“Jiji Lenye Misingi ya Kweli”
KILA jiji lina misingi, kwa hiyo ikiwa moja laelezwa kuwa lenye misingi ya kweli, ni lazima liwe la kudumu sana. Majiji makuu ya kale, kama Babuloni, Petra, Ashuri, na Teotihuakani, hayakuwa hivyo kamwe.[1] Majiji hayo ambayo wakati mmoja yalikuwa na hekaheka na kelele nyingi za watu leo yametokomea yakakimya zii. Ndivyo na mataifa yaliyoyawakilisha.
Kwa kawaida, majiji makuu ya kitaifa ya siku hizi huonwa kwa hakika kuwa na misingi imara. Huenda yasiwe sikuzote ndiyo majiji makubwa zaidi katika nchi zayo mbalimbali, lakini uhakika wa kwamba jiji hutumikia likiwa jiji kuu la taifa lalo hulipa umaarufu hata kama lina ukubwa gani.[2] Acheni tutazame vielelezo vinne.
Ina Hali Zinazotofautiana Kiajabu
Katika 1790 Bunge la United States liliamuru kwamba makao ya kudumu ya serikali ya taifa hayakupasa kuwa ndani ya mipaka ya jimbo lolote moja. Kwa hiyo kizio maalumu kiitwacho Wilaya ya Kolumbia kikafanyizwa kwa kusudi hilo. Jiji la Washington liko katika eneo la mwambao wa mashariki wa pwani ya United States katika Wilaya ya Kolumbia, na halipasi kudhaniwa kwa makosa kuwa ndilo jimbo la Washington, ambalo liko katika pwani ya Pasifiki maelfu ya kilometa kaskazini-magharibi mwa hilo jiji kuu la taifa.[3]
Muundo wa hapo awali, uliokamilishwa katika 1791 na mhandisi Mfaransa Pierre L’Enfant, ulihitaji kuwe na mfumo wenye mapambo mengi ya bustani za umma na nafasi wazi za kutumika kama mazingira ya upande wa nyuma ambayo yangeweza kuongezea uzuri wa Capitol na majengo mengine ya serikali kuu.[4][5] Makao ya urais yenyewe yaliundwa hatimaye na stadi muunda-majengo Mwailandi James Hoban. Mawe yayo ya changarawe yalikuwa na uvutio wa kuonekana wazi sana kwa kutofautiana na yale majengo ya matufali mekundu ya hapo karibu hivi kwamba upesi likabandikwa jina la White House (Nyumba Nyeupe), jina ambalo lilikubaliwa rasmi katika 1902.[7]
Washington halina kifani, hata kama litapimwa kwa viwango gani. Majengo ya serikali kuu, pamoja na makumbusho na sanamu za maumbo zaidi ya 300, hupamba makao haya ya muda ya mamia ya wanasiasa. [8] Na kulingana na chanzo kimoja, hayo ni makao ya wanasheria wasiopungua 55,000 na waandishi wa majarida 10,000![9]
Imesemwa kwamba Washington “ndicho kioo cha kuonyesha mambo yaliyo mabaya zaidi na yaliyo bora zaidi ya Amerika.”[10] Yaliyo mabaya zaidi ni kutia ndani matatizo ambayo hukumba majiji yote ya U.S.: ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, uchafuzi, uhalifu, nyumba za chini ya kiwango, na msukosuko wa ubaguzi wa rangi, kutaja machache tu. Kama vile iitwavyo na kichapo kimoja maarufu cha marejezo, Washington ni “jiji la makutanio ambalo lina hali zinazotofautiana kiajabu, kuanzia sifa mbaya ya kuwa na sura isiyopendeza na uhalifu hadi kuwa na umaarufu wa mapambo ya kuvutia kwelikweli.”[11]
Je! Ni Roma ya Tatu?
Mpaka hivi majuzi, Washington na Moscow yalifanana kidogo kwa kuwa na White House—lile jengo la makao makuu ya jamhuri ya Urusi lilibandikwa jina hilo pia kwa sababu ya kuwa na marimari katika kuta za juu—na yote mawili yalikuwa na mfumo mzuri sana wa magari-moshi ya kusafiri chini ya ardhi uitwao Metro.[12]
Metro ya Moscow ni ya kasi na isiyo na gharama kubwa, nayo ina uvutio ambao hupatikana mara haba katika sehemu za chini ya ardhi. Kufikia Agosti 1993, nauli ya safari moja, bila kujali umbali, ililingana na karibu senti moja ya U.S. Vituo fulani vilijengwa kwa marimari na vina picha za kuvutia, sanamu za maumbo, na michoro ya rangi maridadi iliyonakshiwa moja kwa moja juu ya dari. Mitambo ya kupandisha watu juu huwainua kutoka chini hadi kwenye magari-moshi na kurudi chini mbiombio.[13]
Moscow ni moja la majiji ya zamani zaidi ya Urusi, yaliyoanzishwa katika 1147, kulingana na mapokeo. Katika karne ya 15, lilipata kuwa jiji kuu la jimbo la Urusi uliokuwa umefanyizwa majuzi, lakini likapoteza cheo hicho katika 1712 wakati St. Petersburg lilipokuja kuwa jiji kuu. Karne mbili baadaye, katika 1918, baada ya yale Mapinduzi ya Bolshevik, Moscow lilipata tena cheo chalo cha kuwa jiji kuu la Urusi na likawa jiji kuu la Muungano mpya wa Sovieti pia.[14]
Ile Kremlin, ambayo kwa miongo ya miaka imefananisha Ukomunisti na kuwa tegemeo kubwa la Moscow, imepakana upande wa mashariki na uwanja wa jiji uitwao Red Square (Mraba Mwekundu).[15]
Kwenye ncha ya kusini ya Red Square iko Kathedro ya St. Basil, iliyojengwa muda wa katikati ya karne ya 16 na Maliki Ivan 4, ambaye hujulikana vizuri zaidi kuwa Ivan Mkatili. Muundo wayo na rangi zayo nyangavu hazina kifani. Mapokeo husema kwamba msanii wa ujenzi aliyeijenga alipofushwa baadaye ili kumzuia asifanyize tena kitu chochote kama hicho.[18]
Wanasiasa na wanadini walishirikiana muda wa karne nyingi katika kuta za Kremlin—jambo ambalo lahakikishwa kwa ushuhuda bubu wa makathedro ya huko, hasa baada ya Moscow kuwa kitovu cha Kanisa Orthodoksi la Urusi katika 1326.[19] Baadaye Moscow lilipata kuitwa “Roma ya Tatu,” na “Warusi wakasadiki kwamba walikuwa na cheo maalumu—walikuwa katika upendeleo wa Mungu akiwa ndiye mhifadhi mkuu zaidi wa kweli ya kidini.”[20] Lakini lile kaburi lenye fahari katika Red Square, ambapo mwili wa Lenin umehifadhiwa, na yale makaburi yaliyo katika ukuta wa Kremlin ya Wakomunisti wasioamini kuna Mungu lakanusha dai hilo.[21]
Je! Ni Jiji Kuu Lenye Tumaini?
Wazo la kutafuta jiji kuu katika sehemu ya ndani ya Brazili lilitajwa mapema sana kama 1789 na hata likaingizwa katika katiba 1891. Na bado, ulipofika mwaka 1956 ndipo uwanja fulani ulipochaguliwa. Miaka minne baadaye serikali kuu ya Brazili ilitoa jasho kuja kuhama Rio de Janerio umbali wa kilometa 1,000 na kuanza makao yayo mapya. [22]
Kujenga jiji zima kwa muda mfupi hivyo kulistahili sifa. Wabrazili wengi walijivunia jambo hilo kuwa ishara ya kwamba taifa lao lingekuwa maarufu wakati ujao. Walilisifu kuwa jiji kuu la ki-siku-hizi kupita mengine yote ulimwenguni, wakiliita “jiji kuu lenye tumaini.”[23] Brasília lina majengo ya ki-siku-hizi ya kuvutia, na ukuzi walo wenye utaratibu ni kielelezo chenye kutokeza cha mpango mzuri wa mijengo ya jiji kubwa.[24]
“Kusudi la kuwako kwa Brasília,” yasema The New Encyclopædia Britannica, “lilikuwa kukaza fikira juu ya sehemu ya ndani ya nchi na kuharakisha kukaliwa kwa jimbo hilo na kusitawisha mali zalo za asili zisizotumiwa.”[25] Kwa kadiri fulani malengo hayo yametimizwa. Lakini Brasília imekua, hali moja na Washington ambalo sasa lina eneo kuu la jijini lililo kubwa mara 40 kama Wilaya ya Kolumbia. Sasa watu zaidi ya 1,600,000, badala ya wale 600,000 waliokusudiwa, huishi humo na katika majiji yenye kulizunguka kandokando. Katika sehemu fulani-fulani maisha ni shida.[26]
Kwa njia fulani-fulani, hata mambo yale mazuri ya jiji yamekuwa vipingamizi. “Hali ya Brasília,” lasema gazeti National Geographic, “inafanana kidogo na bustani yenye maumbo yaliyochongwa vizuri na kufanana kidogo na kitu cha ajabu-ajabu kilicho kama ndoto za mwezini.”[27] Kichapo Das Bild unserer Welt (Picha ya Ulimwengu Wetu) chasema hivi: “Kufikia sasa imekuwa haiwezekani kufanya Brasília, lile jiji kuu jipya, liwe na tabia zistahilizo jiji. Badala ya kuwa hivyo, katika jiji hili lililofanyizwa katika hali zisizo za kiasili, mafumbo ya ulimwengu wa roho, vikundi vya wenye ibada za kisiri, na madhehebu zimevuvumka kwa wingi kuliko mahali penginepo—tokeo la watu kujihisi watupu na wapweke.”[28]
Hivyo, ni wazi kwamba “lile jiji kuu lenye tumaini” lina udhaifu fulani mbalimbali. Mazingira yalo ya baridi-baridi, yasiyo ya kuchangamsha na mapengo yalo yenye mianya mikubwa—yapendwayo sana katika majiji makubwa—huonekana wazi sana hasa wakati wanasiasa na wafanyakazi wa ofisini waondokapo jijini kwenda mapumziko ya miisho-juma na ya sikukuu.[28A]
Juu Milimani
Minane kati ya milima kumi iliyo mirefu zaidi ulimwenguni imo kwa sehemu au kwa ukamili katika mipaka ya Nepal.[31] Hivyo, haishangazi kwamba jiji kuu la nchi hiyo liko meta 1,300 juu ya usawa wa bahari.[32] Kwa kulinganishwa na majiji makubwa, idadi ya watu 235,000 wa Kathmandu ni ya kadiri. Kwa kila mwenyeji wa Nepal, zaidi ya raia 80 huishi kwingineko.a[33]
Jiji kuu limo katika Bonde la Kathmandu, ambalo katika nyakati za kale lilikuwa ziwa. Ukubwa wa bonde, ambao ni kama kilometa 19 kwa 24, haulifanyi liwe maarufu. Kwa karne kadhaa lilikuwa kitovu cha biashara nyingi katika njia kuu zilizounganisha India na China na Tibeti.[35] Sikuzote ardhi ya kilimo huwa haba katika nchi za milima-milima, kwa hiyo yahofiwa kwamba majiji yaliyo katika hilo bonde huenda yakawa makubwa mno na kulikosesha taifa ile ardhi ya rutuba iliyo ya thamani kubwa. Hofu hiyo ina sababu nzuri. Idadi ya watu wa Kathmandu imeongezeka zaidi ya maradufu tangu 1960. Makadirio ni ya kwamba kufikia mwaka 2020, karibu asilimia 60 ya hilo bonde huenda ikamalizika kwa sababu ya jiji kusambaa.[36]
Kathmandu, ambalo ndilo jiji kubwa pekee la Nepal, limehusika sana na mambo ya kijamii, kiuchumi, na kisiasa ya taifa hilo kwa muda mrefu,[37] na pia katika mambo ya kidini. The Encyclopedia of Religion yasema kwamba Bonde la Kathmandu “limekuwa na mfuatano wa mawazo ya utamaduni wa hali ya juu na mitindo ya usanii wenye fikira za kidini sana. . . . Hakuna sehemu nyingine ya jimbo la Himalaya ambapo Ubuddha na Uhindu umeshikamana sana kama hapa.”[38] Yafaa kujua yaelekea kwamba mahali alipozaliwa Siddhārtha Gautama, ambaye baadaye alikuja kuitwa Yule Mwangaziwa-Nuru, au yule Buddha, palikuwa Lumbini, Nepal, kilometa zinazopungua 240 kusini-magharibi ya Kathmandu.[39]
Bila shaka, hiyo ilikuwa karibu miaka 2,500 iliyopita. Majuzi zaidi, katika miaka ya 1960, wengine pia walikuja Nepal na Kathmandu ili wapate “mwangazio-nuru,” washirika wa kile kizazi cha mahipi.
Jiji Lenye Misingi ya Kweli
Kwa karne nyingi wanadamu wamejenga majiji ya kutawalia wanadamu wenzao. Lakini somo lenye msiba ambalo historia imefundisha ni kwamba “kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu” kwa usahihi.—Yeremia 10:23; Mhubiri 8:9.
Yaonekana wazi kwamba majiji yamo taabani sana. Yanajikokota kujaribu kuokoka, hali moja na mifumo ya kisiasa ambayo majiji hayo huiwakilisha. Misingi legelege ya utawala wa kibinadamu inavunjika-vunjika. Hata hivyo, sivyo ilivyo kwa “lile jiji lenye misingi ya kweli, ambalo mjenzi na mfanyi wa jiji hilo ni Mungu.”—Waebrania 11:10, NW.
Biblia huliita jiji hilo Yerusalemu la kimbingu. (Waebrania 12:22) Yafaa liitwe hivyo, kwa kuwa Yerusalemu lilikuwa ndilo jiji kuu la kidunia la Israeli la kale, taifa asili la Mungu. Lakini Yerusalemu la kimbingu, likiwa jiji kuu la ulimwengu wote mzima wa Mungu, lina msingi wa kweli, kwa maana Mjenzi walo ni yule Mungu wa milele mwenyewe. Zaburi 46:5 husema hivi kwa unabii: “Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.”
Utawala wa kibinadamu unatikisika ukatokomee. Kwa kutambua uhakika huo, mamilioni ya watu mmoja-mmoja “wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha” wanajitiisha kwa utawala wa kimungu kwa hamu na hekima.—Zaburi 47:8; Ufunuo 7:9, 10.
Kumbuka, Yerusalemu Jipya liko juu kuliko Kathmandu lenye milima, kwa maana liko mbinguni kwenyewe. Na ule “mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri,” ambao hutiririka kupita katika Yerusalemu Jipya ni wenye kutakata na kuleta ufanisi kuliko Mto Potomac kule Washington au Mto Moscow kandokando ya ile Kremlin. (Ufunuo 22:1, 2)[41] Badala ya kuleta hisia zozote za utupu na upweke, Yerusalemu Jipya ndiyo njia ya Mungu ya ‘kushibisha kila kilicho hai matakwa yake.’—Zaburi 145:16.
Jinsi ilivyo vizuri kujua kwamba yajapokuwa matatizo mazito katika majiji ya ulimwengu yanayojikokota kwa shida, kuna tumaini—kwa sababu ya “lile jiji lenye misingi ya kweli”!—Mwisho wa mfululizo wa makala juu ya majiji.
[Maelezo ya Chini]
a Tofauti na hivyo, kati ya kila raia sita wa Nicaragua, mmoja hukaa katika jiji kuu la Managua, na kati ya kila raia wanne wa Senegal, mmoja hukaa katika jiji kuu la Dakar.[34]
[Picha katika ukurasa wa 24]
White House, Washington, D. C.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kathedro ya St. Basil katika Red Square, Moscow, Urusi
[Picha katika ukurasa wa 26]
Hekalu la Kihindu, Kathmandu, Nepal