Brasília—Jiji Changa, Tofauti, na Lenye Kukua Haraka
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Brazili
NI WAPI ulimwenguni ambapo ungeweza kumpigia simu mchoraji wa ramani za awali za jiji kuu la nchi yenu? Ungeweza kumpata wapi msanifu-ujenzi aliyetayarisha na kusimamia ujenzi wa majengo ya kwanza ya serikali katika jiji lenu kuu? Na ni wapi uwezapo kutembea katika jiji kuu na ujue kwa hakika kwamba kila mtu mwenye umri uzidio miaka 40 ambaye unamwona hakuzaliwa huko? Ni katika Brasília, jiji kuu la Brazili—jiji changa na la kipekee ambalo tunapaswa kulichunguza kwa makini zaidi.a
Mwanzo Wenye Kukawia
Inachukua muda wa saa moja na nusu hivi kusafiri kwa ndege kutoka São Paulo hadi Brasília. Basi zenye starehe husafiri kwa muda wa saa 12 hivi. Nilichagua kusafiri kwa basi. Nikapata wakati mwingi wa kusoma historia ya jiji hilo.
Tangu wakati wa maasi ya kwanza yaliyopangwa dhidi ya utawala wa Wareno mwishoni mwa karne ya 18, kulikuwa na tamaa ya kujenga jiji jipya la Brazili. Muda mfupi baada ya Brazili kupata uhuru mwaka wa 1822, kiongozi mmoja wa Brazili José Bonifácio de Andrada e Silva alipendekeza kwamba jiji hilo kuu la wakati ujao liitwe Brasília, jina ambalo wachora-ramani wa karne ya 17 tayari walikuwa wametumia kutaja nchi yote.
Mnamo 1891, katiba mpya ya nchi hiyo ilitangaza kwamba eneo la kilometa za mraba 14,000 katika mbuga litwaliwe katika Uwanda wa Kati wa Milima. Kwenye uwanda huo, kilometa zipatazo 1,000 kutoka pwani, jiji jipya lilipasa kujengwa. Wanasiasa walisababu kwamba kuhamisha jiji kwenye bara kutoka Rio de Janeiro kungeharakisha maendeleo ya sehemu kubwa za bara za nchi hiyo. Lakini, miaka mingine 50 ikapita bila jambo lolote kufanywa. Hatimaye, mnamo 1955, mwanzo wenye kukawia wa Brasília ukaisha, na mwanzo wenye utendaji mwingi ukawa karibu kuanza.
Shindano na Kuchora Ramani
Mwaka huo, mgombea urais Juscelino Kubitschek aliapa kwamba akichaguliwa kuwa rais, jiji kuu jipya lingejengwa hata kabla hajamaliza muda wake wa miaka mitano akiwa rais. Mnamo 1956, Kubitschek alichaguliwa.
Miezi michache awali, serikali ilikuwa imetangaza shindano: Wasanifu-ujenzi, wahandi-si, na wapangaji wa miji nchini Brazili walialikwa wachore ramani ya hilo jiji kuu jipya. Baada ya miezi michache, watu 26 walipeleka michoro yao ya jiji bora. Mnamo Machi 1957, baraza la kimataifa likatangaza mshindi: mpangaji wa miji Lúcio Costa.
Tofauti na michoro ya watu wengine, ramani ya Costa ilikuwa kurasa chache za michoro na maandishi ya mkono yenye kushikana—jiji lote katika bahasha! Aliliomba radhi baraza hilo kwa ramani yake iliyochorwa tu kivivi-hivi lakini akaongezea: “Kama haifai, basi itakuwa rahisi kuiharibu, nami sitakuwa nimepoteza wakati wangu na wakati wa mtu yeyote.” Lakini, baraza hilo likapenda ramani yake na kuitaja kuwa “wazi, ya kueleweka kwa urahisi na kuwa sahili sana.” Ramani yake ilipendekeza nini, na ikawaje kwamba likawa jiji la mawe?
“Ndege” Mavumbini
Njia nzuri ya kujua ni kuzuru Jumba la Ukumbusho la Museu Vivo da Memória Candanga. Kwa kuwa jumba hilo la ukumbusho liko katika jengo ambalo mwanzoni lilikuwa hospitali ya kwanza ya jiji hilo, jumba hili hasa ni chanzo kabisa cha Brasília. Watoto wa kwanza waliozaliwa Brasília miaka 40 iliyopita walianza maisha zao papa hapa. Lakini, leo jengo hilo ambalo zamani lilikuwa hospitali sasa lasimulia kuzaliwa na uchanga wa Brasília. Ni hadithi ya “Mavumbi, Mahema na Saruji,” ndivyo unavyosema wonyesho mmoja katika jumba hilo la ukumbusho.
Laureti Machado, mfanyakazi wa jumba hilo la ukumbusho, kwanza anisimulia kipindi cha “mavumbi.” Atua mbele ya picha iliyopigwa mwaka wa 1957, ya barabara mbili zenye mavumbi zinazopitia mbuga, na kufanyiza makutano porini. “Picha hii,” asema, “yaonyesha hatua ya kwanza kabisa ya ujenzi wa jiji hili.” Kisha, tukitazama michoro ya Costa, twaona jinsi alivyogeuza mojawapo ya barabara hizo ambayo baadaye wafanyakazi, waitwao candangos,b waliipinda mbugani na kutokeza umbo la ndege kwenye mavumbi.
Umbo hilo la ajabu ndilo ramani ya Brasília hadi sasa: Ndege inayoelekea mashariki na mabawa yake yenye kupinda yakielekea kaskazini na kusini. Majengo yenye idara tatu za serikali yako sehemu ya mbele, eneo la biashara ni mwili wa ndege hiyo, na maeneo ya makazi ni mabawa.
Kutoka Kuwa Mahema Hadi Saruji
Sehemu za jumba la ukumbusho la “mahema” na “saruji” zinasimulia jinsi wafanyakazi kutoka kotekote Brazili walivyouza mali zao ili wasafiri kuja penye ujenzi. ‘Baba yangu alinunua lori, akalijaza familia nzima—zaidi ya watu 20—na kusafiri kwa siku 19 ili kufika hapa,’ akumbuka mfanyakazi mmoja aliyefika huko Agosti 1957. Wengine walisafiri kwa basi au mikokoteni yenye kuvutwa na ng’ombe au kuombaomba lifti. Kwa ujumla, wafanyakazi 60,000 walifika.
Kundi hilo la ujenzi, lenye kuishi katika mahema lilihitajika sana kwa sababu jiji lilipangiwa kuzinduliwa Aprili 21, 1960. Hilo lilimaanisha kwamba wahandisi, mafundi, na wafanyakazi wa ujenzi walipaswa kujenga jiji kuu kwa siku 1,000—kazi kubwa kwelikweli! Lakini, siku ya mzinduo ilipofika, wafanyakazi hao walikuwa wamemaliza. Jiji kuu changa zaidi ulimwenguni lilikuwa limeinuka kutoka kwenye mavumbi ya mbuga.
La Kwanza na la Pekee
Jiji hilo na wajenzi wake wangali wanakumbukwa sana katika ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) katika Brasília. “Hakuna mfano mwingine wowote wa ramani ya jiji uliofuatwa kwa uaminifu sana kama ramani ya Costa,” mwakilishi wa mambo ya utamaduni wa UNESCO, Dakt. Briane E. Bicca, aniambia. “Hiyo ni sababu moja inayofanya Brasília liwe jiji la kwanza na la pekee katika karne ya 20 kuwekwa katika Orodha ya Turathi za Ulimwengu ya UNESCO.”c
Brasília pia ndilo jiji la pekee kwenye orodha hiyo ambalo bado linajengwa. Hilo latokeza ugumu, asema Dakt. Bicca. “Tunaweza kuhifadhije ramani ya jiji la awali huku jiji likibadilika?” Alipokuwa hai, msanifu-ujenzi Lúcio Costa bado alikabili tatizo hilo, ingawa alikuwa katika miaka yake ya 90. Alichunguza majengo mapya, akihakikisha kwamba hayakuharibu ramani yake ya awali. Kwa mfano, Costa alipopata kujua juu ya mipango ya kujenga reli ya mjini katika Brasília, yeye alisisitiza kwamba magari-moshi yapitie chini ya ardhi.
Mandhari Yote ya Jiji
Sasa ni wakati wa kutalii jiji. Hata ukiwa mgeni wa mara ya kwanza hatapata tatizo la kupotea. Kuna barabara kuu mbili, na kituo cha basi kiko kwenye makutano ya barabara hizo kuu. Barabara moja inatoka magharibi ikielekea mashariki (kutoka mkia wa “ndege” hadi mbele) nayo inakupeleka kwenye hoteli, majumba ya michezo, benki, na maduka. Ile barabara nyingine inatoka kaskazini ikielekea kusini (tokea bawa moja hadi jingine) nayo inakupeleka kwenye maeneo ya makazi.
Mahali bora kabisa pa kutazama Brasília ni kwenye Mnara wa Televisheni, ambao una kimo cha meta 224 na ambao upo kwenye mwili wa ndege nyuma tu ya mabawa. Lifti ya bure inakuinua meta 75 juu ya ardhi na kukupa mandhari ya katikati ya jiji, ambayo inaitwa Plano Piloto. Utazamapo bustani pana za jiji hilo, ambazo ni pana na tupu hivi kwamba unaona zinashikana na mbingu, unashangazwa na nafasi tele za Brasília. Mtengeneza mandhari Roberto Burle-Marx ametengeneza bustani za Brasília zikiwa pana sana hivi kwamba jiji hilo ladai kuwa na nafasi nyingi kuliko jiji jingine kuu lolote ulimwenguni.
Kuelekea mashariki kuna sehemu pana za nyasi kwenye pande zote za barabara. Kandokando ya barabara kuna majengo 17 yanayofanana. Kila moja ya majengo hayo yenye umbo la sanduku lina idara mbalimbali za serikali. Kwenye mwisho wa zile nyasi kuna ishara ya Brasília: kuba mbili zenye kufanana, moja ikielekea juu na moja ikiwa imepinduliwa, zikiwa chini ya jengo lenye orofa 28 ambalo lina Bunge la Taifa la Brazili.
Umbo la Bunge la Taifa laweza kukukumbusha kidogo makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York—na kwa sababu nzuri. Mmojawapo wa wasanifu-ujenzi ambaye alishiriki kutayarisha ramani ya majengo ya Umoja wa Mataifa alikuwa Oscar Niemeyer—Mbrazili yuleyule aliyechora ramani ya Bunge la Taifa na karibu majengo mengine makuu ya Brasília. Baadhi ya ubuni wake bora zaidi, kama vile majengo ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Kigeni (Palacio Itamaraty) na Wizara ya Sheria (Palacio da Justiça), yako karibu na majengo mawili ya Bunge la Taifa.
Sababu Inayofanya Usiweze Kupotea
Lakini, Brasília ni zaidi ya kuwa tu mahali pa usanifu-ujenzi. Hiyo pia ina nyumba zilizopangwa vizuri za maelfu ya watu. Tunapopitia makazi ya jiji hilo kwa gari, Paulo, wakili anayeishi Brasília, asema: “Watu wengi waliohamia Brasília wanapata utaratibu huo ukiwa jambo la kutuliza kutokana na msukosuko wa miji ambao walikuwa wamezoea katika majiji mengine.”
Wakazi wa Brasília huishi katika majengo yenye nyumba nyingi. Kikundi cha majengo hayo kimejipanga kuzunguka ua na kufanyiza jengo kubwa. Safu za majengo makubwa hujaza sehemu za kaskazini na kusini za jiji hilo. Ni rahisi kupata nyumba unayotafuta. Kwa mfano “N-102-L,” inapatikana sehemu ya kaskazini ya jiji, jengo kubwa 102, halafu sehemu ya L. Na ukikumbuka kwamba nambari za majengo makubwa huongezeka (tokea 102-116) unapoendesha gari ukingoni mwa jiji, huwezi kukosea.
Ili kuwa na utaratibu na starehe, majengo ya makazi hayapiti orofa sita. Kwa njia hiyo, asema Bwa. Costa, mtoto anayecheza katika ua anaweza kumsikia mama akimwita kwenye dirisha: “Manoel, vem cá!” (Manuel, njoo hapa!)
Matatizo ya Ukuzi
Ingawa Brasília inajivunia kuwa jiji lililojengwa kulingana na ramani, ramani ya jiji hilo ilisahau wafanyakazi waliolijenga Brasília. Ilidhaniwa kwamba baada ya kuzinduliwa kwa jiji hilo, wafanyakazi wangefunga virago vyao na kurudi makwao. Lakini kurudi sehemu ambazo hazina hospitali, shule, wala kazi kwa wazi hakukuvutia wafanyakazi hao. Walipendelea kubaki Brasília—lakini wapi?
Wao hawangeweza kugharamia kodi za nyumba ambazo wao walizijenga, basi wakakaa katika eneo ambalo watu hawaruhusiwi kujenga katika vitongoji vya Brasília. Punde si punde, majiji kadhaa yaliyo makubwa kuliko Brasília yalikuwa yamechipuka. Leo, ni watu wapatao 400,000 pekee wanaoishi katika jiji lililopangwa, na nyumba nyingi hazina watu; lakini karibu wakazi milioni 2 wamekaa katika miji ya vitongoji ambayo haijapangwa kwa utaratibu. Japo ramani za jiji hilo ambazo hazikuwa na makusudi ya kugawanya watu katika matabaka, tofauti za mapato zimegawanya jiji hilo kuwa majiji mawili tofauti.
Ukuzi wa haraka ambao haukutazamiwa na tofauti za kijamii, nazo zinatokeza uhalifu na matatizo ya kijamii na kiuchumi yaliyo kawaida katika jiji lolote lile. Jiji kuu changa la Brazili lina tatizo la ukuzi. Barabara zilizopangwa vizuri na majengo mazuri kwa wazi hazitoshi kubadili mioyo na tabia za watu.
“Je, Ni Moyo wa Brazili”?
Mabango yaliyo kandokando ya barabara zinazoingia Brasília hukumbusha wasafiri wanaokuja kwamba wako karibu kuingia katika “Moyo wa Brazili.” Usemi huo una ukweli fulani: Ingawa si katikati halisi ya nchi hiyo, Brasília liko karibu katikati na mahali pa umbali sawa kutoka kwa majiji makubwa ya nchi hiyo. Lakini, vipi juu ya umaana wa ndani wa usemi huo? Je, kweli Brasília ni moyo wa Brazili? Kuna maoni tofauti-tofauti. Ni kuzuru tu jiji hili la kipekee kuwezako kujibu swali hilo. Lakini kumbuka kwamba usihukumu Brasília kijuu-juu tu. Chunguza jiji hilo kwa muda ili lijitokeze, kama mkazi mmoja alivyosema, “Brasília seduz gradualmente.” (Brasília huvutia mtu polepole.)
[Maelezo ya Chini]
a Mchoraji huyo, Lúcio Costa, alikufa akiwa na umri wa miaka 96, Juni 1998, muda mfupi tu baada ya kutayarishwa kwa makala hii.
b Neno lililotoka Angola (ambalo zamani lilitumiwa na Waafrika kuwaita Wareno) na ambalo lilipendwa na wajenzi wa Brasília.
c Orodha hiyo, iliyokusanywa na UNESCO, inataja mahali-mahali 552 kotekote ulimwenguni penye “umuhimu wa kipekee wa kiasili au wa kitamaduni.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Hadithi ya “Mavumbi, Mahema na Saruji”
[Hisani]
Arquivo Público do Distrito Federal
[Picha katika ukurasa wa 15]
Gwaride la “candangos”
[Hisani]
Arquivo Público do Distrito Federal
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Mandhari ya Brasília
1. Wizara mbalimbali
2. Majengo na ofisi za bunge
3. Mahakama Kuu
4. Uwanda wa “Three Powers”
5. Ofisi za Wakuu
[Hisani]
Secretaria de Turismo, Brasília
[Picha katika ukurasa wa 18]
Lina nafasi kubwa zaidi kuliko majiji makuu ya ulimwengu