Kuagizwa Rasmi kwa Wanawake Kwaghadhibisha Makasisi wa Anglikana
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
KATIKA Novemba 1992, Sinodi Kuu ya Kanisa la Uingereza ilikubali shauri la kuagizwa rasmi kwa wanawake kuwa mapadri. Kama tokeo, makasisi Waanglikana 150 hivi wasioridhika wametangaza nia yao ya kujiuzulu kufikia 1995. Wengi wao wanapanga kuhamia Kanisa Katoliki la Roma. Kasisi mmoja wa cheo cha juu ataka kuhama pamoja na parishi yake yote—kutia ndani jengo la kanisa! The Sunday Times la London lilitarajia kwamba kuagizwa rasmi kwa kikundi cha kwanza (ambako hatimaye kulitukia katika Machi 1994) kungekuwa “sherehe yenye kubishaniwa kuliko yote katika historia ya miaka 450 ya Kanisa la Uingereza.”
Kwa nini makasisi wengi wanaghadhibika? Wengine wanahisi tu kwamba si jambo linalofaa kwa wanawake kufanya kazi wakiwa mapadri. Wengine wanahofu kwamba uamuzi wa sinodi unaharibu jitihada za majuzi za kuunganisha Kanisa la Uingereza na dini za Katoliki na Othodoksi. Kwa kweli, msemaji mmoja wa Vatikani alitangaza kwamba papa mwenyewe huona uamuzi wa Kanisa la Uingereza kuwa “kizuizi kikubwa sana kwa kila tumaini la kuunganika tena.”
Hata hivyo, parishi moja-moja za Kanisa la Uingereza bado zaweza kupiga kura ili kufungia mapadri wanawake. Hata wanaweza kuamua kukataa askofu wao na badala yake kuwa na padri asafiriye ambaye, kulingana na New York Times, “atatoa utunzi wa uchungaji kwa wale wanaokataa kuukubali kutoka kwa mapadri wanawake.”
Jinsi ilivyo tofauti na shauri la Paulo kwa Wakristo wa karne ya kwanza kwamba “nyote mseme kwa upatano, na kwamba kusiwe na migawanyiko miongoni mwenu, bali kwamba mpate kuunganishwa kwa kufaa katika akili ileile na katika namna ileile ya fikira.” (1 Wakorintho 1:10, NW) Kadiri hilo bishano linavyozidi, waparishi wengi wanafanya maamuzi yao wenyewe. “Yaonekana hatuna chochote kilichobaki tena cha kuamini hapa katika Kanisa la Uingereza,” akasema mwanamke mmoja. “Nina hisi ya shangwe na kitulizo tu kwa kuliacha Kanisa la Uingereza.”