Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/8 kur. 26-27
  • Wakristo Waioneje Misa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wakristo Waioneje Misa?
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Misa Yapatana na Maandiko?
  • Kristo Atolewa Dhabihu—Mara Ngapi?
  • Misa
    Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko
  • Kanisa Linalobadilika Katika Ufaransa
    Amkeni!—1993
  • Kwa Nini Mashahidi wa Yehova Wanaadhimisha Mlo wa Jioni wa Bwana kwa Njia Tofauti na Dini Nyingine?
    Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi Kuhusu Mashahidi wa Yehova
  • Ukweli Kuhusu Ekaristi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/8 kur. 26-27

Maoni ya Biblia

Wakristo Waioneje Misa?

WAKATOLIKI wacha-Mungu hukubaliana na Papa John Paul wa Pili, ambaye hivi majuzi, “alithibitisha kwamba kanisa linaiona kuwa dhambi kwa Mkatoliki kukosa Misa,” kulingana na The New York Times. Misa ni nini? Je, kanisa linakubaliana na Biblia juu ya misa?

Katika kitabu Things Catholics Are Asked About, padri Mkatoliki Martin J. Scott hufasili Misa ifuatavyo: “Misa ni dhabihu isiyohusisha damu ya Mwili na Damu ya Kristo. Kalvari ilikuwa dhabihu ya Kristo iliyohusisha damu. Kimsingi, Misa ni dhabihu sawa na ile ya msalaba. Hii si tamathali, wala si sitiari, wala si kutia chumvi.” Yeye pia ataarifu hivi: “Misa hudai kumshusha Mwana wa Mungu kwenye madhabahu zetu, na Kumtoa awe dhabihu kwa Mungu.”

Je, Misa Yapatana na Maandiko?

Wakatoliki wenye moyo mweupe huamini kuwa Misa hutegemea fundisho la Kimaandiko. Kwa kuthibitisha, wao hurejezea maneno ya Yesu wakati wa kile kinachoitwa kwa kawaida Chakula cha Jioni. Alipokuwa akiwapa mitume wake mkate na divai, Yesu alisema hivi alipokuwa akirejezea mkate: “Huu ni mwili wangu.” Aliporejezea divai, yeye alisema: “Hii ni damu yangu.” (Mathayo 26:26-28)a Wakatoliki huamini kwamba Yesu alipoyasema maneno haya, aligeuza kihalisi mkate na divai kuwa mwili na damu yake. Hata hivyo, New Catholic Encyclopedia (1967) hutahadharisha hivi: “Hatupaswi kutegemea sana uhalisi wa maneno ‘Huu ni mwili wangu’ au ‘Hii ni damu yangu.’. . . Kwa maana katika mafungu ya maneno kama vile ‘yale mavuno ni mwisho wa ulimwengu’ (Mt 13.39) au ‘Mimi ndimi mzabibu wa kweli’ (Yn 15.1) kile [kitenzi “kuwa”] humaanisha tu kufanana au kuwakilisha.” Hivyo, hata ensaiklopedia hii yenye mamlaka inakiri kwamba yale maneno kwenye Mathayo 26:26-28 hayathibitishi kwamba mkate na divai viligeuzwa kuwa mwili na damu halisi ya Yesu wakati wa Chakula cha Jioni.

Huenda mtu fulani akasema kwamba wakati mmoja Yesu alisema: “Mimi ndimi mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. . . . Yeyote anayekula mnofu wangu na kunywa damu yangu ana uhai wa milele.” (Yohana 6:51, 54) Baadhi ya wale waliokuwa wakimsikiliza Yesu waliyaona maneno yake kuwa halisi na wakastaajabu. (Yohana 6:60) Lakini twaweza kuuliza, Je, Yesu aligeuza mnofu wake ukawa mkate katika pindi hiyo? Kwa hakika la! Yeye alikuwa akizungumza kwa mfano. Alijifananisha na mkate kwa sababu kupitia kwa dhabihu yake angewapa wanadamu uhai. Andiko la Yohana 6:35, 40 huonyesha waziwazi kwamba kula na kunywa kungetimizwa kwa kuweka imani katika Yesu Kristo.

Kwa kuwa Misa ni desturi muhimu ya Kanisa Katoliki, huenda mtu akatarajia Maandiko yaunge mkono misa. Hayaungi mkono. Kichapo The Catholic Encyclopedia (chapa ya 1913) ilieleza kwa nini: “Chanzo hasa cha fundisho letu . . . ni mapokeo, ambayo tangu nyakati za mapema hutangaza thamani ya ombi [sihi] la Dhabihu ya Misa.” Naam, Misa ya Katoliki ya Kiroma hutegemea mapokeo, na wala si Biblia.

Hata liwe linashikiliwa kwa moyo mweupe namna gani, pokeo linalopinga Biblia halikubaliwi na Mungu. Yesu aliwashutumu viongozi wa kidini wa nyakati zake: “Nyinyi mmefanya neno la Mungu likose matokeo kwa [sababu] ya pokeo lenu.” (Mathayo 15:6) Kwa kuwa Yesu alithamini Neno la Mungu, acheni tuchunguze fundisho la Misa kwa kutegemea Maandiko Matakatifu.

Kristo Atolewa Dhabihu—Mara Ngapi?

Kanisa Katoliki hufundisha kwamba kila mara Misa inaposherehekewa, Yesu anatolewa dhabihu, ingawa linasisitiza kwamba yeye hafi kihalisi na kwamba dhabihu hiyo haihusishi damu. Je, Biblia inakubaliana na maoni haya? Angalia kwamba Waebrania 10:12, 14 husema: “[Yesu] alitoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi, kisha akaketi milele, upande wa kulia wa Mungu. Kwa toleo hilo moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wote wale wanaotakaswa.”

Hata hivyo, huenda Mkatoliki mwenye moyo mweupe akabisha hivi: ‘Je, haimpasi Yesu ajitoe dhabihu mara nyingi? Kwa kuwa sote hutenda dhambi mara nyingi.’ Jibu la Biblia limerekodiwa kwenye Waebrania 9:25, 26: “[Kristo] halazimiki kujitoa mwenyewe tena na tena. . . . Yeye ameonekana mara moja na basi, mwishoni mwa nyakati hizi, ili aondoe dhambi kwa kujidhabihu mwenyewe.” Angalia kwa uangalifu jambo hili: Kristo “halazimiki kujitoa mwenyewe tena na tena.” Kwenye Waroma 5:19, mtume Paulo aeleza sababu: “Kwa kutotii kwa mtu mmoja [Adamu] watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kwa tendo la haki la mtu mmoja [Yesu] wengi watafanywa waadilifu.” Tendo moja la kutotii la Adamu lilituletea kifo sote; na tendo moja la ukombozi la Yesu lilituwekea sote tunaodhihirisha imani katika dhabihu hiyo msingi wa kusamehewa dhambi zetu sasa na kupata uhai udumuo milele wakati ujao.

Ni tofauti gani iliyopo iwapo Yesu alitolewa dhabihu mara moja au iwapo anatolewa dhabihu mara nyingi? Hilo linahusisha uthamini kwa thamani ya dhabihu ya Yesu. Hiyo ndiyo zawadi bora kupita zote iliyowahi kutolewa—zawadi yenye thamani sana, iliyo kamilifu, na ambayo haitahitaji kurudiwa tena kamwe.

Kwa hakika dhabihu ya Yesu inastahili kukumbukwa. Lakini kuna tofauti kati ya kukumbuka tukio na kulirudia. Kwa kielelezo, mume na mke wanaosherehekea ukumbusho wao wa kila mwaka wa siku yao ya arusi wanaweza kukumbuka siku waliyofunga ndoa, bila kurudia kihalisi sherehe hiyo. Kila mwaka, Mashahidi wa Yehova huadhimisha ukumbusho wa kifo cha Yesu, wakifanya hivyo kupatana na amri ya Yesu—“kwa kunikumbuka,” si kwa kumdhabihu. (Luka 22:19) Kwa kuongezea, kwa mwaka mzima Wakristo hawa hujitahidi kukuza uhusiano mchangamfu pamoja na Yehova Mungu kupitia Yesu Kristo kwa kupatanisha maisha yao, matendo yao, na itikadi zao na Maandiko Matakatifu.

Kwa kawaida, kufanya hivyo kunamaanisha kufanya mabadiliko katika kufikiri kwao. Lakini Mashahidi hushangilia kwa kujua kwamba watabarikiwa wakiunga mkono kwa uaminifu-mshikamanifu Neno la Mungu badala ya mapokeo ya binadamu. Na wakidhihirisha imani katika damu ya Yesu iliyotolewa dhabihu, ikamwagwa mara moja tu zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, itawasafisha kabisa kutokana na dhambi.—1 Yohana 1:8, 9. 

[Maelezo ya Chini]

a Maandiko yote yaliyonukuliwa katika makala hii ni ya New Jerusalem Bible ya Katoliki.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Misa ya St. Giles (kwa sehemu)

[Hisani]

Erich Lessing/ Art Resource, NY

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki