Karne Moja na Nusu ya Reli za Chini ya Ardhi
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HUNGARIA
WACHIMBA-HANDAKI walitazama kwa butaa kile walichogundua. Ulikuwa mwaka wa 1912. Chini kabisa ya barabara za New York City, walipokuwa wakichimba nyongeza ya reli ya chini ya ardhi, wao walitokea katika chumba kikubwa kilichokuwa kimejificha. Chumba hicho kilikuwa kimepambwa sana—kama jumba la mfalme! Kwenye kuta zayo palikuwa na vioo, vinara vya taa, na michoro. Mapambo ya mbao, yakiwa yanaporomoka kwa sababu ya umri, bado yalikuwa yangali yamepamba kuta. Katikati ya chumba kulikuwa na pambo la bomba la kurusha maji, likiwa liliacha zamani kurusha maji.
Chumba hicho kiliingia katika handaki. Kwa mshangao wa wafanyakazi hao, palikuwa na gari-moshi lililopambwa vizuri sana la kubeba watu 22 likiwa kwenye reli. Je, kulikuwa na reli nyingine chini ya New York kabla ya hii waliyokuwa wakichimba? Ni nani aliyejenga mahali hapa?
Mahandaki na Reli za Chini ya Ardhi
Vipitio vya chini ya ardhi vimekuwa vikitumiwa katika uchimbuzi, kupeleka maji, na katika mambo ya kijeshi kwa maelfu ya miaka. Hata hivyo, usafiri wenye kutumia gari kwa abiria ulitokea hivi majuzi kabisa. Mapema katika miaka ya 1800, njiaza London, Uingereza, zilikuwa zimesongamana sana kwa kila aina ya gari la wakati huo, bila kutaja watembeaji. Maelfu ya watu walivuka Mto Thames kila siku, ama kwa feri ama kupitia Daraja la London. Nyakati nyingine, mwendo ulikuwa wa polepole sana hivi kwamba wafanyabiashara walibaki tu kutazama wakiwa hoi wakati bidhaa walizokuwa wakijaribu kupeleka sokoni zilipokuwa zikinyauka kwenye jua.
Marc Isambard Brunel, mhandisi mmoja Mfaransa aishiye Uingereza alikuwa na wazo ambalo hatimaye lingesaidia kupunguza baadhi ya matatizo ya usafiri ya London. Pindi moja Brunel alikuwa ametazama shipworm aking’ang’ana kuchimba kipande cha mbao ngumu ya oki. Aliona kwamba ni kichwa pekee cha moluska huyo mdogo ndicho kilikuwa kimekingwa na koa. Huyo shipworm alitumia kingo za koa hiyo zilizo kama msumeno ili kuchimba mbao. Alipoendelea, aliacha nyuma tabaka lenye uanana lenye kulinda la chokaa. Kwa kutumia kanuni hii, Brunel alipata haki ya kutengeneza ngao kubwa ya chuma-udongo ya kuchimba, ambayo ingesukumwa mbele na jeki. Wafanyakazi waondoapo udongo kutoka kwa ngao hiyo, ngao hiyo ingezuia mporomoko. Ngao hiyo ilipoendelea kuchimba, wafanyakazi wengine walikuwa wakiweka matofali kwenye kuta za ndani za handaki mpya ili kuliimarisha.
Akitumia ngao yake, Brunel alimaliza handaki la kwanza ulimwenguni lililopita chini ya maji katika udongo mwanana, chini ya Thames, katika 1843. Kwa kufanya hivyo, alionyesha uwezekano wa kuchimba handaki na kufungua njia ya maendeleo ya reli za chini ya ardhi za kisasa. Katika 1863, mfumo wa kwanza wa reli ya chini ya ardhi ulifunguliwa kati ya stesheni kubwa za London, na katika 1865, handaki la Brunel lilinunuliwa ili kupanua mfumo huo wa reli. Handaki hilo lingali sehemu ya Reli ya Chini ya Ardhi ya London.
Hofu—za Kuwaziwa na za Halali
Sikuzote usafiri wa chini ya ardhi umekuwa na wapinzani. Katika miaka ya 1800 watu wengi, wakiamini kwamba helo yenye moto iko mahali fulani ndani ya dunia, waliogopa kwenda chini ya ardhi. Kwa kuongezea, watu wengi walihusianisha mahandaki hayo yenye giza na unyevu pamoja na hewa chafu yenye kuambukiza.
Kwa upande mwingine wa suala hilo, wapangaji wa miji walikuwa wametaka sana kuondoa msongamano kwenye barabara za mjini. Reli ya chini ya ardhi ikawa mjadala motomoto wa kisiasa. Kulikuwa na sababu nzuri ya kuhangaikia hewa safi katika reli ya chini ya ardhi. Njia kadhaa za kupuliza hewa zilijaribiwa, nyingine zikaambulia patupu. Baadhi ya njia za kupuliza hewa zilitumia hewa iliyofanyizwa na magari-moshi yenye kwenda; nyingine zilikuwa na mashimo yaliyosimama wima yenye kufunikwa na wavu nje barabarani baada ya kila umbali fulani, vipepeo vyenye nguvu, au mifumo yenye kutumia njia hizo zote. Ili kushinda mawazo ya kuhofu mahandaki yenye giza, stesheni ziliwekewa taa za gesi. Chini ya hali hiyo, reli ya chini ya ardhi ya New York iliyokuwa imesahaulika ambayo wafanyakazi waligundua ghafula katika 1912, ilifanyizwa.
Reli ya Chini ya Ardhi ya Kwanza ya New York
Ng’ambo ya Atlantiki kutoka London, mvumbuzi mwingine mwenye kipawa, Alfred Ely Beach, alikuwa akifikiria juu ya hali mbaya sana ya msongamano katika New York. Akiwa mchapishaji wa jarida Scientific American, Beach alikuwa mteteaji wa masuluhisho ya kisasa kwa matatizo ya zamani, kama vile barabara za jiji zilizosongamana sana. Katika 1849 yeye alipendekeza mpango tofauti kabisa: “Handaki la Broadway,” mojawapo ya barabara zenye kusongamana zaidi, “lenye vijia na ngazi katika kila pembe. Njia hiyo ya chini ya ardhi inapaswa kuwekewa reli mbili, kukiwa na njia ya watembeaji kwa kila upande.”
Katika miongo miwili iliyofuata, wasitawishaji wengine wa usafiri pia walitoa mapendekezo ya kuharakisha usafiri katika New York. Hayo yote yalikataliwa hatimaye. Mwanasiasa mwenye uwezo aliye mfisadi, Boss Tweed, hakutaka kampuni za usafirishaji zipate upinzani wowote, hizo zilikuwa chanzo kikubwa cha mapato yake yasiyo halali. Lakini Bw. Beach aliye mwerevu, ambaye hakupata kuacha wazo lake, akamshinda Boss mwenye majivuno.
Beach alipata kibali cha kisheria cha kujenga mahandaki mawili yenye kukabiliana, madogo sana kuweza kusafirisha abiria, chini ya Broadway. Mahandaki hayo yalikuwa yatumike “kupeleka barua, vifurushi na bidhaa” kwa posta kuu. Kisha akaomba afanye rekebisho ambalo lingemruhusu kujenga handaki moja kubwa, eti kuokoa gharama. Kwa njia fulani ujanja wake haukutambuliwa, na rekebisho hilo likakubaliwa. Mara moja Beach akaanza kazi lakini kichini-chini. Alianza kuchimba kwenye chumba cha chini cha duka fulani la nguo, akiondoa udongo wakati wa usiku kwa mabogi yenye magurudumu yaliyofunikwa ili yasipige kelele. Kwa usiku 58 tu, handaki hilo la meta 95 lilimalizika.
“Kamba ya Hewa”
Beach alifahamu sana uchafuzi mkubwa ulio katika mahandaki ya London yaliyosababishwa na kutumia magari-moshi ya makaa-mawe. Yeye aliendesha gari lake kwa “kamba ya hewa”—msongo kutoka kwa kipepeo kikubwa kilichojengwa juu kwenye mwisho mmoja wa handaki. Hewa hiyo ilisukuma gari kwa upole kwa mwendo wa kilometa 10 kwa saa, ingawa gari hilo lingeenda mara kumi zaidi ya mwendo huo. Gari hilo lilipofika mwisho mwingine wa handaki, kipepeo hicho kilibadilishwa kivute gari nyuma! Ili kufanya watu wasisite-site kuingia chini ya ardhi, Beach alihakikisha kwamba chumba kikubwa cha kungojea kilikuwa kimetiwa nuru nyingi ya kutosha kwa taa za zircon, ambazo zilikuwa miongoni mwa taa zenye kuwaka zaidi zilizopatikana wakati huo. Naye alikipamba kwa umadaha kwa viti, sanamu, madirisha bandia yenye pazia, na hata piano kubwa pamoja na tangi la samaki aina ya dhahabumikia! Reli hiyo ndogo ilifunguliwa kwa umma usiokuwa na habari Februari 1870 na ikawa na mafanikio makubwa sana mara moja. Kwa mwaka mmoja, watu 400,000 walizuru reli hiyo ya chini ya ardhi.
Boss Tweed alighadhabika! Hila za kisiasa zikatokea, na Tweed akamshawishi gavana aidhinishe mpango wenye kupinga huo wa kuwa na gari-moshi la juu ya ardhi lenye kugharimu mara 16 kuliko lile la chini ya ardhi lililopendekezwa na Beach. Muda mfupi baadaye, Tweed alishtakiwa, akafungwa maisha. Lakini hofu ya ghafula iliyoshika soko la hisa katika 1873 iliondosha akili za waweka-rasilimali na maofisa kwenye reli ya chini ya ardhi, na hatimaye Beach akafunga hilo handaki. Kwa hiyo likasahaulika mpaka lilipogunduliwa bila matarajio katika 1912, zaidi ya miaka saba baada ya kufunguliwa kwa reli ya chini ya ardhi ya sasa ya New York katika 1904. Sehemu ya handaki la awali la Beach baadaye ikawa sehemu ya Stesheni ya City Hall ya sasa, jijini Manhattan.
Reli ya Chini ya Ardhi ya Mileani
Muda uzidio karne moja iliyopita, kulikuwa na matazamio mengi katika Hungaria. Katika 1896, Hungaria ilipaswa kusherehekea miaka 1,000 tangu ianzishwe. Kufikia mwishoni mwa karne ya 19, jiji kuu la nchi hiyo, Budapest, lingekuwa miongoni mwa majiji makubwa zaidi katika Ulaya. Tayari barabara zalo zilikuwa zimesongamana. Reli ya juu ya ardhi yenye kutumia umeme ilipendekezwa kwa ajili ya sherehe hizo za mileani, ili kupunguza mzigo. Lakini wazo hilo halikuwa lile wenye mamlaka wa manispaa walikuwa wakifikiria, na pendekezo hilo likakataliwa. Kwa wakati uo huo Reli ya Chini ya Ardhi ya London ilikuwa imechochea kufikiri kwa wapangaji wa usafiri katika nchi nyinginezo. Mstadi mmoja katika Hungaria, Bw. Mór Balázs, alipendekeza reli ya chini ya ardhi ya umeme. Pendekezo hilo lilikubaliwa, na ujenzi ukaanza Agosti 1894.
Handaki hilo lilijengwa kwa mtindo wa kuchimba na kufunika—barabara iliyokuwapo ilichimbwa, na reli zikatandazwa chini ya ardhi. Kisha paa bapa ilifunika handaki hilo, na ile barabara kurudishwa. Mei 2, 1896, reli ya chini ya ardhi yenye umbali wa kilometa 3.7 ilianzishwa rasmi. Safari katika magari yayo yenye kuendeshwa na umeme ilikuwa bora zaidi kuliko ile Reli ya Chini ya Ardhi ya London yenye kutoa sulfa iliyovumiliwa na wasafiri. Siku chache baada ya kufunguliwa, Mfalme Francis Joseph 1, alizuru mfumo huo mpya na kukubali uitwe kwa jina lake. Hata hivyo, katika nyakati zilizofuata zenye msukosuko wa kisiasa, reli hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Reli ya Chini ya Ardhi ya Mileani. Ilikuwa reli ya chini ya ardhi ya kwanza katika bara la Ulaya. Upesi, nyinginezo zikafuata. Katika 1900 Reli ya Métro ya Paris ikaanza kufanya kazi, na Berlin ikaanza kutoa utumishi wa reli ya chini ya ardhi katika 1902.
Reli ya Chini ya Ardhi Baada ya Miaka 100
Katika sherehe za miaka 1,100 tangu kuanzishwa kwa Hungaria katika 1996, reli ya chini ya ardhi ilipambwa ikawa tena maridadi na yenye kuvutia kama ilivyokuwa zamani. Kuta za stesheni zimepambwa kwa vigae vidogo-vidogo vyeupe na kona zenye rangi nyekundu. Majina ya stesheni yaonekana waziwazi—yakiwa yamewekwa kwenye fremu ukutani. Zile nguzo za chuma zimejengwa upya na kupakwa rangi ya kijani kibichi ili kutokeza mandhari ya karne iliyopita. Stesheni kuu ya Budapest yatia ndani jumba la ukumbusho la reli, ambako unaweza kuona mojawapo magari ya awali ya chini ya ardhi—lenye umri unaozidi miaka 100! Vitu vya maonyesho vinavyohusika na ujenzi wa Reli ya Chini ya Ardhi ya Mileani na vilevile vya Budapest Metro ambayo ni ya kisasa zaidi pia vimo katika wonyesho.
Wakati wa kuzuru jumba hilo la ukumbusho, Mashahidi wa Yehova katika Hungaria hukumbuka wazi kwamba muda usio mrefu sana hiyo reli ya chini ya ardhi ilikuwa na kazi nyingine tofauti kwa Wakristo wanaoishi huko. Katika muda wote ambao kazi yao ilikuwa imepigwa marufuku katika Hungaria, Mashahidi walitumia reli hiyo mashuhuri kwa busara ili kuzungumza na wengine kuhusu Ufalme wa Mungu. Tangu 1989, Mashahidi wamefurahia uhuru wa kuhubiri katika Hungaria. Lakini bado unaweza kuwapata katika Reli ya Chini ya Ardhi ya Mileani, wakitangaza itikadi yao kwamba Mileani inayofafanuliwa katika Biblia—ule utawala wa miaka 1,000 wa Kristo—itafika karibuni.
Urithi wa Reli za Chini ya Ardhi za Kwanza
Leo, reli za chini ya ardhi husafirisha abiria katika majiji makubwa ulimwenguni. Katika nchi fulani matatizo ya zamani ya kelele na uchafuzi wa hewa yameongezwa na uchoraji ovyo-ovyo kwenye kuta na uhalifu. Lakini reli nyingi za chini ya ardhi zinaonyesha umadaha, utulivu, na mapendezi mazuri ya wabuni wa awali wa reli za chini ya ardhi. Tamaa ya kupanua na kuboresha usafiri wa umma inazidi kuwa na nguvu. Reli za chini ya ardhi zilimalizika hivi majuzi au zinaendelea kujengwa katika majiji kama Bangkok, Medellín, Seoul, Shanghai, Taipei, na Warsaw. Je, wabuni wa kwanza wa reli za chini ya ardhi waweza kushangaa kwa hayo yote? Labda sivyo—mweneo huo mkubwa ndio waliotabiri karne moja na nusu iliyopita.
[Picha katika ukurasa wa 23]
1.Stesheni iliyorekebishwa katika Jumba la Ukumbusho la Reli ya Chini ya Ardhi ya Mileani ya Budapest
2-4. Mojawapo ya magari ya umeme ya awali ya Reli ya Chini ya Ardhi ya Mileani ya 1896