Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 9/8 kur. 3-4
  • Kanisa Linalobadilika Katika Ufaransa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kanisa Linalobadilika Katika Ufaransa
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mambo Si kama Yalivyokuwa
  • Je! Waaminifu ni Waaminifu Kweli?
  • Kanisa—Mabadiliko na Mvurugo
    Amkeni!—1993
  • Kwa Nini Kanisa Linapoteza Uvutano?
    Amkeni!—1996
  • Kwa Nini Ule “Wasiwasi Mwingi”?
    Amkeni!—1991
  • Wakristo Waioneje Misa?
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 9/8 kur. 3-4

Kanisa Linalobadilika Katika Ufaransa

Na mleta habari za Amkeni! katika Ufaransa

“‘Karibu watu wote hawahudhurii kanisa. Kila asubuhi mimi hutoa Misa kwa ajili ya mbayuwayu na buibui. Mwaka uliopita niliadhimisha ubatizo mmoja na maziko 26. Kuna kasoro gani? Hakuna hata ndoa moja.’ Kasisi huyo alipofika katika La Bastide [katika kusini mwa Ufaransa] kwa mara ya kwanza, ni watoto 85 waliohudhuria katekisimu. Leo, kutia kila mmoja, kuna watano. Kuna mwanachuo mmoja tu wa kidini katika dayosisi, na parokia 120 hazina makasisi.” —Kasisi, aliyenukuliwa na gazeti la kila siku la Paris, Le Figaro.

“Ni nani atakayeamua kuwarudishia Wakatoliki zile nyimbo za Kigregori, zile nyimbo nzuri-nzuri za Biblia, . . . altare zilizopambwa maua, mavazi ya kidini, uvumba, vinanda, na makasisi wa parokia kwenye mimbari? . . . Mkatoliki aliyepotea kwa muda mrefu, anayeamua kurudia zizi, atafanana na mwana mpotevu. Hata hivyo, siku hizi hatapata uchangamfu wa nyumba ya baba yake bali atapata makanisa ya kisasa yanayotangaza mahubiri yao kwa vikuza-sauti kwenye maegesho ya magari ili kwamba washiriki wa parokia wasilazimike kutoka ndani ya magari yao.” —Geneviève Dormann, akiandika kwenye Le Figaro Magazine.

TANGU mwisho wa miaka ya 1970, kumekuwa na mabadiliko makubwa sana kwa Wakatoliki wanaooa Waprotestanti. Hadi 1966 mwenzi wa ndoa Mkatoliki alipaswa kuandika kiapo kwamba yeye angelea watoto wowote watakaozaliwa kutokana na kifungo hicho kuwa Wakatoliki. Mume au mke Mprotestanti pia alipaswa kutia sahihi mapatano hayo. Siku hizi, kanisa limepoa sana. Sherehe ya arusi yaweza kufanywa kwenye kanisa la Protestanti au Katoliki kukiwa na kiongozi wa kidini wa dini yoyote kati ya hizo au zote mbili.

“Tangu Vatikani 2, Kanisa Katoliki halionekani jipya na tofauti kwa umma tu bali pia lajiona kuwa tofauti lenyewe. . . . Sasa kanisa hilo lina kiasi sana, liko karibu na dini nyinginezo, likitambua uhuru wa dhamiri, na kujitangaza lenyewe kuwa ‘mtumishi wa ulimwengu mzima.’”—gazeti la kila siku la Ufaransa, Le Monde.

Kwa miongo fulani sasa, na hasa tangu Vatikani ya 2, Kanisa Katoliki limefanya mabadiliko mengi. Waungaji mkono waaminifu na viongozi wa kidini wanaonaje mabadiliko hayo?

Mambo Si kama Yalivyokuwa

Katika miaka ya mapema ya 1960, Kardinali Feltin, askofu mkuu wa Paris, aliruhusu makasisi katika dayosisi yake waweke kando mavazi yao ya kikasisi na kuvaa nguo za kawaida zaidi, hata suti na msalaba mdogo kwenye kunjo la koti. Vazi la Katoliki ya Roma lililo kama kanzu halikuvaliwa na makasisi Wafaransa, likivaliwa na makasisi wenye kufuata sana desturi za kanisa. Karibu na wakati huo, Wakatoliki walipewa uchaguzi wa kuhudhuria Misa Jumamosi jioni badala ya Jumapili asubuhi.

Utaratibu wa Ibada za Kidini, ambao haukuwa umebadilishwa kwa karne nyingi, ulifanyiwa mabadiliko mengi. Nyimbo za kisasa ziliingizwa kwenye Misa, ijapokuwa hazikufurahiwa na watu wote. Altare ya kanisa iligeuzwa ili kwamba kasisi aangalie kundi lake wakati wa ibada. Hata hivyo, mojapo mabadiliko makubwa katika Utaratibu wa Ibada za Kidini za Katoliki lilikuwa kule kusherehekea Misa katika lugha ya nchi. Hili lilitokeza kupotea kwa Misa katika Kilatini.

François, Maryse, na Gilles ni mifano ya jinsi baadhi ya Wakatoliki wenye bidii walivyoitikia hali hiyo. François alikuwa muungaji mkono mwenye juhudi ya kutaka Misa isemwe kwa Kifaransa. Yeye alisema: “Angalau ulikuwa unaweza kuelewa kile kasisi alichokuwa akisema.” Maryse hakutaka mabadiliko kwa sababu, kama alivyosema, Misa “ilikuwa yenye kupendeza zaidi mbeleni.” Gilles alihisi kama Maryse. Yeye alisema: “Tulipobadili kutoka Kilatini hadi Kifaransa, kwangu mimi ilionekana kama kuvunjwa kwa imani.”

Miongoni mwa Wakatoliki wanaopendelea mabadiliko hayo, wengi wanahisi kwamba mambo hayajabadilika vya kutosha. Wengine wanahisi kwamba kanisa lapaswa kuwa na daraka zaidi katika mambo ya ulimwengu. Wengine wanapendelea makasisi waoe na wengine hata kuwaweka wanawake wawe makasisi.

Je! Waaminifu ni Waaminifu Kweli?

Mabadiliko hayo yameathiri mengi kuliko kawaida za dini za kanisa. Katika nchi nyingi, hudhurio la kanisa limeshuka sana. Hivyo, asilimia ya Wakatoliki Wafaransa wanaohudhuria Misa angalau mara moja kwa mwezi imepungua kutoka asilimia 45 hadi asilimia 20 katika miaka 25 iliyopita. Kutubu kunakofanywa kikawaida mbele ya kasisi sasa hakupo. Kulingana na utafiti wa karibuni, ni asilimia 14 tu ya idadi ya Wafaransa wanaoenda kutubu angalau mara moja kwa mwaka, ikilinganishwa na asilimia 51 katika 1952.

Usimamizi wa kundi umekuwa tatizo kubwa sana pia. Viongozi wa kidini wanazeeka. Hakuwekwi makasisi wengine mahali pa wale wanaojiuzulu au wanaokufa. Hivyo basi, watu wa kawaida wamekuwa wakijihusisha zaidi katika ibada.

Shida ya ukasisi inahisiwa zaidi katika sehemu za mashambani. Mamia ya parokia za mashambani katika Ufaransa hazina makasisi, na wengi kati ya wafuasi hao husafiri ama kwenye miji midogo ya karibu kwa ajili ya Misa ya Jumapili ama wanapaswa kutosheka na lile ambalo kanisa katika Ufaransa huita ADAP Les Assemblées Dominicales en L’Absence de Pretres (Makusanyiko ya Jumapili Bila Kasisi) Watu huhisije juu ya makusanyiko hayo ambayo hayawezi tena kuonwa kuwa Misa? Mtawa mmoja wa kike alisema dhahiri kuhusu hali hiyo katika Ufaransa ya kati: “Watu hawaulizi jambo lolote. Ikiwa hakuna chochote kinachofanywa Jumapili, hatimaye watatosheka na hilo.”

Vikundi vipya vya Katoliki—kwa ujumla vyenye nguvu za roho—hutoa dalili ya tumaini kwa wengi. Hata hivyo, vikundi hivyo huathiri Wakatoliki waaminifu wachache tu na havitoi utatuzi kwa ile inayoitwa shida ya kanisa.

Lakini kwa nini kuna mabadiliko hayo yote? Yalianza lini? Ni nini kilichoyaanzisha? Ili kujibu maswali hayo, twahitaji kupitia kifupi historia ya Kanisa Katoliki ya miaka zaidi ya 30 iliyopita.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki