Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 4/8 uku. 3
  • Waumini Wako Wapi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Waumini Wako Wapi?
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Kinachopata Hudhurio la Kanisa?
  • Raha na Mapendezi Mbele ya Uchaji
  • Kwa Nini Kanisa Linapoteza Uvutano?
    Amkeni!—1996
  • Kanisa Linalobadilika Katika Ufaransa
    Amkeni!—1993
  • Watu Wanayaonaje Maadili ya Kiroho Leo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • Je, Mwisho wa Dini Uko Karibu?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 4/8 uku. 3

Waumini Wako Wapi?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA

“Hakuna jambo lenye kuharibu dini kama hali ya kutojali.”

EDMUND BURKE, KIONGOZI WA SERIKALI WA UINGEREZA WA KARNE YA 18.

KWENYE uwanda wenye upepo mkali katika eneo la kaskazini mwa Hispania upo mji mdogo wa Caleruega. Mji huo wa enzi za kati umedhibitiwa na makao ya watawa yenye kupendeza yaliyojengwa kwa mtindo wa Kiitalia. Yalijengwa miaka 700 iliyopita kwa kumheshimu Domingo de Guzmán, mwanzilishi wa utaratibu wa watawa wa kiume, ambaye alizaliwa hapa. Kwa karne saba makao hayo ya watawa yalikaa watawa wa kike ambao huchagua kuishi katika ukimya na kujitenga.

Paa la makao hayo ya watawa lavuja, na kuta za kale zimeanza kuporomoka. Lakini mama-mkuu anahangaikia kuzorota kuovu zaidi—kuporomoka kwa dini yenyewe. “Nilipoingia katika makao haya ya watawa miaka 30 iliyopita, kulikuwa na watawa wa kike 40 hapa,” yeye aeleza. “Sasa tuko 16 tu. Hakuna wachanga. Wito wa kimungu wa maisha ya kidini waonekana umekuwa jambo lililopita.”

Jambo linalotendeka Caleruega latukia kotekote katika sehemu kubwa ya Ulaya. Hakujakuwa na wimbi la hisia ya kupinga dini, bali ni kuacha kwa ukimya tu, kusikozuilika. Makanisa yajulikanayo sana ya Ulaya hutumikia watalii badala ya kuvutia “waumini” wa mahali hapo. Kanisa ambalo wakati mmoja lilikuwa imara—iwe ni la Protestanti au Katoliki—linashindwa na ubaridi. Maisha ya watu hutawalwa na mahangaiko ya kilimwengu badala ya mahangaiko ya kidini—mwelekeo ambao wasemaji wa kanisa huuita kufanywa kwa watu kuwa wa kilimwengu. Dini haionekani kuwa yenye umaana wowote tena. Je, hali ya kidini iliyo katika Ulaya yaweza kuwa ni mwonjo wa kufifia kwa dini ambako kwakaribia kukumba sehemu nyinginezo za ulimwengu?

Ni Nini Kinachopata Hudhurio la Kanisa?

Tatizo hilo si jambo jipya katika Ulaya kaskazini. Ni asilimia 5 tu ya Walutheri Waskandinavia wanaohudhuria kanisa kwa ukawaida. Katika Uingereza ni asilimia 3 tu ya wanaodai kuwa Waanglikana ambao huenda kwenye ibada za Jumapili. Lakini sasa, Wakatoliki walio kusini mwa Ulaya yaonekana wafuata kielelezo cha majirani wao wa kaskazini.

Katika Ufaransa, nchi yenye Wakatoliki wengi, ni 1 kati ya wakazi 10 aendaye kanisani mara moja kwa juma. Katika miaka 25 ambayo imepita, asilimia ya Wahispania ambao hujiona kuwa “Wakatoliki watendaji” imeshuka kutoka asilimia 83 hadi asilimia 31. Katika 1992, askofu mkuu Mhispania Ramon Torrella aliuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba “Hispania ya Kikatoliki haipo; watu huenda kwenye maandamano ya Juma Takatifu na Misa ya Krismasi—lakini si [kwenye Misa] ya kila juma.” Wakati wa ziara ya papa huko Madrid katika 1993, John Paul 2 alionya kwamba “Hispania yahitaji kurudi kwenye mizizi yayo ya Kikristo.”

Hali hiyo isiyo ya kidini imeathiri makasisi na vilevile watu wa kawaida. Idadi ya makasisi wapya waliowekwa rasmi katika Ufaransa ilishuka hadi 140 katika 1988 (chini ya nusu ya idadi hiyo kwa 1970), huku katika Hispania kukiwa na wapatao 8,000 ambao wameacha ukasisi ili kufunga ndoa. Kwa upande ule mwingine, wengine wanaoendelea kutumikia makundi yao wana shaka kuhusu ujumbe wao. Ni asilimia 24 tu ya makasisi Walutheri Wasweden wanaohisi kwamba wanaweza kuhubiri juu ya mbingu na helo “wakiwa na usadikisho,” huku robo ya makasisi Wafaransa hata hawana uhakika kuhusu ufufuo wa Yesu.

Raha na Mapendezi Mbele ya Uchaji

Ni nini kinachochukua mahali pa dini? Katika nyumba nyingi tafrija imechukua mahali pa ibada. Siku za Jumapili familia huelekea ufuoni au milimani badala ya kanisani. “Kwenda kwenye Misa huchosha,” akakata tamaa Juan, tineja Mhispania asili. Ibada za kidini haziwezi kushindana na mechi za kandanda au maonyesho ya muziki, matukio ambayo huvutia umati na kujaza stediamu.

Kushuka kwa hudhurio la kanisa si ndio uthibitisho pekee wa kufifia kwa dini. Watu wengi wa Ulaya hupendelea kuteua na kuchagua mawazo yao wenyewe ya kidini. Siku-hizi kanuni kuu ya kanisa huenda ikawa na ufanano mdogo sana na itikadi za kibinafsi za wale wanaodai kuwa wa dini hiyo. Watu wengi mno wa Ulaya—wawe Wakatoliki au Waprotestanti—hawaamini tena katika uhai baada ya kifo, huku zaidi ya asilimia 50 ya Wakatoliki Wafaransa, Waitalia, na Wahispania wakiwa hawaamini miujiza.

Mamlaka ya kanisa yaonekana haina uwezo wa kuzuia ongezeko hili la haraka la kutokubali kanuni za kanisa. Hakuna mahali pengine hili limeonekana zaidi kuliko katika kampeni ya papa dhidi ya upangaji uzazi. Katika 1990, Papa John Paul 2 alisihi wauza-madawa Wakatoliki wasiuze dawa za kupanga uzazi. Yeye alidai kwamba bidhaa hizi “hupinga sheria za asili kwa madhara ya hadhi ya mtu.” Vivyohivyo, Catechism of the Catholic Church yasisitiza kwamba “hivyo upendo wa mume na mkewe uko chini ya wajibu wenye sehemu mbili wa uaminifu na kuzaa sana.”

Licha ya maagizo haya makali, mume na mke Wakatoliki wa kawaida huchagua mwendo wao wenyewe bila kujali. Familia zenye watoto zaidi ya wawili ni chache sana katika nchi za Kikatoliki za kusini mwa Ulaya. Katika Hispania, kondomu—ambazo zilikaribia kuwa bidhaa ya magendo miongo miwili iliyopita—hutangazwa kwa ukawaida kwenye televisheni, na ni asilimia 3 tu ya wanawake Wakatoliki Wafaransa wasemao kwamba wao hutii uamuzi rasmi wa Ukatoliki juu ya upangaji uzazi.

Kwa wazi, watu wa Ulaya wanapuuza makanisa na mafundisho yayo. Askofu mkuu Mwanglikana wa Canterbury George Carey afafanua waziwazi hali iliyoko katika kanisa lake: “Tumekuwa tukivuja damu kufikia kifo,” yeye akasema, “na kwamba hili ni suala la muhimu sana ambalo ni lazima tulikabili.”

Tangu msukosuko wa Marekebisho Makubwa ya Kidini, dini ya Ulaya haijapata kuonekana dhaifu kama sasa. Kwa nini watu wengi wa Ulaya wamekuwa wasiojali dini? Ni nini ulio wakati ujao wa dini?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki