Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 2/8 kur. 23-25
  • Kuza Machipukizi Yako Mwenyewe

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuza Machipukizi Yako Mwenyewe
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matayarisho
  • Kukuza Machipukizi
  • Jinsi ya Kuandaa Machipukizi Mezani
  • Kuhifadhi Mbegu Haraka
    Amkeni!—2002
  • Lazima Mbegu Zitiwe Maji ili Zikue
    Huduma Yetu ya Ufalme—2011
  • Kupanda Mbegu za Kweli ya Ufalme
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Mbegu Inayosafiri Baharini
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 2/8 kur. 23-25

Kuza Machipukizi Yako Mwenyewe

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HAWAII

JE, NYAKATI nyingine wewe hutafuta bila mafanikio mboga zilizotoka shambani karibuni zenye lishe katika soko lenu? Usiendelee kutafuta! Kwa kipindi kifupi sana na jitihada kidogo, unaweza hasa kukuza mboga katika makao yako mwenyewe au katika chumba chako mwenyewe. Kwa njia gani? Kwa kukuza machipukizi!

Machipukizi hutunzwa kwa urahisi sana hivi kwamba hata mtoto anaweza kuyatunza. Hayahitaji nafasi kubwa, wala kulima, wala kupalilia, wala mambo mengi ya kutiwa kemikali. Na jambo bora zaidi ni kwamba unaweza kula mazao yako kwa siku nne au tano tu baada ya hayo kuanza kuchipuka! Na kuna manufaa sana.

Kwanza, machipukizi yana lishe—labda hata kuliko maharagwe au mbegu za kawaida. Kitabu The Beansprout Book, cha Gay Courter chasema hivi: “Mbegu zianzapo kuchipuka, kiwango cha vitamini zilizo nazo huanza kuongezeka. Machipukizi ya kwanza ya maharagwe-soya yalikuwa na miligramu 108 tu ya vitamini C (kwa kila gramu 100 ya mbegu) katika uchunguzi mmoja uliofanywa katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania. Lakini baada ya muda wa saa 72 kiwango cha vitamini C kiliongezeka sana kufikia miligramu 706!”

Machipukizi hupunguza gharama pia. Hata labda tayari una vifaa vyote unavyohitaji.

Matayarisho

Kwanza unahitaji kiwekeo. Gudulia kubwa la gilasi au la plastiki, mtungi, bakuli la gilasi au la kauri, au kombe lenye kina litafaa. Hata inawezekana kutumia sahani, ukieneza tabaka moja ya mbegu kati ya matabaka mawili ya shashi yenye majimaji au taulo za karatasi ili kuzizuia mbegu zisikauke. Uwe umechagua chombo gani, hakikisha kwamba ni kikubwa vya kutosha kuruhusu mbegu zichipuke na bado kuwe na nafasi ya hewa kuzizunguka. Nimepata kwamba gudulia la gilasi ni zuri zaidi kwa mbegu ndogondogo kama alfalfa. Mbegu kubwa-kubwa kama choroko, zaweza kufanya vizuri zaidi katika kombe au nyungu. Hizo huruhusu kuwe na nafasi za ziada zinazohitaji na kulinda machipukizi yasioze au kuchacha.

Pia utahitaji kitu cha kufunika kiwekeo chako. Kifuniko cha plastiki chenye matundutundu, shashi, au hata stokingi ya zamani ya nailoni itafaa. Kinachohitajika tu ni mpira wenye nguvu au kamba ya kuishikanisha kwenye mdomo wa kiwekeo. Bila shaka, kwa kuwa ni lazima mbegu zisuzwe angalau mara mbili kwa siku, pia utahitaji maji na labda chujio cha kuondoa maji kwenye kiwekeo.

Hatimaye, utahitaji mbegu. Karibu kila mbegu inayolika inaweza kuchipuzwa. (Lakini, mimi ni mwangalifu kuepuka mbegu ambazo zimetiwa kemikali.) Mbegu bora zaidi kwa mtu aliye mgeni kwa mambo haya ni kujaribu choroko au mbegu za alfalfa. Hizo ni rahisi kuchipuka nazo ni tamu sana! Sasa, ebu niwaeleze jinsi inavyofanywa.

Kukuza Machipukizi

SIKU YA KWANZA: Kwanza, suza mbegu kwa uangalifu. Kisha jaza kiwekeo chako maji mpaka yafunike mbegu au maharagwe kwa karibu sentimeta tano. Lowesha mbegu hizo kwa angalau muda wa saa nane hadi kumi. Unaweza kulowesha mbegu hizo kabla tu ya wewe kulala. Baada ya muda wa saa nane hadi kumi, mbegu hizo zitafura na ngozi kufunguka kidogo. Sasa hizo ni tayari kuchipuzwa.

SIKU YA PILI: Asubuhi, kaza kifuniko na kuondoa maji ndani ya kiwekeo. (Kwa kuwa maji hayo yana vitamini, mimi huyatia kwenye mimea yangu.) Sasa, jaza kiwekeo hicho tena na maji. Kitingishe mara chache, kipindue, ili maji ya ziada yatoke. Jaza kiwekeo hicho kwa maji tena na tena, ukisuza na kuondoa maji mara tatu. Kama umehamisha mbegu zilizoloweshwa katika sahani, polepole tia maji juu ya shashi, na kuyaondoa maji hayo kwa kuinamisha hiyo sahani. Baadaye, rudia kusuza tena ili mbegu ziwe zimesuzwa kabisa mara mbili kwa siku.

SIKU YA TATU: Kufikia sasa, unapaswa kuona mbegu zako zikichipuka. Endelea kuzisuza mara mbili kwa siku.

SIKU YA NNE: Unaweza kuanza kula machipukizi! Unaweza kuacha machipukizi ya choroko kuwa marefu sana bila hayo kupata ladha chungu. Hakikisha tu kwamba unaendelea kusuza machipukizi haya mara mbili kila siku. Pia unaweza kuanika machipukizi yako kwenye jua kwa karibu saa moja kisha uyaweke kwenye friji. Hayo majani madogo-madogo sana yatatokeza rangi maridadi sana ya kijani-kibichi—yenye kutamanisha sana kula!

Baada ya kupata mafanikio, huenda sasa ukataka kujaribu nafaka na mbegu za aina nyingine. Kila moja ina ladha tofauti kidogo na huchipuka kwa wakati tofauti kidogo. Kwa mfano, unaweza kujaribu kuchipusha mbegu za alizeti zilizotolewa maganda. Machipukizi haya hufaa zaidi kuliwa baada ya siku mbili, wakati ambapo yamechipuka tu kwa sentimeta moja. Yakikua kupita hapo, yanaweza kuwa na ladha chungu.

Jinsi ya Kuandaa Machipukizi Mezani

Machipukizi mengi yaweza kuliwa yakiwa mabichi katika saladi, sandwichi, au chakula chochote ambacho maharagwe na mbegu hutumiwa. Lakini, machipukizi ya maharagwe yaweza kuchemshwa kwa dakika 10 hadi 15 kabla ya kuliwa. Au unaweza kuyakaanga kwa kukoroga-koroga kwa mafuta kidogo sana, kitunguu-saumu, na chumvi. Hufanyiza chakula kitamu sana! Machipukizi ya ngano na rai yana sukari sana nayo hufaa kutiwa katika mikate.

Kwa hiyo kukuza machipukizi ni hobi nzuri isiyo na gharama kubwa. Unaweza kugundua kwamba kufanya hivyo kwaweza kusisimua sana na kuthawabisha. Kwani, ina mafanikio sana na matokeo ni matamu sana!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]

Japanese Stencil Designs

[Picha katika ukurasa wa 24]

SIKU YA KWANZA: Kusanya mbegu na kuzilowesha ndani ya maji kwa muda wa saa nane hadi kumi

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

SIKU YA PILI NA YA TATU: Suza mbegu sana mara mbili kwa siku

[Picha katika ukurasa wa 25]

SIKU YA NNE: Machipukizi (yakionekana hapa kutoka kando, kwenye shashi) yako tayari kuliwa!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki