Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 12/22 kur. 13-18
  • Moscow—Ukumbusho Wake wa Miaka 850

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Moscow—Ukumbusho Wake wa Miaka 850
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kudumu Katika Miaka ya Mapema
  • Kuvumilia Tatizo la Kipekee
  • Moscow Lainuka Kutoka Kwenye Majivu
  • Kudumu na Ufanisi
  • Jiji Linapewa Umbo Jipya
  • Jinsi Kazi Yetu Ilivyosifiwa Huko Moscow
    Amkeni!—2001
  • Ushindi wa Kisheria Baada ya Kupambana kwa Muda Mrefu!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2011
  • Majumba ya Kifalme ya Moscow Yenye Kumetameta Chini ya Ardhi
    Amkeni!—1994
  • “Jiji Lenye Misingi ya Kweli”
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 12/22 kur. 13-18

Jiji Ambalo Limedumu Hadi

Moscow—Ukumbusho Wake wa Miaka 850

“NDUGU, njoo kwangu, Moscow.” Mwaliko huu uliotolewa na Yury Dolgoruky kwa mkuu mwenzake mwaka wa 1147 waonekana kuwa ndio mtajo wa kwanza wa Moscow katika kumbukumbu za historia. Tarehe hiyo—miaka 850 iliyopita—imekubaliwa kuwa kuanzishwa kwa Moscow, jiji kuu la Urusi, hata ingawa uthibitisho wa kiakiolojia waonyesha kwamba kijiji kidogo kilikuwako kwenye eneo hilo muda mrefu hapo awali.

Katika kutarajia siku ya ukumbusho ya miaka 850 ya kuwapo kwa Moscow, mamia ya vifaa vya jiji vilifanyizwa upya na kurudishwa—stediamu, majumba ya michezo, makanisa, stesheni za gari-moshi, bustani, na majengo ya umma. Ni badiliko lenye kustaajabisha kama nini! “Majengo mazima,” alionelea mkazi mmoja wa Moscow, “yamebadilika yasiweze kutambuliwa.”

Katika ziara ya kwenda Moscow Juni huu uliopita, tuliona wafanyakazi wakifanya kazi kwenye miradi ya urudisho kotekote katikati ya jiji, karibu na Red Square. Kazi ilikuwa inaendelea, mchana na usiku. Na kila mahali palikuwa na vikumbusha vya siku ya ukumbusho ya miaka 850—katika madirisha ya maduka, katika reli ya chini ya ardhi iitwayo Metro, juu ya nguzo za taa, kwenye bidhaa za kuuzwa—hata uigizaji wa sarakasi ya Moscow ambao tulihudhuria ulirejezea huo ukumbusho.

Kufikia Septemba, wakati ambapo maelfu ya wageni kutoka ulimwenguni pote walipokuwapo kwa ajili ya sherehe hizi za pekee za mwaka wa 850, sura ya Moscow ilikuwa imefanya maendeleo ya kustaajabisha. Ndiyo, zijapokuwa pindi zenye janga la kutisha muda wote wa historia yake, Moscow imeendelea kuwako na kusitawi.

Msomi mmoja wa Biblia kwa wazi alikuwa akifikiria mojawapo ya pindi kama hizo katika historia ya Moscow ambapo, katika sehemu ya mapema ya karne iliyopita alieleza juu ya lile “pigano” linaloshirikishwa na “Har–Magedoni” katika Biblia. (Ufunuo 16:14, 16, King James Version) Alionelea kwamba wengine walidai kwamba mahali pa Har–Magedoni palikuwa Moscow, ijapokuwa yeye mwenyewe hakukubaliana na maoni hayo.a

Kwa nini wengine walidai hivyo? Basi, fikiria historia ya Moscow yenye kuvutia sana na mara nyingi yenye kuhuzunisha.

Kudumu Katika Miaka ya Mapema

Jiji la Moscow liko kwenye mkingamo muhimu karibu na mito mikubwa (Oka, Volga, Don, na Dnieper) vilevile kwenye njia za bara zilizo za maana. Mkuu Dolgoruky “aliweka misingi ya mji wa Moscow,” yaripoti masimulizi ya matukio ya mwaka wa 1156, kwa wazi ikimaanisha kwamba alijenga ngome za kwanza zenye boma za udongo zikiwa na kuta za mbao juu. Kremlin ilikuwa kwenye eneo lenye umbo la pembetatu kati ya Mto Moskva na kijito, Neglinnaya.

Kwa msiba, miaka 21 tu baadaye, mkuu wa Ryazan ulio karibu “alikuja Moscow na kuchoma mji mzima.” Moscow lilijengwa upya, lakini katika Desemba ya mwaka wa 1237, Wamongol chini ya Batu Khan, mjukuu wa Genghis Khan aliye mashuhuri, aliuteka na kuuchoma Moscow kabisa. Pia Wamongol walipora huo mji mwaka wa 1293.

Je, waona kuwa ni ajabu kwamba Moscow lilidumu baada ya kila pigo kubwa kabisa? Pia jiji hili liliibuka kama kitovu cha kidini cha Urusi mwaka wa 1326, wakati mkuu wa Moscow, Ivan Kalita, aliposhawishi kiongozi wa Kanisa la Othodoksi la Urusi aishi Moscow.

Hatimaye, kufikia wakati wa utawala wa Ivan Mkubwa (kutoka mwaka wa 1462 hadi 1505), Moscow ulikuwa umepata uhuru kutoka kwa Wamongol. Katika mwaka wa 1453 jiji la Constantinople (sasa ni Istanbul) liliangukia Waturuki wa Ottoman, ambapo ilibakisha watawala wa Urusi wakiwa wafalme wa Othodoksi pekee katika ulimwengu. Tokeo ni kwamba Moscow ilikuja kuitwa “Roma ya Tatu” na watawala wa Urusi wakaitwa zari au kaisari.

Kuelekea mwisho wa utawala wa Ivan Mkubwa—wakati ambapo Christopher Columbus alikuwa anasafiri baharini kwenda mabara ya Amerika—ile Kremlin ilikuwa imeongezwa ukubwa, na kuta za matofali na minara ilijengwa ambao imebaki mpaka leo bila mabadiliko. Kuta hizo zina urefu uzidio kilometa 2, zina upana wa meta 6, na kimo cha meta 18, na zimetia ndani eneo la Kremlin lenye karibu eka 70.

Yaweza kukushangaza kwamba kufikia katikati ya miaka ya 1500, Moscow lilisemekana kuwa kubwa kuliko London. Kisha, msiba ukatokea katika Juni 21, 1547, wakati ambapo jiji hilo lilipopatwa na moto wenye kuangamiza kabisa, ambao uliacha watu wote bila makao. Tena, watu wenye hekima wa Moscow wakalijenga upya. Lililojitokeza pia katika wakati huu lilikuwa Kanisa Kuu la St. Basil, ambalo lilijengwa ili kusherehekea ushindi wa kijeshi juu ya Watata, au Wamongol, katika Kazan. Hata leo, kazi bora hii ya ujenzi katika Red Square (iliyokamilishwa mwaka wa 1561) ni ishara ya Moscow inayotambuliwa sana.

Miaka mingine kumi baadaye, mwaka wa 1571, Wamongol wa Krimea walifanikiwa kuingia na kuteka Moscow, wakisababisha uharibifu mkubwa sana. Walichoma karibu kila kitu isipokuwa Kremlin. Rekodi zafunua kwamba kati ya wakazi wa jiji 200,000, ni 30,000 pekee waliobaki hai. “Ule Mto Moscow ulisongamana na miili hivi kwamba njia yake iligeuka kuelekea kwingine, na maji yakageuka kuwa mekundu kwa kilometa kadhaa upande wa chini wa mto,” wahariri wa vitabu Time-Life waripoti katika Rise of Russia.

Mara nyingine tena, Moscow lilihitaji kurudishwa. Na lilirudishwa! Baada ya muda fulani, hilo jiji liling’aa kutoka Kremlin, huku kukiwa na kuta zenye kufuatana zikitia ndani sehemu zilizoitwa Kitayi Gorod, Jiji Jeupe, na Jiji la Mbao. Mpangilio wa duara wa Moscow unaofanana na huo ungali upo leo, kukiwa na barabara zinazozunguka nje ya jiji badala ya kuta za duara zinazozunguka Kremlin.

Katika wakati huu watu wa Moscow walitaabishwa sana na utawala wa kikatili wa Ivan Mkatili, mjukuu wa Ivan Mkubwa. Kisha mwaka wa 1598, mwana na mrithi wa Ivan Mkatili, Fyodor, akafa bila mrithi. Hilo lilianzisha “Nyakati za Taabu,” ambazo Rise of Russia chaita “pindi yenye mvurugo zaidi na yenye kutatanisha zaidi katika historia yote ya Urusi.” Ilidumu kwa karibu miaka 15.

Kuvumilia Tatizo la Kipekee

Upesi baada ya Boris Godunov, ndugu mkwe wa Fyodor, kutwaa kiti cha ufalme, Moscow lilipatwa na ukame na njaa kali. Wakati wa pindi moja ya miezi saba mwaka wa 1602, watu 50,000 waliripotiwa kuwa walikufa. Kwa jumla, zaidi ya watu 120,000 waliangamia katika hilo jiji kati ya miaka ya 1601 na 1603.

Kufuatia maafa hayo, mtu aliyedai kuwa Mkuu Dmitry, mwana wa Ivan the Terrible, alivamia Urusi kwa msaada wa askari-jeshi wa Poland. Kwa kweli, uthibitisho unaonyesha kwamba Dmitry halisi alikuwa ameuawa mwaka wa 1591. Godunov alipokufa kwa ghafula mwaka wa 1605, aliyesemekana kuwa Dmitry Asiye wa Kweli aliingia Moscow na kutawazwa kuwa zari. Baada ya utawala wa miezi 13 tu, alifishwa na wapinzani.

Wengine waliodai kiti cha ufalme walifuata, kutia na Dmitry Asiye wa Kweli wa pili, ambaye pia alisaidiwa na Poland. Njama, vita ya wenyewe kwa wenyewe, na uuaji-kimakusudi ukawa umeenea. Mfalme Sigismund wa Tatu Vasa, wa Poland, alivamia Urusi mwaka wa 1609, na baada ya muda, mkataba ulitiwa sahihi ambao ulitambua mwana wake Władysław wa Nne Vasa kuwa zari wa Urusi. Wakati Wapoland walipoingia Moscow mwaka wa 1610, hilo jiji likawa chini ya udhibiti wa Wapoland. Lakini punde si punde Warusi waliunganika dhidi ya Wapoland na kuwafukuza kutoka Moscow kufikia mwisho wa 1612.

Nyakati hizi zenye taabu ziligeuza Moscow kuwa ‘ardhi isiyotumika iliyofunikwa na mibaruti na magugu ambayo yalienea kwa kilometa nyingi mahali pa barabara za zamani.’ Ule ukuta wa Jiji la Mbao ulikuwa umechomwa kabisa, na majengo ya Kremlin hayakuwa yamerekebishwa. Mjumbe mwenye kuzuru wa Sweden alifikia mkataa: “Huo ukawa mwisho wenye kuogofya na wenye kuleta msiba wa jiji maarufu la Moscow.” Hata hivyo, alikosea.

Zari Mrusi kutoka familia ya Romanov alichaguliwa mwaka wa 1613, na nasaba hii mpya ya wafalme wa zari wa Romanov ilidumu kwa zaidi ya miaka 300. Ijapokuwa zari mpya mchanga, Michael Romanov, yaripotiwa “hakuwa na mahali popote pa kuishi” kwa sababu ya angamizo kubwa, Moscow lilijengwa upya na tena likawa jiji kuu la ulimwengu.

Katika 1712, yule zari Peter Mkubwa, mjukuu wa Michael, alihamisha jiji kuu la Urusi kutoka Moscow mpaka St. Petersburg, ambalo alikuwa amelijenga kwenye Bahari ya Baltiki. Lakini Moscow lilibaki kuwa “moyo” wenye kupendwa wa Urusi. Kwa kweli, yule maliki Mfaransa Napoléon Bonaparte, akitafuta ushindi, aliripotiwa kusema: ‘Nikiteka Petersburg, nitapiga Urusi kichwani, na nikiteka Moscow, nitaangamiza moyo wake.’

Ndiyo Napoléon alitwaa Moscow, lakini kama historia inavyoonyesha, ni moyo wake uliovunjika, si wa Moscow. Kile kilichotukia katika Moscow kilikuwa chenye kutisha sana hivi kwamba kilisababisha wengine kwa wazi kushirikisha hili jiji na Har–Magedoni.

Moscow Lainuka Kutoka Kwenye Majivu

Katika majira ya kuchipua ya 1812, Napoléon alivamia Urusi akiwa na jeshi lililofikia karibu watu 600,000. Wakifuatia sera ya “kuharibu kabisa riziki,” Warusi walitoroka bila kuwacha kitu chochote kwa maadui. Hatimaye, waliamua kuwaachia Wafaransa Moscow lililokuwa ukiwa!

Mamlaka nyingi husema kwamba wakazi wenyewe wa Moscow walichoma moto jiji lao badala ya kuacha Wafaransa walichukue. “Dhoruba kali ya upepo iligeuza huo moto kuwa helo halisi,” yaripoti historia ya Urusi. Wafaransa waliachwa bila chakula au nyasi kavu, kama historia hii inavyoeleza: “Hakukuwa na hata gunia moja la unga au shehena ya nyasi kavu iliyopelekwa na Warusi kwa jeshi la Ufaransa.” Wakiwa bila namna, Wafaransa walitoka Moscow muda upunguao majuma sita baada ya kuingia na kupoteza karibu jeshi lao lote katika kurudi kwao.

Moyo mkuu wa wakazi wa Moscow uliokoa jiji lao lenye adhama, na wakiwa wameazimia, waliliinua kutoka kwenye majivu. Aleksandr Pushkin, ambaye mara nyingi amefikiriwa kuwa mshairi mkubwa kupita wote wa Urusi, alikuwa na miaka 13 wakati Napoléon alipovamia Moscow, mji wa nyumbani wa Pushkin alioupenda sana. Kuhusu Moscow aandika: “Jinsi ambavyo mawazo huja kwa wingi kwa kila Mrusi halisi anaposikia neno hilo! Jinsi linavyosikika likiwa na mwangwi wenye kina kirefu!”

Kudumu na Ufanisi

Wengi wanaoishi leo hukumbuka, ama kutoka kwenye kumbukumbu ama kutoka kwenye sinema nyakati ngumu sana zilizopata Moscow wakati wa mapinduzi ya Urusi yaliyoanza mwaka wa 1917. Na bado, hilo jiji halikudumu tu—lilisitawi. Metro ilijengwa, na vilevile Mfereji wa Moscow-Volga ili kupatia jiji maji. Kwa msingi, kutokujua kusoma na kuandika kuliondolewa, na kufikia mwisho-mwisho wa miaka ya 1930, Moscow lilikuwa na zaidi ya maktaba elfu moja.

Katika mwaka wa 1937 aliyekuwa meya wa Manchester, Uingereza, aliandika katika kitabu Moscow in the Making: “Ikiwa hakutakuwa na vita kuu, . . . ninaamini kwamba mwishoni mwa mpango wa miaka kumi Moscow litakuwa limekaribia kuwa jiji kubwa lililopangwa vizuri zaidi ambalo ulimwengu haujapata kuona kwa habari ya afya, huduma bora, na huduma za maisha kwa ajili ya raia wake wote.”

Lakini katika Juni 1941, bila kuchokozwa Ujerumani ilishambulia Urusi, ambayo ilikuwa imeungana na Ujerumani na ambayo ilikuwa imeweka nayo mkataba wa kutochokozana muda upunguao miaka miwili tu awali. Kufikia Oktoba, askari-jeshi wa Ujerumani walifika kilometa 40 kutoka Kremlin. Anguko la Moscow lilionekana kuwa lisiloepukika. Karibu nusu ya wakazi wa Moscow milioni 4.5 walikuwa wamehamishwa. Viwanda vipatavyo 500 vilikuwa vimefunga mashine na kuzipeleka kwenye maeneo mapya katika sehemu za mashariki mwa Urusi. Na bado, Moscow halikuanguka. Kihalisi hilo jiji lilijichimbia ndani, likajizingira, na kukinga Wajerumani.

Moscow liliteseka sana kama vile majiji mengine ya Urusi. “Moscow limepitia mengi sana katika karne moja,” aandika ripota Mmarekani aliyeishi huko katika miaka ya 1930 na 1940, “hivi kwamba ninashangaa limedumu.” Kwa kweli, inastaajabisha kwamba Moscow limeendelea kudumu na kuwa mojawapo ya majiji makubwa zaidi na lenye umaana zaidi katika ulimwengu wa kisasa.

Leo, Moscow lina watu zaidi ya milioni tisa na eneo la karibu kilometa 1,000 za mraba likiifanya kuwa kubwa zaidi na lenye watu wengi zaidi ya New York City. Mifuatano ya barabara huzunguka ile Kremlin, ile barabara ya Moscow Ring Road yenye umbali wa karibu kilometa 100 hufanyiza kwa kukadiria mpaka wa nje wa Moscow. Njia pana zenye miti pande zote huelekea sehemu za nje, kama tindi za gurudumu, kutoka katikati ya jiji.

Hata hivyo, wakazi wengi wa Moscow husafiri kwa Metro ya hilo jiji yenye kustaajabisha ambayo imepanuka kutia ndani njia tisa na stesheni 150 hivi, zikihudumia sehemu zote za jiji. Stesheni za Metro za Moscow zatajwa kuwa “zenye kuvutia zaidi katika ulimwengu,” na World Book Encyclopedia. Stesheni nyingine huonekana kama majumba ya kifalme, zikiwa zimerembwa na taa zenye vitawi vingi vya taa, sanamu, vioo vya rangi, na marumaru kwa wingi. Kwa kweli, stesheni 14 za kwanza zilizojengwa zilikuwa na zaidi ya meta 70,000 za mraba za marumaru, ambacho ni kiasi chenye kuzidi zile zote zilizoko kwenye majumba ya kifalme yaliyojengwa na Waromanov kwa miaka 300!

Jiji Linapewa Umbo Jipya

Katika ziara yetu kiangazi kilichopita, tulisafiri kwa Metro kuona mmoja wa miradi mikubwa zaidi uliokuwa unafanyizwa upya—ile Stediamu kubwa sana ya Lenin yenye viti 103,000 iliyojengwa kusini mwa Moscow katika miaka ya 1950. Viti vipya vilikuwa vinawekwa tulipowasili, na tuliona paa yenye kuchukulika ambayo itawezesha kuwe na matukio katika mwaka mzima.

Ule upande wa mbele wa GUM (Duka Kubwa la Serikali) maarufu, upande wa pili wa Red Square kutoka Kremlin, lilikuwa na sura mpya nzuri. Kwenye upande mwingine wa Kremlin, ambapo Neglinnaya ulitiririka kabla haujageuzwa uingie chini ya ardhi katika karne iliyopita, mandhari ya nchi sasa hutia ndani kijito ili kuigiza ule mto wa hapo zamani. Moja kwa moja ng’ambo kutoka kwenye kijito, duka kubwa lililo chini ya ardhi lenye orofa kadhaa, likitia ndani mikahawa, na majengo mengine, lilikuwa linajengwa. Mwandishi mmoja wa Moscow aliliita “mahali penye maduka palipo pakubwa zaidi katika Ulaya,” lakini akaongezea, “ndivyo wanavyoamini katika Ofisi ya Meya.”

Katika eneo jingine lisilokuwa mbali na Kremlin, kreni za ujenzi zilionekana kuwa kila mahali, na ujenzi ulikuwa umepamba moto. Hazina za kiakiolojia ziligunduliwa kwenye maeneo yaliyochimbuliwa, kutia ndani, katika mahali pamoja, hifadhi yenye sarafu zaidi ya 95,000 za Kirusi na za Ulaya Magharibi zenye tarehe za kutoka karne ya 15 hadi ya 17.

Makanisa yalikuwa yakirekebishwa na mengine kujengwa upya. Kanisa Kuu la Our Lady of Kazan, katika Red Square, lililoharibiwa mwaka wa 1936 na nafasi yake kuchukuliwa na msala wa umma, lilikuwa tayari limekamilishwa. Lile Kanisa Kuu la Christ the Savior lililo kubwa na lililojengwa kusherehekea ushindi dhidi ya Napoléon, lilikuwa limelipuliwa katika mwaka wa 1931 wakati wa kampeni ya Kikomunisti dhidi ya dini. Wakati wa ziara yetu lilikuwa linakaribia kukamilika kwenye eneo lake la hapo zamani, ambalo kwa miaka mingi lilikuwa eneo la kidimbwi kikubwa cha nje cha kuogelea chenye kupashwa joto.

Kuzuru maeneo ya ujenzi kulivutia sana, hasa tulipofikiria kwa makini sura mpya ambayo Moscow lingekuwa nayo mwishoni mwa mwaka. Na bado, kilichotupendeza na Moscow kilikuwa ni watu wake. “Mgeni hushikwa kabisa na urafiki wote ambao kwa asili wakazi wa Moscow waweza kuonyesha,” akaonelea hivyo wakati mmoja mleta-habari aliyekuwa Moscow. Tulipata hilo kuwa la kweli, hasa wakati tuliposongamana kuzunguka meza ndogo ya jikoni, tukifurahia shauku yenye upendo na ukaribishaji-wageni wa familia ya Warusi.

Kwa furaha, tulipata kwamba wakazi wengi wa Moscow wamejifunza maana ya kweli ya Har–Magedoni, pigano ambalo katika hilo Muumba wetu atasafisha dunia nzima. Hilo litaanzisha kipindi ambacho wote wanaompenda kikweli wataweza kuishi pamoja, si na upendeleo na chuki, lakini wakiwa na uelewano na kutumainiana, kama watoto wa Mungu, wanaopendana na kutumikia Mungu kwa umoja. (Yohana 13:34, 35; 1 Yohana 2:17; Ufunuo 21:3, 4)—Imechangwa.

[Maelezo ya Chini]

a Commentary on the Holy Bible, cha Adam Clarke, Toleo la Buku-Moja, ukurasa wa 1349.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Kanisa Kuu la St. Basil, na Kuta za Kremlin zinazotambuliwa sana kuwa ishara za Moscow

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kila mahali, kuna vikumbusha vya ukumbusho wa miaka 850

[Picha katika ukurasa wa 16]

Lile duka maarufu GUM, likiwa na sura mpya

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Stesheni nyingi za Metro huonekana kama majumba ya kifalme

[Hisani]

Tass/Sovfoto

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kurekebisha Stediamu ya Lenin

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mandhari mpya nje ya Kremlin

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kreni za ujenzi zilionekana kuwa kila mahali, na ujenzi ulikuwa umepamba moto

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki