Kanisa—Mabadiliko na Mvurugo
“Waumini wengi husumbuka kwa mabadiliko wanayotwikwa.” —L’Histoire, July/August 1987.
“Ikiwa tu mojapo desturi ambazo kwazo kanisa limejengwa inatolewa . . . kanisa lapoteza uelekevu wote. . . . Weka [‘mkate uliotakaswa’ unaotumiwa kwenye Misa], mkononi badala ya mdomoni, na ‘unaharibu imani ya Wafaransa wengi.’”—Voyage à l’intérieur de l’Église Catholique.
“Katika kurudisha utaratibu wa ibada za kidini na kuanza kutumia lugha ya wenyeji, inaonekana kanisa lilipoteza waendaji kanisa wengi sana [ambao walikuwa] wamezoea desturi kadhaa zilizofikiriwa kuwa haziwezi kubadilika. . . . Kwa ghafula, hisi ya kuwa na daraka ikavunjika, na imani ikadhoofika.” —Nord Eclair, Aprili 24-25, 1983.
MANUKUU yanayotangulia yaonyesha wazi mvurugo ulioko katika akili za Wakatoliki wengi. Bado swali larudi mara kwa mara: “Wazazi wetu na babu na nyanya zetu walihudhuria Misa iliyosemwa kwa Kilatini na kusali katika njia hususa. Njia hii ya kufanya mambo ingeweza kubatilishwaje kwa ghafula hivyo?”
Mwelekeo mpya wa kanisa kwa dini nyingine ni chanzo cha matatizo pia. Gazeti la Kifaransa la kila siku Le Monde lasema hivi: “Waumini wengi wanahisi wamedanganywa. Walikuwa wameambiwa mara nyingi sana kwamba dini yao ndiyo iliyokuwa ya kweli pekee, au angalau bora zaidi.” Ni kweli, idadi kubwa ya Wakatoliki wanapendelea wazo la kuzungumza na “ndugu zao waliotenganishwa,” wawe ni Waorthodoksi au Waprotestanti. Lakini badiliko hili la maoni kuelekea dini nyingine halieleweki na wengi ambao hapo zamani walifundishwa kwamba ‘hakuna wokovu nje ya kanisa.’ Mtazamo huu mpya wa kanisa umesababisha sana mgawanyiko baina ya Vatikani na washikilia desturi, ambao kiongozi wao wa kiroho, askofu mkuu aliyekufa Marcel Lefebvre, alitengwa na Papa John Paul wa 2 katika 1988.
Mamlaka Yakataliwa
Mara nyingi Wakatoliki huonyesha mfadhaiko wao kwa kutilia shaka mamlaka ya kanisa. Hata ikiwa John Paul wa 2 anathaminiwa kwa msimamo wake wa kupendelea haki ya ulimwengu, Wakatoliki wengi hukataa kufuata kanuni za kiadili ambazo yeye hutetea katika hotuba zake za hadhara. Idadi kubwa ya Wakatoliki waliooana hutumia njia za kupanga uzazi zinazokatazwa na kanisa. Wengine huzoea kutoa mimba.
Mamlaka ya Kanisa inatiliwa shaka katika pande zote. Ukweli wa kwamba papa na maaskofu wengine wa vyeo vya juu wamechukua msimamo hususa juu ya jambo fulani haujazuia watu wa kawaida, makasisi, na hata maaskofu wasiwapinge. Kitabu La Réception de Vatican II chaeleza hivi: “Kwa kuangalia mambo katika njia hii, hali iliyofanyizwa na baraza hilo imeenea kwenye maisha ya kanisa. Kanisa la Roma Katoliki limekuwa kikao cha mabishano makali, ya kudumu. Hata mapendekezo ya papa hujadiliwa na kuchambuliwa mara nyingi. Idadi ya Wakatoliki wa Roma wanaosema kwamba hawaamini baadhi ya matamshi ya papa—kwa kisehemu au kikamili—inaongezeka.”
Baadhi ya Wakatoliki wamekubali mabadiliko kwa kuwa waaminifu kwa kanisa na kuendelea kufuata kawaida za dini hiyo. Wengine wanasumbuliwa na hali hiyo na wanatosheka kuishi wakiwa washiriki ambao hawakubali mambo yote ya kanisa. Kulingana na tarakimu za karibuni, kuna kikundi madhubuti cha tatu cha Wakatoliki kwa jina tu ambao wanashindwa kuunga mkono kanisa kabisa.
Mchafuko wa kidini haumo tu katika Kanisa Katoliki la Ufaransa. Katika Uholanzi pia, shida imeongezeka kwa Wakatoliki na Waprotestanti pia, kama vile makala yetu ifuatayo itakavyoeleza.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe Katika Kanisa la Uingereza?
Na mleta habari za Amkeni! katika Uingereza
NI TUKIO lisilo la kawaida? Si kulingana na The Sunday Times la London. “Kanisa la Uingereza Limegawanyika Kabisa,” likatangaza. “Kanisa Lililogawanyika Laelekea Kwenye Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe.” Ni nini kimefanya kanisa la Uingereza liwe katika hali mbaya hivyo? Yale mapendekezo ya kuwekelewa mikono kwa wanawake kuwa makasisi.
Katika uamuzi wa kihistoria katika Novemba uliopita, baraza la Kanisa la Uingereza lilipiga kura kwa wingi wa theluthi mbili likipendelea kuwekelea wanawake mikono wawe makasisi. Baadhi ya makasisi 3,500, theluthi moja ya jumla ya wale waliomo kanisani, wanasemekana kuwa walipinga uamuzi huo, na wengine tayari wameacha kanisa kwa sababu ya kuhisi wamefadhaishwa. Wengine, wakiwa chini ya uongozi wa aliyekuwa askofu wa London, wanataka kubaki wakiwa Waanglikana ilhali wanatafuta “uhusiano na Upapa” katika Roma.
Askofu Mkuu wa Canterbury aliongoza kampeni hiyo kwa kupendelea badiliko hilo. “Kuwekelewa mikono kwa wanawake kuwa makasisi,” akasema, “hakubadili chochote katika imani za kidini, maandiko au imani ya Kanisa letu.” Akaongezea: “Huenda ikasaidia kufaa kwa kanisa kwa maoni ya ulimwenguni pote. Kwa kweli linafanya yale linalofundisha linapoongea juu ya usawa.”
Lakini si wote wanaokubali. Uamuzi huo ulipojulikana, mtu mmoja wa kawaida, akiubandika uamuzi wa baraza hilo kuwa “uasi-imani,” aliliacha kanisa mara hiyo awe Mkatoliki wa Roma. “Uamuzi wa kuwekelea wanawake mikono wawe makasisi umetushtua. Kuna msukosuko wa kiroho. Watu wengi hawajui la kufanya,” akaomboleza kasisi mmoja wa London. Wakati uleule, Vatikani inapotoa mwaliko wenye hadhari kwa watoro hao, inauona uamuzi huo kuwa “kizuizi kipya na kibaya zaidi kwa mwendo wote wa kupatanisha.”
Wanawake wanaokadiriwa kuwa 1,400 wanangojea kuwekelewa mikono kuwa makasisi, lakini lazima kwanza Bunge la Uingereza likubali hatua hiyo, ambayo lazima ipate Kibali cha Malkia cha Kifalme. Yote hayo yanaweza kuchukua miaka miwili. Itapendeza kuona hali itakavyokuwa katika Kanisa la Uingereza kufikia wakati huo.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 7]
Camerique/H. Armstrong Roberts