Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 5/8 kur. 25-27
  • Fumbo la Dolmen—Kwa Nini, Lini, na Jinsi Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Fumbo la Dolmen—Kwa Nini, Lini, na Jinsi Gani?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Majabali ya Ukumbusho
  • Yalijengwa Lini? Na Nani, Jinsi Gani, na Kwa Nini?
  • Maswali Mengi Yamezuka Kuhusu Kaburi la Newgrange
    Amkeni!—2001
  • Kupambana na Maji kwa Muda Mrefu
    Amkeni!—2004
  • Shida ya Kidini Katika Uholanzi
    Amkeni!—1993
  • Je, Wajua?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 5/8 kur. 25-27

Fumbo la Dolmen—Kwa Nini, Lini, na Jinsi Gani?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UHOLANZI

HUENDA ukauliza, ‘Dolmen ni nini?’ Ni eneo la zamani za kale linalofanyizwa na mawe mawili mazito yaliyo wima yenye kiishilizo, kwa kawaida yakifanyiza chumba, ambacho kwa ujumla hutumiwa kama kaburi. Hupatikana hasa magharibi, kaskazini, na kusini mwa Ulaya.

Katika mkoa wa Uholanzi wa Drenthe, kwa kawaida dolmen hupatikana katika maeneo yenye mandhari za kuvutia. Mchoraji mashuhuri Vincent van Gogh aliandika katika mojawapo ya barua zake: ‘Drenthe ni maridadi sana hivi kwamba afadhali nisingeiona ikiwa siwezi kubaki hapa milele.’ Wapendao mambo ya asili vilevile wale wanaopendezwa na akiolojia mataraja yao hutimizwa kwa kiwango kikubwa hata zaidi wanapozuru dolmen katika Drenthe.

Lakini kwa nini mkusanyo wa zamani wa mawe utupendeze? Jibu moja ni udadisi. Kwa nini watu wa kale wangejisumbua hivyo kusukuma na kuchonga na kuinua uzani huu mkubwa mno? Mawe fulani huwa na uzani wa tani kadhaa. Na katika nyakati hizo, hawakuwa na kreni za kisasa za kuinua! Hivyo, ni nini tuwezacho kupata kuhusu dolmen?

Majabali ya Ukumbusho

Dolmen huainishwa kuwa majabali ya ukumbusho (“megalith,” kutokana na Kigiriki, humaanisha “jiwe kubwa”). Labda unafahamiana na menhir za Ufaransa, zilizoitwa kwa kufuatisha neno la Kibreton linalomaanisha “jiwe refu.” Kisiwa cha Balearic ya Minorca kina majabali yajulikanayo kuwa taula (meza), ambazo huwa na ubamba mzito uliolazwa kwa mlalo juu ya jiwe lililo wima, hivyo yakifanyiza umbo la herufi T kubwa sana.

Watu bado wanaendelea kuvutiwa na Stonehenge, katika Uingereza, duara ya mawe makubwa sana, mengine yao yakiwa na uzani wa tani 50. Yapata nguzo 80 za mawe yenye rangi ya samawati zilisafirishwa zaidi ya kilometa 300 kutoka Milima Preseli katika Wales. Kulingana na kitabu cha National Geographic Society Mysteries of Mankind—Earth’s Unexplained Landmarks, “wasomi hukisia kwamba ile nguzo ya ukumbusho [Stonehenge] . . . lilikuwa hekalu ambalo huenda likawa lilidhihirisha mafuatano ya duara ya milele ya jua, mwezi, na nyota kuzunguka mbingu, lakini halikuwa na kusudi jingine lolote.”

Leo dolmen ni kiunzi tu cha kikumbusho cha kaburi, kwa kuwa miamba mikubwa sana hapo awali haikuonekana ikiwa chini ya lundo la mchanga au ardhi. Uvumbuzi umeonyesha kwamba dolmen ilikuwa ziara la jumuiya. Uthibitisho fulani huonyesha kwamba zaidi ya watu mia moja walizikwa katika dolmen moja—kwa kweli ilikuwa sehemu ya makaburi!

Katika Uholanzi, dolmen 53 zimehifadhiwa kufikia wakati wetu; kati ya haya 52 hupatikana katika mkoa wa Drenthe. Kwa kustaajabisha, hazikusimamishwa ovyoovyo, lakini nyingi hupangwa kuelekea mashariki-magharibi, mwingilio ukiwa upande wa kusini, jambo ambalo huenda lilihusiana kwa kadiri fulani na hali za kimsimu za jua. Wajenzi wa kale walitumia miamba iliyo wima ya kutegemeza na mawe makubwa yenye miishilizo, huku vitundu kati ya miamba vilizibwa kwa vipande vinene vya jiwe. Sakafu ilitandazwa kwa mawe. Katika Uholanzi dolmen kubwa zaidi, karibu na kijiji cha Borger, ina urefu wa meta 22 na bado ina miamba 47. Moja ya mawe yenye viishilizo lina urefu unaokaribia meta 3 na uzani wa tani 20! Jambo hili hutokeza maswali kadhaa.

Yalijengwa Lini? Na Nani, Jinsi Gani, na Kwa Nini?

Majibu ya maswali hayo ni ya juujuu sana kwa sababu hakuna historia iliyoandikwa kutoka Ulaya ya wakati huo. Hivyo, inafaa kurejezea dolmen kuwa nguzo za ukumbusho za kifumbo. Ni nini, basi, kijulikanacho kuzihusu? Kwa vyovyote vile, ni madai gani ambayo hufanywa?

Katika mwaka wa 1660, “Padri” Picardt, wa jiji dogo la Coevorden, katika Drenthe, alimalizia kwamba zilijengwa na majitu. Baada ya muda, wenye mamlaka wa hapo walionyesha upendezi katika makaburi haya. Kwa sababu mawe ya makaburi yalitumiwa kuimarisha mahandaki na vilevile kujenga makanisa na makao, Usimamizi wa Mandhari ya Nchi wa Drenthe ulitunga sheria Julai 21, 1734, ya kulinda dolmen.

Ni kufikia mwaka wa 1912 tu ndipo dolmen zilichunguzwa na wataalamu. Vigae (vipande vya udongo), vyombo (vichwa vya shoka vilivyotengenezwa kwa chuma ngumu sana, chembe ya mshale), na madoido, kama vile shanga za kaharabu, vilipatikana ndani ya dolmen lakini mabaki machache ya kiunzi, kwa kuwa vyombo hivi vilihifadhiwa vibaya ndani ya udongo wenye mchanga. Nyakati nyingine, vigae vingi kufikia vyombo vya kulia 600 vilipatikana. Tukidhania kwamba vyombo viwili au vitatu vya kulia viligawiwa kila mfu, lazima hesabu kubwa ya watu iwe ilizikwa katika maziara fulani.

Wanasayansi hudai kwamba dolmen zilijengwa na majabali yasiyo ya kawaida kutoka Skandinavia, ambayo yalisafirishwa na barafuto wakati wa enzi ya kale ya barafu. Inasisitizwa kwamba wajenzi walikuwa wakulima wa kile kinachojulikana kuwa utamaduni wa “Vyombo vya Kunywea Vyenye Umbo la Faneli,” uliitwa hivyo kwa sababu ya vyombo vya kunywea vyenye umbo la faneli ambavyo vimepatikana.

Nadharia moja kuhusu mtindo wa ujenzi inataarifu: “Huenda ikawa miamba mikubwa ililazwa juu ya mbao zenye mcheduara na kuvutwa na kamba za ngozi. Kusudi wasukume juu mawe yenye viishilizo, yadhaniwa kuwa tuta la mchanga na udongo lilijengwa.” Lakini hakuna mtu yeyote aliye na uhakika jinsi jambo hili lilivyofanywa. Kwa nini wafu hawakuzikwa kwa njia ya kawaida? Wajenzi walikuwa na itikadi gani kuhusu maisha baada ya kifo? Kwa nini vyombo hivyo vya kale viliachwa ndani ya makaburi? Watafiti wanaweza kukisia tu majibu. Kwa sababu dolmen zilijengwa zamani za kale, haiwezekani kusema kwa usahihi zilijengwa lini, na nani, kwa nini, na jinsi gani.

Wakati uliowekwa wa Mungu, ufikapo, wafu wafufuliwapo, wale warudio huenda wakajibu baadhi ya maswali haya. (Yohana 5:28; Matendo 24:15) Huenda wakati huo, wajenzi wa dolmen hatimaye, wakafunua wakati walipoishi, walikuwa nani, kwa nini walijenga nguzo zao za ukumbusho zenye kuvutia, na jinsi walivyofanya.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Taula katika Minorca, Hispania

[Picha katika ukurasa wa 25]

Dolmen karibu na Havelte, Uholanzi

[Picha katika ukurasa wa 26, 27]

Stonehenge, Uingereza

Chini: Ile Dolmen Kubwa, karibu na Borger, Uholanzi

[Picha katika ukurasa wa 26]

Dolmen iliyojengwa upya karibu na kijiji cha Schoonoord, Uholanzi, ikionyesha tuta la udongo na mawe yaliyowekwa wazi

[Picha katika ukurasa wa 27]

Ziara refu katika Emmen (Schimmeres), Uholanzi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki