Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 3/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maji Yasiyo Matakatifu
  • Tatizo la Mabomu ya Kutegwa Ardhini
  • Watoto Hawana Namna
  • Ubishi Juu ya Useja
  • Tembo Wenye Utovu wa Nidhamu
  • Aksidenti ya Kwanza Angani ya Mgongano na Kutoroka
  • Sifongo Ndizo Zilikuwa za Kwanza
  • Wacheza-Kamari Hupoteza
  • Majangili Wenye Kutumia Nyoka
  • Mabomu ya Ardhini—Kuchunguza Athari Zake
    Amkeni!—2000
  • Jinsi Vita Huwaharibu Watoto
    Amkeni!—1997
  • Pembe za Tembo—Zina Thamani Gani?
    Amkeni!—1998
  • Sifongo Hawana Muundo Tata Lakini Wanavutia
    Amkeni!—2006
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 3/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Maji Yasiyo Matakatifu

Daktari mmoja mpasuaji katika Ireland alitatanishwa wakati mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 72 aliposhikwa na maambukizo mabaya ya macho mara mbili kabla tu ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mtoto wa jicho. Ni nini kilichosababisha maambukizo hayo? Maji “matakatifu” ya Lourdes ambayo alikuwa amenawa nayo uso. “Tatizo,” lasema The Irish Times, “ni kwamba hayo maji matakatifu mara nyingi huwa yameambukizwa na bakteria hatari.” Mwanamke huyo huenda angepofuka kwa urahisi kutokana na ambukizo hilo kama ule upasuaji ungefanywa kama ulivyoratibiwa. Gazeti hilo la The Irish Times laendelea kusema: “Baraka haziui kamwe vijidudu. Na kunyunyizwa kwa maji matakatifu ambayo hukusudiwa kuponya, hasa kwaweza kusababisha ambukizo hatari kwa afya katika hali fulani.” Kulingana na ripoti hiyo, marafiki na watu wa ukoo wenye nia njema wanaokunyunyizia maji “matakatifu” unapokuwa hospitalini waweza kuwa “hatari kubwa zaidi kwa uhai wako.”

Tatizo la Mabomu ya Kutegwa Ardhini

“Kampeni ya duniani pote ya kuondoa mabomu ya kutegwa ardhini katika ulimwengu imepata kwamba lengo hilo ni gumu sana kutimizwa kama mabomu yenyewe,” lasema The Wall Street Journal. “Hakuna vifaa vya kutosha vya kuweza kuhakikisha kuondolewa kwa njia salama kwa mabomu ya kutegwa ardhini.” Leo, wanajeshi hutumia zilezile mbinu za msingi ambazo mababu zao walitumia katika Vita ya Ulimwengu 2—vichunguzi vilivyo kama kijiti na vivumbua-metali. Lakini ni vigumu zaidi kugundua aina mpya za mabomu ya kutegwa ardhini kwa kuwa mengi ni ya plastiki nayo yamezikwa pamoja na vipande vya mizinga na vitu vingine ambavyo hufanya vilipuke kwa urahisi. Kivumbua-chuma kinapohisi kitu fulani, fimbo ya fiberglass huingizwa ardhini kwa uangalifu kwa mwinamo fulani. Lengo ni kupata bomu hilo ardhini kwa kugonga ubavu walo. Iwapo bomu hilo la ardhini limeinama kwa njia fulani na kichwa chalo kiguswe, litalipuka kwenye uso wa mtu. Ingawa mabomu ya kutegwa ardhini hugharimu kiasi kinachopungua dola 5 kila moja, kuyaondoa kwaweza kugharimu zaidi ya dola 1,000 kwa kila moja. Kati ya mabomu ya kutegwa ardhini milioni 1.5 na milioni 2 hutegwa ardhini kila mwaka, na zaidi ya watu 25,000—kutia ndani watoto wengi—hulemazwa au kuuawa na mabomu hayo.

Watoto Hawana Namna

“Kwa ujumla watoto walianza kuwa wahasiriwa wa ugomvi wa watu wazima wakati vita vilipoanza kuwa kamili: mabomu na makombora hayatofautishi umri yanapoua,” lasema The Economist. “Vita za wenyewe kwa wenyewe—ambazo ndizo nyingi leo—huangamiza nchi zote. Katika sehemu fulani mashirika ya kutoa msaada sasa yanalazimika kutoa uangalifu mwingi kwa kuondoa watoto jeshini sawa tu na yanavyoandaa vyakula vya msingi. Kila mahali waendapo wao waweza kutazamia kupata watoto miongoni mwa wakimbizi, waliojeruhiwa na wafu.” Ingawa kila mtu hudai kupenda watoto, watoto ndio huteseka zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Mashirika ya kutoa msaada yakadiria kwamba watoto milioni 24 walio chini ya umri wa miaka 18 walipoteza makao kwa sababu ya vita mwaka uliopita na kwamba wapatao milioni 2 waliuawa katika miaka kumi ambayo imepita. Wengine zaidi milioni nne hadi tano walilemazwa. “Athari za kiakili hazijulikani kihususa,” lasema The Economist.

Ubishi Juu ya Useja

“Kanisa Katoliki ya Kiroma linapoteza makasisi wengi sana kwa sababu linasisitiza kwamba makasisi wadumishe useja,” kulingana na ripoti iliyochapishwa katika ENI Bulletin. Katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Makasisi Waliofunga Ndoa, lililofanywa Brasília, iliripotiwa kwamba makasisi wa Roma Katoliki 100,000 ulimwenguni pote wameacha ukasisi na kufunga ndoa. Kulingana na Jorge Ponciano Ribeiro, aliyekuwa kasisi na ambaye sasa ni profesa kwenye Chuo Kikuu cha Brasília, kasisi 1 kati ya kila makasisi 5 wameacha ukasisi ili wafunge ndoa. Brazili pekee ina makasisi 3,500 ambao wamefunga ndoa. Ribeiro akasema: “Useja ulianzishwa ili kuepuka matatizo kati ya kanisa na urithi wa makasisi, wala si kwa sababu ya kwamba Neno la Mungu laweza kutangazwa vizuri zaidi na wale ambao hawajiingizi katika mahusiano wa kingono.”

Tembo Wenye Utovu wa Nidhamu

“Kama ilivyo na watoto, tembo wachanga wahitaji nidhamu ikiwa watakuwa washiriki wa jumuiya yao wenye kutumainika,” lasema New Scientist. “Wanabiolojia wa wanyama wa pori wasema kwamba tembo madume ambao ni mayatima katika Hifadhi ya Wanyama ya Pilanesberg huko Afrika Kusini wamekuwa wenye utovu wa nidhamu kwa sababu hawajapata kutiwa nidhamu na tembo wenye umri mkubwa.” Tembo hao wakaidi wameshambulia wanadamu, wamegonga kwa pembe zao vifaru 19 na kuwaua katika miaka mitatu ambayo imepita, na hata wamejaribu kujamiiana na vifaru. Watu wawili waliuawa, kutia ndani mwindaji stadi aliyetumwa kupiga risasi tembo mbaya baada ya kushambulia kikundi cha watalii. Katika kila kisa, hao tembo wenye utovu wa nidhamu walikuwa katika kikundi cha tembo wachanga wa kiume walioletwa katika hifadhi hiyo kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Kruger baada ya kundi zima kuuawa ili kupunguza idadi ya tembo. Ingawa kuna mambo kadhaa ambayo yametokeza mkazo kwa tembo, wanasayansi wanahisi kwamba utovu wa nidhamu na kulelewa na tembo wenye umri mkubwa, jambo ambalo ni kawaida sana katika maisha ya kawaida ya familia za tembo, imechangia kwa kadiri fulani tabia yao potovu. Sasa, ni familia nzima-nzima za tembo ndizo zitakazohamishwa ili madume wachanga “waendelee kupokea nidhamu kali wanayohitaji kutoka kwa wazazi,” yasema makala hiyo.

Aksidenti ya Kwanza Angani ya Mgongano na Kutoroka

Aksidenti ya kwanza angani ya mgongano na kutoroka iliyothibitishwa imetukia zaidi ya kilometa 700 juu ya dunia, laripoti New Scientist. Satelaiti ya Ufaransa iitwayo Cerise iliyumbayumba sana wakati kikono cha usawaziko kiliposagwa-sagwa baada ya kugongwa na sehemu ya roketi ya Ariane ambayo ilikuwa ikisafiri kwa mwendo wa kilometa 50,000 kwa saa kwa altitudo hiyohiyo. Uwezekano wa migongano kama hiyo huongezeka kila mwaka huku takataka zikijikusanya katika mzunguko wa dunia. Tayari, kuna zaidi ya vipande vya takataka vinavyojulikana vipatavyo 20,000 vinavyozunguka-zunguka dunia. Ingawa takataka zilizo katika anga za chini huondolewa kupitia njia za asili, kama vile mpanuko wa anga ya dunia, vile vilivyo katika anga za juu zaidi vyaweza kudumu huko kwa maelfu ya miaka. Vinapogongana na vipande vingine vya takataka, hivyo humomonyoka na kuwa vipande vidogo zaidi ambavyo vyaweza kupenya mavazi ya kinga ya mwanaanga au ngao ya chombo cha anga. Hata vipande vya rangi ni hatari. Kwa wakati huu kuna satelaiti 4 hivi zilizokufa katika anga kwa kila 1 ambayo inatenda kazi, na roketi zilizotumika ambazo zimelipuliwa katika anga ni robo ya takataka za anga zinazojulikana.

Sifongo Ndizo Zilikuwa za Kwanza

“Mengi kati ya mawazo yenye akili za wanadamu hupatikana kuwa ni mambo ya asili,” lasema The Washington Post. “Chukua mfano wa maonzi-tembwe. Wanasayansi walitengeneza tembwe zilizo kama gilasi ili kunasa nuru na kuitawanyisha kote katika 1951. Imegundulika kwamba sifongo zinazokuwa chini sana katika Bahari ya Ross katika Antaktika zimekuwa zikifanya hivyo kwa muda mrefu sana.” Hizo sifongo kubwa sana, zinazopatikana majini kufikia kina cha meta 30, zina viunzi vidogo vinavyotokeza nje vya kunasa nuru na kuipitisha, hata katika mpindo wa digrii 90, hadi kwa mwani wa usanidimwanga ambao umo katikati ya mwili wa sifongo hiyo. Majaribio yameonyesha kwamba nuru inayokuja kwa mwinamo fulani hukusanywa pia, ikionyesha kwamba viunzi vilivyo katika pande za sifongo pia vina uwezo wa kuulisha mwani nuru.

Wacheza-Kamari Hupoteza

“Kasino zimetengenezwa kwa njia ya kwamba wenyewe hawawezi kupoteza pesa,” asema mwanauchumi wa Brazili Ricardo Gazel. “Uwezekano wa mtu kupata pesa kwa kucheza kamari ni mdogo sana.” Akionya kwamba kupatikana kwa kasino nyingi kutatokeza tu waraibu wengi wa kucheza kamari, Gazel aongezea: “Kuna dhana bandia ya kuwa mtu atapata pesa bila jitihada nyingi. Watu hufikiri kuna uwezekano wa kwamba kwa bahati nzuri, watakuwa matajiri haraka.” Na zaidi, Veja lamnukuu Gazel akisema kuhusu ukosefu wa msingi katika uchambuzi wa kanisa au serikali: “Serikali ndiyo ina kamari kubwa zaidi nchini. Kuna aina sita za kamari zinazoendeshwa na serikali, bila kutaja bahati na nasibu za serikali. Kanisa haliwezi kuchambua kuhalalishwa kwa kamari kwa sababu ili kupata pesa za parokia zalo, kanisa huendeleza tabia ya kucheza kamari katika soko, ambako sikuzote lina kibanda ambamo waumini hupoteza pesa zao wakicheza kamari.” Kulingana na Gazel, ‘wataalamu wasema kwamba ‘wacheza kamari wenye ushurutisho ambao hawatafuti msaada hujihatarisha kufungwa gerezani, kujiua, au kurukwa akili.’

Majangili Wenye Kutumia Nyoka

Wezi wamekuwa wakiwakabili wakazi wa Diriamba, mji wa Nikaragua ulio kilometa 50 kusini ya Managua, kwa kutumia nyoka wenye sumu. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti la El Nuevo Diario, genge hilo lilikuwa likishika nyokakayamba katika nyanja zilizo karibu, wakiondoa sumu zao, na kisha kunyang’anya watu vitu vyao wasafiripo katika barabara zilizo nje ya mji kwa kuwatisha kwamba wataumwa na nyoka. Msichana mmoja ambaye alizirai alipoona meno ya nyoka, aligundua alipozinduka kwamba mikufu yake ya dhahabu ilikuwa imeibiwa. Genge hilo pia limeibia wakulima vyakula na pesa.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki