Je! Ni Wakati wa Kuwaaga?
VITA isiyo ya kikawaida inawaka moto katika Afrika. Si ubishi juu ya eneo, miongozo ya kisiasa, au imani za kidini. Hasara ambayo imeletea uhai wa kibinadamu, ijapokuwa yenye msiba, imekuwa ndogo sana kwa kulinganishwa na vita vilivyo vingi. Hata hivyo pigano hili limevuta fikira za mataifa kuzunguka ulimwengu. Ni vita juu ya tembo (ndovu).
Vita hiyo ni ya wakagua-mbuga na walinda-wanyama dhidi ya wawindaji haramu. Wakagua-mbuga na walinda-wanyama wanaungwa mkono na sheria, serikali zao, na wahifadhi-mazingira. Wawindaji haramu wanaungwa mkono na silaha za ki-siku-hizi na wasukumwa na shida na pupa—meno ya tembo huleta pesa, ambazo mara nyingi huwa utajiri mwingi usiowaziwa katika nchi zilizo maskini zaidi. Pande zote mbili zinafyatua risasi ili kuua. Kwa nini tembo wahangaikiwe sana kadiri hiyo? Je! kweli tisho lililo dhidi yao ni zito kadiri hiyo?
Uwindaji haramu Waua
Basi, fikiria hivi: Katika miaka ya 1930 kulikuwako tembo kama milioni kumi katika Afrika. Kufikia 1979 kulikuwa na milioni 1.3. Sasa, miaka kumi baadaye, hesabu hiyo imepunguzwa ikawa nusu. Makadirio juu ya hesabu ya tembo wa Kiafrika leo huonyesha karibu 625,000. Kwa nini kukawa na mzoroto wa haraka hivyo? Uwindaji haramu hulaumiwa kotekote. Ni uhalifu wa kale unaovuvumka kama uyoga siku hizi, kwa msaada wa tekinolojia (ufundi).
Zamani, wawindaji haramu wa Afrika walikuwa wanakabila wenye silaha za pinde na mishale au mikuki, wakiwa tayari kutimua mbio waonapo mlinda-wanyama asiye na silaha. Leo, wote wawili, walinda-wanyama na wawindaji haramu, wana silaha, lakini mwindaji haramu ana za kadiri kubwa zaidi. Miaka ya msukosuko wa wenyewe kwa wenyewe katika Afrika imeacha nyuma uzidifu wa bunduki, zenye kupatikana vyepesi na wahalifu. Wawindaji haramu wa leo husafiri wakiwa magenge na huwinda tembo wakiwa na silaha zenye kujifyatusha kwa hali ya juu. Mnamo dakika chache wao waweza kuangusha tembo kadhaa, wang’oe meno mengi kwa kukata upande wa mbele wa vichwa kwa msumeno-mnyororo, na kusonga mbele wakiwinda. Huku bei za meno ya tembo zikipanda juu sana ulimwenguni pote, wawindaji haramu waweza kupata maelfu ya dola kwa siku moja; hata wapagazi (wabebaji-mizigo) wao waweza kupata mamia. Kama vile wazo hilo liwekwavyo na U.S. News & World Report: “Hawa si wanakabila wa kienyeji bali ni wataalamu wa hali ya juu wasio na huruma, wanaoendesha biashara yenye madonge manono.”
Biashara imekuwa ikienda vema sana. Tangu 1973 idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 85 katika Kenya, asilimia 53 katika Tanzania, na asilimia 89 katika Uganda. Kwa uhakika, kila mwaka tembo kama 70,000 wa Kiafrika huchinjwa ili kupata meno yao. Zote mbili, Zimbabwe na Kenya, juzijuzi zimewapa mamlaka walinda-wanyama wawafyatulie risasi wawindaji haramu wawaonapo. Taabu ni kwamba, wawindaji haramu nao huwafyatulia risasi—tena wakiwa na ufyatuzi wenye nguvu zaidi. Wameua wakagua-mbuga na raia kimakusudi kabisa. Katika vuli ya 1988, genge la wawindaji haramu lilishambulia makao makuu ya walinda-wanyama, likawafunga na kuwapiga wakagua-mbuga, kisha likaua faru weupe watano wa mbuga hiyo, hao wakiwa ndio wa mwisho wa aina hiyo katika yoyote ya mbuga za Kenya. Bila shaka, hao wawindaji haramu walizichukua pembe tu. Waliiacha mizoga mikubwa ya hao hayawani haba ioze.
Kwa Nini Kuwaokoa Tembo?
Wakagua-mbuga wanakufa katika jaribio la kuwalinda tembo. Kwa sasa, jitihada ya uhifadhi wa kimataifa inatayarishwa ili tembo wasitoweke kabisa kabla ya karne hii kumalizika. Lakini huenda watu wengi wakajiuliza hivi, ‘Mbona tembo wahangaikiwe sana hivyo?’ Ala, mambo ya kutoweka kabisa si mapya katika sayari hii. Kielelezo kijulikanacho sana ni wale dainosari. Sasa wasiwasi ni wa nini tembo wakitoweka kabisa?
Kwa watu wengi jibu ni kwamba kiumbe mwenyewe huyo ana fahari nyingi. Yeye ana umbo lililoundwa kwa ustadi sana. Bila shaka mtu yeyote ambaye ameona kundi la tembo porini angehisi huzuni kali atazamiapo kutoweka kwao. Njia yao ya kuzoeza na kulinda wachanga wao, matumizi ya kiufundi ya mikonga yao, hata ukubwa wao wa kuogopesha—hivyo vyote ni vizibiti halisi vya Mbuni mwenye hekima isiyolinganika.
Lakini kuna zaidi. Tembo hushiriki pia sehemu ya maana katika mifumo-mazingira wanamoishi. Tembo hubadili na kufanyiza mazingira yake kuliko kiumbe mwingine yeyote isipokuwa mwanadamu. Hata hivyo, tofauti na mwanadamu, tembo hufanya mazingira hayo yafae zaidi kukaliwa na viumbe wenzake. Jinsi gani? Jawabu lahusu hamu yao ya kula kwa pupa. Tembo hula kama kilo 136 za majani kila siku!
Katika mapori yenye kusongamana miti, tembo hukwangua matawi na miti midogo, wakiruhusu nuru zaidi ipenye ndani ya funikizo hilo la majani yenye kusongamana. Nuru hiyo huharakisha ukuzi wa majani yaliyo karibu na ardhi, hivyo yakiandaa chakula kwa wanyama wadogo zaidi, kuanzia nyati wa mwituni na nyani-watu hadi nguruwe-mwitu. Katika nyika pana za Kiafrika, au savana, tembo hufanya huduma kama hiyo: Kukwangua-kwangua kwao majani-miti ya kula huendeleza ukuzi wa maeneo yenye nyasi na miti, ambayo huruzuku namna nyingi za viumbe wenye kula mimea, kuanzia twiga na punda-milia hadi paa na nyumbu-mwitu, nyingi kuliko zile zingekuwako kama wasingefanya hivyo.
Ingawa hivyo, huu mfululizo tata wa kutegemeana huwa ni rahisi kuvunjika. Waweza kuvunjika wakati eneo lipotezapo tembo wengi mno ama wajazanapo kwa wingi mno katika eneo moja. Ainabinadamu hufanya yote mawili—huua tembo kwa wingi nje ya mbuga na kuwafanya wasongamane ndani yazo. Hivyo, shida kubwa ya tembo ni kielezi cha jambo lililo tofauti kuhusu mitoweko ambayo mwanadamu husababisha: Hiyo si sehemu ya kusudi kubwa au ubuni. Bali, husababishwa na ubinafsi, bila kujali sana matokeo. Zaidi ya hilo huonyesha kwamba mwanadamu asiyekamilika na mwenye ubinafsi hafai kusimamia sayari hii.
Pigano la Kuwaokoa
Kuna wale wanaopigana ili kuzuia wimbi hilo la machinjo. Mashirika ya hifadhi na serikali dazani moja zinafanya jitihada ya kufa na kupona ili kumlinda tembo. Lakini si zote zilizo na maafikiano juu ya jinsi ya kufanya hivyo. Kikundi kimoja kimeamua kisitafute upigaji marufuku juu ya biashara ya meno ya tembo, kikihisi kwamba marufuku hiyo ingeshurutisha uchuuzi huo uendeshwe kichinichini tu na kuufanya uwe mgumu hata zaidi kudhibiti. Ingawaje, marufuku yenye kuwekwa juu ya biashara ya pembe ya faru haijafanya lolote kupunguza harakati ya muda mrefu inayoelekeza mnyama huyo kwenye mtoweko. Hata hivyo, katika Juni 1989 vikundi kadhaa vya hifadhi vilitoa wito wa kumaliza biashara ya meno ya tembo. Siku tatu baadaye, George Bush rais wa United States aliharamisha uingizaji nchini wa meno ya tembo.
Kikundi kimoja cha hifadhi chatumainia kuhifadhi tembo karibu 200,000 au 300,000 tu, shabaha yao ikiwa ni kulinda maeneo ya dazani kadhaa. Chatumainia kuzuia biashara ya meno ya tembo kwa kusihi wanadamu waone kwamba uzuizi huo ni kwa faida yao wenyewe, kikisadikisha wakaaji wa mahali kwamba tembo waweza kuletea eneo pesa nyingi wakati uwindaji haramu uzuiliwapo. Programu hiyo imeonyesha ishara fulani za mafanikio.
Lakini ikiwa uokokaji wa tembo wategemea kujifaidi kwa binadamu, wao wako salama kiasi gani? Je! kwani si kujifadi kwa binadamu ambako kwawatisha pale mwanzoni? Ingawaje, biashara ya meno ya tembo yaendelea kusitawi, ikiwachinja hawa viumbe majumbo ili kugawia ulimwengu vifungio, vipambo, na vivalio—asilimia 80 kati yavyo ikiwa imefanyizwa kutokana na meno ya tembo yaliyopatikana kiharamu. Serikali ya Kenya imelazimika kuachisha kazi kwa muda au kufuta kabisa karibu dazani nne za wakagua-mbuga na walinda wanyama waliosemekana walishindwa kukinza uvutio wa pesa zote zile nao wakashirikiana kwa siri na wawindaji haramu. Nani angekana kwamba kizazi hiki hakikuona jamii ya kibinadamu ikifikia vina vipya vya kujifaidi yenyewe? Kadiri ainabinadamu ijishughulishavyo mno kufikiria mambo ya kibinasi, ulimwengu wazidi kukosa usalama kuliko wakati mwinginewo wote.
Kwa nasibu, Biblia yatoa tumaini zuri zaidi kwa sayari yetu na wanyama-mwitu wayo. Yatuambia kwamba karibuni Muumba atarudisha dunia kwenye hali aliyoikusudia hapo kwanza—paradiso ya tufe lote, ambapo amani itadumu. Vita ya mwanadamu juu ya tembo, na juu ya maajabu yote ya mazingira, itakwisha hatimaye.—Isaya 11:6-9.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Kwa hisani ya Clive Kihn