Vijana Huuliza . . .
Kudhulumu—Kuna Ubaya Gani?
‘Nilikuwa nacheza tu. Hakuna ubaya. Isitoshe, Ron alistahili kudhulumiwa.’
HUENDA ikawa kwamba wewe ni mkubwa zaidi na mwenye nguvu zaidi kuliko marika wako wengi. Au labda una akili nyepesi, maneno makali, na mwenye kutaka ugomvi. Kwa hali yoyote ile, matisho, mzaha, au kuchekelea mwingine huonekana kuwa rahisi kwako.
Ingawa kuwadhulumu wengine huenda kukawafanya marafiki wako wacheke, hilo si jambo dogo. Hata watafiti fulani wanapata kwamba dhuluma huwadhuru zaidi wenye kudhulumiwa kuliko walivyopata kujua. Uchunguzi mmoja wa vijana wenye umri wa kwenda shule Marekani ulipata kwamba “asilimia 90 ya wale waliodhulumiwa walisema kwamba wao waliathirika—kuzorota kwa maksi zao, kuongezeka kwa hangaiko, kukosa marafiki au kushirikiana na wengine.” Katika Japani kijana mmoja mwenye umri wa miaka 13 “alijinyonga baada ya kuandika barua ndefu ambayo ilifafanua kindani jinsi alivyodhulumiwa kwa miaka mitatu.”a
Ni nini hufanya mtu awe mdhulumu? Na kama wewe unatenda kama mdhulumu, unaweza kubadilikaje?
Mdhulumu Ni Nini?
Biblia yasema juu ya wadhulumu walioishi kabla ya Furiko la Noa. Wao waliitwa Wanefili—neno linalomaanisha “watu wanaoangusha wengine.” Katika wakati wao wenye kuogofya, “dunia ikajaa dhuluma.”—Mwanzo 6:4, 11.
Hata hivyo, si lazima upige watu au kuwapigia ubwana ndipo uwe mdhulumu. Mtu yeyote anayetendea watu wengine—hasa walio dhaifu na wasioweza kujikinga—kwa ukatili au vibaya ni mdhulumu. (Linganisha Mhubiri 4:1.) Wadhulumu hujaribu kutisha, na kudhibiti, na kuongoza. Lakini wengi hutumia midomo, wala si ngumi. Kwa hakika, dhuluma ya kihisia-moyo ndiyo njia ya kawaida zaidi ya tendo hili baya. Basi, hiyo inaweza kutia ndani matukano, kejeli, dhihaka, na kuita mtu majina yenye kuudhi.
Lakini, nyakati nyingine kudhulumu kwaweza kuwa kwa kichinichini. Kwa mfano, fikiria kile kilichompata Lisa.b Alikua pamoja na kikundi cha marafiki wasichana. Lakini alipotimia umri wa miaka 15, mambo yalianza kubadilika. Lisa akawa mrembo sana akaanza kuvutia uangalifu sana. Yeye aeleza: “Marafiki wangu wakaanza kuniacha na kunisengenya vibaya—au hata kuniambia mambo mabaya ana kwa ana.” Wao pia walieneza uwongo juu yake, wakijaribu kumvunjia sifa. Ndiyo, kwa sababu walichochewa na wivu, wao walimdhulumu kwa njia mbaya sana yenye ukatili.
Kufanyizwa kwa Tabia ya Mdhulumu
Tabia ya uchokozi mara nyingi huhusika na mazingira ya nyumbani. “Baba yangu alikuwa mwenye kutaka ugomvi,” asema kijana aitwaye Scott, “kwa hiyo nikawa mwenye kutaka ugomvi.” Aaron pia alikuwa na maisha magumu nyumbani. Yeye akumbuka: “Nilitambua kwamba watu walijua kuhusu hali ya familia yetu—kwamba ilikuwa tofauti—na sikutaka watu wanisikitikie.” Kwa hiyo Aaron alipokuwa akicheza, ilikuwa lazima ashinde. Lakini hata kushinda hakukutosha. Ilikuwa lazima awaaibishe wapinzani wake—akirudia-rudia kufanya hivyo.
Kwa upande mwingine, Brent alilelewa na wazazi wenye kumhofu Mungu. Lakini yeye akiri hivi: “Ningechekesha watu, lakini nyakati nyingine sikujua wakati wa kuacha, na ningeumiza hisia za mtu.” Tamaa ya Brent ya kutaka kufurahia na kuvutia uangalifu ilimfanya apuuze hisia za watu wengine.—Mithali 12:18.
Vijana wengine huonekana kuathiriwa na televisheni. Vipindi vya uhalifu hukweza ‘mashujaa’ na kufanya ionekane kwamba si kiume kuwa mwenye fadhili. Vipindi vya vichekesho vimejaa kejeli. Mara nyingi ripoti za habari hukazia mapigano na maneno machafu yanayoendelea katika michezo. Marafiki wetu pia waweza kuathiri jinsi tunavyowatendea wengine. Marika wetu wakiwa wadhulumu, ni rahisi kwetu kujiunga nao ili tusinyanyaswe.
Hali yako iwe gani, kama unatumia mbinu za kudhulumu, basi si wahasiriwa wako pekee wanaopatwa na madhara.
Matokeo ya Maisha Yote
Gazeti Psychology Today laripoti: “Kudhulumu kwaweza kuanza utotoni, lakini huendelea mpaka utu-uzima.” Uchunguzi mmoja wa utafiti ulioripotiwa katika The Dallas Morning News ulipata kwamba “asilimia 65 ya wavulana waliotambuliwa kuwa wadhulumu katika kidato cha pili tayari walikuwa wameshtakiwa makosa mabaya walipofikia umri wa miaka 24.”
Ni kweli kwamba si wadhulumu wote huja kuwa wahalifu. Lakini kuwa na tabia ya kupuuza hisia za wengine kwaweza kukusababishia matatizo baadaye maishani. Tabia hiyo ikiingizwa katika ndoa, inaweza kutokeza mkazo mkali sana kwa mwenzi wako na watoto wako. Kwa kuwa waajiri hupendelea watu ambao wanajua jinsi ya kupatana na wengine, tabia hiyo yaweza kufanya usipate kazi. Pia unaweza kuyakosa mapendeleo ya wakati ujao katika kutaniko la Kikristo. “Siku moja, ningependa kustahili kutumikia nikiwa mzee,” asema Brent, “lakini baba yangu alinisaidia kuelewa kwamba watu hawatanijia na matatizo yao ikiwa watafikiri kwamba nitawakejeli.”—Tito 1:7.
Jinsi ya Kufanya Mabadiliko
Mara nyingi hatuoni makosa yetu waziwazi. Maandiko yatuonya kwamba mtu hata anaweza ‘kujipendekeza machoni pake kuwa upotovu wake hautaonekana na kuchukiwa.’ (Zaburi 36:2) Basi unaweza kujaribu kumwuliza mzazi, rafiki unayemtumaini, au Mkristo aliyekomaa akupe maoni yake. Ukweli unaweza kuumiza, lakini waweza kukusaidia uone ni mabadiliko gani unayohitaji kufanya. (Mithali 20:30) “Nafikiri kusikiliza mashauri ndiko kulinisaidia zaidi,” asema Aaron. “Wale waliokuwa wenye kufuatia haki waliniambia mahali nilipokuwa nikikosea. Halikuwa jambo ambalo ningependa kusikia wakati wote, lakini ndilo nililohitaji.”
Je, hilo lamaanisha kwamba ni lazima ufanye mabadiliko makubwa katika utu wako wote? La, yaelekea ni kurekebisha upya njia yako ya kufikiri na tabia yako. (2 Wakorintho 13:11) Kwa kielelezo, kufikia sasa labda umejidhania kuwa bora kwa sababu ya ukubwa wako, nguvu zako, au kwa akili yako nyepesi. Lakini Biblia inatutia moyo tutende “kwa hali ya akili ya kujishusha chini mkifikiria kwamba wengine ni wakubwa.” (Wafilipi 2:3) Tambua kwamba wengine—hata wawe na miili au nguvu za aina gani—wana sifa zenye kutamanika ambazo wewe huna.
Pia huenda ukahitaji kujiondolea mwelekeo wa kuwa mchokozi au mwenye kutawala wengine. Fanyia kazi ‘kuangalia, si masilahi ya kibinafsi ya mambo yako mwenyewe tu, bali pia masilahi ya kibinafsi yale ya wengine.’ (Wafilipi 2:4) Ukihitaji kusema kwa ujasiri, sema bila kuwa mwenye kutukana, au mwenye kukejeli.—Waefeso 4:31.
Ukishawishika kudhulumu, kumbuka kwamba Mungu aliwaharibu Wanefili wenye kudhulumu. (Mwanzo 6:4-7; 7:11, 12, 22) Karne kadhaa baadaye, katika siku za nabii Ezekieli, Mungu alionyesha jinsi hakufurahia wale waliokuwa na hatia ya “kuwasukuma” na “kuwapiga” wasio na hatia. (Ezekieli 34:21) Kujua kwamba Yehova anachukia udhalimu kwaweza kuwa kichocheo chenye nguvu kwa mtu kufanya mabadiliko yanayotakikana!
Inasaidia pia kutafakari juu ya kanuni za Biblia. Ile Kanuni Bora yasema: “Kwa hiyo, mambo yote mtakayo watu wawafanyie nyinyi, lazima mwafanyie wao pia hivyohivyo.” (Mathayo 7:12) Unaposhawishika kumtisha mtu, jiulize: ‘Je, mimi napenda kudhulumiwa, kutishwa, au kuaibishwa? Basi ni kwa nini nawafanyia wengine hivyo?’ Biblia yatuamuru ‘tuwe wenye fadhili sisi kwa sisi, wenye huruma kwa njia nyororo.’ (Waefeso 4:32) Yesu aliweka kielelezo chema kwa habari hii. Ingawa alikuwa bora kuliko wanadamu wengine wote, yeye alitendea kila mtu kwa fadhili, hisia-mwenzi, na kwa staha. (Mathayo 11:28-30) Jaribu kufanya hivyo ikipatana na mtu ambaye ni dhaifu kuliko wewe—au mwenye kukukasirisha sana.
Lakini, namna gani ikiwa tabia yako ya kutaka ugomvi hutokana na hisia za hasira kwa sababu ya jinsi unavyotendewa nyumbani? Katika visa fulani, hasira hiyo huenda ikawa sawa. (Linganisha Mhubiri 7:7.) Lakini, Biblia yatuambia kwamba mwanadamu mwadilifu Ayubu alionywa: “Basi ujitunze, isije hasira ikakuvuta hata ukafanya mzaha; . . . Jitunze, usiutazame uovu; kwani umeuchagua huo zaidi ya taabu.” (Ayubu 36:18, 21) Hata kama unatendewa vibaya, huna haki ya kuwatendea wengine vibaya. Njia bora yaweza kuwa kujaribu kujadili mambo hayo na wazazi wako. Kama umetendewa vibaya sana, huenda msaada wa nje ukahitajika ili kukulinda usiendelee kupatwa na madhara.
Huenda isiwe rahisi kubadilika, lakini inawezekana. Asema Brent: “Mimi husali karibu kila siku juu ya jambo hili, na Yehova amenisaidia kufanya mabadiliko mazuri.” Wewe vilevile ukifanya mabadiliko katika njia unayowatendea wengine, bila shaka utaona kwamba watu watakupenda zaidi. Kumbuka kwamba huenda watu wakaogopa wadhulumu, lakini hakuna mtu anayewapenda kikweli.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mazungumzo juu ya jinsi wenye kudhulumiwa wawezavyo kuepuka kunyanyaswa, ona “Vijana Huuliza . . . Nifanyeje Kuhusu Wadhulumu wa Shule?,” katika toleo letu la Agosti 8, 1989, (Kiingereza).
b Baadhi ya majina yamebadilishwa.
[Blabu katika ukurasa wa 19]
“Kudhulumu kwaweza kuanza utotoni, lakini huendelea mpaka utu-uzima”
[Picha katika ukurasa wa 18]
Matukano ni njia moja ya kudhulumu