Majumba ya Kifalme ya Moscow Yenye Kumetameta Chini ya Ardhi
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA URUSI
HAIKUWA vigumu kukisia ni wapi ilipokuwa njia ya usafiri wa chini ya ardhi, au Metro. Tiririko lisilokoma la watu lilimiminika ndani ya mwingilio mmoja wenye kuongoza chini ya ardhi. Juu ya mwingilio huo ilikuwako herufi M, iking’aa kwa nuru nyekundu nyangavu ya neoni. Milango ya njia ya mwingilio ilinifungukia. Humo ndani nikashangaa kuona watu wakishuka kasi na kupotea kama kwamba ndani ya shimo lisilo na kikomo. Kwanza nilisita. Halafu, nilipoweza kujidhibiti, nikafuata.
Kwa mara ya kwanza maishani mwangu, nilikuwa katika njia ya usafiri wa chini ya ardhi. Tena si njia yoyote tu ya usafiri wa chini ya ardhi—ilikuwa ile Metro ya Moscow! Lakini katika ulimwengu ambamo mwanadamu aweza kusafiri angani, kuipasua atomi, na hata kufanya upasuaji mgumu wa ubongo, kuna jambo gani maalumu katika njia ya usafiri wa chini ya ardhi?
Kwanza, nilikuwa nimeambiwa kwamba Metro ya Moscow labda ndiyo njia ya usafiri wa chini ya ardhi iliyo maridadi zaidi ulimwenguni. Kama vile mithali ya Kirusi isemavyo, “ni afadhali kuona kitu fulani mara moja kwa macho yako mwenyewe kuliko kusikia habari zacho mara mia moja.”[1] Nilipohudhuria mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika Moscow Julai uliopita, nilikuwa na hamu nyingi ya kusafiri nikiwa katika ile Metro.
Jinsi Ilivyotokea
Katika 1902 mwanasayansi na mhandisi Mrusi jina lake Bolinsky alidokeza juu ya kujenga mfumo wa usafiri katika uso wa ardhi ambao ungeuambaa ukuta wa Kremlin na kuzunguka kitovu cha jiji.[3] Lakini baraza la jiji la Moscow lilikataa mipango ya kusitawisha mfumo huo wakati huo. Miaka kumi baadaye baraza lilianza kufikiria wazo hilo kwa uzito—ungekuwa ndio wa kwanza wa aina yao katika Urusi—lakini kutokea ghafula kwa Vita ya Ulimwengu 1 katika 1914 kukakawiza usitawi zaidi. Wazo hilo halikufufuliwa mpaka 1931. Huo ndio wakati Halmashauri Kuu ya Chama cha Ukomunisti cha Muungano wa Sovieti ilipotangaza rasmi kwamba reli ya kwanza ya kupitia chini ya ardhi ingejengwa katika Moscow. Hivyo Urusi ikawa nchi ya 11, na Moscow jiji la 17, kuanza mradi mkubwa hivyo wa ujenzi.[4]
Njia ya Metro ya Usafiri wa Chini ya Ardhi katika Moscow ilifungua reli yao ya kwanza, yenye karibu mwendo wa kilometa 11, saa moja ya asubuhi siku ya Mei 15, 1935, miaka mitatu tu baada ya ujenzi kuanza.[5] Magari-moshi manne yalihudumia vituo 13, yakaweza kubeba abiria karibu 200,000 kwa siku.[6] Wakaaji wa Moscow na wageni wenye kuzuru walivutiwa. Lilikuwa jambo jipya sana, jambo lisilo la kawaida sana! Nyakati za jioni watu walingoja wakiwa wamepanga mstari ili wawe miongoni mwa baadhi ya walio abiria wayo wa kwanza. Ilikuwa shani. Na ingali hivyo.
Tangu 1935 mfumo huo umepanuliwa kuwa reli tisa ziendazo jumla ya kilometa 200 na zenye vituo 149.[7] Karibu namna nyingine zote za usafiri wa umma katika Moscow, kutia na uwanja wa ndege na mapito ya mito, wahusiana kwa njia fulani na usafiri katika ile Metro.[8] Kwa kweli, wakaaji wa Moscow hawangeweza kuwazia kuishi bila ile Metro. Sababu yaeleweka, kwa kuwa kila siku mfumo huo hubeba wastani wa abiria milioni tisa, ambao ni wengi kuliko wakaaji wa Finland kwa karibu mara mbili. Kwa kulinganisha, njia za usafiri wa chini ya ardhi za London na New York City zikiwa pamoja hubeba karibu nusu tu ya idadi hiyo.[9]
Kutazama kwa Ukaribu Zaidi
Je! wewe una hamu ya kutaka kuona ni nini kilicho chini ya ardhi katika ghorofa ya 20 kule chini? Mtambo wa orofani watupeleka chini haraka. Huo ni mmoja tu wa mitambo ya orofani ipatayo 500 katika mfumo mzima, ambao kama ungeunganishwa ncha na ncha ungefika kilometa zaidi ya 50.[10] Nao ni msisimko ulioje, kuteremka chini katika mwinamo wa digrii 30 kwa mwendo upatao meta moja kwa sekunde—karibu mara mbili za mwendo wa mitambo ya orofani iliyo katika nchi nyingine nyingi![11]
Tumeingia kituo cha Mayakovskaya. Namna kilivyojengwa yatufanya tuhisi kana kwamba tumo katika jumba la kifalme kuliko kuwa katika kituo cha usafiri wa chini ya ardhi. Mimi naona vigumu kuwazia kwamba kweli tuko chini ya ardhi. Ni mara haba ambapo nimeona ujenzi mzuri hivyo katika ardhi, sembuse chini ya ardhi. Si ajabu kwamba maonyesho ya kimataifa ya ujenzi yaliyofanywa kati ya 1937 na 1939 yalivitunuka tuzo za heshima vituo vitano vya Metro ya Moscow, kutia na hiki.[12] Bila shaka, si vituo vyote 149 vilivyo na sura ya majumba ya kifalme kama kituo cha Mayakovskaya; vilivyo vingi kati ya vile vipya zaidi ni vya kiasi zaidi—lakini bado ni vya kuvutia—kila kimoja kikiwa bila kifani katika mtindo na muundo.[13]
Karibu vituo vyote vinaonyesha jambo fulani juu ya historia ya Urusi. Marimari, serami, na graniti zilichukuliwa sehemu tofauti 20 za Urusi ili zitumiwe kwa mapambo.[14] Hivyo, kiongozi kimoja cha picha chasema hivi: “Bara zima lilijitupa kazini kusaidia kujenga ile Metro ya Moscow.”[15] Graniti ilitumiwa sana kwa mapambo ya sakafu kwa sababu ya udumifu wayo. Hilo ni jambo la maana kwa kufikiria umati wa watu wasongamanao kila siku katika vituo hivyo.
Tunapofurahia mazuri ya hili jumba la kifalme la chini ya ardhi, twayaona magari-moshi yakipita huku na huku kwa mwendo wa kasi. Zapata sekunde 90 hivi baada ya moja kuondoka katika kile kituo, taa za lile lifuatalo zaweza kuonwa tayari zikikaribia. Je! sikuzote magari-moshi hukimbiakimbia mara nyingi hivi? Hayo hufanya hivyo saa zile zenye pirikapirika nyingi za watu. Ama sivyo huwa yakiachana kwa dakika tatu hadi tano.
Hata hatujastarehe kabisa katika viti vyetu vyenye starehe katika gari-moshi kabla hatujajionea wenyewe jinsi lile gari-moshi huchapusha mwendo kufikia kwenda kasi sana. Lachapa mwendo kupitia mrija-handaki wenye kipenyo cha meta sita tu, nyakati fulani kwa mwendo unaokaribia kilometa 100 kwa saa. Naam, mtu angeweza kusafiri mwendo wote wa Metro kwa muda wa karibu saa sita![16] Wakaaji wa Moscow huipendelea Metro si kwa sababu tu hiyo ndiyo njia ya kasi zaidi ya usafiri bali kwa sababu ni ya gharama ndogo zaidi na ya starehe.[17] Julai uliopita, wakati wa mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova, usafiri wa kwenda popote katika ile Metro uligharimu rubo kumi, ambazo wakati huo zilikuwa sawa na senti moja ya Marekani.
Vipindi vipitavyo kati ya magari-moshi ni vifupi sana hivi kwamba huenda ukashangaa huwezekanaje magari-moshi hayo kusafiri kwa mwendo wa juu jinsi hiyo. Elezo ni sahili. Mfumo wa kujidhibiti wenyewe mwendoni umefanyizwa kuendesha mambo moja-kwa-moja ili kuzuia aksidenti. Mfumo huu huhakikisha kwamba umbali ulio kati ya magari-moshi si mfupi kamwe kuliko ambao ungekuwa wa lazima ili kulisimamisha gari-moshi likiwa katika mwendo huo. Yaani, gari-moshi linalosafiri kilometa 90 kwa saa ambalo lakaribia gari-moshi la mbele kwa kuupita unaohitajiwa ili kulisimamisha huanza kujifunga breki moja-kwa-moja. Kuongezea hilo, dreva aliye katika gari-moshi tangulizi huonywa na king’ora. Bila shaka, mfumo huu huongezea sana usalama wa kusafiri.[18] Je! hiyo ingeweza kuwa ndiyo sababu wakaaji wa Moscow wanaosafiri kwa Metro huonekana wakiwa watulivu na wenye kustareheka sana? Walio wengi kati yao huketi kwa unyamavu wakisoma, wakiwa na uhakika wa wazi kwamba watafika salama waendako.
Taa na Hewa
Mapema kila asubuhi, wakati maelfu ya mota za nguvu za umeme zianzapo kuvuma na mamia ya maelfu ya taa kuanza kumweka, mamilioni ya watu huanza kumiminika kwa mikururo wakishika njia kupita katika majumba ya kifalme ya chini ya ardhi yaliyosongamana watu ambako mabehewa yapatayo 3,200 ya usafiri wa chini ya ardhi yatafungua na kufunga milango yayo zamu kwa zamu siku kutwa. Yote haya huwezeshwa na nguvu nyingi ajabu za umeme.[19]
Utendaji huu hutokeza joto jingi sana, ambalo sehemu yalo hufyonzwa na ardhi yenye kuzunguka. Lakini namna gani kuhusu joto la ziada ambalo lingeweza kusababisha mahandaki na vituo viwe na joto jingi mno? Basi, kama istahilivyo majumba ya kifalme, kila kituo huhudumiwa na mfumo wa hewa ambao huingiza hewa upya mara nne kwa saa. Hewa safi hupatikana nyakati zote, bila kujali ile Metro imesongamana kadiri gani. Kwa kweli, mfumo wa kuingiza hewa katika ile Metro ya Moscow huonwa na wengi kuwa ndio bora zaidi ulimwenguni.[20]
Hata hivyo, katika majira ya baridi, joto hili huwa na mafaa. Hakuna mfumo wa kupasha joto unaohitajika, isipokuwa kwa ajili ya majengo na njia za mwingilio zilizo juu ardhini. Kwa kuwa yale magari-moshi, ule umati wa watu, na ardhi yenyewe, huwa zimekwisha kuweka akiba ya joto wakati wa majira ya masika na ya kiangazi, hizo hutokeza kwa wingi joto la kutosha kuendeleza majumba ya kifalme ya chini ya ardhi yakiwa na ujoto wa kustarehesha.
Sifa Kutoka Pande Zote
Kama vile iwezavyo kutarajiwa, kile kijitabu cha mwongozo wa Metro chenye vielezi chaisifu sana: “Metro ya Moscow huhesabiwa kwa haki kuwa kimojapo vituo vya ulimwengu vyenye kuvutia zaidi, chenye vituo vilivyo kama jumba la kifalme vikiwa na ufungamano wa mapito, waya, mitaimbo na nyugwe nyingi ambazo ni changamano la kuvutia sana la jitihada ya usanii na uhandisi wa akili murua kabisa. Majengo hayo si vituo vya hivihivi tu, bali yamesaniiwa kwa upambo na uvutio usio na kifani uliotiwa madoido ya kupendeza yakiwa na marimari, graniti, chuma-cha-pua na vigae maridadi, vilivyorembwa na taa zilizoundwa kwa ubuni wa namna yake, kwa michongo, batobato, mifinyango, paneli, vioo vya madoa na kwa marembo ya kufinyiliwa. Wachoraji ramani za ujenzi na wasanii walio hodari zaidi nchini,” kutia na wachonga-maumbo, “walichangia kutokezwa kwa ule mpangilio na upambaji.”[21]
Sasa, baada ya kuzuru Moscow na kuiona Metro mimi mwenyewe, ningekubaliana na hilo. Wengi wa wajumbe wenzangu kwenye ule mkusanyiko walivutiwa pia. Mjerumani mmoja aliniambia hivi: “Nilihisi kama kwamba nilikuwa nimeingia katika jumba la matumbuizo lenye taa za kuvutia zenye vitawi vya taa nyingi. Nilifurahi upeo.” [22] Mgeni mmoja mwenye kuzuru kutoka Marekani alivutiwa na utendaji usiochelewa, usafi, na uendeshaji mzuri wa ile Metro.[23] Na mjumbe mmoja wa mkusanyiko aliyetoka Siberia ya mbali alishangazwa sana na ukubwa wa ajabu na mweneo wa yale majengo ya chini ya ardhi.[24]
Ukipata kuwa katika Moscow wakati fulani, ningekuhimiza uzuru majumba haya ya kifalme yenye kumetameta chini ya ardhi. Kumbuka: “Ni afadhali kuona kitu fulani mara moja kwa macho yako mwenyewe kuliko kusikia habari zacho mara mia moja.”
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Sovfoto/Eastfoto
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Vituo vichache vya Moscow vyenye uzuri wa kuvutia vya usafiri wa chini ya ardhi
[Hisani]
Sifa kwa picha (kufuata mwendo wa saa kutoka juu kushoto): Laski/Sipa Press; Sovfoto/Eastfoto; Sovfoto/Eastfoto; Laski/Sipa Press; Laski/Sipa Press; Sovfoto/Eastfoto