Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 3/22 kur. 15-19
  • Pembe za Tembo—Zina Thamani Gani?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Pembe za Tembo—Zina Thamani Gani?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uwindaji-Haramu Wenye Kupita Kiasi
  • Marufuku ya Tufeni Pote
  • Tembo wa Kusini mwa Afrika
  • Akiba ya Pembe za Tembo
  • Mahangaiko Yaendelea
  • Kuna Wakati Ujao Gani kwa Tembo?
  • Je! Ni Wakati wa Kuwaaga?
    Amkeni!—1990
  • Tembo—Marafiki au Maadui?
    Amkeni!—1994
  • Kufuga na Kuzoeza Tembo
    Amkeni!—2009
  • Uhifadhi Dhidi ya Utoweko
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 3/22 kur. 15-19

Pembe za Tembo—Zina Thamani Gani?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA

Katika mkutano wa kimataifa huko Harare, Zimbabwe, katika Juni 1997, wajumbe kutoka nchi 138 walipiga kura ili kuondoa marufuku ya miaka saba juu ya biashara ya pembe za tembo. Uamuzi uliofuata mjadala mkali, waruhusu nchi tatu katika kusini mwa Afrika—Botswana, Namibia, na Zimbabwe—kuuza pembe za tembo chini ya masharti kwa nchi moja, Japani. Wawakilishi kutoka kusini mwa Afrika walifurahia uamuzi huo, wakaanza kuimba. Wajumbe wengine walifikiria wakiwa na wasiwasi juu ya athari ya uamuzi huo kwa tembo wa Afrika.

WAKATI Hannibal alipotoa mwito wa ushindani kwa jeshi la Roma katika karne ya tatu K.W.K., alikuwa na mlolongo wa tembo wa Afrika waliofugwa. Katika siku hizo huenda tembo wa Afrika walikuwa wamefikia makumi ya mamilioni na kusitawi kuanzia Cape hadi Cairo.

Mambo yalibadilika. Mtazamaji mmoja alisema: “Visiwa vya kibinadamu katika bahari ya tembo vilibadilika kwa haraka kuwa visiwa vidogo vya tembo katika bahari ya watu.” Kadiri idadi ya watu ilivyoongezeka, mashindano kwa ajili ya ardhi yaliwaacha tembo bila makao. Jambo jingine lililochangia kupungua kwa tembo lilikuwa kuenea kwa Jangwa la Sahara kuelekea kusini.

Hata hivyo, sababu kubwa lilikuwa lile dai la kutaka pembe za tembo. Tofauti na mfupa wa simbamarara na pembe ya kifaru, pembe ya tembo haihusianishwi na ngano yoyote ya kwamba ina uwezo wa kutibu. Hata hivyo, ni yenye starehe, maridadi, yenye kudumu, na rahisi kuchonga. Tangu nyakati za kale, pembe ya tembo imewekwa kati ya vitu vya thamani na vyenye kutamanika.

Miaka 400 baada ya Hannibal, Milki ya Roma iliangamiza idadi kubwa ya tembo katika kaskazini mwa Afrika ili kuridhisha tamaa kubwa ya pembe za tembo. Kutamani huko kulipigwa marufuku katika ulimwengu wa Magharibi, tangu wakati huo. Mapema katika karne hii, pembe zikawa zinatakikana sana—hasa si kwa sababu ya kazi za usanii na vitu vya kidini kama awali lakini kwa sababu ya utokezaji wa kibodi za piano. Kulingana na kitabu Battle for the Elephants, katika mwaka wa 1910 pekee, karibu tani 700 za pembe za tembo (zikiwakilisha tembo 13,000 waliochinjwa) zilitumika kutengenezea kibodi 350,000 katika Marekani.

Uwindaji-Haramu Wenye Kupita Kiasi

Kufuatia vita ya ulimwengu ya kwanza, kutakikana kwa pembe za tembo kulipungua, sheria mpya za uhifadhi wa wanyama wa pori zilipitishwa, na idadi ya tembo ikaanza kuongezeka. Hata hivyo, kufikia mapema katika miaka ya 1970, uuaji mwingi ukaanza upya. Sasa uhitaji wa pembe za tembo ukatoka katika nchi zilizoanza kuwa tajiri za Asia.

Wakati huu, mambo mawili yalitokeza msiba kwa tembo katika Afrika. Jambo la kwanza lilikuwa kuzidi kupatikana kwa silaha nyepesi za kisasa. Kwa ghafula ikawa rahisi kupiga risasi si tembo mmoja-mmoja tu bali makundi mazima. Pili, vifaa vya kuchongea vya stima vilimaanisha kwamba pembe za tembo zingeweza kubadilishwa haraka kuwa vitu vilivyo tayari kuuza sokoni. Zamani, mchongaji Mjapani huenda alitumia mwaka mzima kuchonga pembe moja ya tembo. Hata hivyo, kukiwa na vifaa vya stima, katika juma moja tu, kiwanda cha watu wanane wanaotengeneza mapambo ya vito na hanko (mihuri ijulikanayo sana katika Japani) wangeweza kutumia pembe 300 za tembo. Kutakikana sana kwa pembe za tembo kulifanya bei kupanda haraka. Bila shaka, pesa nyingi hazikuwaendea wawindaji-haramu bali ziliwaendea walanguzi na wauza-bidhaa, ambao wengi wao walikuja kuwa matajiri sana.

Upotezo wa tembo ulikuwa wenye kuogofya. Karibu miongo miwili hivi, Tanzania ilipoteza asilimia 80 ya tembo wake, wengi kwa wawindaji-haramu. Kenya ilipoteza asilimia 85 ya tembo wake. Uganda ilipoteza asilimia 95. Mwanzoni, wawindaji-haramu waliwapiga risasi hasa madume, kwa sababu walikuwa na pembe kubwa zaidi. Lakini kadiri tembo hao wenye umri mkubwa zaidi walivyopungua, wawindaji-haramu walianza kuwapiga risasi hata ndama kwa ajili ya pembe zao ndogo. Katika kipindi hicho, zaidi ya tembo milioni moja huenda ikawa walikuwa wamechinjwa kwa ajili ya pembe zao, ikipunguza idadi ya tembo wa Afrika kuwa 625,000.

Marufuku ya Tufeni Pote

Jitihada ya kudhibiti biashara ya pembe za tembo na kukomesha uchinjaji mwingi wa kinyama ulishindwa vibaya sana. Mwishowe, katika Oktoba 1989, katika mkutano mmoja huko Uswisi, ule Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Spishi Zilizohatarishwa za Mimea na Wanyama (CITES) ulipiga marufuku biashara zote za pembe za tembo kati ya mataifa yanachama. Marufuku hiyo iliungwa mkono kwa pesa nyingi ili kuwalinda tembo katika eneo hilo.

Wengine walitabiri kwamba kupiga marufuku pembe za tembo kungetokeza bei za juu sana katika magendo na hilo lingeongezea uwindaji-haramu. Kinyume cha hilo kilitokea. Bei zilianguka kwa ghafula, na masoko ambayo kwa wakati mmoja yalikuwa makubwa sana yalianguka polepole. Kwa kielelezo, katika India bei za rejareja za pembe za tembo zilianguka kwa asilimia 85, na wengi wa wachongaji wa pembe za tembo katika nchi hiyo walilazimika kutafuta kazi nyingine. Uwindaji-haramu ulipunguka sana. Kabla ya marufuku hiyo, wawindaji-haramu katika Kenya walikuwa wamewachinja angalau tembo 2,000 kwa mwaka. Kufikia 1995, tarakimu ilikuwa imepungua kufikia 35. Zaidi ya hilo, idadi ya tembo katika Kenya iliongezeka kutoka 19,000 katika mwaka wa 1989 kufikia karibu 26,000 leo.

Kwa sababu hizi, Shirika la Uchunguzi la Kimazingira, lililoko London, lilisifu marufuku ya biashara ya pembe za tembo kuwa “mojawapo ya mafanikio makubwa ya historia ya karibuni ya uhifadhi.” Hata hivyo, si kila mtu anayeshiriki shauku hii, hasa katika kusini mwa Afrika.

Tembo wa Kusini mwa Afrika

Nchi za kusini mwa Afrika zina tembo zaidi ya 200,000, au karibu thuluthi moja ya idadi ya tembo wa Afrika. Hili kwa kiasi fulani ni kwa sababu ya sera za uhifadhi zenye kufaa na kwa kiasi fulani uhakika wa kwamba nchi hizi ziliepuka wanamgambo waliokuwa na silaha kali ambao walichinja makundi ya tembo katika Afrika Mashariki na ya Kati.

Hata hivyo, kadiri idadi za tembo zinavyoongezeka, kwa kawaida kuna hitilafiano kati ya tembo na watu wanaoishi katika sehemu za mashambani. Kwani, tembo aliyefikia utu mzima ana hamu kubwa sana ya kula, na anaweza kula kufikia kilogramu 300 za mimea kwa siku. Ikiwa tembo aishi katika ujirani wako wajua hilo.

Shirika la Mali ya Afrika, lililoko huko Zimbabwe, lataarifu: “Tembo huonwa kwa woga, shuku, na uhasama na Waafrika wengi wa mashambani. Katika muda wa saa chache, tembo wanaweza kuharibu riziki ya watu kwa kula mimea yao au kuwakanyaga-kanyaga mifugo yao hadi wafe. Pia wao huharibu nyumba na shule, vibanda vya ng’ombe, miti ya matunda, mabwawa ya maji, na mchanga. Kila siku magazeti ya habari ya mahali hapo huwa na ripoti za uharibifu wa tembo.”

Nchi za kusini mwa Afrika hujivunia mafanikio yao ya kuweza kudumisha idadi za tembo wenye afya. Lakini uhifadhi ni ghali, na hawaamini kuwa wanapaswa kuadhibiwa kwa matatizo ya nchi nyingine za Afrika. Biashara ya pembe za tembo iliyodhibitiwa, wao husababu, ingeweza kuruhusu pesa zitumiwe kutegemeza jitihada za uhifadhi na zingesaidia kulipia hasara ya wakulima wa mashambani.

Akiba ya Pembe za Tembo

Katika nchi ambazo tembo huzurura huku na huku, pembe za tembo hurundika. Hutoka kwa tembo ambao wameuawa ili kupunguza idadi yao, kutoka kwa tembo wanaokufa vifo vya kawaida, na kutoka kwa akiba haramu zilizofichwa ambazo zimetwaliwa. Ni nini hufanywa na pembe hizi za tembo?

Kenya huchoma pembe zake za tembo. Tangu Julai 1989, Kenya imeteketeza hadharani pembe za tembo zenye thamani ya mamilioni ya dola, bila kuwa na fidia yoyote ya moja kwa moja kutoka nchi za nje. Katika 1992, Zambia pia ilichoma akiba yake ya pembe za tembo. Ujumbe ulikuwa wazi: Nchi za Kenya na Zambia hazikutaka kamwe kushiriki katika biashara ya pembe za tembo.

Nchi nyingine zimeweka akiba yao kuwa kitega-uchumi cha wakati ujao. TRAFFIC, Shirika kubwa zaidi ulimwenguni la usimamizi wa wanyama, lakadiria kwamba jumla ya idadi ya pembe za tembo kwa sasa zilizo akibani katika nchi za Afrika ni angalau tani 462, zenye thamani ya dola milioni 46. Botswana, Namibia, na Zimbabwe, zile nchi tatu ambazo sasa zaruhusiwa kufanya biashara na Japani zina tani 120 za pembe za tembo. Kwa hiyo, wengi huuliza, ‘Katika eneo ambapo watu wanang’ang’ana kiuchumi, mbona mwache pembe za tembo zikae tu bila kutumiwa kwenye bohari? Kwa nini zisiuzwe na kuelekeza pesa hizo kwenye uhifadhi?’

Mahangaiko Yaendelea

Ingawa nchi fulani za Afrika hubisha kwamba kupunguza marufuku ya pembe za tembo kutasaidia kuhifadhi tembo, wengine husisitiza kwamba marufuku kamili ndiyo njia pekee ya kuzuia kuanza upya kwa ukichaa wa uwindaji-haramu. Mahangaiko yahusu kadiri biashara hiyo inavyodhibitiwa. Je, mifumo ya uuzaji yaweza kutoa njia zisizo halali ambazo pembe za tembo haramu zaweza kuingia katika soko halali la biashara? Pia, namna gani kuhusu uwindaji-haramu wa kukisia? Je, kupunguza marufuku huenda kukamaanisha kwamba tembo watauawa na pembe za tembo kufichwa na wale wanaotumaini kwamba marufuku hiyo itapunguzwa zaidi katika siku za baadaye?

Kuongezea hofu hizi ni uhakika wa kwamba bunduki ni nyingi zaidi katika Afrika sasa kuliko wakati mwingine wowote. Vita vya wenyewe kwa wenyewe hapa vimeweka bunduki za kujiendesha katika mikono ya watu ambao, wakichochewa na hali ngumu za kiuchumi, wako tayari kuzitumia ili kupata pesa. Nehemiah Rotich, mkurugenzi wa Shirika la Wanyama-Pori la Afrika Mashariki, aliandika: “Kwa vile sasa pembe ya tembo imekuwa bidhaa iwezayo kuuzwa [kwa sababu ya biashara iliyofunguliwa upya], hakuna shaka kwamba bunduki hizi zitageukia tembo—kwa vyovyote vile ni rahisi kumpiga risasi tembo katika mbuga kubwa kuliko kuiba benki ya mjini.”

Tatizo jingine ni kwamba hatua za kuzuia uwindaji-haramu si ghali tu bali pia ni ngumu. Kupiga doria katika maeneo makubwa ambapo tembo huzurura huku na huku hutaka kuwe na fedha nyingi. Katika Afrika Mashariki, ni vigumu kuzipata.

Kuna Wakati Ujao Gani kwa Tembo?

Matokeo ya uamuzi wa kupunguza marufuku juu ya biashara ya pembe za tembo yangali yangojewa kuonwa. Na bado, hata kama mambo yatakuwa mazuri, tisho kwa tembo halitaisha. Tembo wanatishwa pia na idadi inayoongezeka ya watu ambao wanahitaji ardhi ili kulima na kwa sababu nyingine. Katika kusini mwa Afrika pekee, watu hukata misitu, hasa kwa ajili ya kilimo, hektari zaidi ya 850,000 za ardhi kila mwaka—eneo linalotoshana na nusu ya Israeli. Kadiri bahari ya watu iwavyo kubwa, visiwa vya tembo kwa hakika vitazidi kuwa vidogo.

Gazeti World Watch lataarifu: “Kuna hoja moja ambayo kila mtu ambaye amechunguza tatizo hilo hukubali: tembo wa Afrika akabili wakati ujao mgumu. Tatizo la makao [kwa sababu ya idadi inayoongezeka ya watu] lamaanisha kwamba tembo wengi watakufa kabla ya wakati wao, kwa njia moja au nyingine. Ikiwa hawatauawa na wawindaji wenye kibali au shughuli za kuwapunguza—au kuchinjwa na wawindaji-haramu—wengi zaidi watakufa njaa katika upungufu wa ghafula wa idadi za tembo.”

Tazamio hili lenye kuhuzunisha halifikirii kwa uangalifu maoni wala kusudi la Muumba wa tembo, Yehova Mungu. Hangaikio la Mungu kwa viumbe wake aliowaumba laonekana wazi katika maneno ya Yesu Kristo, aliyesema: “Shore watano huuzwa kwa sarafu mbili za thamani ndogo, sivyo? Na bado hakuna hata mmoja wao hupata kusahaulika mbele ya Mungu.” (Luka 12:6) Ikiwa Mungu hasahau shore mdogo sana, twaweza kuwa na uhakika kwamba hapuuzi hali mbaya ya tembo mkubwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 16]

Kuhusu Pembe za Tembo

“Bila shaka pembe za tembo ni kitu kizuri. Zina uwezo wa kutoa nuru na uvutio ulio tofauti na vitu vingine vitumiwavyo kwa madoido au uchongaji. Lakini kila wakati mimi huhisi kwamba watu husahau ya kwamba pembe ya tembo ni jino la tembo. Mtu aelekea kuihusianisha pamoja na yado, mvule, mpingo, kaharabu, hata dhahabu na fedha, lakini kuna tofauti moja kuu: Hivyo vitu vingine vyote havikutoka kwa mnyama; pembe ya tembo ni jino la mbele lililo kubwa. Mtu ashikapo bangili maridadi ya pembe ya tembo au mchongo maridadi katika mkono wake, mtu ahitaji kupanua uelewevu wake ili kutambua ya kwamba kipande hicho cha pembe ya tembo kilitoka kwenye tembo ambaye wakati mmoja alitembea huku na huku akitumia pembe yake kwa kula, kuchimba, kuchoma, kucheza na kupigana, na zaidi ya hilo kwamba ilikuwa lazima tembo huyo afe ili kipande hicho cha pembe ya tembo kiwe mkononi mwako.”—Elephant Memories, kilichoandikwa na Cynthia Moss.

[Sanduku katika ukurasa wa 19]

Kuhusu Tembo

Tembo ni wenye nguvu sana, na wanapokasirika, ardhi hutetemeka. Tembo aweza kukukamata kwa mkonga wake na kukuvurumisha hewani kama jiwe. Na bado, tembo aweza kukupapasa kwa mkonga wake au kwa uanana kuchukua chakula kutoka mkononi mwako. Tembo ni wenye akili, tata, na wenye kuchekesha. Wao huonyesha uaminifu-mshikamanifu wenye nguvu kuelekea familia na watatunza majeraha ya mmoja na mwenzake, kuwatunza wagonjwa, na kuathiriwa na kifo cha mshiriki wa familia. Huku wakipuuza mabaki ya wanyama wengine, wao hutambua mifupa ya tembo wengine na huitikia kwa kuitawanya au kuizika.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nchi mbili zimechoma pembe zao za tembo; nyingine zimeweka akiba pembe zao zikiwa kitega-uchumi

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki