksirei ya matiti

[Blabu katika ukurasa wa 10]

Wanawake wachovu, wenye kushuka moyo, au wanaokosa utegemezo wa kihisia-moyo waweza kufanya mfumo wa kinga wa mwili wao udhoofike

[Sanduku katika ukurasa wa 9]

Kujichunguza—Uchunguzi wa Kila Mwezi

KUJICHUNGUZA matiti kwapaswa kufanywe siku nne hadi saba baada ya kipindi cha hedhi. Wanawake waliokoma hedhi wapaswa pia kujichunguza kila mwezi siku iyo hiyo.

Ishara za Kuangaliwa Kila Mwezi Siku Iyo Hiyo

• Uvimbe wa ukubwa wowote (uwe mdogo sana au mkubwa) au msongamano ndani ya matiti.

• Kukunjamana, kutokea kwa vishimo, au kugeuka rangi kwa matiti.

• Kurudi ndani au kuingia ndani kwa chuchu la titi.

• Kutokea kwa vipele au kubambuka kwa chuchu la titi au kutoka kwa umajimaji.

• Kuvimba kwa matezi makwapani.

• Mabadiliko katika vishimo vya matiti.

• Kuwa na alama zisizo na mpango maalumu tofauti na alama za kawaida.

Kujichunguza

Ukiwa umesimama, inua mkono wa kushoto. Ukitumia mkono wa kulia na ukianzia msingi wa matiti, finya sehemu bapa ya vidole vyako kwa mizunguko midogo, ukisonga polepole kwenye matiti ukielekea chuchu. Fanya vivyo hivyo na sehemu iliyo katikati ya kwapani na matiti.

Ukiwa umelala tambarare chini, weka mto chini ya bega la kushoto, na uweke mkono wa kushoto juu au nyuma ya kichwa. Tumia ule mwendo wa mzunguko kama ulivyoelezwa hapo juu. Geuka ufanye upande wa kulia.

Kamua chuchu kwa upole uone kama kuna mitoko yoyote. Fanya vivyo hivyo na titi la kulia.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki