Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • ijwyp makala 12
  • Nifanye Nini Ninapoonewa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nifanye Nini Ninapoonewa?
  • Vijana Huuliza
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kuonewa ni nini?
  • Kwa nini watu huwaonea wenzao?
  • Ni nani wanaoweza kuonewa kwa urahisi?
  • Unaweza kufanya nini unapoonewa?
  • Nifanye Nini Ninapoonewa Shuleni?
    Majibu Ya Maswali 10 Ambayo Vijana Huuliza
  • Kuacha Udhalimu
    Amkeni!—2003
  • Dhuluma Baadhi ya Visababishi na Matokeo
    Amkeni!—2003
  • Dhuluma Tatizo la Ulimwenguni Pote
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Vijana Huuliza
ijwyp makala 12

VIJANA HUULIZA

Nifanye Nini Ninapoonewa?

  • Kuonewa ni nini?

  • Kwa nini watu huwaonea wenzao?

  • Ni nani wanaoweza kuonewa kwa urahisi?

  • Unaweza kufanya nini unapoonewa?

Pia, soma madokezo kutoka kwa vijana wenzako na maelezo ya mwalimu kuhusu kuwaonea wengine, na usome maswali kuhusu kuwaonea wengine.

Kuonewa si jambo dogo. Uchunguzi fulani nchini Uingereza unasema inaonekana kwamba zaidi ya asilimia 40 ya ripoti katika vyombo vya habari vya kitaifa kuhusu vijana wanaojiua zilisema kwamba kuonewa kulichangia sana kuwafanya wajiue.

Kuonewa ni nini?

Kuonewa hutia ndani mengi kuliko kushambuliwa kimwili. Kunaweza pia kutia ndani mambo yafuatayo.

  • Kushambuliwa kwa maneno. “Wasichana wanaweza kutumia maneno makali,” anasema Celine mwenye umri wa miaka 20. “Siwezi kusahau majina waliyonibandika au mambo waliyosema. Walinifanya nijihisi sifai, sipendwi, na nihisi kuwa bure kabisa. Afadhali wangenipiga badala ya kuniambia maneno hayo.”

  • Kutengwa. “Wanafunzi walianza kuniepuka,” anasema Haley mwenye umri wa miaka 18. “Wangenizuia nisiketi nao wakati wa chakula cha mchana kwa kuonyesha kana kwamba meza imejaa. Kwa mwaka mzima, nililia sana na nilikula peke yangu.”

  • Kupitia Intaneti. “Kwa kuandika mambo machache tu kwenye kompyuta,” anasema Daniel mwenye umri wa miaka 14, “unaweza kumharibia mtu sifa kabisa​—au hata kuharibu maisha yake. Huenda ukafikiri ninatia chumvi, lakini hilo linaweza kutukia!” Kumwonea mtu kwa njia hii kunatia ndani kutumia simu ya mkononi kutuma picha au ujumbe mfupi wenye kudhuru.

Kwa nini watu huwaonea wenzao?

Hizi ni baadhi ya sababu za kawaida.

  • Wao wamewahi kuonewa. “Nilikuwa nimechoshwa kwa sababu wenzangu walinitendea vibaya hivi kwamba nikaanza kuwaonea wengine ili rafiki zangu wanipende,” anasema kijana anayeitwa Antonio. “Baadaye nilitafakari na kutambua kwamba lilikuwa kosa kubwa sana!”

  • Wanaiga watu wenye sifa mbaya. “Mara nyingi vijana wanaowaonea wengine . . . wanawaiga wazazi, ndugu na dada zao wakubwa, au watu wengine wa familia,” anaandika Jay McGraw katika kitabu chake Life Strategies for Dealing With Bullies.

  • Wanajifanya eti wana uhakika​—lakini wana wasiwasi. “Watoto wanaowaonea wengine huonekana kana kwamba wana ujasiri na uhakika lakini wao hufanya hivyo ili tu kuficha uchungu na hisia za kwamba hawastahili,” anaandika Barbara Coloroso katika kitabu chake The Bully, the Bullied, and the Bystander.

Ni nani wanaoweza kuonewa kwa urahisi?

  • Wanaojitenga. Vijana fulani ambao hawajui kuchangamana na wenzao hujitenga na wengine na wanaweza kuonewa kwa urahisi.

  • Vijana wanaoonwa kuwa tofauti na wenzao. Huenda baadhi ya vijana wakaonewa hasa kwa sababu ya sura, rangi, au dini au hata kwa sababu wana udhaifu fulani wa kimwili​—jambo lolote ambalo mwoneaji anaweza kutumia kuwadhihaki.

  • Vijana ambao hawajiamini. Vijana wanaowaonea wengine wanaweza kutambua mtu anayejidharau. Mara nyingi watu wa aina hiyo ndio wanaoonewa kwa urahisi kwa kuwa si rahisi kwao kujitetea.

Unaweza kufanya nini unapoonewa?

  • Usionyeshe hisia zozote. “Waoneaji hutaka kujua ikiwa wamefaulu kukuhuzunisha,” anasema msichana anayeitwa Kylie. “Usipoonyesha kwamba wamefaulu, wanachoka na kuacha.” Biblia inasema hivi: “Mwenye hekima huituliza [roho yake] mpaka mwisho.”​—Methali 29:11.

  • Usilipize kisasi. Kulipiza kutazidisha tu tatizo, hakutalitatua. Biblia inasema hivi: “Msimlipe yeyote uovu kwa uovu.”​—Waroma 12:17; Methali 24:19.

  • Usijiingize katika matatizo. Kwa kadiri unayoweza, waepuke watu au hali ambazo unaweza kuonewa.​—Methali 22:3.

  • Toa jibu lisilotazamiwa. Biblia inasema hivi: “Jibu, linapokuwa la upole, hugeuza ghadhabu.”​—Methali 15:1.

  • Tumia ucheshi. Kwa mfano, mwoneaji anaposema kwamba umenenepa kupita kiasi, lipuuze jambo hilo na useme: “Inaonekana ninapaswa kupunguza kilo kadhaa!”

  • Ondoka. “Kunyamaza kunaonyesha kwamba una nguvu kuliko yule mtu anayekusumbua,” anasema Nora mwenye umri wa miaka 19. “Kufanya hivyo kunaonyesha unaweza kujizuia​—yule anayekuonea hana uwezo huo.”

  • Jitahidi kujiamini. “Watu wanaowaonea wengine watatambua iwapo hujatulia,” anasema msichana anayeitwa Rita, “na watahakikisha kwamba wanakufanya usijiamini hata kidogo.”

  • Mwambie mtu. Kulingana na uchunguzi mmoja, zaidi ya nusu ya watu wote walioonewa kwenye mtandao hawakuripoti kilichowapata, labda kwa sababu ya kuaibika (hasa wavulana) au kwa sababu waliogopa watadhulumiwa wakiripoti. Lakini kumbuka kwamba waoneaji hufaulu zaidi jambo wanalofanya lisipofichuliwa. Kufunua kinachoendelea kunaweza kuwa hatua ya kwanza ya kukomesha hali ngumu unayokabili.

Madokezo kutoka kwa vijana wenzako

“Epuka maeneo au hali ambazo mtu anayetaka kukuonea atafanya hivyo kwa urahisi. Kumbuka pia kwamba watu wanaowaonea wengine wanapitia hali zao wenyewe ngumu. Unapotambua hilo, hutaumizwa sana na maneno yao.”​—Antonio.

“Jiamini. Usiogope kutetea unachoamini. Waoneaji wengi huacha wanapoona kwamba huwaruhusu wakutawale na huogopi.”​—Jessica.

Maelezo ya mwalimu

“Kuwaonea wengine ni tatizo kubwa. Katika shule niliyokuwa nikifundisha, mara nyingi vita vilizuka darasani​—hata kati ya watoto wa darasa la tatu! Watoto wengine hupenda kuwaonea wengine kila wakati kwa kuwa kunawafanya wawe mashuhuri na wawadhibiti wengine.

“Mara nyingi, wanaoonewa hawaripoti visa hivyo kwa sababu wanaogopa anayewaonea atawadhulumu baadaye au wenzao watawaona kuwa wasaliti. Huenda pia wakahofu kwamba hakuna hatua itakayochukuliwa. Hata hivyo, bado ningemsihi mtu yeyote anayeonewa aseme. Hilo ndilo jambo linalofaa, na huenda likazuia mtu mwingine asionewe.”​—Jenilee, aliyekuwa mwalimu nchini Marekani.

Maswali kuhusu kuwaonea wengine

Kweli au Si kweli

  1. Watu wamekuwa wakiwaonea wengine kwa maelfu ya miaka.

  2. Kuwaonea wengine hakuna madhara. Ni mzaha tu.

  3. Njia bora ya kumfanya mwoneaji aache ni kukabiliana naye.

  4. Mtu huonewa kwa sababu ya makosa aliyofanya.

  5. Watu fulani wanaoonewa huwa waoneaji baadaye.

  6. Ukiona mtu akitendewa kwa uonevu, ni vizuri kupuuza jambo hilo.

  7. Mara nyingi waoneaji wana wasiwasi ingawa wanazungumza kwa majivuno.

  8. Waoneaji wanaweza kubadilika.

MAJIBU

  1. Kweli. Kwa mfano, Biblia inawataja Wanefili​—watu ambao jina lao linamaanisha “Wale Wanaowaangusha Wengine.”​—Mwanzo 6:4.

  2. Si kweli. Mtu anaweza kufa kwa sababu ya kuonewa. Kwa kusikitisha, wengine wamejiua kwa sababu ya kuonewa kwa kuendelea.

  3. Si kweli. Mara nyingi, waoneaji huwa na nguvu kuliko wale wanaowaonea, kwa hiyo ni jambo la bure kulipiza kisasi.

  4. Si kweli. Hakuna mtu anayestahili kuonewa! Mwoneaji anapaswa kulaumiwa kwa mambo anayofanya.

  5. Kweli. Kwa kusikitisha, watu fulani huwatendea wengine kwa njia isiyofaa kwa sababu wao pia wametendewa hivyo.

  6. Si kweli. Ukiona mtu akionewa na usiseme lolote, huenda ukawa sehemu ya tatizo badala ya kusaidia kulitatua.

  7. Kweli. Ingawa waoneaji fulani wana ujasiri, wengi wao wana wasiwasi mwingi nao huwashushia wengine heshima ili kuficha hali hiyo.

  8. Kweli. Wanapopata msaada, waoneaji wanaweza kubadili njia yao ya kufikiri​—na tabia yao.​—Waefeso 4:​23, 24.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki