Wakaa-Mapangoni wa Kenya Wasio na Kifani
Na Mleta Habari za Amkeni! Katika Kenya
TULIENDA kwa utaratibu katika njia iliyokanyagwa-kanyagwa sana. Sauti ya poromoko la maji yaliyotoa mwangwi kupitia matawi ya pori la miberoshi ilitudokezea kwamba mwisho wa kijia chetu ulikuwa karibu. Juu, mwingilio wa pango ulikuwa wazi, viumbe tuliokuja kuona baada ya safari ndefu walikuwa wamejificha humo ndani.—ndovu wa Elgoni.
Mwingilio wa pango ulikuwa karibu mita 8 urefu na mita 8 upana. Tulipokuwa tukiingia mioyo yetu ilidunda kwa mtazamio. Hata hivyo, kelele zenye kidoko za popo wenye kupuruka zilithibitisha shuku zenye kukatisha tamaa. Ama tulikuja tumechelewa mno au mapema mno. Sakafu yenye mavumbi iliyo na alama za kwato, ilitoa ushuhuda kwamba tayari ndovu walikuwa hapa na wamekwisha ondoka.
Hata hivyo, kwa nini tulitumaini kuona ndovu katika mwinuko wa karibu mita 2,134 katika mahali hapa juu ya mlima, isitoshe ndani ya pango? Hilo latokeza hadithi yenye kuvutia.
Makao ya Pangoni ya Mlima Huo
Wenye kutandaa mpakani mwa Kenya na Uganda ni ule Mlima wa Elgoni mrefu sana wa volkeno wenye sura ya pia. Ukiwa na urefu wa meta 4,322, ni mmojawapo milima mirefu zaidi iliyo peke yake katika Afrika Mashariki. Wengine hukisia kwamba kabla ya kumomonyolewa, huenda kileleta chake kifanya hata kilele cha Kilimanjaro kinachofunikwa na theluji kionekane kifupi sana. Mlima huo unajitokeza juu ya misitu yenye kuvutia, chemchemi za maji moto, na maziwa yenye maji baridi. Hata hivyo, labda mapango mengi ya Elgoni ndiyo hasa yenye kuvutia zaidi. Mapango hayo ndiyo makao ya ndovu tuliotamani sana kuona.
Wakati mmoja mapango haya yalikuwa makao ya Wakonyi, au Wamaasai wa Elgoni. Wengine wanahisi kwamba mlima huu unaitwa kwa jina lao. Wakonyi walifika hapa mara ya kwanza zaidi ya miaka 300 iliyopita. Wakati Joseph Thomson, mzungu wa kwanza kuvumbua eneo hilo, alipopitia hapo katika 1883, bila shaka alishangaa kupata vijiji vingi vilivyojengwa katika baadhi ya mapango hayo.
Kwa sehemu kubwa, Wamaasai hao wameyaacha makao yao ya mapangoni, ingawa baadhi ya Wamaasai wangali wanaishi katika baadhi ya mapango ya chini kandokando ya Mlima Elgoni. Baada ya muda wanyama wenye kupamba misitu hii walianza kuishi katika mapango hayo yaliyoachwa. Nyati walivutwa na vidimbwi vya matope vyenye kutamanisha vipatikanavyo ndani yayo. Vijumbamshale na mbayumbayu walikuwa na hamu ya kula wadudu wote watamu waliomo humo ambao walivutwa na uchepechepe wa viziwa vya mapango hayo.
Hata hivyo, jambo la kustaajabisha, mapango hayo yalikuwa yenye kuvutia pia kwa wasioelekea sana kuwa wakaaji wa mapango hayo—ndovu. Mpaka leo hii majitu hao wazito sana husukumiza mili yao ya uzito wa tani nne hadi sita wakipanda kupitia vijia vilivyoiinuka sana na vilivyo vyembamba ili kufikia mapango hayo. Ni nini kinachowaleta hapa?
Wachimbua Chumvi
Ndani yamapango hayo mnapatikana mlo wa ziada ambao mili yao mikubwa huhitaji sana. Kwa kawaida, majani yanaandaa chumvi ya kutosha katika mlo wao, lakini kwenye mwinuko huu wa juu, chumvi imemomonyolewa na mvua kutoka katika udongo. Kwa hiyo ndovu hupiga safari hiyo ndefu na yenye kuchosha ili kupata chumvi (chumvi ya Glauber) ambayo hupatikana katika tabaka nyororo ya mwamba ndani ya mapango.
Ili kufikia chumvi, ndovu wanatumia ustadi wa aina ya pekee. Wanaweka mkonga wao mahali panapochomoza au penye ufa katika ukuta wa pango. Halafu, kwa msukumo wenye nguvu wa mili yao iliyo kama buldoza (trekta) wanang’oa vipande vya jiwe. Baada ya kuweka kipanda cha jiwe mdomoni mwao kwa mkonga wao mwepesi, ndovu hao wanakisaga kwa magego yao yenye nguvu na kumeza changarawe na chumvi pamoja. Hilo hurudiwa-rudiwa mpaka ndovu wanapotosheka. Baadaye, usingizi kidogo katika shimo hilo la chumvi lenye giza na baridi, yaonekana husaidia kuyeyusha chakula.
Kwa kupendeza, ingawa pembe za ndovu huendelea kukua katika muda wote wa maisha, mara nyingi hizo huzidi kufupika na kuwa vigutu tu—hiyo ikiwa hasara wanayopata kwa jitihada ya kupata vidonge vya chumvi.
Baada ya ndovu kukaa ndani na karibu na mapango kwa majuma kadha, wanapata tena hamu ya kutanga-tanga. Wanaweza kuandamana mpaka kwenye pori la mianzi kuguguna machipukizi yayo mororo au maganda yayo magumu. Ndovu hutumia karibu saa 18 kwa siku kula, nao hula kufikia kilogramu 170 za majani. Baada ya wakati fulani kupita mapango ya Elgoni huwavuta kwa sababu ya hamu yao nyingi ya chumvi.
Kwa kufikiria maelekeo yao ya kuhamahama na idadi yao ndogo (mia moja ni kisio kubwa), si ajabu kwamba tulikosa kuwaona ndovu hao wenye kusafiri.
Hatimaye Ndovu!
Tulipokuwa tukitoka kambini asubuhi iliyofuata, tuliendesha polepole kupitia msitu uliolowana umande, ambao ulijaa mbega na ndege wenye kuimba. Ghafula, kukawa na kishindo kikubwa, kikifuatwa na mtikisiko wa ghafula wa vichaka vilivyokuwa karibu! Tuliendesha polepole kufikia mita chache kutoka kwenye ule msukosuko.
Tukiwa tunangojea kwa kimya, tulisikia sauti iliyosikika kidogo tu ya mili ile yenye kujisukumiza upande wa nyuma wa kichaka kirefu kilichokuwa sambamba na njia yetu. Mwishowe, mmoja wa hayawani hao wenye haya, dume mchanga, akajivumisha karibu meta tatu kutoka gari letu, baada ya kuchoshwa na mchezo wetu wa mwajificho. Alikuwa mwenye kupendeza na mwenye afya, na rangi yake ya udongo mwekundu ilikuwa inametameta katika jua jangavu la asubuhi. Kijapokuwa kimo chake kifupi, sura yake ya kutia hofu ilistahili heshima.
Nilijaribu kuweka kamera katika hali ambayo ingetokeza picha zuri. Lakini kizibo hakikufunguka; nilikuwa nimeishiwa na filamu! Halafu ndovu-mama akatokea na kusindikiza mtoto wake kupitia mbele ya gari letu. Kufikia wakati ambao nilikuwa nimetia filamu katika kamera yangu, ndovu hao walikuwa mbali sana nisiweze kupiga picha ya karibu yenye kutokeza, lakini nilipiga picha ambayo ingethibitisha kwamba angalau niliwaona majitu hao ambao ni vigumu kuwaona.
Hao ni viumbe wenye kushangaza kama nini! Waweza kuwa wanyamavu kama panya, hali ni wazito kuliko gari. Wakubwa kuliko baadhi ya magari ya kubebea mizigo, hali si rahisi kuonekana. Lakini hilo lisikuzuie kutembelea makao ya wakaa-mapangoni wa Kenya wasio na kifani.