Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 8/22 kur. 10-13
  • Mambo ya Msingi ya Kunyonyesha Maziwa ya Mama

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mambo ya Msingi ya Kunyonyesha Maziwa ya Mama
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kabla Mtoto Hajazaliwa
  • Siku Baada Tu ya Kujifungua
  • Wakati wa Kuachisha Kunyonya
  • Uthibitisho wa Muumba Mwenye Upendo
  • Uthibitisho wa Mafaa ya Maziwa ya Mama
    Amkeni!—1993
  • Kuwa na Watoto— Daraka na Thawabu
    Kufanya Maisha ya Jamaa Yako Yawe Yenye Furaha
  • Jinsi Watoto Wanavyobadili Ndoa
    Unaweza Kuwa na Familia Yenye Furaha
  • Kile Ambacho Watoto Wanahitaji
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 8/22 kur. 10-13

Mambo ya Msingi ya Kunyonyesha Maziwa ya Mama

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA NIGERIA

Ikiwa wewe, kama vile akina mama wengi, umeamua kumnyonyesha mtoto wako, umechagua kutumia mojapo maandalizi yaliyofanyizwa kwa upendo na Muumba wa jamii ya kibinadamu. Maziwa ambayo mwili wako mwenyewe hutoa yatatosheleza mahitaji barabara ya kilishe ya mtoto wako, yakiendeleza ukuzi na maendeleo yenye afya. Yatasaidia pia kukinga mtoto wako dhidi ya maradhi. Likiwa na

sababu nzuri WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) lasema: “[Maziwa ya matiti] ndicho chakula bora zaidi ambacho mtoto anaweza kupata. Vibadala vingine kutia ndani maziwa ya ng’ombe, michanganyiko ya maziwa ya unga na maji, na nafaka ni duni.”

Kunyonyesha maziwa ya mama hukuletea wewe manufaa pia. Hakuna chupa za kuosha wala kuulia viini na hakuna safari za kwenda jikoni katikati ya usiku kumtayarishia mtoto wako mlo. Kunyonyesha maziwa ya mama kutakunufaisha wewe kimwili pia, kwa vile kutakusaidia kupunguza uzani uliopata ukiwa mja-mzito pia kutasaidia mji wa mimba urudie ukubwa wao wa kawaida. Na uchunguzi mbalimbali unadokeza kwamba wanawake wanaowanyonyesha watoto wao hawaelekei kupatwa na kansa ya matiti.

“Karibu kila mama aweza kumnyonyesha mtoto wake,” lahakikisha Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo yaelekea wewe waweza pia. Hata hivyo, huenda ukagundua kwamba kunyonyesha si rahisi kama ulivyotazamia, hasa ikiwa unajaribu kufanya hivyo kwa mara ya kwanza. Hii ni kwa sababu kunyonyesha, hata ingawa ni jambo la kawaida, si jambo la kisilika, ni ustadi ambao lazima ujifunze. Huenda ukapata kwamba inakuchukua wewe na mtoto wako siku kadhaa au hata majuma machache kuweka ratiba yenye kustarehesha na yenye kufurahisha.

Kabla Mtoto Hajazaliwa

Ikiwa hujafaulu kumnyonyesha mtoto hapo awali, ongea na akina mama ambao wamefaulu. Wanaweza kukusaidia kuepuka au kushinda matatizo. Wanaweza pia kukusaidia kujenga uhakika katika uwezo wako wa kumnyonyesha mtoto wako vizuri.

Wakati wa uja-uzito na baada ya hapo, ni muhimu upate pumziko la kutosha. Kwa kuongezea, hakikisha kwamba wala chakula cha kutosha. Breastfeeding, kichapo cha WHO, chasema: “Lishe lisilofaa kabla au wakati wa uja-uzito laweza kuwa kisababishi cha ukuzi mbaya wa mtoto ndani ya mji wa mimba. Yaweza pia kumaanisha kwamba mama hawezi kuweka akiba ya mafuta ya kutosha ili kutoa maziwa ya kutosha baadaye. Kwa hivyo, mama ahitaji lishe bora linalotegemea vyakula mbalimbali, muda wote wa uja-uzito na kipindi chote cha kunyonyesha.”

Utunzaji wa matiti ni wa maana pia. Wakati wa miezi ya mwisho ya uja-uzito, suza matiti yako kwa maji unapooga, lakini usiyapake sabuni. Tezi katika sehemu nyeusi inayozunguka chuchu hutoa kizuia-bakteria yenye mafuta inayoziweka chuchu zikiwa na unyevunyevu na kulinda dhidi ya ambukizo. Sabuni yaweza kukausha chuchu na kuondoa au kupunguza nguvu ya mafuta hayo. Matiti yako yakikauka au yawashe, huenda ukataka kupaka krimu au losheni ya kulainisha. Lakini yazuie yasifikie chuchu au sehemu nyeusi inayoizunguka.

Wakati mmoja madaktari walipendekeza kwamba akina mama “waimarishe” chuchu zao wakati wa uja-uzito kwa kuzisugua kwa nguvu. Ingawaje hili lilikusudiwa kuzuia vidonda vya chuchu wakati wa kunyonyesha, uchunguzi mbalimbali waonyesha kwamba utendaji kama huo husaidia kidogo tu. Vidonda kwa kawaida hutokana na kutomweka mtoto anayenyonya ifaavyo kwenye matiti.

Ukubwa na umbo la matiti si mambo ya muhimu katika kufaulu kunyonyesha, lakini mtoto hawezi kushikilia chuchu iliyopinduka au isiyotokea. Waweza kujitahini mwenyewe kwa kufinya kwa uanana nyuma tu ya kila chuchu ukitumia kidole cha gumba na kidole cha shahada kuhakikisha kwamba chuchu zatokea upande wa nje. Kama hazitokezi, ongea na daktari wako. Huenda akapendekeza uo la matiti, chombo sahili kinachovaliwa wakati wa uja-uzito au kati ya vipindi vya kulisha. Uo kwa kawaida hufanyia maendeleo umbo la chuchu zisizotokea au chuchu zilizopinduka.

Siku Baada Tu ya Kujifungua

Ni vizuri kuanza kumnyonyesha mtoto wako katika muda wa saa moja baada ya kujifungua. Huenda wengine wakafikiri kwamba baada tu ya kazi hiyo yote ya kujifungua, wote wawili mama na mtoto huenda wakawa wamechoka sana hivi wasiweze kuamkiana. Lakini kwa kawaida mama huchangamka wakati huo, na mtoto, baada ya dakika chache za kuzoea hali za nje ya mji wa mimba, hutafuta kwa hamu faraja ya matiti.

Akina mama wapya waweza kuwaandalia watoto wao waliozaliwa karibuni umaji-maji wa kimanjano au ulio mweupe uitwao kolostromi. “Umajimaji huu wa dhahabu” hunufaisha sana mtoto. Yana mchanganyiko ambao huua bakteria zenye kudhuru. Pia yana proteini nyingi na kiasi kidogo cha sukari na mafuta yanayofanya yawe chakula kifaacho katika siku chache za kwanza za maisha. Isipokuwa kuwe na tatizo la kitiba, mtoto hatahitaji chakula wala kinywaji kingine chochote. Malisho ya ziada kwa chupa, yaweza kumzuia mtoto asilishe kwenye matiti, kwa vile jitihada ndogo zaidi inahitajiwa kunyonya kutoka kwenye chupa.

Kwa kawaida akina mama huanza kutoa maziwa bila kolostromi baada ya siku mbili hadi tano baada ya kujifungua. Mtiririko ulioongezeka wa damu katika matiti wakati huu huenda ukasababisha matiti yako yawe makubwa na yenye uchungu. Hii ni kawaida. Kwa kawaida kunyonyesha kutapunguza maumivu hayo. Hata hivyo nyakati nyingine, matiti yaliyovimba yatasababisha chuchu zisitokee. Kwa vile hii hufanya iwe vigumu kwa mtoto wako kunyonya, huenda ukalazimika kutoa maziwa kwa mkono. Waweza kufanya hivi kwa kutumia mikono yote miwili kufinya kila titi kuanzia nyuma kuelekea kwenye chuchu.

