Kwa Nini Kanisa Linapoteza Uvutano?
“Kila Mstoiki alikuwa Mstoiki; lakini yu wapi Mkristo katika Jumuiya ya Wakristo?”
RALPH WALDO EMERSON, MWANDIKAJI INSHA NA MSHAIRI MMAREKANI WA KARNE YA 19.
“MIMI ni Mkatoliki—lakini asiye mtendaji,” aeleza mama mmoja mchanga. “Sijishughulishi na dini,” aongeza tineja mmoja. Maelezo yao ni ya kawaida sana miongoni mwa kizazi kichanga cha watu wa Ulaya. Ingawa wazazi wao—au yaelekea zaidi wazazi-wakuu wao—bado ni waenda-kanisani, imani ya kidini haijaziba pengo la kizazi.
Kwa nini mazoea ya kidini yaliyoheshimiwa sana na vizazi vya watu wa Ulaya yameachwa?
Hofu Si Kichocheo Tena
Kwa karne nyingi hofu ya moto wa helo au purgatori ilikuwa na uvutano wenye nguvu kwa watu wa Ulaya. Mahubiri yenye hisia mno na michoro ya kanisa inayoonyesha wazi helo iwakayo isiyoweza kuzimika iliwasadikisha watu wa kawaida kwamba ni uhudhuriaji kanisa wenye staha tu utakaowaokoa kutokana na hukumu. Catechism of the Catholic Church huendelea kutaarifu kwamba “Kanisa huwajibisha waumini ‘kushiriki katika Ushirika Mtakatifu Jumapili na sherehe za kidini.’”a Katika maeneo ya mashambani msongo wa kijamii pia ulikuwa wa kadiri kubwa—kila mtu alitarajiwa kuhudhuria kanisa kila Jumapili.
Lakini nyakati zimebadilika. Watu sasa wajihisi huru kufanya watakalo. Hofu si kichocheo tena. Kanisa limeacha kimya-kimya kukazia fundisho la helo, kwa kuwa Wakatoliki wengi wa Ulaya hata hawaliamini.
Kwa uhakika, ile “dhambi” ya kukosa kuhudhuria Misa ya Jumapili haionwi tena kuwa nzito. Tirso Vaquero, kasisi Mkatoliki katika Madrid, Hispania, akiri: “Mkristo [Mkatoliki] akikosa kuja kwenye Misa Jumapili, tunasikitika kwa unyoofu kwa sababu amepoteza muda huu wa mawasiliano pamoja na Mungu na ndugu zake, si kwa sababu ametenda dhambi. Hilo si jambo la maana sana.”
Kwa hiyo hofu haichochei ujitoaji tena. Namna gani mamlaka ya maadili ya kanisa na viongozi walo—je, wanaweza kudai uaminifu-mshikamanifu wa makundi yao?
Tatizo la Mamlaka
Kukoma kwa hofu ya kidini kumepatana na mzoroto wenye kutokeza katika hali ya maadili ya kanisa. “Kwa karne nyingi tumekuwa na . . . walimu wengi sana wa maadili na walimu wachache sana wenye adili,” alalamika mwanahistoria Mwitalia Giordano Bruno Guerri. Ukosefu huu wa uongozi wa maadili ulionyeshwa wazi na vile vita viwili vya ulimwengu vilivyoharibu Jumuiya ya Wakristo. Makanisa ya Ulaya hayakuwa na uwezo wa kuzuia waumini kujiingiza katika pindi hiyo yenye umwagikaji damu. Vibaya hata zaidi, makanisa yalijihusisha sana katika jitihada za vita—pande zote mbili.
“Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, iliyokuwa vita ya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa mafarakano ya Kikristo, ilifungua kipindi cha msiba na aibu kwa Ukristo,” aonelea mwanahistoria Paul Johnson. “Vita ya Ulimwengu ya Pili ilitokeza mashambulizi yenye kuhuzunisha hata zaidi kwa hali ya maadili ya imani ya Kikristo kuliko ile ya Kwanza. Ilifunua ukosefu wa uvutano wa makanisa katika Ujerumani, chanzo cha yale Marekebisho Makubwa ya Kidini, na woga na ubinafsi wa Makao Matakatifu ya papa.”
Mikataba ya Vatikani pamoja na utawala wa Nazi wa Hitler na serikali za Ufashisti za Mussolini katika Italia na Franco katika Hispania pia ziliharibu mamlaka ya maadili ya kanisa. Hatimaye, gharama ya kidini kwa manufaa hiyo ya kisiasa ilikuwa upotezo wa sifa ya ustahili.
Kanisa na Serikali —Kukifungua Hicho Kifungo
Katika karne ya 20, nchi nyingi za Ulaya mwishowe zimefungua kile kifungo kinachounganisha Kanisa na Serikali. Kwa hakika, hakuna nchi yoyote kubwa ya Ulaya inayotambua sasa Ukatoliki wa Kiroma kuwa dini yayo rasmi.
Ingawa huenda bado makanisa makuu yakasaidiwa kifedha na serikali, yamepoteza uvutano wa kisiasa yaliyokuwa nao. Si makasisi wote wamekubali uhalisi huu mpya. Myesuiti mashuhuri Mhispania José María Díez-Alegría aamini kwamba “viongozi wa kanisa [Katoliki] hufikiri—wengi wao kwa unyoofu wote—kwamba hawawezi kutimiza wajibu wao wa kidini bila utegemezo wa serikali.”
Lakini huu utegemezo wa serikali umeporomoka. Hispania, ambayo ilikuwa na serikali ya “kitaifa ya Kikatoliki” tangu 1975 hutolea kielelezo hali hii. Katika miaka ya majuzi mamlaka ya kanisa ya Hispania imekuwa na pigano lenye kuendelea na serikali ya Kisoshalisti kuhusu kutegemeza kanisa kifedha. Askofu wa Teruel, Hispania, hivi majuzi alilalamika kwa wanaparishi wake kwamba ahisi “kunyanyaswa akiwa Mkatoliki” kwa sababu serikali ya Hispania haitolei kanisa utegemezo wa kutosha wa kifedha.
Katika 1990 maaskofu wa Hispania walitangaza kwamba jamii ya Kihispania ilikuwa ikiathiriwa na “tatizo zito sana la dhamiri na adili.” Walimlaumu nani kwa hilo ‘tatizo la maadili’? Hao maaskofu walidai kwamba mojawapo visababishi vikuu kilikuwa “mtazamo wa kiakili wenye shaka unaochochewa mara nyingi na mamlaka ya umma [serikali ya Hispania].” Kwa wazi, maaskofu hao wanatarajia serikali iunge mkono fundisho la Kikatoliki na vilevile kuandaa misaada ya kifedha.
Je, Makasisi Hutenda Yale Wanayohubiri?
Utajiri mkubwa sana wa Kanisa Katoliki sikuzote umekuwa aibu kwa makasisi wanaofanya kazi katika parishi maskini. Iliaibisha hata zaidi wakati Banki ya Vatikani ilipopasishwa hatia katika kile gazeti Time liliita “kashifa mbaya kuliko zote katika Italia ya baada ya vita.” Katika 1987, amri zilitolewa na mahakimu wa Italia za kukamatwa kwa askofu mkuu na maofisa wengine wawili wa banki ya Vatikani. Hata hivyo, kwa sababu ya hadhi ya kipekee ya enzi ya Vatikani, makasisi walioshtakiwa waliepuka kukamatwa. Banki ya Vatikani ilisisitiza kwamba hakuna kosa lililotendwa lakini ilishindwa kufuta wazo la kwamba kanisa halikuwa likitenda yale lifundishayo.—Linganisha Mathayo 23:3.
Mwenendo mbaya wa kingono wenye kutangazwa sana umetokeza madhara hata zaidi. Katika Mei 1992 askofu mmoja wa Ireland, ajulikanaye sana kwa kuunga mkono useja, aliomba dayosisi yake “imsamehe” na “kumwombea.” Alilazimishwa kujiuzulu baada ya kufunuliwa kwamba alikuwa baba ya mvulana mwenye umri wa miaka 17 na alikuwa ametumia fedha za kanisa kumlipia elimu. Mwezi mmoja mapema kasisi Mkatoliki alitokea kwenye televisheni ya Ujerumani pamoja na “mwandamani” wake na watoto wao wawili. Yeye alisema alitamani “kufungua mazungumzo” juu ya suala la hayo mahusiano ya kisiri ambayo makasisi wengi sana huendeleza.
Kashifa hizo hazina budi kuacha alama yazo yenye kudumu. Mwanahistoria Guerri, katika kitabu chake Gli italiani sotto la Chiesa (Waitalia Walio Chini ya Kanisa), adai kwamba “kwa karne nyingi Kanisa limechukiza Waitalia.” Tokeo moja, yeye asema, ni “kusitawi kwa upingaji ulioenea wa uvutano wa makasisi kwa mambo ya kilimwengu, hata miongoni mwa waumini wenye msimamo mzuri.” Huenda Wakatoliki wenye kuchukizwa wakahisi kuuliza makasisi wao swali lilelile ambalo mtume Paulo aliwauliza Warumi: “Kwa kielelezo, wewe wahubiri dhidi ya wizi, lakini je, una uhakika juu ya ufuatiaji wa haki wako mwenyewe? Unashutumu zoea la uzinzi, lakini je, una uhakika juu ya usafi wako mwenyewe?”—Warumi 2:21, 22, Phillips.
Pengo Kati ya Makasisi na Watu wa Kawaida
Tatizo lisilo wazi sana lakini liwezalo kudhoofisha sana ni lile pengo kati ya makasisi na watu wa kawaida. Barua za miongozo ya kiroho kutoka kwa maaskofu yaonekana huudhi wanaparishi badala ya kuwafundisha. Katika uchunguzi mmoja wa Hispania, ni asilimia 28 tu ya wale waliohojiwa “walikubaliana na taarifa za maaskofu.” Idadi sawa na hiyo “haikujali hata kidogo,” na asilimia 18 ilisema kwamba “haikuelewa kile [maaskofu] walichokuwa wakizungumzia.” Askofu mkuu Ubeda wa Majorca, Hispania, alikiri: “Ni lazima sisi maaskofu tukubali lawama yetu ya kuhusika katika taratibu ya kugeuza watu kutokuwa Wakristo—jambo ambalo ni hakika.”
Ukosefu wa ujumbe ulio wazi wa Kimaandiko hutenga hata zaidi watu wa kawaida. Kulingana na Catholic Herald, “makasisi wengi [katika Ufaransa] wameamua kujiingiza katika mambo ya kisiasa ili ‘wafae,’” hata ingawa wengi wa wanaparishi wao wangewapendelea wakazie fikira mambo ya kiroho. Kasisi mmoja aliye pia mtaalamu wa elimu ya jamii Mwitalia Silvano Burgalassi akiri: “Labda [vijana] wamejitenga na Mungu kwa sababu ya kielelezo chetu kibaya. Tumewapatia mchanganyo wa kuridhiana, dini na biashara, ubinafsi na ughoshi.” Haishangazi kwamba makasisi wanapoteza hadhi yao ya kijamii. “Mimi ni Mkatoliki, lakini siamini katika makasisi” ni msemo unaosikiwa mara nyingi kutoka kwa Wahispania Wakatoliki.
Wakatoliki fulani huona ikiwa vigumu kueleza makasisi yaliyo mioyoni mwao, na wengine wana shaka nzito kuhusu mafundisho ya kanisa—hasa yale wanayoona kuwa yasiyo na kiasi au yasiyofanya kazi.
Mafundisho Yasiyoweza Kufahamika
Kielelezo kibaya kilicho wazi ni fundisho rasmi la Katoliki juu ya habari ya helo. Catechism of the Catholic Church hutaarifu: “Fundisho la Kanisa lathibitisha kuwapo kwa helo na umilele wayo.” Hata hivyo, uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kwamba ni robo tu ya Wakatoliki Wafaransa na thuluthi ya wenzao Wahispania wanaoamini kwamba helo ipo.
Vivyohivyo, inapohusu masuala ya maadili, watu wa Ulaya huelekea kuwa “Wakristo wa fanya-mambo-yako-mwenyewe.” Mimmi, tineja Mlutheri kutoka Sweden, aamini kwamba maswali ya maadili, kama vile kuwa na watoto nje ya kifungo cha ndoa, ni “jambo la mtu kujiamulia.” Wakatoliki Wafaransa walio wengi watakubaliana naye. Wanapokabiliwa na maamuzi ya maana katika maisha, asilimia 80 ilisema kwamba ingefuata mwongozo wa dhamiri yayo badala ya ule wa kanisa.
Wakati uliopita mamlaka ya kanisa ilikuwa na nguvu ya kukomesha sauti yoyote ya kupinga. Kumekuwa na mabadiliko machache sana kulingana na maoni ya Vatikani. Catechism hutaarifu kwa uthabiti kwamba “yote ambayo yamesemwa kuhusu namna ya kufafanua Maandiko ni jambo la uamuzi wa Kanisa.” Hata hivyo, njia hiyo ya kimamlaka ya kushughulikia mambo haiungwi mkono hata kidogo. “Bishano la mamlaka huendelea bila kuzuiwa,” alalamika Antonio Elorza, profesa Mhispania wa mafunzo ya kisiasa. “Kanisa huchagua kujenga mnara uliozungushiwa ukuta, likiimarisha uhalali wa desturi zalo mbele ya historia kuwa usioweza kudhuriwa.” Nje ya huo “mnara uliozungushiwa ukuta,” uvutano wa kanisa na mamlaka yalo huendelea kufifia.
Kando na uchakavu wa kiroho, visababishi vya kijamii ni jambo jingine la maana linalochangia hali ya kutojali dini. Jamii yenye kuzingatia ununuaji wa vitu huandaa vitumbuizo vingi mno na fursa za tafrija—na watu wengi wa Ulaya wana tamaa na njia ya kuvifurahia. Kwa kulinganisha, kwenda kanisani huonekana kuwa njia yenye kuchosha ya kutumia asubuhi ya Jumapili. Isitoshe, ni mara chache sana ibada za kanisa huonekana kushughulikia mahitaji ya kiroho ya watu.
Haielekei kwamba dini ya kidesturi itapata mshiko wayo tena kwa kundi la Ulaya. Je, dini ni kani ya wakati uliopita—ikielekea kutoweka?
[Maelezo ya Chini]
a Catechism of the Catholic Church ilitangazwa mara ya kwanza katika 1992 na inanuiwa kuwa taarifa rasmi ya fundisho kwa ajili ya Wakatoliki ulimwenguni pote. Katika utangulizi Papa John Paul 2 aifafanua kuwa “rejezo hakika na asilia la kufundisha mafundisho ya kikatoliki.” Mara ya mwisho katekisimu ya Kikatoliki kama hiyo ya ulimwenguni pote ilipotolewa ilikuwa katika 1566.
Blurb katika ukurasa wa 6]
Farakano la raha limeshinda kitovu cha Jumuiya ya Wakristo
[Picha katika ukurasa wa 7]
Wanapokabiliwa na chaguo la mahubiri au kuota jua, watu wengi wa Ulaya bila kusita huelekea ufuoni