Uhifadhi Dhidi ya Utoweko
VITA baina ya uhifadhi na utoweko yaendelea kupiganwa. Mashirika mengi ya kutoa msaada yanakaza serikali ziweke sheria kali zaidi za uhifadhi ili kulinda spishi zilizo hatarini mwa kutoweka.
Kwa kielelezo, hivi majuzi vikundi kadhaa vilikutana na maofisa wa China na kuwashawishi washirikiane navyo katika jitihada za kuondosha kutegwa kwa dubu-weusi wa Asia. Wanyama hao walikuwa wakinaswa kwa sababu ya nyongo na kibofu chao cha nyongo, ambazo hutumiwa katika dawa za kienyeji za Mashariki.
Msaada wa Kimataifa
Kulinda spishi katika nchi moja lakini kuiwinda itoweke kwingineko hakufanikishi uhifadhi wayo. Kufuatia hilo, mapatano ya kimataifa yamefanywa kwa wakati ufaao—na ni mapatano mengi ambayo yamefanywa. Ule Mkutano wa Mambo Mbalimbali ya Kibiolojia, Mkataba wa Rio, ulianza kutekelezwa mwishoni mwa 1993, ukifuatwa kwa ukaribu na Mwafaka wa Hifadhi ya Popo Katika Ulaya. Tume ya Kimataifa ya Kuhifadhi Nyangumi iliongeza pia hifadhi ya nyangumi ya Bahari Kuu za Kusini kwa ile hifadhi ya Bahari Kuu ya Hindi katika majaribio ya kulinda nyangumi mkuu na nyangumi minke. Lakini labda mwafaka ulio na nguvu zaidi ni ule Mkutano wa Kupinga Biashara ya Kimataifa ya Spishi Zilizo Hatarini mwa Kutoweka.—Ona sanduku.
Mwanadamu angali ana mengi ya kujifunza juu ya mahusiano yaliyo kati ya viumbe. Wavuvi wa Afrika Mashariki walioingiza mbuta katika Ziwa Viktoria ili kuongezea ugavi wa chakula walianzisha kile ambacho mtaalamu wa wanyama Colin Tudge akiita “msiba mkubwa zaidi wa ikolojia uliopata kutukia katika karne hii.” Spishi zipatazo 200 kati ya 300 ambazo zilikuwako zilitoweka. Ingawa uthibitisho wa majuzi walaumu mmomonyoko wa udongo kwa kuharibu usawaziko wa spishi, serikali za zile nchi tatu ambazo zimepakana na ziwa hilo sasa zimeanzisha shirika moja la kuamua ni spishi zipi za samaki ziwezazo kuingizwa katika ziwa bila kuhatarisha samaki wa ziwa hilo.
Mwingilio wa Binadamu
Eneo moja ambalo limepata mafanikio ni programu ya ufugaji wa wanyama waliofungiwa ambayo makao mengi sana ya wanyama huendesha. “Makao yote ya wanyama ulimwenguni yakitegemeza ufugaji wa wanyama waliofungiwa, na umma ukitegemeza makao ya wanyama, basi kati yao wao waweza kuhifadhi viumbe vyote vyenye uti wa mgongo ambavyo yaelekea vitahitaji kufugwa vikiwa vimefungiwa katika wakati ujao ulio karibu.”—Last Animals at the Zoo.
Kao moja la wanyama katika kisiwa kidogo cha Uingereza cha Jersey hufuga wanyama walio nadra kwa kusudi la kuwarudisha porini. Katika 1975, ni kasuku 100 pekee wa St. Lucia waliokuwa wamebaki nyumbani katika Karibea. Ndege saba kati yao walipelekwa Jersey. Kufikia 1989 kao hilo la wanyama lilikuwa limefuga ndege wengine 14 na kuwarudisha wengine St. Lucia. Sasa inaripotiwa kwamba zaidi ya ndege 300 wamo katika kisiwa hicho.
Mipango kama hiyo imefaulu kwingineko. National Geographic laripoti kwamba mbwa mwitu wekundu 17 waliobaki Amerika Kaskazini walizaana vema sana katika makao ya kufungiwa hivi kwamba zaidi ya 60 sasa wamerudishwa porini.
Je, Ni Mafanikio Mno?
Si kwamba wanyama walio hatarini sikuzote wametishwa na kutoweka. Kulingana na kitabu Endangered Species—Elephants, kati ya 1979 na 1989, idadi ya tembo wa Afrika ilipunguka toka 1,300,000 hadi 609,000—baadhi ya upungufu huo ukisababishwa na uwindaji haramu wa pembe. Ndipo mkazo wa umma wa kupiga marufuku biashara ya pembe ukaongezeka. Lakini upinzani dhidi ya marufuku nao ukawaka. Kwa nini?
Katika Zimbabwe na Afrika Kusini, sera za uhifadhi zilifanikiwa sana hivi kwamba mbuga zao za kitaifa na hifadhi zao zilikuwa na tembo wengi kupita kiasi. Gazeti New Scientist liliripoti kwamba Zimbabwe ilihitaji kuondoa tembo 5,000 kutoka Mbuga ya Kitaifa ya Hwange. Vikundi vya hifadhi vikapendekeza kwa bidii kwamba suluhisho ni kuwahamisha mahali pengine. Maofisa wa mbuga wakataka kuuza tembo wa ziada na kusema kwamba mashirika ya nchi za Magharibi yanayopinga kuuawa kwa tembo dhaifu “yatoe msaada wa kifedha wa kuwahamisha badala ya kupayuka.”
Matazamio ya Kutilika Shaka
Hata hivyo, kutofanikiwa hutukia pia. Wengi huhangaikia spishi zinazorudishwa porini. Simbamarara wa Siberia hufanya vema katika makao ya kufungiwa, lakini porini anahitaji kilometa 260 za mraba za misitu bila wawindaji haramu. Isitoshe, “mweke simbamarara aliyelelewa katika makao ya wanyama katika mazingira yake,” lasema The Independent on Sunday, “na kwa hakika karibu atakufa njaa.” Tazamio lenye kuhuzunisha kwelikweli!
Kwa hakika, si kila spishi ambayo ina kikundi chayo tu cha kuisaidia. Na si kukosa tu watu wa kufanya kazi hiyo kunakotokeza tatizo. Hata wahifadhi wawe wamejitolea kadiri gani, wanapokabiliwa na ufisadi serikalini, pupa, kutojali na vilevile vita na hata tisho la kuuawa, wao wana tumaini gani la kufanikiwa? Basi, kuna suluhisho gani kwa tatizo la spishi zilizo hatarini mwa kutoweka? Na wewe unahusikaje?
[Sanduku katika ukurasa wa7]
Silaha ya Kimataifa
Mkutano wa Kupinga Biashara ya Kimataifa ya Spishi Zilizo Hatarini mwa Kutoweka ni silaha yenye nguvu katika vita dhidi ya biashara haramu ya spishi zilizo hatarini mwa kutoweka. Ngozi za chui, pembe za tembo, mifupa ya simbamarara, pembe za kifaru, na kasa ni miongoni mwa bidhaa ambazo zimepigwa marufuku. Mwafaka huo hata watia ndani miti na samaki walio hatarini mwa kutoweka.
Lakini, Time lilionya hivi: “Mataifa wanachama yasipotafuta njia za kuhakikisha kwamba sheria hizo zinafuatwa, . . . hayo yanaweza kugutuka kupata kwamba kumbe wanyama yanaojaribu kulinda wametoweka.”
[Picha katika ukurasa wa 8]
Je, jitihada fulani za uhifadhi zimefanikiwa mno?
[Hisani]
Kwa hisani ya Clive Kihn