Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 5/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kujitayarishia Mwaka wa 2000
  • Ugonjwa wa Malale Warudi
  • Kudumisha Afya Njema
  • Hatari za Kompyuta Angani
  • Njia Mpya ya Kuzaa kwa Kupasuliwa Tumbo
  • Athari Isiyotakiwa
  • Mnyama Tardigrade Mwenye Uwezo
  • Kutuliza Abiria kwa Muziki Bora
  • Daraka la Kila Mtu
  • Mwaka wa 2000—Je, Kuvurugika kwa Kompyuta Kutakuathiri?
    Amkeni!—1999
  • Ni Nini Kinachohusika ili Ziendelee Kusafiri Angani?
    Amkeni!—1999
  • Jinsi ya Kupambana na Msongamano wa Magari
    Amkeni!—2005
  • Kuongoza Ndege Kunukulindaje?
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 5/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Kujitayarishia Mwaka wa 2000

“Huenda mwaka wa 2000 ukasababisha mchafuko wa kitekinolojia, lakini shirika la Marekani la Federal Reserve Board linataka kuhakikisha kwamba chochote kitakachotukia, Wamarekani wataweza kununua vyakula katika milenia itakayofuata,” lasema The Wall Street Journal. “Benki kuu imeagiza dola bilioni 50 za ziada za fedha mpya kwa matumizi iwapo wanunuzi watatoa madai makubwa sana kwa benki zao na kwa mashine za kuhesabia fedha.” Fedha za ziada zapasa kuwa tayari kufikia mwisho wa Septemba 1999. Kompyuta za zamani zaidi zinazotumia tarakimu mbili za mwisho ili kutambulisha miaka zaweza kufasiri mwaka wa 2000 kuwa mwaka wa 1900. Wataalamu fulani wanahofu kwamba kompyuta fulani zitakosa kufaulu kwa sababu ya kasoro hii, inayojulikana kama Y2K. Tatizo hilo laweza kutatuliwa kwa kupanga upya programu jambo linalohusisha kazi kubwa sana inayochukua wakati mwingi, lakini benki nyingi na makampuni yameanza programu hiyo hivi majuzi tu. “Wasiwasi fulani wa umma juu ya uwezekano wa kukwama kwa uchumi unazidishwa na vikundi vya kidini vya kievanjeli ambavyo vinaona mwisho wa milenia kuwa ishara ya unabii wa kibiblia wenye kuonya juu ya hatari” na “mvunjiko wa jamii,” yasema ripoti hiyo.

Ugonjwa wa Malale Warudi

Mnamo 1974, nchi ya Angola iliripoti visa vitatu vya malale. Hivi karibuni, Shirika la Afya Ulimwenguni lilikadiria idadi ya visa katika nchi hiyo kuwa angalau 300,000. Labda, maelfu au hata mamilioni ya watu wamo hatarini. Malale husababishwa na kuumwa na mbung’o. Baada ya kufyonza damu ya mtu mwenye vimelea, nzi huyo huenda kwa mtu mwingine na kumwambukiza. Watu wanaoweza kuambukizwa kwa urahisi ni—wale wanaofanya kazi shambani au kufua nguo kwenye mto—na zaidi sana, watoto waliobebwa migongoni na mama zao. Mwanzoni watu walioambukizwa huumwa na kichwa, hupata homa, na kutapika. Kwa kawaida wao husinzia mchana, huku wakikosa usingizi usiku. Kimelea hiki huvamia mfumo mkuu wa neva na hatimaye ubongo, tokeo likiwa ni kichaa, kuzirai kwa muda mrefu, na kifo. Kuvunja utaratibu huu wa kuambukiza na kumtibu mgonjwa ni ghali na ni vigumu—matibabu yanagharimu takriban dola 90, ambayo ni “ghali sana katika Angola,” laripoti The Daily Telegraph la London.

Kudumisha Afya Njema

“Mazoezi ya kimwili hayahitaji kuwa makali sana ili kuboresha afya yako,” chasema kichapo The Physical Activity Guide, kilichotolewa hivi karibuni na shirika la Health Canada. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la The Toronto Star, “unaweza kuboresha afya yako na moyo wako kwa kufanya mazoezi sahili kwa vipindi vya dakika 10 na kuvijumlisha kufikia saa moja kila siku.” Ni baadhi ya mazoezi yapi yanayopendekezwa? Yanatia ndani kutembea, kupanda ngazi, kulima, na kujinyoosha. Kazi za nyumbani kama vile kufagia mikeka au kusafisha sakafu pia ni za maana, na huzidisha uwezo wa kunyumbulika. Kitabu hicho cha mwongozo chadokeza kwamba mradi wa kufikia dakika 60 kwa siku “waweza kutimizwa kwa kufanya mazoezi ya kimwili kuwa jambo la kawaida maishani mwako.” Dakt. Francine Lemire, msimamizi wa Chuo cha Matabibu wa Familia cha Kanada asema hivi: “Uchunguzi unaonyesha kwamba ikiwa hufanyi mazoezi yoyote, ungekabili hatari za kiafya zilizo sawa na kuvuta sigareti.”

Hatari za Kompyuta Angani

“Wataalamu wanaamini kwamba siku moja kifaa cha kibinafsi cha elektroni (PED) kama vile kompyuta ndogo, simu ya kuchukulika, chombo cha kuchezea CD au kompyuta ya michezo kitasababisha msiba mkubwa kwenye ndege kama ule wa bomu la gaidi,” lasema gazeti la Daily Telegraph la Sydney, Australia. “Ripoti mpya inathibitisha visa 50 ambapo ndege za kubebea abiria nusra zipatwe na msiba wenye kuletwa na matatizo ya usafiri kwa sababu ya abiria kutumia vifaa vyao vya elektroni.” Mfano uliotolewa ulihusu ndege iliyokuwa ikitua kwenye uwanja wa ndege wa Melbourne, Australia. Ndege hiyo, iliyokuwa na kifaa cha kuielekeza, kwa ghafula iliegemea upande wa kushoto, na kuruka kiubavu-ubavu takriban digrii 30. Lakini hakuna mtu aliyekuwa amegusa vifaa vya kuielekeza. Uchunguzi ulifunua kwamba abiria aliyekuwa katika safu ya tatu alikuwa akitumia kompyuta yake ndogo, licha ya onyo dhahiri kutoka kwa rubani kwamba vifaa vyote vya elektroni vizimwe. Vifaa hivyo vimesababisha ndege zipande, zishuke ghafula, zibadili mwendo, na hata zishindwe kudhibiti kanieneo wakati wa safari za angani. Ishara za elektroni kutoka kwa PED zaweza kupokewa na mifumo ya uendeshaji ndege ya moja kwa moja na zaweza kuiathiri. Abiria wanaoketi kwenye sehemu ya mbele ya ndege husababisha tatizo kubwa zaidi, kwa kuwa wanakuwa juu ya vyumba vyenye vifaa vya elektroni.

Njia Mpya ya Kuzaa kwa Kupasuliwa Tumbo

“Njia mpya ya kuzaa kwa kupasuliwa tumbo ingeweza kutokeza uzaaji wa haraka na usio na matatizo,” laripoti gazeti la habari la Ujerumani Augsburger Allgemeine. “Kwa kutumia njia iitwayo Misgav-Ladach, daktari-mpasuaji akitumia mikono huvuta tishu za mafuta, tumbo, na misuli ya mwanamke anayejifungua, badala ya kuzikata kwa kutumia kisu kidogo cha kupasulia kama ilivyo sasa.” Kwa kuwa kuna mipaka katika kupasua, kutokwa damu hakuwi tatizo baya sana, na ni tabaka tatu tu za ngozi na tishu zinazohitaji kushonwa baadaye, kwa kulinganishwa na tabaka saba kwa kutumia njia ya kawaida. Zaidi ya hilo, njia hii huchukua muda mfupi, ni vigumu kupitisha maambukizo, ni dawa chache zaidi za kutuliza maumivu zinazohitajiwa, na wanawake wanaweza kutoka hospitalini baada ya siku tatu hadi tano. Njia hii imepewa jina la hospitali moja huko Israeli iliyokuwa ya kwanza kuifanyia majaribio.

Athari Isiyotakiwa

Mara nyingi mwendo wa magari katika jiji hujaribu vikali sana saburi ya dereva. Uchunguzi uliofanywa na mwanasaikolojia kwenye Chuo Kikuu cha La Sapienza, Rome, umefunua kwamba kadiri magari yanavyoongezeka, ndivyo na matusi yanayohusisha masuala ya kidini. Kulingana na gazeti la habari la Corriere della Sera, kwenye barabara kuu za mashambani “asilimia 54 ya viapo na tabia ya kutostahi dini” yalichochewa na matatizo yaliyohusisha mwendo wa magari. Hata hivyo, katika majiji makubwa yenye magari mengi, “mwelekeo wa kulaumu watakatifu na bikira Maria” ni dhahiri zaidi. “Siku hizi katika majiji makubwa, asilimia 78 ya matusi, yanayojulikana kikawaida kuwa viapo, husababishwa na mwendo wa magari,” likasema gazeti hilo la habari. Hivi karibuni mwendo wa magari umekuwa tatizo kubwa zaidi katika Rome kwa sababu ya ujenzi wa kujitayarishia mwaka wa 2000, ambao umetangazwa kuwa mwaka wa Yubile ya Wakatoliki ambapo rehema itaonyeshwa. “Ni utanakuzi lakini ni kweli,” aeleza mratibu wa shirika la raia la Jubilee-Watcher, “kwamba katika Rome, athari ya kwanza ya Yubile hiyo yaweza kuwa kuongezeka kwa viapo, wala si rehema.”

Mnyama Tardigrade Mwenye Uwezo

Mnyama tardigrade, mwenye urefu unaopungua nusu milimeta, anadhaniwa kuwa kiumbe awezaye kustahimili hali ngumu zaidi duniani, laripoti gazeti la New Scientist. Ana miguu minane na huonekana kana kwamba amefunikwa kwa deraya. Anaweza kustahimili halijoto ya nyuzi –270 Selsiasi hadi nyuzi 151 Selsiasi, kuelekezewa miale X au kuwekwa ndani ya ombwe, na kanieneo iliyo na nguvu mara sita zaidi kuliko sehemu ya chini ya bahari yenye kina kirefu zaidi. Anaweza kupatikana katika michirizi ya paa na katikati ya mianya katika vibamba. Baadhi ya viumbe hawa wadogo wameamshwa tena baada ya kulala bwete kwa muda unaozidi miaka 100 katika mkusanyo wa kuvumwani zilizokaushwa za jumba la makumbusho. Ni nini hufanya jambo hili liwezekane? Ni kukomesha utendaji muhimu kwa muda wakati “ukubwa wa mwili unapopungua kwa asilimia 50 au zaidi, pamoja na kupoteza karibu maji yote,” asema Profesa Kunihiro Seki, wa Chuo Kikuu cha Kanagawa, Japani.

Kutuliza Abiria kwa Muziki Bora

Katika stesheni 18 za reli ya chini ya ardhi za Rio de Janeiro, sasa abiria husikiliza muziki bora uliochezwa na waimbaji kama vile Strauss, Vivaldi, Chopin, Tchaikovsky, Mozart, Bach, Bizet, Schubert, na Brahams wanapongojea treni. Kwa njia hii, wasimamizi wa treni za chini ya ardhi wanatumaini “kuwatuliza abiria wakati wa mapumziko kwenye vituo,” lasema gazeti la habari la O Globo. Orodha ya nyimbo ilipoteuliwa, “nyimbo zilizoteuliwa ni zile ambazo zingewatuliza abiria na bado zisiwape wazo la kucheza dansi kwenye jukwaa.” “Watu waliitikia vizuri zaidi ya ilivyotarajiwa,” akasema Luiz Mário Miranda, mkurugenzi wa uuzaji wa mfumo wa reli za chini ya ardhi wa Rio de Janeiro.

Daraka la Kila Mtu

“Wanadamu wameharibu zaidi ya asilimia 30 ya viumbe vya asili tangu mwaka wa 1970 wakiangamiza misitu vibaya sana, maji safi na viumbe vya baharini vinavyotegemeza uhai,” yasema makala moja katika gazeti la habari la The Guardian Weekly. Makala hiyo, ikitegemea ripoti ya karibuni ya mashirika matatu yanayohusika, kutia ndani shirika la Hazina ya Ulimwengu ya Viumbe Asili (WWF), yasema kwamba ijapokuwa kwa kawaida nchi za Magharibi ndizo zimekuwa zikitumia maliasili kwa kiwango kikubwa zaidi, sasa nchi zinazositawi “zinamaliza maliasili zao kwa kiwango chenye kuogofya.” Ofisa mmoja wa shirika la WWF asema hivi: “Tulijua ilikuwa vibaya, lakini hadi wakati tulipokusanya ripoti hii hatukuwa tumejua tatizo hili ni baya kadiri gani.” Ingawa ripoti hiyo inalaumu serikali kwa sababu ya kushindwa kukomesha zoea hilo, inataja kwamba “kila mtu ana daraka kwa sababu ya kutojali maliasili za ulimwengu,” lasema gazeti hilo la habari.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki