Shida ya Kidini Katika Uholanzi
Na mleta habari za Amkeni! katika Uholanzi
“KASISI wa mwisho aweza kuzima taa tafadhali?” Mzaha huu wenye dhihaka unasambaa kwenye nyumba za watawa katika Uholanzi. Unaona kimbele wakati ambapo mtawa au kasisi wa mwisho atakapoondoka katika nyumba ya mwisho ya watawa inayofanya kazi katika nchi hiyo na kuiacha ukiwa. Na unamuuliza ahakikishe kwamba haachi taa zikiwaka katika jengo lililoachwa! Je! jambo hilo kweli lingeweza kutokea? Je! viongozi wa kidini wamo katika hatari ya kutoweka katika Uholanzi, pamoja na makundi yao?
Kuacha Ukasisi
Kuhusiana na Kanisa Katoliki, kila mwaka idadi ya makasisi hupungua. Kuanzia 1968 hadi 1978, idadi ya makasisi ilipungua kwa asilimia 27.2, na mwendo huo umeendelea tangu wakati huo. Kwa nini? Sababu moja inayotolewa ni useja wa kulazimishwa. Katika 1970 Baraza la Ukasisi la Kitaifa liliamua kwamba “takwa la useja wa kulazimishwa kwa kutimiza wajibu wa mtu akiwa mhudumu lapaswa kuondolewa mbali.” Maaskofu Waholanzi walihisi kwamba wafuasi wangeweza hata kunufaika ikiwa wangetumikiwa na makasisi waliooa. Hata hivyo, Papa Paulo wa 6, alikataa kwa nguvu wazo hilo. Bila shaka hiyo ndiyo iliyokuwa sababu ya makasisi zaidi ya 2,000 kujiuzulu ukasisi baadaye kuanzia 1980 na hesabu ya wale wanaoingia ukasisi ikapungua.
Akizungumzia upungufu wa ukasisi katika Uholanzi, Kardinali aliyekufa Alfrink alikumbuka wakati ambapo mjumbe wa papa, alipokuwa akitazama seminari iliyokuwa mbele ya nyumba ya kardinali, aliuliza ni kwa nini maaskofu walifunga majengo hayo mazuri. Kardinali alijibu: “Ni wazi kwamba huelewi. Maaskofu hawakufunga seminari zozote; walifunga tu milango baada ya wanafunzi kwenda.”
Si makasisi tu wanaoacha kanisa bali makundi yao pia yanaacha kanisa katika Uholanzi. Na hilo si tukio jipya. Huko nyuma katika 1879 hesabu ya watu ilionyesha kwamba punde kuliko asilimia 1 ya idadi ya watu wote ilikuwa watu wa kilimwengu, yaani, wasiokuwa washiriki wa kanisa. Kufikia 1920, karibu asilimia 8 ya idadi hiyo ilidai kutokuwa wa dini. Katika 1930 hesabu hiyo ilipanda hadi asilimia 14.4. Kufikia 1982 ilikuwa hesabu yenye kushtua ikiwa asilimia 42, na uchunguzi wa karibuni zaidi umeonyesha kwamba zaidi ya asilimia 51 ya Waholanzi si wa kanisa lolote.
“Enzi ya Barafu” kwa Kanisa
Jambo lenye kutazamisha zaidi kuliko kupungua kwa ushirika wa kanisa ni ule upungufu wa hudhurio la wale washiriki wa kanisa. Katika 1988 gazeti De Telegraaf lilikuwa na kichwa kikuu “Enzi ya Barafu Yaingia Kanisani.” Gazeti lilisema hivi: “Mtu yeyote hashtuki kamwe kanisa linapobomolewa. Hudhurio la kanisa linapungua kwa njia yenye kuogofya sana. Hilo ni kweli si katika Ukatoliki pekee bali pia katika makanisa ya Reformed na Kalvini. Hali hiyo ya kilimwengu ikiendelea, katika vizazi vichache, hakuna mtu yeyote atakayehudhuria kanisa tena.”
Gazeti hilo liliendelea kusema kwamba upungufu katika Katoliki ya Roma ndio mbaya zaidi. Lilitaja kwamba katika 1965 karibu asilimia 60 ya Waholanzi wote Wakatoliki bado walihudhuria Misa. Katika 1975 hesabu hiyo ilikuwa asilimia 28. Katika miaka ya karibuni imeshuka hadi chini ya asilimia 16.
Upungufu wa hudhurio la kanisa umeathiri majengo ya kanisa, ambayo hufungwa wakati gharama za juu za kuyatunza na kuyatumia zinapolemea makutaniko yanayopungua. Hivyo basi, majengo mengi ya kidini yamebomolewa au kuuzwa kwa ajili ya matumizi mengine. Watu wachache leo hushangaa kuingia jengo la kanisa na kupata likitumiwa kuwa hifadhi ya vitu vya kale, duka la baiskeli, jumba la michezo, jumba la michezo ya kuigiza, duka la maua, mkahawa, au vyumba vya kukodisha.
Basi, si ajabu kwamba wakuu wa kidini hawatarajii mazuri wakati ujao. Baada ya Papa John wa 2 kutembelea Uholanzi, askofu mmoja alisema: “Papa alitembelea maiti, au angalau mgonjwa mahututi ambaye anafikiri bado angali hai.”
Sababu Inayowafanya Waache Kanisa
Kupungua kwa washiriki wa kanisa kumezidishwa na mambo mengi mapya. Miongoni mwayo ni ukosefu wa heshima kwa mamlaka. Watu hawako tayari tena kukubali mambo kwa sababu tu mtu aliye katika mamlaka anawaambia wafanye hivyo. Jambo linalohusiana na hilo ni ule mkazo unaotiliwa juu ya uhuru wa mtu mmoja-mmoja. Leo, watu wanataka kujiamulia wenyewe watakaloamini na watakavyotenda.
Mambo mengine mawili yenye kuongezea yasemwa kuwa ni uvutano wa vyombo vya habari na mwelekeo wa kisasa wa kutoamini dini. Kuna hisi pia kwamba dini madhubuti huondoa uhuru na utu wa kibinafsi. Zaidi ya hilo, hata kama watu bado wana mwelekeo wa kidini, hali zinaweza kuwafanya waache kanisa lao. Kwa mfano, washiriki wa kanisa wenye kupendelea desturi hawahisi starehe katika kanisa lenye mhudumu au kasisi mwenye kupendelea mabadiliko. Na waenda-kanisani wenye kupendelea maendeleo huhisi kutofaa wakiwa kwenye makutaniko yasiyopenda mabadiliko.
Kwa upande wa Protestanti, Kanisa la Kalvini lina sifa ya muda mrefu ya kushikilia maadili ya zamani. Kwa hiyo, wengi walishangazwa katika 1979 wakati Baraza la Dini ya Kalvini la Uholanzi liliposihi makanisa yaruhusu wagoni-jinsia-moja kwenye ekaristi na kwenye huduma. Katika 1988 Mkutano Mkuu wa Maaskofu uliokuwa wa kimataifa uliuliza Wakalvini walioko Uholanzi wafikirie uamuzi huo tena, lakini baraza hilo likapeleka habari kwamba uamuzi huo haungeweza kubadilishwa. Katika 1989 baraza hilo la Dutch Reformed Church la Uholanzi pia lilipinga hatua zozote za kuadhibu wagoni-jinsia-moja. Hebu wazia Waprotestanti “wa kizamani” walivyohisi wakati mhudumu Mkalvini, mgoni-jinsia-moja aliposema kanisani kwamba “ugoni-jinsia-moja ni zawadi kutoka kwa Mungu; Mungu pia hupenda [ugoni-jinsia-moja]”!
Je! Ukristo Utakoma Kuwapo?
Kwa sababu ya mambo hayo yanayoendelea na mengine mengi, je, inashangaza kwamba wengi sana wameacha makanisa katika Uholanzi na nchi nyinginezo nyingi? Kwa kweli, watu wenye kufikiri kwa uzito hata wameamua kwamba labda Ukristo wa kweli hauwezi kupatikana mahali popote pale. Je! Ukristo utakoma kuwapo hatima?
Biblia ilitabiri kukauka kwa utegemezo kwa Jumuiya ya Wakristo, pamoja na dini nyinginezo, katika siku yetu. (Ufunuo 16:12; 17:15) Lakini pia iliona kimbele kwamba wengine wangeacha dini bandia si kwa sababu tu ya kutoridhika au kuvunjika moyo bali kwa sababu ya kusudi lifaalo. Biblia husihi kiunabii hivi: “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.” (Ufunuo 18:4) Yule anayerejezewa kuwa “kwake” ni kahaba wa kidini wa ufananisho, ‘Babuloni Mkubwa,’ ambaye ni kutia ndani dini zote za ulimwengu, pamoja na zile za Jumuiya ya Wakristo ya ki-siku-hizi. Yale maneno “watu wangu” ni watafutaji kweli wenye moyo mweupe wanaoacha Babuloni Mkubwa kwa sababu wanataka kumtumikia Mungu katika njia ambayo Yesu alifundisha. Jumuiya ya Wakristo imekengeuka mbali na Ukristo wa kweli hivi kwamba watu wenye moyo mweupe lazima watoke kati yake ili wamtumikie Mungu kwa njia inayokubalika.
Ukristo wa kweli upo na unaendelea kusitawi katika Uholanzi na pia kotekote ulimwenguni. Wajapokuwa si wakamilifu, Mashahidi wa Yehova, wanafuata mafundisho na mazoea ya Kristo. Hutazamiwi kukubali tu maneno hayo. Kwa nini usichunguze imani za Mashahidi kwa kutumia Biblia, na ujionee mwenyewe. Jifunze kutoka Neno la Mungu Ukristo wa mitume wa Yesu, ukilinganisha na mambo ambayo makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yamefundisha na kufanya kwa karne nyingi. Kufanya hivi kutakuletea manufaa za “uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye,” kama vile mtume Paulo alivyoeleza.—1 Timotheo 4:8.
[Picha katika ukurasa wa 10 and 11]
Makanisa mengi katika Ulaya sasa yanatumiwa kwa makusudi ya kilimwengu. Ukurasa 10: Gereji katika Uholanzi. Ukurasa 11: Jumba la watu waliostaafu, karakana, klabu cha wavulana, na kanisa lililoachwa katika Penygraig, Wales