Tembo—Marafiki au Maadui?
NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA AFRIKA KUSINI
TEMBO huthaminiwa kwa sababu hizi na kuchukiwa kwa sababu zile. Kwa watu fulani tembo ni wafanyakazi wenye thamani, wastadi wa kukokota magogo makubwa na kuyapanga mistari-mistari kwa uzuri.[1] Wengine huwathamini tembo kwa meno yao, ngozi, na nyama. Na bado wengine huwaona kuwa tisho tu kwa ardhi na mazao yao.
Ingawa hivyo, watafiti wengi huwathamini tembo kwa njia zao za kutumbuiza. Cynthia Moss alitumia miaka 13 akiwachunguza tembo katika mbuga ya Amboseli ya Kenya. Katika kitabu chake Elephant Memories, mwanamke huyo aandika hivi: “Nimeona wale wamama wazee waheshimiwa wakiongoza na kulinda familia zao na nimewaona pia wakiacha kabisa kujiheshimu na kukimbia-kimbia kimchezo mikia yao ikiwa imekunjwa migongoni pao na wakiangalia-angalia kwa macho maangavu yaliyokodolewa sana.”[3]
Daphne Sheldrick wa Kenya amelea tembo mayatima wengi kisha akawaachilia warudi mbugani. Katika hoji moja pamoja na gazeti Getaway, alieleza hivi: “Tembo wadogo wote ambao huja wanatofautiana katika tabia za moyoni, sawa na vile watoto wa kibinadamu walivyo. . . . Kidogo wao ni wenye mashindano, huoneana wivu na uwakemeapo huenda wakanuna. . . . Wengine wao watakuwa watukutu au wasiotii kwa makusudi. Sisi hulazimika kuwatia nidhamu, sawa na vile uwatiavyo nidhamu watoto wa kibinadamu.”[7]
Zaidi ya kuwa wenye kutumbuiza, tembo hutimiza fungu lenye mafaa katika maumbile. Tembo wa hesabu isiyopita kiasi katika eneo lililowekewa mipaka huongeza wingi na unamna-namna wa mimea.[4] Kitabu Elephants, Economics and Ivory huorodhesha kazi zenye thamani kubwa, kama kufanyiza maeneo mapya yenye nyasi, kutawanya mbegu, na kupunguza “mtokeo wa mbung’o.” Watungaji wa kitabu hicho wamalizia kwamba, “tembo wana fungu la maana katika mazingira ya mbuga na misitu ya Afrika.”[5]
Hata hivyo, tembo wakiwa wengi mno husababisha hasara kwa mimea. Hapo ndipo wao huwa adui kwa watu fulani. Kwa sababu hiyo, wahifadhi-mazingira hupunguza hesabu ya tembo katika maeneo yaliyowekewa mipaka. Katika sehemu nyingine za Afrika ambako tembo wangali na nafasi tele, upunguzaji haujaanza. Jambo hilo lina faida fulani-fulani. “Katika mbuga ya Amboseli ya Kenya,” laeleza gazeti New Scientist, “ambamo hakujawa upunguzaji wowote, tembo hutembea kwa uhuru miongoni mwa wanadamu na hawaonyeshi kuwaogopa hata kidogo.”[6]
Wanasayansi wanatafuta njia tofauti za kupunguza mwendo wa kuzaana kwa tembo. Kwa sasa, mwanadamu ajifunzapo mengi zaidi juu ya tembo, bila shaka atapata sababu nyingi zaidi za kuwaona kuwa marafiki.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]
Animals/Jim Harter/Dover Publications, Inc.