Huwezi kupima kiasi cha maziwa ambacho mtoto wako hupata kutoka matitini lakini usihangaike—mwili wako una uwezo wa kutoa kiasi chote ambacho mtoto anahitaji, hata ikiwa ni mapacha! Kadiri unyonyeshavyo mara nyingi zaidi ndivyo utakavyotoa maziwa mengi zaidi. Hii ni sababu moja ambayo hupaswi kumnywesha mtoto vinywaji vingine kwa chupa kama vile michanganyiko ya maziwa ya unga na maji au maziwa ya ng’ombe. Ukifanya hivyo, mtoto wako atapata kiasi kidogo zaidi kutoka kwako. Kisha hii itamaanisha kwamba, utatoa kiasi kidogo zaidi cha maziwa.

“Watoto wa kawaida waliozaliwa kwa wakati wao kamili hawawi hoi wakati wa kuzaliwa kama ambavyo imedhaniwa na wanaweza kuratibu milo yao wenyewe iwafae wao na pia miili ya mama zao, ikiwa tu watu wengine watawaruhusu wafanye hivyo,” akaandika Gabrielle Palmer katika The Politics of Breastfeeding. Kanuni inayoongoza ni ile ya kudai na kutoa—wakati mtoto wako anapodai chakula (kwa kawaida ikiwa kwa kulia), unampa. Mwanzoni, madai yatakuwa baada ya kila muda wa saa mbili au tatu. Wapaswa umruhusu mtoto wako anyonye kwenye matiti yote mawili kila wakati anaponyonya. Watoto wengi huchukua muda wa dakika 20 hadi 40 kumaliza kunyonya, ingawa watoto wengine hupenda kula kwa starehe, wakitua-tua. Walaji hawa wa polepole, wanaweza kuchukua hadi dakika 60 kumaliza mlo wao. Kwa kawaida, mtoto wako anapata chakula cha kutosha ikiwa ananyonya angalau mara nane katika muda wa saa 24, na ikiwa unaweza kumsikia akimeza anaponyonya, na ikiwa ana nepi nane au zaidi zilizoloa kwa siku moja baada ya siku ya tano.

Stadi muhimu zaidi unayohitaji kujifunza unaponyonyesha ni jinsi ya kumshika mtoto vizuri matitini. Kumshika vibaya kwaweza kusababisha mtoto wako asipate maziwa ya kutosha. Watoto wengine hata hukataa kunyonya.

Kumshika mtoto vibaya kwaweza kusababisha tatizo jingine la kawaida: chuchu zilizokatika au zilizo na vidonda. Kitabu Breastfeeding Source Book chaeleza: “Chuchu zenye vidonda husababishwa na mambo kadhaa, lakini la maana ni jinsi mtoto ‘anavyojishikilia matitini,’ na hilo pia lategemea sana jinsi mtoto ameweka kichwa chake kulingana na titi. Ili kumweka vizuri, mtoto wako apaswa awe karibu na matiti, kichwa chake kikiwa katikati (bila kuangalia juu, chini au upande) na akaribie chuchu moja kwa moja ili kuzuia asivute kuelekea upande mmoja.”

Kwa kawaida midomo ya mtoto yapaswa kufunika titi kabisa, angalau sentimeta tatu nyuma ya chuchu. Utajua ikiwa kikao ni sawa ikiwa mwili wote wa mtoto umekugeukia, ikiwa anavuta maziwa sana, kama amestarehe na amefurahi, na ikiwa huhisi uchungu kwenye chuchu.

Wakati wa Kuachisha Kunyonya

Baada ya majuma machache ya kwanza, wewe na mtoto wako mtakuwa mmejuana na labda mtakuwa mmesitawisha ratiba yenye kustarehesha na yenye kufurahisha. Kwa miezi minne hadi sita itakayofuata, mtoto wako hatahitaji chakula au kinywaji kingine chochote isipokuwa maziwa ya matiti. Baada ya hapo unapaswa kuanza kumpa vyakula vingine kidato kwa kidato kama vile mboga zilizopondwa, nafaka, au matunda. Hata hivyo, hadi mtoto wako afikie umri wa miezi tisa au kumi, chakula chake cha msingi bado kitatoka kwenye maziwa yako; kwa hiyo ni vizuri kuendelea sikuzote kumnyonyesha mtoto wako kabla hujampa vyakula vigumu.

Unapaswa kuendelea kunyonyesha kwa muda gani? Muda mrefu iwezekanavyo, lapendekeza WHO. Akina mama wengi huendelea kunyonyesha hadi kufikia mwaka wa pili, wakifikiria hali njema ya mtoto wala si umri wake. Kitabu Mothering Your Nursing Toddler chasema: “Si vigumu kuona uhitaji walio nao watoto wetu wa kuendelea kunyonya—furaha yao katika kunyonya na kutamauka kwao wanaponyimwa. Sababu sahili lakini lenye kushurutisha ya kuendelea kumnyonyesha mtoto ni ili umfurahishe.”

Uthibitisho wa Muumba Mwenye Upendo

Kadiri unavyomnyonyesha mtoto wako, labda usiku sana wakati wengine katika familia wanalala usingizi, fikiria Muumba wa mpango huu. Hata ikiwa huelewi kawaida za kimwili zilizo tata ambazo huwezesha jambo hilo, ajabu ya kunyonyesha itakusaidia uone hekima na upendo wa Muumba wetu.

Fikiria hili—hakuna chakula bora zaidi kwa watoto kushinda maziwa ya mama. Yanatimiza kabisa mahitaji ya mtoto ya chakula na kinywaji katika miezi ya mapema ya maisha. Wakati uleule, ni dawa ya ajabu inayokinga dhidi ya magonjwa. Ni salama, safi, haihitaji matayarisho yoyote, na haigharimu chochote. Inapatikana kote ulimwenguni, na inaongezeka kadiri mtoto aendeleapo kukua.

Fikiria pia jambo la kwamba kunyonyesha kunamletea mama furaha na mtoto pia. Kutoa chakula, ule uhusiano wa mdomo na wa ngozi-kwa-ngozi, na ule ujoto wa kimwili wa kunyonyesha yote husaidia kukuza kifungo chenye nguvu cha upendo na ukaribu kati ya mama na mtoto.

Kwa kweli, Muumba wa mpango huu wa ajabu ni wa kusifiwa sana. Bila shaka utarudia maneno ya mtunga-zaburi Daudi, aliyeandika: “Nitakushukuru [Yehova] kwa kuwa nimeumbwa kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. Matendo yako ni ya ajabu.”—Zaburi 139:14.

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

Waume, Mwe Wenye Kuunga Mkono

• Mwache mke wako ajue kwamba umekubali anyonyeshe. Mhakikishie na kumwunga mkono kwa wororo.

• Msaidie mke wako awe na lishe bora wakati wa uja-uzito na pia wakati ananyonyesha.

• Hakikisha kwamba apata pumziko la kutosha. Mwanamke aliyechoka huenda akawa na ugumu wa kutoa maziwa ya kutosha. Je, waweza kupunguza mizigo yake kwa kuwatunza wale watoto wengine au kushiriki kazi za nyumbani?

• Mke wako akiwa amestarehe na mwenye furaha, maziwa yake yatatiririka vizuri zaidi. Mfurahishe kadiri uwezavyo. Sikiliza matatizo yake, na usaidie kuyatatua.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Matiti kwa Kulinganisha na Chupa

“Maziwa ya matiti ni bora zaidi katika kulisha, ni safi zaidi, hukinga watoto dhidi ya maradhi ya kawaida, na yapunguza uwezekano wa mama kupatwa na kansa ya matiti na ya mji wa mimba. Maziwa ya unga, zaidi ya kuwa ghali, mara nyingi huchanganywa na maji mengi kupita kiasi yasiyo safi na kupewa watoto kupitia chupa ambazo hazikuuliwa viini. Katika jumuiya zenye umaskini, tofauti ni kubwa sana hivi kwamba uhai wa wachanga milioni 1 ungeweza kuokolewa kila mwaka ikiwa akina mama ulimwenguni wangerudia kunyonyesha watoto pekee kwa miezi ya kwanza minne hadi sita.”—The State of the World’s Children 1993, kichapo cha Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki